Je, Uingereza inaiuzia Israel silaha?

.

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock

Muda wa kusoma: Dakika 6

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Lammy alilaani mwenendo wa Israel huko Gaza, akisema kuwa Uingereza "huenda ikatathmini msimamo wake wiki zijazo" ikiwa serikali ya Israel haitabadilisha mtazamo wake wa kuendesha vita katika Ukanda huo.

Lammy alielezea hasira yake kwa "kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kumaliza vita hivi," na akasema "alichukizwa" na mauaji ya Wapalestina katika vituo vya misaada na majeshi ya Israeli katika siku za hivi karibuni.

Tangu Israel ianze kampeni yake ya kijeshi huko Gaza kufuatia mashambulizi ya Oktoba 7, tahadhari ya umma imezingatia sana suala la msaada wa Uingereza. Silaha nyingi zilizotumiwa katika mashambulizi ya jeshi la Israel kwenye Ukanda huo zilitengenezwa au kuuzwa na nchi za Magharibi.

Hata hivyo, habari kuhusu kiwango cha msaada wa kijeshi wa Uingereza kwa Israeli mara nyingi hubakia kuwa haijulikani au siri, na baadhi ya wajumbe wa Bunge wametaka uchunguzi wa umma kuhusu kiwango cha msaada huo.

Pia unaweza kusoma

Je, Uingereza inatoa silaha kwa Israel?

Uingereza sio mojawapo ya wauzaji wakubwa wa silaha wa Israel, lakini Marekani ndiyo nchi kubwa zaidi, ikiisaidia Israel kuendeleza moja ya jeshi lilioendelea zaidi duniani, ikifuatiwa na Ujerumani na Italia.

Tangu 2015, Uingereza imeidhinisha leseni za kuuza silaha kwa Israeli zenye thamani ya zaidi ya pauni milioni 500 ($ 676.4 milioni), na kufikia kilele mwaka wa 2018, kulingana na kikundi cha kampeni dhidi ya Biashara ya Silaha (CAAT).

Hata hivyo, umakini mkubwa zaidi umeelekezwa katika uungaji mkono wa Uingereza kwa Israel kuhusiana na sehemu zilizotengenezwa na Uingereza za ndege za F-35, ambazo Israel imezitumia sana kuishambulia Gaza.

Uingereza hutoa kati ya asilimia 13 na 15 ya vifaa vinavyotumika katika ujenzi wa ndege hiyo, ikiwa ni pamoja na viti vya kutolea kombora, fusela ya nyuma, mifumo inayotumika ya kukatiza, leza zinazolenga na nyaya za kurushia silaha. Hatahivyo, toleo la ndege la Israel halijumuishi baadhi ya sehemu hizi.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baada ya Chama cha Labour kuingia madarakani mwaka jana, kilisimamisha leseni 30 kati ya 350 za kuuza nje silaha, na kuathiri vifaa kama vile vipuri vya ndege za kivita, helikopta na ndege zisizo na rubani.

Kampuni yoyote ya Uingereza inayotaka kuuza silaha nje ya nchi lazima iombe leseni, na serikali ilisema wakati huo kwamba kulikuwa na "hatari ya wazi" kwamba

vifaa vinaweza kutumika kufanya ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.

Lakini muhimu zaidi, vipuri vya F-35 havikuzuiwa na marufuku ya kuuza nje.

Serikali ilidai kwamba haiwezi kuzuia Israel kupata vifaa hivi kwa sababu vilikuwa vinatumwa kwenye vituo vya utengenezaji nje ya nchi kama sehemu ya mpango wa kimataifa-sio moja kwa moja kwa Israel.

Anna Stavrianakis, mtaalam wa mauzo ya silaha wa Uingereza, alielezea uamuzi wa serikali wa kuruhusu msamaha huu kama "mwanya mkubwa wa kisheria."

"Sehemu nyingi za F-35 zinazotengenezwa na Uingereza huenda Marekani, ambako zinaunganishwa katika ndege zinazopelekwa Israel," aliiambia BBC Fact Check, akibainisha kuwa marufuku ya kuuza nje ya Uingereza ilikuwa na ufanisi mdogo kutokana na "msisitizo wa White House wa kuunga mkono Israeli."

Uingereza pia ilishiriki katika utengenezaji wa ndege isiyo na rubani ya Hermes, ambayo imekuwa ikitumika sana huko Gaza.

Wakati toleo la Uingereza la ndege hiyo isiyo na rubani, inayojulikana kama Watchkeeper 450, haina silaha, ndege isiyo na rubani ya Hermes iliyotengenezwa na Israel inaweza kuwa na makombora ya Spike na iliripotiwa kutumika katika shambulio lililoua wafanyakazi saba wa kutoa misaada katika Jiko Kuu la Dunia{ Wolrd Central Kitchen} mwaka jana.

Ni vigumu kubainisha ni nini Uingereza bado inasafirisha kwa Israeli chini ya leseni halali. Waziri wa mambo ya nje David Lammy alisema mwaka jana kuwa vikwazo hivyo si "vikwazo vya kila kitu au silaha," akisisitiza haja ya Israel kuweza kujilinda dhidi ya shambulio lolote.

Kulingana na Wizara ya Biashara, leseni 161 kati ya zilizopo ni za bidhaa za kijeshi.

Ripoti iliyotolewa na Bunge la Uingereza ilisema kwamba leseni zilizosalia zinaweza kujumuisha "vitu kama vile ndege za mafunzo na vifaa vya majini, na vitu viwili vya matumizi ya raia katika uwanja wa mawasiliano na vifaa vya data.

Je, Uingereza inashirikiana kijasusi na Israel?

Kiwango cha ushirikiano wa kijasusi wa Uingereza na Israel tangu mashambulizi ya Oktoba 7 bado hakijulikani wazi.

Serikali ina "ushirikiano wa ulinzi" wa muda mrefu na Israel, ambao maafisa wa ulinzi wanasema unajumuisha "elimu ya pamoja, mafunzo, na ukuzaji uwezo."

Jeshi la Wanahewa la Royal limefanya mamia ya safari za ndege za upelelezi juu ya Gaza tangu Desemba 2023, ikiripotiwa kutumia ndege za kijasusi za Shadow R1 zilizopo katika kambi yake huko Akrotiri, nchi jirani ya Kupro.

Katika mahojiano siku ya Jumatatu, Lammy alisisitiza kuwa safari za ndege za RAF juu ya Gaza hazikusababisha mabadilishano yoyote ya ujasusi wa kijeshi na IDF.

Waziri wa Mambo ya Nje alisema: "Itakuwa makosa kabisa kwa serikali ya Uingereza kusaidia kuendesha vita hivi huko Gaza. Hatufanyi hivyo.

Mwaka wa 2023, Uingereza ilikubali kwamba baadhi ya ndege zake "zisizo na silaha" zinazoruka juu ya Ukanda wa Gaza zilikuwa zikisaidia katika kutafuta mateka wa Israel waliotekwa nyara na Hamas wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7.

Takriban watu 50 bado wanazuiliwa na Hamas, na takriban 20 kati yao wanaaminika kuwa hai.

Waziri wa Vikosi vya Wanajeshi wa Uingereza Luke Pollard alithibitisha msimamo huu mnamo Aprili 2025, akiambia bunge kwamba safari za ndege za Uingereza juu ya Gaza zilifanyika "kwa madhumuni pekee ya kuwapata mateka."

Wizara ya Ulinzi ilikataa kutoa maoni yake kuhusu iwapo ndege za Israel zinaweza kufikia kituo cha RAF huko Cyprus.

Hata hivyo, tovuti ya BBC Fact Check pia ilifichua kuwepo kwa ndege za Jeshi la Wanahewa la Israel katika anga ya Uingereza katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kufuatia ripoti za tovuti huru ya DropSight.

Ndege nyingi za RIM za kuongeza mafuta zimeonekana kwenye tovuti ya kufuatilia safari za ndege juu ya vituo vya RAF huko Brize Norton na Fairford.

Je, majeshi ya Israel yanatoa mafunzo nchini Uingereza?

.

Chanzo cha picha, Reuters

Uingereza mara nyingi hupanga kozi za mafunzo kwa wanajeshi wa mataifa washirika, ambayo mengi yanalenga uongozi, vifaa na uendeshaji wa mtandao. Kwa mfano, maelfu ya wanajeshi wa Ukraine wamewasili Uingereza tangu Urusi ilipoanzisha vita vyake vikubwa dhidi ya Kyiv mwaka 2022 kwa ajili ya kupata mafunzo ya kimsingi.

Lord Cocker, waziri wa nchi katika Wizara ya Ulinzi ya Uingereza, alisema mwezi Aprili kwamba wanajeshi "chini ya 10" wa Israel wamekuwa wakipokea mafunzo ya kijeshi yasiyo ya vita nchini Uingereza kila mwaka tangu 2020.

Alikataa kufichua idadi ya wanajeshi wa IDF walioshiriki katika mafunzo kwa kipindi hicho, au kozi walizojiandikisha "ili kulinda taarifa za kibinafsi." Hata hivyo, mawaziri hao walisisitiza kuwa kozi hizo zinasisitiza umuhimu wa kufuata sheria za kimataifa za kibinadamu.

Mwezi Juni, Waziri wa ulinzi Luke Pollard alithibitisha kwamba "idadi ndogo ya wanajeshi wa Israel" walikuwa wakishiriki katika mafunzo nchini Uingereza, lakini alikataa kutoa maelezo zaidi.

Je, Uingereza iliiwekea Israel vikwazo kutokana na vita vyake dhidi ya Gaza?

Mtazamo wa Uingereza wa kuiwajibisha Israel kwa vitendo vyake katika vita vya Gaza ulibadilika baada ya uchaguzi mkuu wa 2024.

Serikali mpya ya Leba ilitupilia mbali upinzani wake dhidi ya hati za kukamatwa zilizotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu dhidi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Waziri wa zamani wa Ulinzi Yoav Gallant.

Tangu wakati huo, amekuwa na sauti zaidi katika ukosoaji wake kwa viongozi wa Israeli, akiungana na nchi zingine 27 wiki hii kulaani "mauaji ya kinyama ya raia" wanaotafuta chakula na maji huko Gaza.

Serikali ya chama cha Labour ilisitisha mazungumzo ya kuimarisha makubaliano ya biashara huria na Israel mwezi Mei, huku Lammy akielezea jinsi Israel inavyowatendea Wapalestina kama "kudharau maadili ya watu wa Uingereza."

Lakini wakati serikali ya Uingereza imewawekea vikwazo mawaziri wawili wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Israel kwa "kuchochea ghasia" katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, bado haijaiwekea Israel vikwazo vyovyote moja kwa moja kutokana na hatua yake huko Gaza, ambayo imesababisha vifo vya takriban watu 59,029, kulingana na Wizara ya Afya ya Palestina huko Gaza.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla