Uchambuzi: Diplomasia yasambaratika baada ya Israel kuwashambulia viongozi wa Hamas nchini Qatar

Maelezo ya video, CCTV yanawa wakati Israel ilipowashambulia viongozi wa Hamas mjini Doha
    • Author, Jeremy Bowen
    • Nafasi, Mhariri wa Kimataifa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Takriban mwaka mmoja uliyopita nilimhoji kiongozi wa Hamas na mpatanishi mkuu Khalil al-Hayya in Doha. Nilikutana naye katika nyumba moja ambayo haikuwa mbali na jengo ambalo lilishambuliwa na Israel siku ya Jumanne.

Tangu vita vya Gaza vilipozuka, al-Hayya amekuwa mpatanishi mkuu wa Hamas, akituma na kupokea ujumbe kwa Waisraeli na Wamarekani kupitia wapatanishi wa Qatar na Misri.

Wakati ambapo kulikuwa na matumaini ya kufikiwa kwa makubaliano ya kusitishaji mapigano, al-Hayya, pamoja na wanaume ambao pia walilengwa hiyo jana, walikuwa umbali mfupi tu kutoka kwa wajumbe wa Israeli na Marekani.

Waliposhambuliwa, al-Hayya na viongozi wengine wakuu wa Hamas walikuwa wakijadili mapendekezo ya hivi punde ya kidiplomasia ya Marekani ya kumaliza vita huko Gaza na kuwaachia huru mateka wa Israel waliosalia.

Tamko la haraka la Israel la kile ilichokifanya mara moja lilichochea uvumi kwenye mitandao ya kijamii kwamba mapendekezo ya hivi punde ya Marekani yalikuwa ni njama tu ya kuupata uongozi wa Hamas katika sehemu moja ambapo wangeweza kuwashambulia.

Tarehe 3 Oktoba mwaka jana, Khalil al-Hayya alipoingia kwenye ukumbi kwa ajili ya mkutano wetu katika jumba la kawaida la ghorofa la chini, nilishangaa kwamba alikuwa na usalama mdogo sana. Ilitubidi kuacha simu zetu, na walinzi kadhaa wakaingia naye ndani ya nyumba.

Nje ya nyumba hiyo kulikuwa na polisi wa Qatar ambao hawakuwa wamevalia sare rasmi, Walikuwa wakivuta sigara ndani ya gari aina ya SUV. Walinzi mia moja hawangeweza kuzuia shambulio la anga, lakini al-Hayya na watu wake walikuwa wametulia na kujiamini.

Kinachojitokeza ni wazi kwamba kulingana na wao Qatar ilipaswa kuwa mahali salama, na walihisi kuwa salama kiasi cha kundelea na shughuli zao bila hofu.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Miezi michache kabla ya hapo, tarehe 31 Julai 2024, Israel ilikuwa imemuua Ismail Haniyeh, kiongozi wa kisiasa wa Hamas mjini Tehran, ambapo alikuwa akihudhuria kuapishwa kwa Rais Masoud Pezeshkian.

Kutokana na vita vinavyoendelea Gaza vikiendelea, Nilikuwa na mashaka kuwa katika chumba kimoja na Khalil al-Hayya. Lakini sawa na alivyodhania mimi pia nilifikiri Qatar ilikuwa nje ya mipaka.

Katika miongo michache iliyopita Qatar imejaribu kujijengea nafasi kama Uswizi ya Mashariki ya Kati, mahali ambapo hata maadui wanaweza kufanya makubaliano.

Wamarekani walifanya mazungumzo na Taliban wa Afghanistan huko Doha. Na katika takriban miaka miwili tangu mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba 2023, Qatar imekuwa kitovu cha juhudi za kidiplomasia kujadili usitishaji mapigano na pengine hata kukomesha vita.

Juhudi za kutafuta amani, zilizoendeshwa na mjumbe wa Rais Trump, Steve Witkoff, zilikuwa zikiyumba. Lakini sasa wamesambaratika. Nikinukuu kauli ya mwanadiplomasia mmoja mkuu wa magharibi "hakuna diplomasia."

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amewaambia Waisraeli kwamba maadui zao kamwe hawatapata lepe la usingizi na wanatajuta kuamuru mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba.

Picha ya Khalil al-Hayya akiwa pamoja na wanaume wengine watatu

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kiongozi wa Hamas na mpatanishi mkuu Hamas Khalil al-Hayya

Mashambulizi ya Israel mjini Gaza yanaendelea kuongezeka.

Saa chache kabla ya shambulio la Doha, jeshi la ulinzi la Israel, IDF, iliwaambia Wapalestina wote kuondoka katika mji wa Gaza na kuelekea eneo la kusini.

Inasadikiwa kuwa watu karibu milioni moja wataathiriwa na hatua hiyo.

Katika hotuba yake kupitia televisheni, Netanyahu aliwaambia Wapalestina huko Gaza "msipotoshwe na wauaji hawa. Simama upiganie haki na mustakabali wako. Chagua kufikia amani nasi. Kubali pendekezo la Rais Trump. Usijali, unaweza kufanya hivyo, na tunakuahidi mustakabali tofauti, lakini unapaswa kuwaondoa watu hawa njiani. Tukifanya hivyo, tutapata utulivu usio na kifanini siku za usoni."

Wapalestina wa Gaza wakiitikia mwito wake, watafanya hivyo kinyonge sana.

Israel imeharibu maelfu ya nyumba zao, pamoja na hospitali, vyuo vikuu na shule.

Wakati eneo la Gaza likikumbwa na baa la njaa, ukame mkubwa katika jiji la Gaza lenyewe, na janga kubwa la kibinadamu kote katika ukanda huo, kulazimishwa kwa watu wengi zaidi kuhama kutazidisha tu shinikizo hatari la Israel dhidi ya raia wa kawaida.

Israel tayari imewaua zaidi ya Wapalestina 60,000 huko Gaza, wengi wao wakiwa raia.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anakabiliwa na hati ya kukamatwa kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa tuhuma za uhalifu wa kivita, na Israel inachunguzwa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa tuhuma za mauaji ya halaiki (genocide).

Shambulio lililotokea mjini Doha ni ishara kwamba Netanyahu na serikali yake wako tayari kuongeza shinikizo kwa nguvu katika nyanja zote si Gaza pekee.

Wanaamini kuwa, kwa msaada wa Marekani, jeshi la Israel linaweza kutekeleza matakwa yao bila pingamizi.

Shambulio hilo limepelekea shutuma adimu kutoka Ikulu ya Marekani (White House).

Qatar ni mshirika wa karibu wa Marekani, mwenyeji wa kambi kubwa ya kijeshi ya Marekani na pia ni mwekezaji mkubwa nchini humo.

Hata hivyo, inaonekana Netanyahu anahesabu kwamba Donald Trump, kiongozi pekee anayempa uzito wa kweli, atatosheka na lawama ya kidiplomasia isiyo na athari kubwa.

Mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza yanaendelea.

Na kadri tarehe ya kutambuliwa kwa uhuru wa Palestina katika Umoja wa Mataifa inavyokaribia mwishoni mwa mwezi huu na mataifa ya Magharibi kama Uingereza, Ufaransa, Kanada, Australia na mengine yakipanga kuunga mkono hatua hiyo washirika wa Netanyahu wenye misimamo mikali ya kizalendo ndani ya baraza lake la mawaziri wanazidisha miito ya kuitikia kwa kuchukua hatua ya kutwaa rasmi maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu katika Ukingo wa mto Jordan yaani Westbank.