Ni upi mustakabali wa Hamas huko Gaza?

Chanzo cha picha, EPA-EFE / REX / Shutterstock
- Author, Hanan Abdel Razek
- Nafasi, BBC Arabic correspondent
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema anajiandaa "kuchukua udhibiti kamili wa Ukanda wa Gaza na kuiondoa Hamas." Hata hivyo, katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Marekani Fox News, alionyesha kuwa Israel haina nia ya "kubaki katika Ukanda huo kama mamlaka itakayotawala."
Kauli za Netanyahu zinaongeza shinikizo zaidi kwa Hamas, ambayo tayari inakabiliwa na madai ya kikanda na kimataifa ya kujihami. Hamas imekataa shinikizo hilo, ikisema kuwa haitachukua hatua hiyo hadi taifa la Palestina litakapoundwa na uvamizi wa Israel katika maeneo ya Palestina utakapoisha.
Hamas ilitangaza msimamo wake kuhusu jambo hili kupitia taarifa iliyotolewa siku chache zilizopita, katikati ya shinikizo linaloongezeka la kulazimisha iache silaha zake zote na kufungua njia ya mchakato wa kidiplomasia wa mazungumzo ya amani unaoelekea katika utekelezaji wa suluhisho la mataifa mawili.
Katika mkutano wa kimataifa uliofanyika Julai iliyopita katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, uliofadhiliwa na Saudi Arabia na Ufaransa, mataifa 17 pamoja na Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya nchi za kiarabu, yalitoa tamko la pamoja kuhusu utatuzi wa amani wa suala la Palestina na utekelezaji wa suluhisho la mataifa mawili.
Tamko la New York, lenye vifungu 42, liliitaka Hamas kuachia udhibiti wa ukanda wa Gaza na kukabidhi silaha zake kwa mamlaka ya Palestina.
Miongoni mwa nchi zilizotia saini tamko hili zilikuwa Misri na Qatar, ambazo mara nyingi hufanya upatanishi katika mazungumzo kuhusu Gaza. Hata hivyo, Israel na Marekani hazikusaini tamko la New York na hazikushiriki kabisa katika mkutano huo.
Hamas itaendelea kupigana

Chanzo cha picha, EPA
Katika mahojiano ya televisheni na Al Jazeera Mubasher, yaliyotangazwa kutoka Doha, kiongozi wa Hamas Ghazi Hamad alisema kuwa harakati hiyo haitaweka silaha chini," na kwamba "silaha zinamaanisha suala la Palestina." Alisisitiza kuwa Hamas iko tayari kuendelea kupigana hadi taifa la Palestina litakapoundwa.

Chanzo cha picha, Amr Alfiky / Reuters
Hussam Al-Dajani, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Al-Ummah jijini Gaza, anaamini kuwa vyombo vya habari vinaangazia zaidi Kifungu cha 11 cha tamko la New York, ambacho kinasema kwamba "utawala bora, utekelezaji wa sheria, na usalama katika maeneo yote ya Palestina utakuwa jukumu pekee la Mamlaka ya Palestina."
Kifungu hicho pia kinataka "Hamas kuachia udhibiti wa ukanda wa Gaza na kukabidhi silaha zake kwa Mamlaka ya Palestina."
Al-Dajani anaeleza kuwa kuna vifungu vingine 41 katika tamko hilo, baadhi vikitoa wito wa kuanzishwa kwa taifa la Palestina na kuishi kwa amani na Israel. Anaiambia BBC: "Iwapo vifungu vingine vya tamko la New York vitatekelezwa, kifungu cha 11 kitakuwa jambo lililo wazi."
Taifa la Palestina kwanza

Chanzo cha picha, Haitham Imad / EPA-EFE / REX / Shutterstock
Hamas imetajwa kuwa shirika la kigaidi na Marekani, Uingereza, na mataifa mengine ya Magharibi. Harakati hiyo imetangaza mara kadhaa kuwa itakabidhi silaha zake kwa Mamlaka ya Palestina mara baada ya taifa la Palestina kuanzishwa.
Afisa mmoja wa usalama wa Hamas aliwahi kuambia BBC kuwa harakati hiyo imepoteza sehemu kubwa ya udhibiti wake wa Gaza.
Hamas bado ina muundo wa kiutawala ndani ya Ukanda huo. Kitengo chake kipya cha usalama, kinachojulikana kama "Arrow," kinafanya kazi kwa lengo la kudumisha utulivu wa umma na kuzuia wizi wa misaada inayoingia Gaza.
Lakini miezi 22 baada ya harakati hiyo kufanya mashambulizi dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023, na hatua ya kijeshi iliyofuata ya Israel, Hamas na jeshi lake la kijeshi linaonekana kuwa dhaifu zaidi.

Chanzo cha picha, Mohammed Saber / EPA-EFE / REX / Shutterstock
Kwa muktadha huu, Profesa Yossi Mekelberg, mshauri mwandamizi kutoka Chatham House, taasisi ya utafiti yenye makao yake London, Uingereza anasema Hamas "ilikosea kukadiria" matokeo ya mashambulizi ya Oktoba 7.
Kwa upande mwingine, vyanzo vya ndani Gaza vinaripoti kuwa Hamas bado inamiliki silaha, lakini akiba yake ya risasi inakaribia kuisha.
Vyanzo vinaongeza kuwa wapiganaji wa harakati hiyo wanatumia tena mabaki ya mabomu yaliyosalia baada ya mashambulizi ya Israel ambayo mengi hayakulipuka ili kupata vilipuzi vinavyowawezesha kutengeneza mabomu ya kienyeji kwa mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Israel.
Israel inazuia waandishi wa habari wa kimataifa kuingia Gaza, hivyo hatuwezi kuthibitisha hili kwa uhuru.
Wakati huohuo, Wapalestina ndani ya Gaza wanaonyesha hasira dhidi ya Hamas, huku Amnesty International ikilaani kampeni ya harakati hiyo ya "ukandamizaji na vitisho" dhidi ya waandamanaji waliopinga Hamas mwezi Mei.
Msimamo wa nchi za Kiarabu

Chanzo cha picha, EPA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, yenye wanachama 22 ikiwemo mataifa yanayoaminika kuwa wasaidizi wa Hamas kama Qatar, ilisaini tamko la New York linaloihimiza harakati hiyo ya kukabidhi silaha.
Profesa Mekelberg anaamini kuwa Israel na Marekani zinaendeleza misimamo yao ya kawaida kuhusu Hamas. Hata hivyo, anasema msimamo wa mataifa ya Kiarabu umebadilika. Anaona kuwa shinikizo linaloongezeka kutoka mataifa ya Kiarabu na kikanda linaweza kuiacha Hamas "ikiwa imezingirwa kabisa" na kuzidi kuwa dhaifu.
Kikanda, harakati hiyo ya silaha imebaki na idadi ndogo ya washirika. Baada ya vita vya siku 12 kati ya Israel na Iran mnamo Julai iliyopita, uwezo wa Tehran kuendeleza msaada kwa Hamas umepungua sana.
Hezbollah, moja ya nguvu kubwa za kikanda washirika wa Iran, pia imepungua nguvu kutokana na mashambulizi ya Israel na kuuawa kwa viongozi wake wakati wa mapigano makali zaidi ya mwaka mmoja. Hezbollah tayari inakabiliwa na madai kutoka serikali ya Lebanon ya kujihami.
Mustakabali wa Hamas

Chanzo cha picha, Amir Cohen / Reuters
Kutabiri mustakabali wa Hamas ni jambo gumu sana. Harakati hiyo inasema itakabidhi silaha zake iwapo taifa la Palestina litaanzishwa, jambo ambalo linaonekana halina uwezekano hadi serikali ya Israel ibadilishe msimamo wake wa sasa kuhusu suala hilo.
Lakini wachambuzi wanaamini kuwa kujihami ama kukabidhi silaha kwa Hamas, hata kama kutatokea, hakumaanishi kuwa harakati hiyo itatoweka.
Yossi Mekelberg anatabiri kuwa Hamas inaweza kuwa na nafasi ya "kujijenga upya siku zijazo" na kubaki kinara katika siasa za Palestina, ndani na nje ya maeneo ya Palestina.
Lakini yote haya yatategemea msimamo wa Israel kuhusu uwezekano wa taifa la Palestina, pamoja na umaarufu wa Hamas, ikizingatiwa hali mbaya inayowakabili Wagaza baada ya mashambulizi ya Oktoba 7 na operesheni ya kijeshi ya Israel iliyofuata.












