Kwanini utambuzi wa Taifa la Palestina unaleta utata?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Sammy Awammy
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer ametangaza mpango wa nchi hiyo kulitambua taifa la Palestina ikiwa Israel haitasitisha mapigano Gaza na ikishindwa kuruhusu msaada wa chakula na mingine ya kibinadamu kuwafikia watu wa Gaza.
Masharti mengine ambayo Starmer ametoa ni pamoja na hakikisho la Israel kwamba halitalimega eneo lingine la Wapalestina liitwalo Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ama West Bank na kuitaka Israel ikubali mpango wa muda mrefu wa kufikia amani eneo hilo kwa kufuata mpango ujulikanao kama Two-State Solution, unaotafuta kuunda mataifa mawili huru ya Israel na Palestina.
Wengi wamepongeza hatua hii ya Uingereza, japo wapo walioshangazwa na masharti aliyoyaweka Waziri Mkuu wa nchi hiyo kama yasiyokuwa na maana au ulazima.
Msimamo huu wa Uingereza unakuja mwezi mmoja tu tangu Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kutangaza kwamba nchi yake italitambua taifa la Palestina hapo mwezi Septemba baadae katika Baraza la Umoja wa Mataifa.
"Kwa kuzingatia dhamira yake ya kihistoria ya kuunga mkono amani ya haki na ya kudumu katika Mashariki ya Kati, nimeamua kwamba Ufaransa itaitambua rasmi nchi ya Palestina" alisema Macron.
Uingereza na Ufaransa wamekuja juzi wakiwa wamechelewa. Kati ya nchi wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa, 144 wamelitambua taifa la Palestina – ikiwemo Norway, Hispania na Ireland waliofanya hivyo mwaka jana.
Kwa upande mwingine kuna nchi kama 28 hivi wanachama wa Umoja wa Mataifa ambazo hazilitambui taifa la Israel. Hizi ni pamoja na Indonesia, Cuba na zingine za Kiarabu takribani kumi na tano kutoka Mashariki ya Kati.
Baada ya Uingereza kuifuata Ufaransa, na hivi punde Canada kuna imani kwamba nchi nyeingine za Ulaya, na Australia zitafuata pia katika kulitambua taifa la Palestina.
Hamasa hii imeibua matumaini mapya juu ya kuanzishwa kwa taifa la Palestina, jambo ambalo limekuwa sehemu ya mpango unaofahamika kama Two-State Solution (Mpango wa Mataifa Mawili), uliobuniwa mwanzo na Umoja wa Mataifa mwaka 1947, ikiwa ni sehemu muhimu ya jitihada za kumaliza mapigano kati ya Wayahudi na Wapalestina na kuleta amani eneo hilo la Mashariki ya Kati.
Mpango wa Mataifa Mawili ni nini?
Huu ni mpango wa amani unaolenga kutambua uwepo wa mataifa mawili – Israel na Palestina. Kwa kufanya hivi, matumaini ni kwamba kila taifa litakuwa na haki na uhuru wa kujiamulia mambo yake ikiwa ni pamoja na ustawi wa wananchi wake, huduma za msingi za kijamii na haki zote za binadamu.
Kwa sasa, Wapalestina wanakaliwa kwa mabavu na Israel. Katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, Wapalestina hawaruhusiwi kusafiri kwa uhuru – hata ikiwa kwenda kutafuta chakula na huduma za msingi za afya zinazopatikana maeneo ambayo Israel inayadhibiti kijeshi. Mpango huu, unalenga kutatua hilo.
Mpango wa Mataifa Mawili: Ulivyoanza na unavyoendelea

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mpango huu ulianza mwaka 1947 baada ya kupendekezwa na Umoja wa Mataifa.
Wazo la mpango huu lilikuja baada ya zaidi ya miaka kumi ya vurugu za kushambuliana kati ya watu wenye asili ya Kiyahudi na wale wenye asili ya Kiarabu waliokuwa wakiishi katika eneo hili moja lililojulikana kama Palestina likiwa chini ya utawala wa mkoloni Mwingereza.
Kwa sehemu kubwa, Uingereza ilikuwa kiini cha mapigano haya, lakini baada ya kushindwa kuyatuliza, ikaamua kuukabidhi mgogoro huu kwa Umoja wa Mataifa mnamo mwezi Februari 1947.
Miezi tisa baadae, Umoja wa Mataifa ndio ukaja na wazo kwamba ili kukomesha mapigano hayo, eneo hilo lililokuwa likijulikana kama Palestina, ligawanywe kati ya Waarabu na Wayahudi – ili kila mtu aishi kwa amani katika eneo lake.
Mpango wa Mataifa Mawili unaofahamika zaidi hii leo ni ule uliotiwa saini jijini Oslo nchini Norway. Hii ndio ilikuwa mara ya kwanza ambapo wawakilishi wa Israel na Palestina walifanya majadiliano ya moja kwa moja baada ya miaka zaidi ya 40 ya mapigano kati yao.
Mpango huu uliibua matumaini mapya ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Palestina

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanzoni, uongozi wa wakati ule wa Israel uliuunga mkono mpango huu kishingo upande – lakini kadiri siku zinavyokwenda, ndio wanaendelea kuuhujumu zaidi na hadi siku za hivi karibuni Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu – anayeongoza serikali yenye msimamo mkali kupata kutokea Israel - akasema kulitambua taifa la Palestina itakuwa ni kuwatuza magaidi.
Ni asilimia chini ya 30 tu ya Waisraeli wanaounga mkono mpango huu. Wengi wanaamini haiwezekani pakawa na taifa la Palestina ambalo halitataka kuiacha Israel iishi kwa amani au hata kutaka kuiangamiza kabisa.
Kwa sehemu kubwa serikali ya Israel imeendelea kuuhujumu mpango huu, si tu kwa vurugu na ukandamizaji ambao imekuwa ikiwafanyia Wapelestina lakini kwa ongezeko la uvamizi wa maeneo ambayo yanatambulika kimataifa kuwa ni ya Wapalestina.
Hadi hivi sasa, inakadiriwa kuna walowezi wa kiyahudi takribani Laki Saba (700,000) wanaoishi maeneo ya Jerusalem Mashariki na Ukingo wa Magharibi.
Kwa upande wa Wapalestina, ni asilimia arobaini tu (40) ndio wanaouunga mkono mpango huu wa Mataifa Mawili. Wengi wanauona kuwa si wa haki na hawaamini kwamba jumuiya ya kimataifa itautekeleza vizuri. Lakini pia wamejawa na maswali mengi.
Kwanza; Ikiwa Wapalestina wataukubali mpango huu, ardhi yao itakuwa ipi na kiasi gani? Kwa sababu pamoja na Israel kusaini mkataba wa Oslo.
Uliowataka kuwaondoa wanajeshi wao na kuyaachia maeneo ya Wapalestina, walifanya hivyo kidogo tu halafu wakasimama.
Isitoshe, si tu kwamba Israel imefanya uvamizi kuwa sera rasmi ya serikali ya sasa, inawatia moyo pia wananchi wake kwenda na kuvamia maeneo ya Wapalestina.
Lakini pia mpango huu hautatui suala la wakimbizi wa Kipalestina wapatao milioni saba ambao sasa wanaishi Ukingo wa Magharibi. Kwa asili, hawa makazi ya mababu zao ni katika eneo linalojulikana hivi sasa kama Israel, na wanataka kurudi katika maeneo yao.
Mapendekezo mengi ya Mataifa Mawili yanawanyima Wapalestina hawa kurudi katika ardhi ya mababu zao. Wapalestina wanaona hii ni dhulma kubwa ya haki yao hivyo hawawezi kuunga mkono mpango wa Mataifa Mawili
Tatu, suala la mji wa Jerusalem. Kwamba, pakiwa na mtaifa mawili, mji huo utakuwa chini ya taifa gani? Huu ni mji wenye maana kubwa kwa dini zote tatu za Kiislam, Kikristo na Kiyahudi.
Pamekuwepo na jitihada nyingi za kutafuta mwafaka juu ya mji huu uende wapi, lakini zote zimeshindwa.
Mapendekezo ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 1947 yalitaka Jerusalem uwe mji wa Kimataifa – kwamba kila mtu autumie.
Wapalestina wameweka eneo la Jerusalem Mashariki kuwa mji wao mkuu mara tu watakaposimamisha taifa lao.
Israel kwa upande mwingine baada ya kuichukua Jerusalem Mashariki kutoka kwenye usimamamizi wan chi ya Jordan katika ile vita ya siku sita ya mwaka 1967, imeufanya mji wote kuwa wake huku ikiutangaza kuwa mji wake mkuu.
Nchi nyingi za jumuiya ya kimataifa haziutambui rasmi kama mji mkuu wa Israel, hivyo utaona hata balozi karibu zote zipo Tel Aviv. Lakini katika utawala wake wa kwanza Rais wa marekani Donald Trump, alihamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv na kuuweka hapo Jerusalem. Hii ilikuwa ishara ya kuunga mkono msimamo wa Israel juu ya mji huo wa Jerusalem.
Nne, kuna masuala ya mipaka na usalama wa mipaka hiyo. Hadi hivi sasa Israel ndio inaamua mpaka gani uwe wao na upi uwe na Wapalestina, ambapo imechukua eneo kubwa, na hasa lile lenye rutuba na linalofaa zaidi kwa kilimo.
Lakini mpango wa Mataifa Mawili pia unawapa Israel mamlaka ya kudhibiti mipaka na usalama wa mipaka hiyo. Kwa miaka yote ya Israel kuwa na wajibu huu, imeminya sana haki za Wapalestina si tu kujiendeleza kijamii bali hata kutembea kutoka eneo moja Kwenda lingine
Tano, ni kuhusu ukanda wa Gaza. Ikatokea kuna mataifa mawili, nani atauchukua ukanda huo? Wote Wapalestina na Waisrael wanataka kuumiliki ukanda wa Gaza.
Na baada ya vita hii ambayo Israel imeiendesha hapo Gaza, sauti kutoka Israel za kutaka kuuchukua ukanda huo moja kwa moja zimeongeza zaidi na zaidi – na mara kadhaa kuungwa mkono na Rais wa Marekani Donald Trump na serikali yake.
Pasi na shaka, kuongezeka kwa mateso ya Wapalestina wanayofanyiwa na Israel hapo Gaza – na hasa mauwaji ya watu wa rika zote baada ya kunyimwa chakula, kumekuza na kuimarisha sauti za kurejelewa kwa Two-State solution, suluhisho la nchi mbili.
Hata hivyo, wengi wanasubiri kuona majadiliano rasmi ya mpango huo kuanza na utashi wa kisiasa kati ya Israel na Wapalestina lakini hata jumuiya ya kimataifa pia – kabla hawajafikia hitimisho kwamba kweli Mataifa Mawili ya Israel na Palestina yanaweza kufikiwa.














