Ndege 3 hatari zaidi za kivita inazojivunia Israel

Chanzo cha picha, Thinkstock
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi Kenya
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Huku vita kati ya Iran na Israel vikiingia siku yake ya sita, jamii ya kimataifa imetoa wito kwa pande husika kujizuia na kusitisha vita hivyo ambavyo tayari vinaonekana kusababisha madhara makubwa ya kiuchumi kwa pande zote mbili.
Israel ambayo imekuwa ikisaidiwa na Marekani katika vita vya awali dhidi ya maadui zake imeripoti kuwa na uwezo wa kushambulia eneo lolote lile ndani ya Iran kupitia makombora na ndege za kivita, huku Iran ikitumia makombora yake yenye kasi ya hypersonic kutekeleza mashambulizi nchini Israel.
Lakini ni silaha gani haswa ambazo Israel inajivunia dhidi ya wapinzani wao Iran katika vita hivi ambavyo havijulikani mwisho wake?
BBCswahili imeangazia baadhi ya ndege za kivita za Israel ambazo zinatumika katika operesheni ya 'Rising Lion' dhidi ya Iran na kuandaa taarifa ifuatayo.
Ndege aina ya F-35

Chanzo cha picha, LOCKHEED MARTIN
Wakati utawala wa rais Bill Clinton ulipotoa wazo la ndege ya kivita yenye 'majukumu mawili tofauti' 1995 , ndio iliokuwa suluhu kwa changamoto chungu nzima za kijeshi.
Lengo lilikua kutengeneza ndege ya kijeshi ilio na teknolojia ya kisasa ili kuweza kutekeleza operesheni tofauti kwa vitengo vitatu vya jeshi la Marekani.
Jeshi la wanaanga wangeitumia ndege hiyo kama mbadala wa ndege ya kivita ya F-16 katika mashambulizi ya angani , kushambulia maeneo ya ardhini na kutoa usaidizi kwa wanaanga hewani.
Ifahamu f-35
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lockheed Martin F-35 Lightning II ni familia ya Kiamerika ya ndege za kivita za mashambulizi zenye kiti kimoja , injini moja, na zenye uwezo wa kushambulia wa hali ya juu.
Haionekani na maadui. Wakati ndege ya F-35 inaposhiriki katika mazoezi, kawaida huzishinda ndege za adui kwa kiwango cha 20 kwa 1.
Ingefanya vivyo hivyo wakati wa vita dhidi ya wanajeshi wa Urusi au Wachina, kwa sababu iliundwa kunyonya au kupotosha nishati ya rada, kwa hivyo marubani wa ndege za adui hawawezi kuiona kabla haijashambulia.
Kwa kuongezea, F-35 ina mfumo wa hali ya juu ambao unadanganya au kukandamiza rada za adui, angani na ardhini.
Rada hizo zinaweza kugundua kitu kwa mbali, lakini haziwezi kuifuatilia au kuishambulia F-35.
Pia, injini ya ndege hiyo ina uwezo wa kupunguza joto kabla ya makombora yanayotafuta joto kuishambulia.
Ni zaidi ya ndege ya kivita . F-35 sio tu ndege ya kupambana bali pia ni ndege inayoweza kuishi muda mrefu kuwahi kuundwa.
Ndege hii ina kasi ya juu ya Mach 1.6 ambayo ni sawa na kilomita 1,960 kwa saa.
Lakini huo ni mwanzo tu. Sensa za ndani za F-35 zinaweza kukusanya na kusambaza habari za ujasusi katika maeneo mbalimbali.
Mfumo wake wa kuweza kuzuia mifumo ya ndege nyengine pamoja na vifaa vyake vya mashambulizi angani inaifanya ndege hiyo kuwa bora dhidi ya ndege nyengine za kivita.
Uwezo wake wa kupaa angani wima na kuweza kutua mahali popote ambapo wanamaji watataka huku ikiwa na uwezo wa kubeba silaha za nyuklia ili kutoa ulinzi.
F-16

Chanzo cha picha, Reuters
F-16 ni ndege ya kivita ya Kimarekani yenye injini moja.
Ndege hii ina uwezo mwingi na inajulikana kwa ujanja wake, kasi, na uwezo wa hali ya juu katika mashambulizi ya angani.
Ni mfumo wa silaha ya bei ya chini lakini yenye utendaji wa hali ya juu.
Ni mojawapo ya ndege muhimu zaidi za kivita za Nato
Ndege ya kivita ya F-16 ndiyo ndege tegemeo kwa wanajeshi wengi duniani, ikiwa imetumika katika migogoro mingi, ikiwemo sasa nchini Ukraine.
Inaweza kubadilika kwa kiwango cha juu na imejidhihirisha katika mapigano ya angani na angani na ardhini.
F-16 ya leo -The Block 70/72 - ndiye mpiganaji wa kiwango cha juu zaidi wa kizazi cha 4 kuwahi kutengenezwa na imeleta kiwango kipya cha uwezo kwa vikosi vya anga kote duniani.
Ijapokuwa sio ndege bora ya kivita ya kizazi cha 4 iliyotengenezwa. Ni ndege yenye uwezo mkubwa lakini rekodi yake ya kivita na uwezo wake ni mdogo ikilinganishwa na ile ya F-1.
Umuhimu wa F-16
F-16 inaweza kufanya kazi katika hali mbalimbali za hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha silaha kwa usahihi katika hali ya milipuko isiyoonekana
Inasifika kwa kasi na wepesi, hivyo kuifanya kuwa ndege ya kivita ya kutisha.
Vilevile ina rekodi iliyothibitishwa ya mapigano na inasalia katika huduma ya jeshi la Marekani na mataifa mengine mengi.
Ndege ya kivita ya F -15

Chanzo cha picha, Reuters
Kwa nini ndege hii inaogopwa sana?
F-15 ilikuwa mpiganaji wa kwanza ambaye angeweza kushambulia shabaha nyingi za adui kwa wakati mmoja kutoka umbali wa hadi maili 100.
Kwa kutumia mfumo wake wa kisasa wa rada, na makombora ya hali ya juu ya kuongozwa na rada ya angani hadi angani ina uwezo wa kuwalipua maadui kabla hata hawajajua ni nini kiliwapiga.
Inaweza kupenya ulinzi wa adui na kuzishinda ndege za adui.
Ikiwa na matanki ya mafuta yasiyo rasmi yaliyowekwa kandokando yake F-15E inaweza kuruka maili 2,400 - karibu umbali wa maili 50 kwa hivyo inahitaji kujazwa mafuta angani.
Mchakato huo unachukua dakika tano hadi 10.















