Athari za kulitambua taifa la Palestina
Na James Landale ,
Mwandishi wa Diplomasia ,

Chanzo cha picha, Reuters
Wakati mapigano na mateso yakiendelea huko Gaza, na ghasia zikiongezeka katika Ukingo wa Magharibi, matarajio ya watu wa Palestina kupata taifa lao yanaweza kuonekana mbali zaidi kuliko hapo awali.
Uamuzi wa nchi kadhaa za Ulaya kutambua rasmi uwepo wa taifa la Palestina hautazidi nguvu ya ukweli kwamba azma hiyo bado inakabiliwa na vikwazo vikubwa.
Lakini matamko ya Ireland, Uhispania na Norway yataweka shinikizo kwa mataifa mengine barani Ulaya - ikiwa ni pamoja na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani - kufuata yao katika kuunga mkono kujitawala kwa Wapalestina.
"Hii ni muhimu sana," mwanadiplomasia mmoja wa Kiarabu alisema. "Inaonyesha kuchanganyikiwa kwa Ulaya na kukataa kwa serikali ya Israeli kusikiliza.
"Na inaweka shinikizo kwa Muungano wa Ulaya (EU)kufuata mkondo huo."
Lakini mawaziri wa Israel wanasisitiza kuwa hii itawatia moyo Hamas na kuuzawadi ugaidi, na hivyo kupunguza zaidi uwezekano wa kupatikana kwa suluhu kwa mazungumzo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Nchi nyingi - takriban 139 kwa jumla - zinatambua rasmi taifa la Palestina.
Mnamo Mei 10, wajumbe 143 kati ya 193 wa mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa walipiga kura ya kuunga mkono pendekezo la Wapalestina la kutaka uanachama kamili wa Umoja wa Mataifa, jambo ambalo liko wazi kwa mataifa pekee.
Kwa sasa Palestina ina aina ya hadhi ya waangalizi iliyoimarishwa katika Umoja wa Mataifa, ambayo inawapa nafasi lakini sio kura katika mkutano huo.
Pia inatambuliwa na mashirika mbalimbali ya kimataifa yakiwemo Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu.
Nchi chache za Ulaya tayari zinatambua taifa la Palestina. Ni pamoja na Hungary, Poland, Romania, Jamhuri ya Czech, Slovakia, na Bulgaria ambayo ilipitisha azma hiyo 1988; na zingine zikiwemo Uswidi, Cyprus na Malta.
Lakini mataifa mengi ya Ulaya - na Marekani - yanasema yatalitambua taifa la Palestina tu kama sehemu ya suluhisho la muda mrefu la kisiasa kwa mzozo wa Mashariki ya Kati.
Hii mara nyingi hujulikana kama 'suluhisho la serikali mbili' ambapo Waisraeli na Wapalestina wanakubali kuwa na nchi zao na mipaka yao wenyewe.
Nchi za Ulaya na Marekani zinatofautiana juu ya lini zinapaswa kutambua taifa la Palestina.
Ireland, Uhispania na Norway wanasema wanafanya hivyo sasa ili kuanzisha mchakato wa kisiasa. Wanasema kutakuwa na suluhu endelevu kwa mzozo wa sasa ikiwa tu pande zote mbili zinaweza kulenga aina fulani ya upeo wa kisiasa.
Nchi hizi pia zinajibu shinikizo ya kisiasa ya ndani ili kuonyesha uungaji mkono zaidi kwa Wapalestina.
Hapo awali, msimamo wa nchi nyingi za Magharibi ulikuwa kwamba utaifa wa Palestina unapaswa kuwa tunu kwa makubaliano ya mwisho ya amani.
Lakini Bwana Cameron, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, na baadhi ya nchi nyingine za Ulaya katika miezi ya hivi karibuni wamebadilisha misimamo yao, wakisema kutambuliwa kwa taifa la Palestina kunaweza kuja mapema, kusaidia kusukuma kasi kuelekea suluhu la kisiasa.
Mwezi Februari, Rais Macron wa Ufaransa alisema: "Kutambuliwa kwa taifa la Palestina sio mwiko kwa Ufaransa."
Na mapema mwezi huu, Ufaransa iliunga mkono uanachama wa Wapalestina wa Umoja wa Mataifa katika kura ya mkutano mkuu.
Marekani imejadili suala hili kwa faragha na washirika wa Ulaya lakini iko makini zaidi na inataka kueleweka wazi zaidi sera hiyo ingemaanisha nini kiutendaji.
Kwa hivyo mjadala muhimu nyuma ya pazia ni juu ya lini nchi hizi zilizoshikilia zinapaswa kulitambua taifa la Palestina: wakati mazungumzo rasmi ya amani yanapoanza kati ya Waisraeli na Wapalestina, wakati Israeli na Saudi Arabia zinarekebisha uhusiano wa kidiplomasia, wakati Israeli inashindwa kuchukua hatua fulani, au wakati Wapalestina. kuchukua hatua fulani.
Kwa maneno mengine, wanataka kutambuliwa kwa taifa la Palestina kuwa wakati mkubwa uliopangwa kufikia matokeo ya kidiplomasia.
"Ni karata kubwa ambayo nchi za Magharibi zinapaswa kucheza," ofisa mmoja wa Magharibi alisema. "Hatutaki kuitupa."
Shida ni kwamba kutambua taifa la Palestina kwa kiasi kikubwa ni ishara tu ikiwa haishughulikii pia maswali muhimu yanayoambatana.
Je, mipaka inapaswa kuwa ipi? Mji mkuu unapaswa kuwa wapi? Je, pande zote mbili zinapaswa kufanya nini kwanza ili jambo hilo litokee?
Haya ni maswali magumu ambayo hayajakubaliwa - au hata kujibiwa - kwa njia ya kuridhisha kwa miongo kadhaa.
Hadi leo, nchi chache zaidi barani Ulaya sasa zinaamini kunapaswa kuwa na taifa la Palestina.
Wafuasi watashangilia hatua hiyo, wapinzani watailaumu.
Ukweli wa kutisha kwa Wapalestina walioko mashinani ni kwamba huenda hali isibadilike.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












