Nani atachukua jukumu la usalama huko Gaza baada ya vita?

gg

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Salma Khattab
    • Nafasi, Mwandishi wa BBC Arabic
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Wakati mazungumzo ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza yanaendelea, na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akitangaza azma ya kuudhibiti ukanda huo, pendekezo la kuundwa kwa kikosi cha pamoja cha milki za Kiarabu kwa ajili ya kuusimamia na kudumisha usalama baada ya vita limeibuka upya.

Kwa mujibu wa mpango wa Netanyahu ambao umekumbana na upinzani mkubwa wa ndani na nje ya Israel wa vikosi vya Israel vitadhibiti Ukanda mzima wa Gaza, kuwaondoa kikamilifu wanamgambo wa Hamas, na baadaye kuukabidhi usimamizi kwa vikosi vya mataifa ya Kiarabu.

Katika kikao chake cha hivi karibuni, Baraza la Usalama la Israel liliidhinisha mpango wa kuikali mji wa Gaza, lakini halikutoa maelezo ya kina kuhusu namna ya kudhibiti ukanda mzima.

Mkuu wa Majeshi wa Israel alitoa idhini ya awali kwa kile alichokiita "wazo kuu" la kutwaa udhibiti wa jiji la Gaza.

Soma pia:

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ma'an la Palestina, vipengele vya makubaliano yanayojadiliwa kwa msaada wa Marekani vinajumuisha:

  • kusitisha mapigano,
  • kuondoka kwa jeshi la Israel kutoka Gaza,
  • kuingia kwa vikosi vya Kiarabu chini ya usimamizi wa Marekani,
  • kuteuliwa kwa Gavana wa Kipalestina kusimamia masuala ya kiraia na usalama,

na uratibu wa mchakato wa ujenzi upya wa Gaza.

Hata hivyo Palestina imepinga mpango wa kutenganishwa kwa Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ama West Bank ikilitaja jambo hilo kuwa sehemu ya "mradi wa Israel."

Serikali ya Palestina imesisitiza kuwa Gaza ni sehemu isiyotenganishwa na Dola ya Palestina, na kwamba usimamizi wake ni jukumu la Mamlaka ya Palestina pekee.

Pia unaweza kusoma:

Hadi sasa, haijafahamika iwapo pande mbili hasimu Israel na Hamas zitaridhia kuundwa kwa kikosi hicho cha pamoja cha Kiarabu.

Swali kubwa linabaki: je, pendekezo hilo linatekelezeka katika hali halisi ya kivita?

Awali, wazo hilo liliibuliwa na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Galant, kupitia mpango wake wa "Siku Baada ya Vita", uliopendekeza kuundwa kwa kikosi cha kimataifa chini ya uongozi wa Marekani na ushiriki wa mataifa ya Kiarabu.

Hata hivyo, wazo hilo lilikataliwa na mataifa kadhaa ya Kiarabu, hususan Jordan, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje Ayman Safadi alisema:

"Hatutaruhusu Wapalestina watuone kama maadui wao. Pendekezo la kutuma majeshi ya Kiarabu Gaza si la kweli wala halitekelezeki."

Mwezi Aprili, Misri na Jordan walifikia makubaliano ya mpango wa ujenzi upya Gaza, ukiambatana na mafunzo kwa maafisa wa polisi wa Palestina, kama maandalizi ya kurejeshwa kwao baada ya kumalizika kwa mapigano.

Kizungumkuti cha usalama

Hali katika Ukanda wa Gaza ni "jinamizi ya usalama" kwa nguvu yoyote inayoingilia kati.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Hali katika Ukanda wa Gaza ni "jinamizi ya usalama" kwa nguvu yoyote inayoingilia kati.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Alistair Burt, aliyewahi kuwa Waziri wa Mashariki ya Kati katika Serikali ya Uingereza, aliuelezea mpango wa kuunda kikosi cha Kiarabu Gaza kuwa "suluhisho la vitendo zaidi," lakini akatahadharisha kuwa utekelezaji wake ni changamoto.

Akihojiwa na BBC, Burt alisema:

"Ni lazima kuwe na makubaliano ya moja kwa moja na Hamas. Hakuna taifa la Kiarabu litalituma majeshi yake Gaza ikiwa vita bado vinaendelea."

"Pia, ni lazima kuwe na hakikisho kwamba vikosi vya Kiarabu havitalengwa na mashambulizi kutoka kwa wapiganaji wa Hamas waliobaki."

Aliongeza kuwa changamoto kubwa ya kisiasa na kijeshi pia ipo upande wa Israel:

"Ni nani atakayehakikisha usalama wa Israel? Na ni kwa namna gani wataepusha kurudiwa kwa matukio kama ya Oktoba 7?"

Kwa mujibu wa Burt, Gaza kwa sasa ni "jinamizi la kiusalama" kwa chombo chochote cha kusimamia. Ukanda huo, amesema, umejaa magenge, silaha, na uhalifu.

"Kazi ya kwanza itakuwa ni kuzuia uporaji, kuondoa silaha mikononi mwa raia, na kurejesha hali ya kawaida. Hili linaweza kuchukua muongo kutekelezwa ipasavyo."

Kuwapokonya Hamas silaha ni muhimu

Brigedia Jenerali Samir Ragheb, Mkuu wa Taasisi ya Kiarabu ya Masuala ya Kimkakati, aliiambia BBC kuwa hadi sasa hakuna taarifa rasmi kutoka nchi yoyote ya Kiarabu inayoonesha utayari wa kushiriki kwenye kikosi hicho, na kwamba huu ni mpango wa upande mmoja kutoka kwa Netanyahu.

Kulingana naye "Hamas haitakubali kikosi hicho isipokuwa kama kutakuwa na makubaliano mapana yatakayohakikisha kuondoka kwa Israel Gaza. Kukubali kikosi cha kigeni kunamaanisha Hamas ijisalimishe na isiwe na silaha."

Akaongeza kuwa, kukubali hilo pia ni kumaanisha Hamas haitakuwa tena sehemu ya usalama wa Gaza, bali nafasi hiyo itachukuliwa na vikosi vya mpito hadi serikali ya Kipalestina itakapokuwa tayari kushika usimamizi.

Ragheb alibainisha kuwa kufikia suluhu ya kina kunahitaji pande zote mbili Hamas na Israel kukubaliana kwenye masuala yanayowatofautisha:

  • Hamas inataka misaada iingizwe Gaza,
  • Jeshi la Israel liondoke,
  • Na operesheni za kijeshi zisitishwe ili kuanza ujenzi.

Israel, kwa upande mwingine, inataka:

1. Hamas ivunje silaha

2. Viongozi wake waondoke Gaza

3. Na serikali mpya isiyohusiana na Hamas wala Fatah iundwe.

Kulingana na Ragheb, ambaye anaongeza, "Kuhusu mahali pa kuingilia misaada na kurejeshwa kwa mateka, halitakuwa suala la mzozo ndani ya mfumo wa suluhu ya kina."

Mazungumzo ya kusitisha vita Cairo

Makubaliano ya vikosi vya Waarabu kuingia Ukanda wa Gaza inamaanisha kuwapokonya silaha Hamas.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Makubaliano ya vikosi vya Waarabu kuingia Ukanda wa Gaza inamaanisha kuwapokonya silaha Hamas.

Mapema wiki hii, ujumbe wa Hamas uliwasili Cairo kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano, kwa mujibu wa vyombo vya habari vinavyoendeshwa na Hamas Filastin.

Kundi hilo lilifanya mikutano na maafisa wa Misri kujadili utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Misri imekuwa mmoja wa wapatanishi wakuu katika mazungumzo kati ya Israel na Hamas.

Hapo awali, Hamas ilitoa taarifa ikisema inazishukuru Jordan na Misri kwa kukataa kuhama kwa Wapalestina.

Hii ilikuwa ni kujibu mpango wa Trump wa kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza na kuwapeleka katika mataifa mengine.

Wakati huo huo, Mustafa Barghouti, katibu mkuu wa mkakati wa kitaifa wa Palestina amesema kwamba matakwa ya Israel ya kutaka mateka wote waliozuiliwa na Hamas waachiliwe huru kufikia Jumamosi haiwezekani.

Huku mazungumzo ya amani yakianza kutokota shughuli za kawaida zimerejea Khan Younis eneo ambalo limekuwa likikumbwa na vita vya mara kwa mara.

Licha ya mchakato wa kusitisha mapigano Gaza kuendelea kutekelezwa, Israel bado inalenga mji wa Hezbollah ulioko Lebanon.

Hii ni baada ya Israel kuomba muda kabla ya kuondoa vikosi vyake kusini mwa Lebanon unaotarajiwa kukamilika Jumanne ijayo.

Israel sasa inataka wanajeshi wake wabaki katika sehemu tano nchini humo kwa siku zingine kumi, chanzo cha kidiplomasia ya Magharibi chaiambia BBC.

Serikali ya Lebanon inaendelea kujitahidi kurejesha uhuru wa nchi yao na mamlaka hiyo imepinga vikali kuchelewa kuondoka kwa wanajeshi wa Israel.

Kwa upande wa Israel imeapa kuendelea kushambulia kikosi kilicho na silaha kinachoungwa mkono na Iran wakidai ni njia ya kukisambaratisha kisiendeleze na mapigano.

Katika taarifa wiki hii, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Misri, Badr Abdel Aty, alisema kuwa Misri haitapinga kutumwa kwa vikosi vya kimataifa katika Ukanda wa Gaza ili kuwezesha Mamlaka ya Palestina "kujumuisha serikali" na kuhakikisha usalama wa pande zote.

Waziri wa Misri pia alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa kigeni nchini Misri Jumanne jioni kwamba kundi la watu 15 wasio na makundi ya Wapalestina wako tayari kusimamia Ukanda wa Gaza kwa kipindi cha mpito cha miezi sita baada ya kumalizika kwa vita, na baada ya hapo Mamlaka ya Ndani ya Palestina itachukua jukumu la kusimamia Ukanda huo.

Alieleza kuwa "kilichopo mezani kwa sasa ni ufufuaji wa mpango wa Witkoff, ambao umejikita katika usitishaji vita wa wiki sita kwa ajili ya kuachiliwa na kubadilishana idadi fulani ya mateka na wafungwa, na kuingia bila vikwazo kwa msaada katika Ukanda wa Gaza."

Changamoto kubwa

Brigedia Jenerali Khaled Okasha, Mkurugenzi wa Kituo cha Kimisri cha Tafakuri na Masuala ya Kimkakati, alisema wazo la kuunda kikosi cha Kiarabu halijajadiliwa rasmi katika mazungumzo ya sasa.

"Ripoti za vyombo vya habari kuhusu kuundwa kwa kikosi hicho ni mbali na hali halisi. Mazungumzo ya sasa yanajikita kwenye pendekezo la Mjumbe Maalum wa Marekani, Steve Witkoff, la kusitisha vita na kuachiliwa kwa mateka wote."

Alisisitiza kuwa suala hilo halihusiki na mazungumzo ya sasa, bali linahitaji majadiliano ya kina baada ya hatua za awali kukamilika.

Kulingana naye, "Misri na mataifa ya Kiarabu wamesema wazi kuwa hakuna nafasi kwa Hamas baada ya vita. Lakini Hamas nayo imetangaza kuwa haitahusika na usimamizi wa Gaza endapo Israel itajiondoa. Hizi ndizo misimamo mikuu inayojadiliwa" aliambia BBC.

Okasha alihitimisha kwa kusema kuwa:

"Pendekezo la kupeleka vikosi vya usaidizi linaweza kujadiliwa baadaye, lakini kwa sasa, hakuna taifa la Kiarabu wala Misri lililo tayari kuwa sehemu ya kikosi cha 'kukalia kwa mabavu' badala ya Israel."

Misri ilisema haitapinga kutumwa kwa vikosi vya kimataifa katika Ukanda wa Gaza

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Misri ilisema haitapinga kutumwa kwa vikosi vya kimataifa katika Ukanda wa Gaza

Mpango wa mjumbe wa Marekani Steve Witkoff wa kumaliza vita huko Gaza unajumuisha usitishaji vita wa siku 60 na kuachiliwa kwa wafungwa tisa walio hai na miili 18 ya mateka katika awamu mbili, kwa muda wa wiki moja, ili kubadilishana na Israel kujiondoa katika mhimili wa Netzarim.

Katika kipindi hiki, mazungumzo yanaendelea ili kumaliza vita.

Iwapo hakuna makubaliano yatakayofikiwa mwishoni mwa mazungumzo hayo, Israel inaweza kurejea kwenye mapigano au kuendelea na mazungumzo badala ya kuachiliwa kwa mateka zaidi.

Duru ya awali ya mazungumzo nchini Qatar ilikwama wiki tatu zilizopita, huku Witkoff akiishutumu Hamas kwa "kuzuia mazungumzo na kutotaka kusitishwa kwa mapigano."

Hamas baadaye ilikataa shutuma hizo, ikisema ilijibu vyema maoni yote iliyopokea, na kueleza kushangazwa na taarifa za Witkoff.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari Jumanne jioni kwamba hatakubali makubaliano yoyote ya sehemu ya kurejea kwa mateka.

Alisema kuwa "anaelekea kwenye makubaliano ya kina ya kuwarudisha mateka wote, chini ya masharti yaliyowekwa na Israel," akibainisha kuwa aliamuru ukaliaji wa mji wa Gaza upunguzwe.

Huku kukiwa na taarifa zinazokinzana za vyombo vya habari na duru za mazungumzo na mazungumzo, takriban Wapalestina milioni mbili katika Ukanda wa Gaza wanaugua kutokana na uzito wa vita vya umwagaji damu.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya inayoongozwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza, vita hivyo vimesababisha vifo vya watu 60,000 katika muda wa chini ya miaka miwili, pamoja na njaa na hali ya kibinadamu inayoelezwa na mashirika ya kimataifa na Umoja wa Mataifa kuwa "zaidi ya janga."

Mada zinazohusiana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid