Simulizi ya ajuza anayetuhumiwa kujaribu kumuua Netanyahu

Chanzo cha picha, Reuters
Wiki mbili zilizopita, mamlaka ya usalama ya Israel ilimkamata mwanamke kutoka Israel ya kati ambaye alijaribu kumuua Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, kulingana na Shirika la Utangazaji la Israel.
Vyombo vya habari vya Israel viliripoti kwamba Huduma ya Usalama wa Ndani (Shabak) ilimkamata mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 70, ambaye alifanyiwa uchunguzi wa polisi.
Kulingana na habari, mshukiwa anahusika katika harakati za maandamano na hapo awali alikuwa ameelezea kwa wengine nia yake ya kumuua Netanyahu kwa kutumia kilipuzi.
Pia aliripotiwa kuwasiliana na wanaharakati wengine ili kupata vifaa vya kupigana na kujadili maelezo ya mipango ya usalama inayomzunguka Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
Mwanamke huyo aliachiliwa lakini kwa kuwekewa vikwazo, ikiwa ni pamoja na kukaa mbali na taasisi za serikali na ofisi ya waziri mkuu, kulingana na ripoti ya shirika la utangazaji.
Mwanamke huyo ambaye jina na anwani yake vilihifadhiwa, amepangwa kufikishwa mahakamani siku ya Alhamisi kwa tuhuma za "kula njama ya kutenda uhalifu na njama ya kutekeleza kitendo cha kigaidi," kulingana na ripoti hiyo.
Septemba iliyopita, polisi wa Israel walitangaza kumkamata mwanamume mmoja wa Israel kwa tuhuma kwamba ujasusi wa Iran ulimtumia kupanga njama ya mauaji ya maafisa mashuhuri akiwemo Netanyahu.
Maandamano mjini Tel Aviv kudai kukomeshwa kwa "njaa" huko Gaza
Wakati huo huo, maelfu ya waandamanaji waliandamana hadi eneo la Kirya la Tel Aviv, nyumbani kwa makao makuu ya jeshi la Israeli, kutaka kumalizika kwa vita huko Gaza na kuangazia ripoti za kuongezeka kwa njaa katika eneo hilo, kulingana na The Times of Israel.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Waandamanaji walibeba magunia ya unga na picha za watoto kutoka Gaza walioripotiwa kufariki kwa njaa.
"Tunashikilia picha za watoto wa Kipalestina huko Gaza ambao walikufa kwa njaa," mratibu wa maandamano Alon Lee-Green aliambia gazeti hilo. "Walikufa wakati Israeli ilizuia msaada kutoka kwa Gaza, na tuko hapa kudai kukomesha njaa.
Kinyume chake, Israel inakanusha ripoti za "njaa" huko Gaza, ikisema "inaruhusu misaada ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na chakula, kuingia."
Hakuna mtu aliyekamatwa kati ya waandamanaji, kulingana na Times of Israel.
Haya yanajiri huku Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Tedros Adhanom Ghebreyesus akionya kuhusu "njaa" inayoenea huko Gaza, kwani shehena za chakula zinazoingia katika eneo lililozingirwa na lililoharibiwa "ni kidogo sana kuliko kile kinachohitajika kwa maisha ya watu."
"Sehemu kubwa ya wakazi wa Gaza wanakabiliwa na njaa," Ghebreyesus aliongeza. "Sijui nini kingine cha kuiita zaidi ya njaa kubwa, na inasababishwa na mwanadamu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Israel imesema "haihusiki" na uhaba wa chakula huko Gaza, ikishutumu Hamas kwa "kutengeneza mgogoro" katika eneo lililozingirwa.
"Hakuna njaa katika Gaza iliyosababishwa na Israel, lakini uhaba unaosababishwa na Hamas," msemaji wa serikali David Mincer aliwaambia waandishi wa habari, akiwashutumu wanachama wa vuguvugu hilo kwa "kuzuia usambazaji wa chakula na uporaji wa misaada."
Matamshi hayo yametolewa siku ambayo zaidi ya mashirika 100 yasiyo ya kiserikali yalionya juu ya "njaa kubwa" katika Ukanda wa Gaza na kuitaka Israel kuruhusu msaada katika Ukanda huo.
Wizara ya Afya huko Gaza iliripoti kwamba hospitali katika Ukanda huo zilirekodi vifo vipya 10 kutokana na "njaa na utapiamlo" katika saa 24 zilizopita, na kufanya jumla ya vifo kutokana na njaa kufikia 111, kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza.
Israel inakabiliwa na ongezeko la shinikizo la kimataifa kuhusu hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, ambayo imeharibiwa na vita vinavyoendelea kwa zaidi ya miezi 21.
Chini ya mzingiro unaoendelea na mashambulizi ya mara kwa mara, maelfu ya familia zinakabiliwa na karibu kunyimwa mahitaji yao ya kimsingi, ikiwa ni pamoja na chakula, maji, na dawa, huku vifo vinavyotokana na njaa na utapiamlo, hasa miongoni mwa watoto, vikiripotiwa kila siku.
Kwa upande wao, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaonya kwamba vituo vya kusambaza misaada vinavyoungwa mkono na Marekani na Israel vimegeuka kuwa kile wanachokitaja kuwa "mitego ya kifo cha kusikitisha," wakati ambapo shutuma dhidi ya Israel ya kutumia njaa kama silaha ya vita zinaongezeka.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












