Uchambuzi: Uingereza 'kuitambua' Palestina ni kufufua mchakato wa amani

Chanzo cha picha, EPA
- Author, Jeremy Bowen
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Tangazo la Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer kwamba nchi hiyo italitambua taifa la Palestina ni mabadiliko makubwa katika sera za nje za Uingereza.
Amesema Uingereza itaahirisha kulitambua taifa hilo kama Israel itachukua "hatua madhubuti kukomesha hali mbaya huko Gaza, kwa kukubali kusitisha mapigano na kujitolea kusaka amani ya muda mrefu na endelevu na kufufua suluhisho la mataifa mawili."
Kuleta amani haitakuwa rahisi, hasa baada ya Hamas kuuwa karibu watu 1,200, wakiwemo mamia ya raia wa Israel, na kuchukua mateka tarehe 7 Oktoba 2023, na kufuatiwa na jibu la kulipiza kisasi la Israel ambalo limeua maelfu ya raia na kuiacha Gaza ikiwa magofu.
Pia ikumbukwe kuwa kila jaribio la kuleta amani limeshindwa. Miaka ya mazungumzo ya amani katika miaka ya 1990 iliishia katika umwagaji damu. Na kila jaribio la kufufua amani tangu wakati huo limeporomoka.
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alichapisha maneno makali ya kukashifu kwenye mitandao ya kijamii kupinga mpango wa Starmer:
"Starmer anatoa zawadi kwa ugaidi wa kutisha wa Hamas na kuwaadhibu waathiriwa wa ugaidi huo. Nchi ya kijihadi kwenye mipaka ya Israel LEO, itakuwa tishio kwa Uingereza KESHO."
"Kuwafurahisha magaidi wa jihadi daima hakufaulu. Nawe utashindwa pia. Haitatokea."
Mipango ya Israel
Netanyahu anakanusha kuwa Israel imesababisha njaa na maafa huko Gaza. Lau angekubali masharti ya Uingereza ya kusitisha vita, serikali yake ingesambaratika. Anategemea kuungwa mkono na watu wenye msimamo mkali wa kitaifa wanaotaka kunyakua maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na kuwalazimisha Wapalestina waondoke, na sio kuwapa uhuru.
Netanyahu alijenga taaluma yake ya kisiasa kwa kupinga suluhisho la serikali mbili, wazo la kuleta amani kwa kuundwa taifa huru la Palestina pamoja na Israel. Mapema mwezi huu alisema taifa la Palestina litakuwa chanzo cha majaribio zaidi kama lile la Oktoba 7 la kuiangamiza Israel.
Netanyahu ana matumaini ya kuendelea kuungwa mkono na serikali ya Marekani. Msimamo wake ni kwamba kulitambua taifa la Palestina sasa itakuwa ni zawadi kwa ugaidi wa Hamas.
Donald Trump aliwaambia waandishi wa habari alipokuwa akirejea Marekani baada ya mchezo wake wa gofu nchini Scotland kwamba haungi mkono hatua ya Uingereza.
Hadi wiki chache zilizopita Keir Starmer hakuwa ameshawishika kwamba ni wakati sahihi wa kuitambua Palestina. Lakini picha za watoto wa Kipalestina huko Gaza wakiwa na njaa hadi kufa, lilikuwa ni jambo la mwisho asiloweza kulikubali baada ya mauaji na uharibifu mkubwa.
Msimamo wa Uingereza
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Uamuzi wa Uingereza kujiunga na Ufaransa katika kuitambua Palestina ni ishara nyingine ya kuzidi kutengwa kwa Israel kidiplomasia. Washirika wake wawili wakuu wa nchi za magharibi, Uingereza na Ufaransa, na ni zote wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Jijini New York mara tu baada ya kauli ya Starmer, David Lammy, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, alishangiliwa sana alipotangaza uamuzi wa Uingereza katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu suluhisho la mataifa mawili na kulitambua taifa la Palestina.
Alipuuzilia mbali shutuma kwamba uhuru wa Palestina unaweza kuwa hatari kwa Israel.
"Hakuna mkanganyiko kati ya kuunga mkono usalama wa Israel na kuunga mkono taifa la Palestina."
"Niseme wazi: kukataa kwa serikali ya Netanyahu juu ya suluhu ya serikali mbili ni makosa - ni makosa kimaadili na ni makosa kimkakati."
Lammy aliendelea kuzama katika historia ya zamani ya Ufalme wa Uingereza huko Palestina ambayo inaingiliana sana na mizizi ya mzozo kati ya Wayahudi na Waarabu juu ya udhibiti wa ardhi ambayo Uingereza iliwahi kuitawala.
Uingereza iliiteka Jerusalem kutoka himaya ya Ottoman mwaka 1917 na kuitawala Palestina hadi mwaka 1948, ikiwa imechoka na kukosa mawazo ya jinsi ya kukabiliana na mvutano kati ya Waarabu na Wayahudi, ikakabidhi jukumu hilo kwa Umoja wa Mataifa na kuondoka Palestina.
Papo hapo, waziri mkuu wa kwanza wa Israel David Ben Gurion alitangaza uhuru wa Israel, na Israel ikashinda vita dhidi ya uvamizi wa majeshi ya Waarabu.
Huko Umoja wa Mataifa David Lammy alieleza jinsi Arthur Balfour, mtangulizi wake kama Waziri wa mambo ya nje alivyotia saini mwaka 1917 barua iliyoahidi 'kupendekeza uanzishwaji wa taifa la Kiyahudi katika ardhi ya Palestina.'
Lakini waraka huo unaojulikana kama Azimio la Balfour, pia ulisema "hakuna kitakachofanyika ambacho kitaathiri haki za kiraia na kidini za jumuiya zisizo za Kiyahudi huko Palestina." Haukutumia neno Waarabu, lakini ndivyo ilivyokusudiwa.
Lammy alisema Uingereza inaweza kujivunia jinsi ilivyosaidia kuweka misingi ya kuanzishwa kwa Israel, lakini ahadi iliyowekwa kwa Wapalestina, Lammy anasema, haikutekelezwa, na hiyo "ni dhuluma ya kihistoria inayoendelea kujitokeza."
Ahadi zinazokinzana za Uingereza zilichochea na kuchagiza mzozo huo.
Mkutano huo uliofanyika New York uliongozwa na Ufaransa na Saudi Arabia, umetoa waraka wa kurasa saba unaolenga kuunda njia ya kufufua suluhisho la mataifa mawili, ikiwa ni pamoja na mataifa ya Kiarabu kuilaani Hamas na mashambulizi yake ya Oktoba 7 dhidi ya Israel.
Dirisha la amani kupitia suluhisho la serikali mbili lilionekana kufungwa baada ya kuporomoka kwa mchakato wa amani ulioanza kwa matumaini ya kweli katika miaka ya 1990.
Uamuzi wa Uingereza kuitambua Palestina ni kibarua cha kidiplomasia cha kujaribu kulifungua tena dirisha hilo.















