Israel yazindua satelite mpya ya kijasusi yenye uwezo wa kipekee duniani

a

Chanzo cha picha, Israel Foreign Ministry X

Maelezo ya picha, Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Israel, satelaiti ya kijasusi ya "Horizon 19" ilirushwa angani kutoka kituo cha anga cha Belmahim katikati mwa Israel.
Muda wa kusoma: Dakika 3

Israel imesema imefanikiwa kurusha satelaiti mpya ya kijasusi angani, hatua ambayo itaimarisha kwa kiwango kikubwa uwezo wake wa upelelezi katika eneno la Mashariki ya Kati. Kwa mujibu wa maafisa wa Israel, satelaiti hii inaweza kupiga picha za vitu vidogo hadi ukubwa wa sentimita 50, mchana na usiku.

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, alisema uzinduzi wa satelaiti hiyo, iliyopewa jina la "Horizon 19," ni ujumbe wa moja kwa moja kwa maadui kwamba "tunawaangalia kila wakati na katika hali zote."

Bw. Katz alielezea urushaji huo kuwa ni "mafanikio ya hali ya juu kabisa" ambayo ni mataifa machache pekee duniani yanaweza kuyafikia.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Israel, satelaiti hiyo ilirushwa angani usiku wa Jumanne, Septemba 2, kwa msaada wa roketi cha Shavit, na kufika kwenye obiti ya dunia kwa mafanikio.

Urushwaji wa satelaiti hii mpya unafuatia miezi miwili baada ya vita vya siku 12 kati ya Israel na Iran, ambapo Israel ilishambulia vituo vya kijeshi na vile vya nyuklia vya Iran pamoja na baadhi ya maeneo ya makazi vilivyoko zaidi ya umbali wa kilomita 1,000.

Iran ilijibu mapigo kwa kurusha makombora dhidi ya Israel, mengi hayakufanikiwa yakizuiwa na mifumo ya ulinzi wa anga, lakini baadhi pia yaliweza kupenya licha ya ulinzi wa zaidi ya mifumo 100.

Kwa mujibu wa ripoti, baada ya urushaji wa satelaiti hiyo, baadhi ya wakaazi wa Tel Aviv na maeneo ya katikati ya Israel waliona kitu chenye mwanga angani na mwanzoni walidhani kombora lilikuwa limezuiliwa, jambo lililosababisha taharuki kwa muda mfupi

Chanzo cha picha, Israel Foreign Ministry X

Maelezo ya picha, Kwa mujibu wa ripoti, baada ya urushaji wa satelaiti hiyo, baadhi ya wakaazi wa Tel Aviv na maeneo ya katikati ya Israel waliona kitu chenye mwanga angani na mwanzoni walidhani kombora lilikuwa limezuiliwa, jambo lililosababisha taharuki kwa muda mfupi

Urushaji wa Horizon 19 ulifanyika kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Ulinzi na kampuni ya taifa ya masuala ya anga inayoitwa Israel Aerospace Industries (IAI).

Mkuu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo wa Wizara ya Ulinzi, Daniel Gold, alisema zaidi ya picha 12,000 za satelaiti zilitumika kuongoza mashambulizi dhidi ya Iran.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa upande wake, Meja Jenerali Amir Baram, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Ulinzi ya Israel, alisema kuwa Horizon 19 ni sehemu ya mpango mpana wa taifa la Israel wa kufanikisha "ufuatiliaji wa kudumu na wa wakati mmoja wa kila nukta katika eneo la Mashariki ya Kati."

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema nchi yake kwa sasa inashiriki vita kwenye inavyoviita "seven fronts"; na katika kipindi cha miezi 23 tangu kuanza kwa vita vya Gaza, Israel pia imefanya mashambulizi nchini Lebanon, Syria, Yemen na Iraq, sambamba na vita vya siku 12 dhidi ya Iran.

Boaz Levi, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya IAI, aliyeshirikiana na Wizara ya Ulinzi katika mradi huu, alisema kuwa tukio la vita vya hivi karibuni dhidi ya Iran limeonesha wazi kuwa "kuwa na uwezo wa kuona mapema (kinachoendelea) katika eneo letu ni jambo la lazima ili kupata mafanikio angani na ardhini."

Satelaiti ya Horizon 19 inategemea teknolojia ya radar kwa ajili ya kupiga picha, jambo linaloipa uwezo wa kufanya kazi usiku na mchana bila kuathiriwa na hali ya hewa. Kwa mujibu wa Bw. Levi, chombo hicho cha angani kinaweza kupiga picha za vitu vidogo zaidi ya sentimita 50.

Israel ilijiunga rasmi na orodha ya mataifa yenye nguvu za anga mwaka 1988 baada ya kuzindua satelaiti yake ya kwanza, iliyojulikana kama "Horizon," katika obiti ya dunia.