Je, mwisho wa vita Gaza wakaribia?

Moshi ukiongezeka kufuatia milipuko katika mji wa Gaza siku ya Jumapili

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Moshi ukiongezeka kufuatia milipuko katika mji wa Gaza siku ya Jumapili
    • Author, Mariam Mjahid
    • Nafasi, BBC News Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 12

Hata kwa Donald Trump rais anayefurahia kuwa kitovu cha matukio ya dunia hili lilikuwa tukio la kusisimua.

Siku ya Jumatano mjini Washington DC, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, aliingia ghafla kwenye kikao kilichokuwa kikiendeshwa moja kwa moja na Rais Trump.

Alimkabidhi ujumbe muhimu: Rais alihitajika kutangaza kwa dunia kwamba makubaliano yamefikiwa.

Trump alieleza hadhira ukumbini na mamilioni waliotazama tukio hilo kupitia video kwamba alilazimika kuondoka.

"Wananihitaji…" alisema, akikatiza shughuli za siku hiyo. "Nahitaji kwenda sasa hivi kusaidia kutatua baadhi ya matatizo ya Mashariki ya Kati."

Baada ya siku tatu za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja huko Misri, Israel na Hamas walikubaliana hatua ya kwanza ya kile ambacho Trump anatarajia kuwa mchakato mpana wa makubaliano ya amani ya kudumu.

Wapatanishi kutoka Qatar na Misri walikuwa wakihama kati ya wawakilishi wa Israel na Palestina waliokuwa katika ghorofa tofauti za hoteli moja katika mji wa mapumziko wa Sharm El-Sheikh. Ili kuongeza uzito kwenye meza ya mazungumzo na kuweka shinikizo kwa Israel, Trump alimtuma mkwe wake Jared Kushner pamoja na mjumbe wake maalum, Steve Witkoff.

Kwa upande wa Hamas, waziri mkuu wa Qatar na wakuu wa idara za ujasusi kutoka Misri na Uturuki walikuwepo kuwawakilisha.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Makubaliano haya ni mafanikio makubwa lakini hayamaanishi kuwa vita vimeisha.

Hata hivyo, kwa mara ya kwanza tangu mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel, kuna mwangaza wa matumaini ya kumaliza machungu ya miaka miwili.

Trump mwenyewe amedai kwamba makubaliano haya yanaweza kuwa "tukio kubwa zaidi Mashariki ya Kati katika kipindi cha miaka 3,000."

Kauli hiyo ni ya mtindo wa kawaida wa kupindukia wa Trump.

Lakini kama ubadilishanaji wa mateka wa Waisraeli kwa wafungwa wa Kipalestina utafuatwa na mafanikio katika vipengele vingine vya mpango wa Trump, basi kuna uwezekano halisi wa kuondoa baadhi ya mateso ya pande zote mbili.

Wajumbe kutoka Israel na Hamas walifanya siku yao ya kwanza ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja nchini Misri siku ya Jumatatu kuhusu mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kusitisha vita huko Gaza, wakikabiliana na masuala yenye utata kama vile kutaka Israel ijiondoe na Hamas kupokonywa silaha.

Israel na Hamas zote zimeidhinisha kanuni za jumla nyuma ya mpango wa Trump, ambapo mapigano yatakoma, mateka wanaachiliwa na misaada kumiminika Gaza.

Mpango huo pia unaungwa mkono na mataifa ya Kiarabu na Magharibi.

Trump ametaka mazungumzo yafanyike haraka kuelekea mapatano ya mwisho, katika kile ambacho Washington inakitaja kuwa ndio pande za karibu zaidi za kumaliza mzozo huo uliodumu kwa miaka miwili.

Trump, ambaye amejiweka kuwa kiongozi pekee wa dunia mwenye uwezo wa kufikia amani huko Gaza, amewekeza mtaji mkubwa wa kisiasa katika juhudi za kumaliza vita ambavyo vimeua makumi kwa maelfu na kumwacha mshirika wa Marekani Israel akizidi kutengwa katika jukwaa la dunia.

Mazungumzo hayo yanapangwa kuendelea Ijumaa katika mji wa Sharm El-Sheikh nchini Misri.

Maafisa wa Palestina na Misri wameiambia BBC kwamba vikao hivyo vinalenga "kuunda mazingira" ya uwezekano wa mabadilishano ambayo yatawezesha kuachiliwa kwa mateka wote wa Israeli kama malipo ya wafungwa kadhaa wa Kipalestina.

Hatua hiyo huenda ikamaanisha kuwa vita vilivyoendelea kwa miaka miwili sasa vinaelekea kufikia tamati.

Mpango huo umeibua matumaini ya kuwepo kwa amani miongoni mwa Wapalestina lakini hakukuwa na kukoma kwa mashambulizi ya Israel huko Gaza siku ya Jumapili huku ndege na vifaru vikishambulia maeneo katika eneo hilo, na kuua takriban watu 19, mamlaka ya afya ya eneo hilo ilisema.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Je, mashambulizi yamekoma Gaza?

Bado.

Licha ya wito wa Rais Trump wa kusitisha mashambulizi na hali ya utulivu siku ya Jumamosi siku moja baada ya Hamas kujibu mpango huo hakuna dalili ya kupungua kwa mashambulizi ya anga na mabomu kwa kiasi kikubwa.

Ripoti kutoka Gaza zinasema Israel iliendelea na mashambulizi ya anga na mizinga usiku kucha na hadi Jumapili, na kuharibu idadi kubwa ya majengo ya makazi katika mji wa Gaza.

Mwandishi wa BBC alisikia milipuko kutoka ndani ya Gaza na kuona moshi mwingi akiwa karibu na mpaka wa Kibbutz Be'eri, Israel, Jumapili asubuhi.

Watu wengine 65 waliuawa na operesheni za kijeshi za Israel katika muda wa saa 24 kabla ya saa sita mchana, wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas ilisema.

Pia unaweza kusoma:

Je, makubaliano haya yanamaanisha vita vinaelekea kumalizika?

Inawezekana.

Licha ya changamoto kubwa zilizo mbele, wapo wanaoamini kuwa mwisho wa vita vya Gaza unaweza kufungua ukurasa mpya wa amani Mashariki ya Kati.

Hilo, hata hivyo, litahitaji jitihada za kweli na uthabiti wa kisiasa mambo ambayo Trump bado hajaonyesha kwa kiwango kinachohitajika.

Mazungumzo ya haraka na ya shinikizo kama yaliyofanyika Misri yanaendana na mtindo wa Trump wa moja kwa moja na wa kishindo.

Lakini kutatua mgogoro wa zaidi ya miaka 100 kati ya Waisraeli na Wapalestina juu ya udhibiti wa ardhi kati ya Mto Jordan na Bahari ya Mediterania, kutahitaji mbinu za kisiasa zilizo tulivu, za kina, na za muda mrefu.

Kama mpango wa Trump wa vipengele 20 utaleta mwisho wa vita, basi Marekani italazimika kuendelea kuihimiza Israel.

Swali kuu ni: je, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, atajaribu kurejea vitani baada ya mateka kurudi nyumbani? Washirika wake wa siasa kali za mrengo wa kulia ndani ya baraza la mawaziri wanashinikiza hilo lifanyike.

Nchi tajiri za Ghuba ambazo Trump anazishinikiza na anazitaka zishiriki katika kujenga upya Gaza zinatarajiwa kuendelea kuishinikiza Marekani kuhakikisha kuwa hali ya vita hairejei tena.

Trump akisema ana dhamira ya kumaliza mzozo huu kupitia mpango wake wa vipengele 20.

Kupitia ujumbe alioutuma Ijumaa, alisema: "Hili si suala la Gaza peke yake, bali ni juhudi za muda mrefu za kuleta amani Mashariki ya Kati."

Hata hivyo, makubaliano haya yanakuja baada ya majaribio kadhaa ya awali ya kusitisha vita moja kwa moja mwanzoni mwa vita mnamo 2023 na jingine mapema mwaka huu ambayo yalidumu kwa muda mfupi kabla ya mapigano kurudi tena.

Soma pia:

Nini kimekubaliwa?

Sasa kwa kuwa makubaliano yameidhinishwa rasmi na baraza la mawaziri la Israel, inatarajiwa kwamba usitishaji wa mapigano utaanza kutekelezwa.

Ripoti kutoka vyombo vya habari vya Israeli zinapendekeza kuwa hatua hiyo itaanza mara moja, ingawa msemaji wa ofisi ya waziri mkuu alisema itaanza ndani ya saa 24 tangu kuidhinishwa kwa makubaliano hayo.

Msemaji huyo alisema kuwa jeshi la Israel litaondoka hadi katika mstari utakaowaacha wakidhibiti takriban asilimia 53 ya Ukanda wa Gaza.

Kulingana na ramani iliyotolewa na Ikulu ya White House wiki iliyopita, hii ni awamu ya kwanza kati ya tatu za kuondoka kwa jeshi la Israel kutoka Gaza.

Jeshi la Israel lilitangaza Alhamisi kuwa maandalizi yanaendelea kwa ajili ya "kubadilisha mistari ya doria kwa mujibu wa hali mpya."

Baada ya hapo, saa 72 za kuhesabu zitaanza, ambapo Hamas itatakiwa kuwaachilia mateka wote 20 wanaoaminika kuwa hai.

Miili ya mateka 28 waliokufa itarudishwa baadaye, ingawa haijafahamika ni muda gani utahitajika kwa hilo kutekelezwa.

Baadaye, Israel itawaachilia takriban wafungwa 250 wa Kipalestina waliokuwa wakitumikia vifungo vya maisha katika magereza ya Israel, pamoja na wafungwa wengine 1,700 kutoka Gaza, kwa mujibu wa chanzo cha Kipalestina kilichoeleza BBC.

Majina yao bado hayajajulikana, lakini orodha iliyowasilishwa na Hamas kabla ya kufikiwa kwa makubaliano hayo inajumuisha watu mashuhuri waliokuwa wanakabiliwa na vifungo vingi vya maisha kwa kuhusika na mashambulizi hatari dhidi ya Waisraeli.

Mmoja wa wafungwa maarufu zaidi, Marwan Barghouti, hataachiliwa kama sehemu ya mpango wa kubadilishana mateka, kwa mujibu wa msemaji wa Israeli.

Israel pia itarudisha miili ya Wapalestina 15 kwa kila mwili mmoja wa mateka wa Kiyahudi, kulingana na mpango wa Trump.

Mamia ya malori yaliyobeba misaada ya kibinadamu pia yataanza kuingia Gaza, ambako janga la njaa lilithibitishwa na wataalam wanaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa mnamo Agosti.

Mpango wa Trump umeainisha kuwa malori 600 ya misaada yatakuwa yanaingia kila siku, lakini vyanzo vya Kipalestina vimesema kuwa awali kutakuwa na kiwango cha chini cha malori 400 kwa siku, idadi ambayo itakuwa inaongezeka hatua kwa hatua.

Nini kinafuata, na lini?

Iwapo awamu ya kwanza ya mpango wa vipengele 20 wa Trump itatekelezwa kikamilifu, hatua hiyo itafuatiwa na mazungumzo kuhusu vipengele vya awamu zinazofuata ingawa baadhi ya hoja hizo zinaweza kuwa ngumu kufikiwa makubaliano juu yake.

Pendekezo hilo ambalo linaweza kusomwa kwa ukamilifu linaeleza kuwa iwapo litakubaliwa na pande zote mbili, basi vita vitaisha mara moja.

Linasema kuwa Gaza itakuwa eneo lisilo na silaha na kuwa miundombinu yote ya kijeshi, ugaidi, na mashambulizi itaharibiwa.

Gaza itatawaliwa na kamati ya mpito ya muda, itakayojumuisha wataalamu wa Kipalestina (technocrats) chini ya usimamizi wa "Bodi ya Amani" itakayoongozwa na Donald Trump na kushirikisha pia aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair.

Uongozi wa Ukanda wa Gaza hatimaye utakabidhiwa kwa Mamlaka ya Palestina (Palestinian Authority – PA), baada ya kufanyiwa mabadiliko muhimu.

Hamas haitakuwa na nafasi yoyote katika uongozi wa Gaza moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kulingana na mpango huo.

Wanachama wa Hamas watapewa msamaha iwapo watakubali kuishi kwa amani, au kupewa njia salama ya kwenda nchi nyingine.

Hakuna Mpalaestina atakayelazimishwa kuondoka Gaza, na wale wanaotaka kuondoka watakuwa huru kurejea.

"Mpango wa Trump wa maendeleo ya uchumi wa Gaza" utaandaliwa na jopo la wataalamu, kwa ajili ya kujenga upya na kuhuisha uchumi wa eneo hilo.

Vikwazo katika awamu zijazo

Hata hivyo, kuna uwezekano wa kutokea kwa mvutano mkubwa kuhusu baadhi ya vipengele vya awamu za baadaye za mpango huu.

Hamas imewahi kusema wazi kuwa haitakubali kuweka silaha chini hadi pale taifa la Palestina litakapoundwa rasmi.

Katika majibu yake ya awali kuhusu mpango huu mwishoni mwa wiki iliyopita, kundi hilo halikutaja chochote kuhusu kuachana na silaha, jambo ambalo limezua hisia kuwa msimamo wao bado haujabadilika.

Na ingawa Israel ilikubali mpango huo kwa ujumla, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alionekana kupinga wazo la ushiriki wa Mamlaka ya Palestina katika kuiongoza Gaza baada ya vita hata alipokuwa jukwaani pamoja na Rais Trump wiki iliyopita akisisitiza kwamba Mamlaka ya Palestina haitakuwa na nafasi ya kuongoza eneo hilo.

Hamas, kwa upande wake, imesema inatarajia kuwa na nafasi fulani katika uongozi wa Gaza kama sehemu ya "harakati ya pamoja ya Wapalestina."

Kikwazo kingine ni kuhusu kiwango cha kuondolewa kwa majeshi ya Israeli.

Israel imesema kuwa katika awamu ya kwanza itadhibiti takriban asilimia 53 ya Gaza.

Mpango wa White House unaonesha kuwa kutakuwa na awamu za ziada za kuondoka kwa majeshi hadi kufikia asilimia 40, kisha 15.

Awamu ya mwisho itakuwa "eneo la usalama" ambalo litaendelea kuwepo hadi Gaza itakapoonekana kuwa salama dhidi ya tishio lolote la ugaidi kuibuka tena.

Hata hivyo, maelezo haya ni ya jumla na hayajabainisha ratiba maalum ya kuondoka kikamilifu kwa majeshi ya Israeli jambo ambalo huenda likawa suala nyeti ambalo Hamas italitaka lijadiliwe kwa uwazi zaidi.

Oren Setter, mtafiti mwandamizi katika Kituo cha Belfer cha Chuo Kikuu cha Harvard na aliyewahi kuwa mkuu wa mipango ya kimkakati wa Jeshi la Ulinzi la Israel, aliiambia shirika la Reuters kuwa : "Hii ni hatua kubwa ya kidiplomasia aliyofanikisha Trump, lakini ni mwanzo tu wa mchakato, si mwisho wake."

Je, Hamas na Israel wana karata zipi za kisiasa?

Wapalestina walilazimika kutoroka Khan Yunis mnamo Septemba 2024, bila maji, vyoo, au chakula.

Chanzo cha picha, getty

Maelezo ya picha, Wapalestina walilazimika kutoroka Khan Yunis mnamo Septemba 2024, bila maji, vyoo, au chakula.

Wote Israel na Hamas wanaonekana kuonyesha mwitikio chanya kwa mpango wa Trump, lakini kila upande una malengo yake ya kisiasa.

Kwa Netanyahu, kukubali mpango huu kunaweza kuwa njia ya kuendeleza uhusiano wake na Marekani mshirika muhimu kwa Israel huku akijitahidi kutotoa nafasi kubwa kwa Wapalestina ili kuwalinda washirika wake wa kisiasa wa mrengo wa dini na utaifa, ambao wamekuwa wakipinga vikali makubaliano yoyote ya amani na Palestina wakitaka vita viendelee.

Kwa upande wa Hamas, kukubali kuachilia mateka huku wakiacha baadhi ya masuala bila majibu ya moja kwa moja kunaweza kuwa mkakati wa kuhamisha shinikizo kwa mataifa mengine, hususan Qatar, Misri, na nchi nyingine za Kiarabu au Kiislamu ambazo zimekuwa zikimtaka Rais wa Marekani kuingilia kati kumaliza mzozo.

Amjad Iraqi, mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka kundi la International Crisis Group, akizungumza na Reuters,"Hamas imecheza karata ya busara kwa kusema 'ndiyo, lakini…'. Kwa njia hiyo, wamefanikiwa kuurudisha mpira mikononi mwa Netanyahu, lakini pia kwa mataifa ya Kiarabu."

Wakati huo huo, kamanda anayesimamia Hamas huko Gaza, Ez al-Din al-Haddad, anajiandaa kwa kile kamanda mmoja wa Hamas alielezea kwa BBC kama "vita vya mwisho" vinavyohusisha wapiganaji wapatao 5,000.

Je, Trump amepanga nini kuhusu majibu ya Hamas?

Rais wa Marekani Donald Trump

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump

Trump, alipoulizwa na Jake Tapper wa CNN nini kitatokea ikiwa Hamas itasisitiza kusalia madarakani huko Gaza, alijibu kwa ujumbe mfupi kwamba kundi hilo litakabiliwa na "kufutwa kabisa".

Rais wa Marekani alichapisha kwenye mitandao ya kijamii kwamba Israel imekubali njia ya awali ya kujiondoa huko Gaza, ikiwa ni ya kwanza katika msururu wa mapendekezo ya vikosi vya Israel vya kujiondoa.

Hata haya yakiendelea kutia wasiwasi utekelezaji wake, Israel inajipata katika njia panda hasa katika macho ya dunia, wengi wakiliona kuwa linahujumu haki za kibinadamu.

Haya yalidhihirika wazi katika mkutano wa Umoja wa Mataifa uliokamalika mwezi jana mjini Newyork.

Vita bado vinaendelea licha ya hatua za makubaliano

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio anasema kuhusu makubaliano ya Gaza: "Hakuna anayeweza kusema ni asilimia 100.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio anasema kuhusu makubaliano ya Gaza: "Hakuna anayeweza kusema ni asilimia 100.

Waziri wa masuala ya Kigeni nchini Mareni Marcus Rubio alisema kuwa vita bado havijaisha, ingawa Israel na Hamas zimekubaliana na baadhi ya vipengele vya mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu Gaza.

Raia wa Gaza wamekuwa wakitoa wito wa utekelezaji wa haraka wa mpango huo ili kuhitimisha mateso yao.

"Tutajua haraka kama Hamas ina nia ya dhati au la, kulingana na jinsi mazungumzo ya kiufundi yatakavyokwenda kuhusu maandalizi ya kuwaachilia mateka," Rubio alisema kwenye Meet the Press ya NBC News.

Mashambulio ya mabomu ya Israel yaliendelea katika maeneo kadhaa ya Ukanda wa Gaza siku ya Jumatatu kabla ya kuanza kwa mazungumzo.

Israel inaendesha mashambulizi katika mji huo, ambayo imesema inalenga kuwaachilia mateka waliosalia.

Mahmoud Basal, msemaji wa ulinzi wa raia wa Gaza unaoendeshwa na Hamas, aliiambia BBC kwamba "hakuna lori za misaada zimeruhusiwa kuingia Gaza City tangu mashambulizi yaanze wiki nne zilizopita".

"Bado kuna miili ambayo hatuwezi kuipata kutoka maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa Israel," alisema.

Mamia kwa maelfu ya wakaazi wa Mji wa Gaza wamelazimika kutoroka baada ya jeshi la Israel kuamuru kuhamishwa hadi katika eneo lililoteuliwa la "kibinadamu" kusini, lakini mamia ya maelfu ya wengine wanaaminika kusalia.

Waziri wa ulinzi wa Israel ameonya kwamba watakaosalia wakati wa mashambulizi hayo watakuwa "magaidi na wafuasi wa ugaidi".

Katika saa 24 zilizopita, Wapalestina 21 wameuawa huko Gaza na wengine 96 kujeruhiwa, wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas ilisema katika sasisho lake la hivi punde.

Waandishi wa habari wa kimataifa wamepigwa marufuku na Israel kuingia Ukanda wa Gaza kwa uhuru tangu kuanza kwa vita hivyo na kufanya kuthibitisha madai ya pande zote mbili kuwa ngumu.

Tofauti ya mchakato wa kusitisha vita na awali

Tofauti kuu katika mazungumzo haya ni ushiriki wa moja kwa moja wa Rais Trump,

ambaye ameweka shinikizo kubwa si tu kwa Hamas bali pia kwa Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu.

Trump anataka makubaliano yafikiwe haraka, ndani ya siku chache, huenda hata kabla ya Ijumaa, siku ambayo Tuzo ya Amani ya Nobel itatangazwa.

Hivyo basi kuna msukumo mkubwa wa kufikia makubaliano, lakini kuna mengi yanayoweza kwenda kombo.

Changamoto za utekelezaji wa awamu kwa awamu

Awamu zilizopita za kusitisha mapigano kati ya Hamas na Israel zilipendelewa ziwe ni za awamu jambo ambalo halikutimia kwani kila upande ulihisi kuwa mwenzake hafuati mapendekezo kikamilifu.

Mapema mwaka huu awamu ya kubadilishana mateka iliisha ghafla baada ya kutoaminiana kwa pande zote mbili.

Upande wa Israel walianza kulalamika kuwa baadhi ya mateka waliopatiwa sio walivyoahidiwa baada ya kufanya uchunguzi wa msimbojeni kwa miili hiyo.

Nao wanamgambo wa Hamas walitumia fursa hiyo ya ubadilishanaji mateka kuwa hafla ya kuonyesha kuwa walikuwa wakiwahudumia vizuri mateka wa Israel waliokuwa mikononi mwao kwa kuwapa zawadi za kurudi nazo makwao.

Shirika la msalaba mwekundu ndio zilikuwa na jukumu la kusafirisha mateka hao.Hta hivyo huenda pande zote mbili zilijifunza na athari ya kilichotokea baada ya kusitisha ubadilishanaji mateka na huenda duru hii mambo yakawa yana utofauti na kufua dafu.

Kwa sasa, eneo hilo linashikilia pumzi yake huku wapatanishi wakiingia mezani nchini Misri, wakitumai kwamba licha ya kutoaminiana sana na udhaifu wa kisiasa duru hii inaweza hatimaye kufungua njia kuelekea usitishaji mapigano bila kujirudia tena.

Soma pia:

Imehaririwa na Ambia Hirsi