Ripoti zinaonyesha mpatanishi mkuu wa Hamas miongoni mwa walengwa

Chanzo cha picha, Reuters
Kama tulivyoripoti, afisa wa Hamas anatuambia kwamba wanachama wa timu yao ya mazungumzo walilengwa wakati wa mkutano.
Maelezo zaidi sasa yanaanza kujitokeza.
Afisa wa ngazi ya juu wa Israel anaviambia vyombo vya habari vya Israel kwamba wanachama wa Hamas waliolengwa ni pamoja na Khalil al-Hayya, mpatanishi mkuu wa Gaza aliye uhamishoni, na Zaher Jabarin, kiongozi wa Ukingo wa Magharibi aliye uhamishoni.
"Tunasubiri matokeo ya mashambulizi. Kuna maelewano kati ya uongozi wa kisiasa na usalama," afisa huyo anaongeza.
Siku ya Jumatatu, Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz alikuwa amewaonya viongozi wa Hamas wanaoishi nje ya nchi kwamba wanakabiliwa na "maangamizi" na Gaza itaangamizwa ikiwa kundi hilo halitawaachilia mateka wake na kuweka silaha zake chini.
Jeshi la Israel lilianzisha kampeni huko Gaza kujibu shambulio lililoongozwa na Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 wakichukuliwa mateka.
Takriban watu 64,605 wameuawa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.















