'Niko radhi kufa kupata mfuko mmoja wa unga'

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Swaminathan Natarajan & Gaza Lifeline
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 8
"Watoto wangu wote wanne wanalia kwasababu hawajakula chakula kwa siku nne," anasema baba mmoja wa Gaza.
"Nilienda katika kituo kinachotoa chakula cha misaada nikiwa na matumaini ya kupeleka nyumbani angalau mfuko mmoja wa unga. Lakini nilipofika hapo, sikujua la kufanya," aliiambia BBC Idhaa ya Kiarabu.
"Nisaidie kuwaokoa waliojeruhiwa, nisaidie kuondoe miili ya waliouawa, au nitafute mfuko wa unga? Haki ya Mungu, niko radhi kufa kupata mfuko mmoja wa unga ili watoto wangu wapate kula."

Chanzo cha picha, Getty Images
Utapiamlo, njaa na mauaji karibu na maeneo ya kutoa misaada yamezidi huko Gaza, kwani watu wanategemea msaada unaosambazwa na Wakfu wa Kibinadamu wa Gaza unaoungwa mkono na Marekani na Israel (GHF).
"Zaidi ya Wapalestina 1000 sasa wameuawa na jeshi la Israel wakijaribu kutafuta chakula huko Gaza tangu Wakfu wa Kibinadamu wa Gaza [GHF] kuanza shughuli zake tarehe 27 Mei," anasema Thameen Al-Kheetan, msemaji wa Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.
"Kufikia tarehe 21 Julai, tumerekodi vifo vya 1,054 vya watu waliouawa huko Gaza walipokuwa wakijaribu kupata chakula; 766 kati yao waliuawa karibu na maeneo ya GHF na 288 karibu na misafara ya misaada ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kibinadamu," aliiambia BBC.
Kuongezeka kwa vifo
GHF ilianza shughuli zake huko Gaza mwishoni mwa Mei, ikisambaza misaada michache kutoka maeneo kadhaa ya kusini na kati ya Gaza. Hii ni baada ya Israel kuzuia msaada wowote kuingia Gaza kwa takribani wiki 11.

Chanzo cha picha, Getty Images
Dk Mohammed Abu Salmiya, mkurugenzi wa hospitali ya Shifa katika Jiji la Gaza, anasema watoto 21 wamekufa kwa utapiamlo na njaa katika eneo hilo katika muda wa saa 72 zilizopita.
Watoto wapatao 900,000 huko Gaza wanakabiliwa na njaa, na 70,000 kati yao wako katika hali ya utapiamlo, aliambia BBC.
Wanakabiliwa na tishio la kufa, daktari anaonya, na wagonjwa wa kisukari na figo pia wako hatarini.
Msemaji wa wizara ya afya inayoongozwa na Hamas anasema watu 33 wakiwemo watoto 12 wamefariki katika muda wa saa 48 zilizopita.
Jumla ya vifo kutokana na utapiamlo vinafikia 101, ambapo 80 ni watoto, tangu kuanza kwa vita mwaka 2023, wanaongeza.
Wanakabiliwa na njaa
Wakaazi wote wa Gaza wanakabiliwa na nja, kulingana na Shirika la Chakula Duniani (WFP).

Chanzo cha picha, Getty Images
"Utapia mlo umekithiri huko kina mama na watoto 90,000 wakihitaji matibabu ya dharura. Takribana mtu mmoja kati ya watatu anakosa kula kwa siku kadhaa," WFP ilisema katika taarifa siku ya Jumapili, akiongeza kuwa:
"Msaada wa chakula ndiyo njia pekee itakayowasaidia wakaazi hawa - kwani gharama ya mfuko wa kilo moja ya unga imepanda hadi zaidi ya dola 100 katika masoko ya ndani."

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwezi Machi, Israel ilifunga vivuko vyote kuelekea Gaza, na kuzuia bidhaa zote, ikiwa ni pamoja na chakula, mafuta na madawa kuingia - na ilianza tena mashambulizi yake ya kijeshi wiki mbili baadaye, na kuhitimisha usitishaji mapigano wa miezi miwili na Hamas.
Vizuizi hivyo pia vimekata dawa muhimu, chanjo na vifaa vya matibabu vinavyohitajika na mfumo wa afya uliozidiwa wa Gaza.
Wizara ya mambo ya nje ya Israel ilisema Jumapili kwamba lori 4,400 za misaada ya kibinadamu zimeingia Gaza kutoka Israel tangu katikati ya Mei. Mizigo mingine 700 ya lori ilikuwa ikisubiri kuchukuliwa na Umoja wa Mataifa kutoka upande wa Gaza wa maeneo yake ya vivuko, iliongeza.
Israel inasisitiza kuwa hakuna uhaba wa misaada katika eneo hilo, na kuwashutumu Hamas kwa kuiba na kuhifadhi misaada ya kibinadamu ili kuwapa wapiganaji wake au kuuza ili kupata pesa.
Siku ya Jumatatu, nchi 28 zikiwemo Uingereza, Canada na Ufaransa, zilitoa wito wa kukomeshwa mara moja kwa vita huko Gaza, ambapo walisema mateso ya raia "yamefikia pabaya".
Taarifa ya pamoja ilisema mtindo wa utoaji wa misaada wa Israel ni hatari na kulaani kile ilichokiita '' misaada na mauaji ya kinyama ya raia" wanaotafuta chakula na maji.
Wizara ya mambo ya nje ya Israel ilipinga kauli ya nchi hizo, ikisema "haiendani na halisi na kutuma ujumbe usio sahihi kwa Hamas".
Lakini karibu kila siku kuna ripoti za Wapalestina kuuawa walipokuwa wakitafuta msaada GHF ya Israel inayoungwa mkono na Marekani kuanza kusambaza misaada mwishoni mwa mwezi Mei.
'Sisi ni masikini'

Chanzo cha picha, Getty Images
"Leo, kilo moja ya unga inagharimu shekeli 300 [dola 90] sokoni… na sisi ni maskini," Alaa Mohammed Bekhit anaiambia BBC News Arabic. "Hatuwezi kutoa hata mahitaji ya kimsingi."
Pia anazungumzia mashambulizi ya kila siku ambayo watu karibu na vituo vya misaada wanakabiliwa nayo.
"Kijana mmoja alikuwa ameketi karibu nami, na ghafla alipigwa risasi ya kichwa," anasema. "Hatujui risasi ilitoka wapi, tulikuwa hapo kuyanusuru maisha yetu kutokana na njaa, lakini tulijikut kwenye mafuriko ya damu, leo hii mtu yeyote aliyechukua mfuko wa unga alikutana na risasi."
Mwezi uliopita, jeshi la Israel liliiambia BBC kwamba lilikuwa likichunguza ripoti za raia "kujeruhiwa" wakati wakikaribia vituo vya kusambaza misaada huko Gaza vinavyoendeshwa na GHF.
Taarifa hiyo ilisema kwamba "ripoti za matukio ya madhara zilikuwa zikichunguzwa" na kwamba madai yoyote ya ukiukaji wa sheria au maagizo ya IDF [Majeshi ya Ulinzi ya Israeli] yatachunguzwa kwa kina, na hatua zaidi zitachukuliwa kama inavyohitajika.
Israel imeishutumu mamlaka ya Hamas ya Gaza kwa kutumia takwimu zilizokithiri kwa vifo vya Wapalestina lakini inakiri kuwa "ilifyatua risasi za onyo" ili kuondoa "tishio la mara moja".
Mashambulizi ya hivi punde
Wiki hii magari ya kivita ya Israel yaliingia Deir al-Balah katikati ya Gaza kwa mara ya kwanza, na kusababisha wimbi jipya la kuhama kwa raia.

Siku ya Jumapili, jeshi la Israel liliamuru kuhamishwa mara moja kwa vitalu sita vya miji katika eneo la kusini la Deir al-Balah, na kusababisha maelfu ya familia kukimbia makazi yao.
Raia wa neo hilo waliiambia BBC kwamba hawana pa kwenda.
Deir al-Balah ni mojawapo ya maeneo machache ya Gaza ambako Israel haijaendesha operesheni kubwa ya ardhini wakati wa vita vyake vya miezi 21 na Hamas.
Vyanzo vya habari vya Israel vimesema jeshi limekaribia wilaya ya Deir al-Balah kwa sababu linashuku wapiganaji wa Hamas huenda wanawashikilia mateka katika eneo hilo. Takriban mateka 20 kati ya 50 waliosalia mikononi mwa Hamas huko Gaza wanaaminika kuwa bado hai.
Umoja wa Mataifa ulisema amri ya kuwataka watu kuhama Deir al-Balah iliathiri maelfu ya Wapalestina ni "pigo kubwa" katika juhudi za kushughulikia hali ya kibinadamu.
Vitongoji hivyo vina kambi kadhaa za familia zilizohamishwa na vile vile maghala ya misaada, kliniki za afya na miundombinu muhimu ya maji.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema vituo vyake vilishambuliwa wakati wa operesheni ya Israel huko Deir al-Balah, na kwamba makazi ya wafanyikazi yalishambuliwa mara tatu, na kuwaacha wakaazi - wakiwemo watoto "wakiwa na kiwewe".
Shirika la Umoja wa Mataifa linasema kuwa wanajeshi wa Israel waliingia ndani ya majengo hayo, wakiwafunga pingu, kuwavua nguo na kuwahoji wafanyakazi wa kiume "papo hapo", wakiwazuilia watu wanne, watatu kati yao waliachiwa huru.
Jeshi la Israel halijazungumzia matukio hayo.
'Maafa yaliyosababishwa na binadamu'

Chanzo cha picha, Getty Images
Umoja wa Mataifa unasema wafanyakazi wake watasalia Gaza, kulinda miundombinu muhimu, ikiwa ni pamoja na kiwanda cha kuondoa chumvi licha ya kuanza kwa mashambulizi mapya.
"Kinachotokea Gaza ni janga la mwanadamu," anasema Juliette Touma, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina (Unrwa).
Akizungumza na BBC, Touma anasema hatua ya Israel ya kupiga marufuku Unrwa kufanya kazi huko Gaza imewazuia kusambaza lori 6,000 zilizosheheni misaada.
"Katika muda wa saa 24 zilizopita, wafanyakazi wetu walituambia kuwa baadhi ya wafanyakazi wenzetu wa Unrwa walizirai wakiwa kazini kutokana na njaa na njaa," anasema akionyesha tozo ya wafanyakazi wa misaada.
"Njaa iliyosababishwa na uamuzi wa makusudi wa kisiasa wa kuwaadhibu kwa pamoja watu wa Gaza - kati yao watoto milioni 1," anasema.
Mnamo Novemba 2024, jopo la majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita waliamua kwamba kulikuwa na "sababu za kuridhisha" kuamini kwamba waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wake wa zamani wa ulinzi Yoav Gallant walibeba "wajibu wa jinai" kwa kutumia "njaa kama njia ya vita".
Lakini Israel inakanusha kuwa imetumia njaa kama chombo cha vita, huku Netanyahu akiyaita madai hayo "mashtaka ya uwongo na ya kipuuzi".
Wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas inasema idadi ya watu waliouawa Gaza tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi yake Oktoba 2023 sasa imezidi 59,000.
Mashambulizi hayo yalianza kulipiza kisasi mashambulizi yaliyoongozwa na Hamas ambayo yaliua takriban watu 1,200 na kushuhudia 251 wakichukuliwa mateka.
Hamas imeteuliwa kama shirika la kigaidi na nchi zikiwemo Marekani, Uingereza na Israel.
Umoja wa Mataifa unasema wafanyakazi wake watasalia Gaza, kulinda miundombinu muhimu, ikiwa ni pamoja na kiwanda cha kuondoa chumvi licha ya kuanza kwa mashambulizi mapya.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi








