Je, Putin ana mpango wa kumshawishi Trump kumtimua Zelensky madarakani? - gazeti la Times

Chanzo cha picha, Getty Images
Uchambuzi wa leo unaangazia makala mbili kuhusu mkutano unaotarajiwa kufanyika kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Urusi Vladimir Putin huko Alaska, na pia kuhusu "vikwazo" vya Ulaya kuhusu mikataba ya biashara huria.
"Usimdharau Trump ambaye ni mpatanishi," kinasomeka kichwa cha habari cha mwandishi wa Uingereza Roger Boyes katika makala yake katika gazeti la The Times.
Mwandishi huyo alisema kwamba mkutano wa Trump na Putin utakuwa "changamoto kubwa zaidi kwa wapatanishi wa amani" katika mkutano wa kilele ulioelezewa kama jaribio linalowezekana la kurejesha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu, ambayo inaweza hatimaye kusababisha makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Ukraine.
Lakini mwandishi alionya juu ya mgawanyiko wa muda mrefu wa Ukraine "ikiwa Putin atapata anachotaka."
Kinyume chake, mwandishi alitaja kauli za Trump kutaka kurejesha baadhi ya maeneo ya Ukraine kwenye Bahari Nyeusi ambayo Urusi iliyateka, badala ya kuyatambua maeneo makubwa ya mashariki mwa Ukraine yanayokaliwa kwa mabavu na Urusi kama sehemu ya Moscow.
Mwandishi anaelezea kuwa mkutano muhimu wa Alaska kati ya Donald Trump na Vladimir Putin huenda hauhusiani na mipaka ya ardhi tu, bali unaweza kusababisha "kusitisha vita kwa miaka mingi", jambo ambalo litawazuia Ukraine nafasi ya kujiunga na NATO.
Aliongeza kuwa kuna lengo lingine la Putin ambalo halijawekwa wazi: kumshawishi Trump kumwondoa Volodymyr Zelensky madarakani, hususan baada ya Rais huyo wa Ukraine kutokualikwa katika mkutano huo.
Mwandishi huyo naamini kuwa Trump, ambaye anajitahidi kuonekana kama mpatanishi wa amani katika karne hii ya 21, anatamani kupata Tuzo ya Amani ya Nobel.
Ili kufanikiwa, lazima aanze kuonekana kama kiongozi mwenye ujasiri na haki katika mkutano wa Ijumaa huko Alaska.
Mkutano wa Alaska unachukuliwa kama mtihani wa filosofia ya 'kutimiza mambo na kusuluhisha kwa manufaa ya pande zote'.
Lakini mwandishi anaonya kuwa kutumia ushuru na diplomasia ya shinikizo si mikataba endelevu bali ni njia za kuamua ngazi za ushawishi hasa kwa mataifa dhaifu na uchumi.
Hii inaonekana katika mipango ya Trump kufanikisha amani mwaka huu kwakudai kuwa ;
1. Amepunguza mvutano kati ya Pakistan na India kuhusu Kashmir
2. Kusuluhisha migogoro kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
3. Kumaliza vita kati ya Cambodia na Thailand
4. Kuzuia mapigano kati ya Armenia na Azerbaijan
5. na kufanikisha maamuzi ya nyuklia ya Iran.
Mwandishi anaamini mafanikio haya yanaweza kumuwezesha Trump kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel.
Kuendelea kwa vita ni pigo kwa taswira ya Trump

Chanzo cha picha, Getty Images

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika muktadha wa mkutano wa kilele uliofanyika Alaska, Raphael Beer aliandika makala katika gazeti la The Guardian yenye kichwa: "Uaminifu wa Trump kwa uongo wa Putin ni tishio kubwa zaidi kwa Ukraine kuliko mabomu."
Beer anaanza kwa kudokeza kuwa Trump na Putin wana maslahi ya pamoja katika kuonesha kana kwamba mgogoro wa Ukraine unaweza kutatuliwa bila ushiriki wa Waukraine katika meza ya mazungumzo.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa hali hiyo si halisi.
Kwa mujibu wa mwandishi, kuendelea kwa mapigano miezi saba tangu Trump aingie madarakani kwa muhula wa pili licha ya ahadi yake ya kumaliza vita ndani ya siku chache baada ya kurejea Ikulu ya White House ni pigo kwa taswira yake kama mweledi wa kufanya makubaliano ya kimataifa.
Putin, aliyeanzisha uvamizi wa Ukraine mwaka 2022, alikuwa na matarajio kuwa mji mkuu wa Kyiv ungeanguka kwa haraka.
Hata hivyo, matarajio hayo hayakutimia.
Beer anasema kuwa Putin sasa anaonekana kuamini kuwa ushindi wa Urusi dhidi ya Ukraine haukwepeki, kwa kuwa suluhisho lolote mbadala hata usitishaji wa mapigano unaomwezesha kuendelea kushikilia maeneo aliyoyateka halitimizi dhamira yake ya kihistoria.
Aidha, anaeleza kuwa mradi Rais Volodymyr Zelensky atasalia kuwa kiongozi wa taifa huru linalojiamulia mambo yake na kujitahidi kujiunga na mataifa ya kidemokrasia barani Ulaya, basi Putin ataendelea kuwa na chuki na nia ya kulipiza kisasi.
Kwa mtazamo wa mwandishi, mipaka au makubaliano yoyote yanayozuia Kremlin kuelekeza mkondo wa kisera wa Ukraine hayatambuliki kwa Putin.
Hata hivyo, hilo halitazuia Urusi kusaini makubaliano ya muda kwa sababu za kimkakati.
Zelensky, ambaye aliweza kujiondoa kwa hali ya aibu aliyokumbana nayo White House, alipata mafanikio ya kidiplomasia kupitia usaidizi wa viongozi wa NATO.
Mafanikio haya yalipelekea Trump kukiri kwamba hali ni tata zaidi kuliko alivyoelewa awali, kwamba Putin anashikilia misimamo isiyo na mashiko, na kwamba madai yake ya kupendelea amani hayaendani na mashambulizi ya mabomu dhidi ya raia wa Ukraine yanayoendelea.
Mkutano wa Alaska unafanyika wakati ambapo Trump ameanza kuweka tarehe ya mwisho ya kupatikana kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, huku Moscow ikitishia kuiwekea Marekani vikwazo vya kiuchumi.
Mwandishi anaonya kwamba msimamo wa Trump wa kumpendelea Putin unaweza kugeuza mkutano huo kuwa ushindi kwa Urusi.
Athari zitakuwa kubwa endapo Trump atatoka kwenye majadiliano hayo akirudia misimamo ya Kremlin, hali ambayo imezua wasiwasi miongoni mwa washirika wa Ulaya wa Ukraine.
Wana hofu kwamba Trump anaweza kupendekeza usitishaji wa mapigano kwa masharti ambayo Zelensky hawezi kuyakubali yakiwemo mgawanyo wa Ukraine kwa misingi iliyowekwa na Putin.
Wakati huo huo, kumbukumbu ya kihistoria inajitokeza.
Trump na Putin wanakutana Alaska, eneo ambalo Marekani ilinunua kutoka Urusi kwa takribani dola milioni 7.
Je, ina maana gani kuandaa mkutano huo muhimu katika eneo hilo?
Kuteleza kwa Ulaya katika sera ya biashara huru
Tukiachana na hayo ya Trump na Putin kukutana ili kusuluhisha mgogoro uliopo unaoendelea Ukraine kinachogonga vichwa vya habari pia ni athari ya ushuru wa Trump kwa Jumuiya ya Ulaya.
Katika tahariri iliyochapishwa na Wall Street Journal, wahariri wa gazeti hilo waliandika makala yenye kichwa: "Kuteleza kwa Ulaya katika biashara huru."
Gazeti hilo linaeleza kuwa, licha ya lawama kutoka kwa mataifa ya Ulaya kuhusu ushuru wa forodha uliowekwa na Trump, matarajio yalikuwa kuwa Umoja wa Ulaya ungefanya juhudi za kuimarisha biashara huria katika maeneo mengine duniani.
Hata hivyo, wakati mazungumzo ya kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani yalikuwa yakiendelea mwezi uliopita, jumuiya hiyo ilisitisha makubaliano ya biashara huria na kundi la nchi za Amerika Kusini.
Makubaliano hayo, yaliyokuwa yakijadiliwa kwa muda mrefu, yalilenga kuimarisha biashara kati ya Umoja wa Ulaya na mataifa ya Argentina, Brazil, Paraguay na Uruguay.
Kwa mujibu wa Tume ya Ulaya, mauzo ya bidhaa kutoka nchi hizo kwenda Umoja wa Ulaya yalifikia euro bilioni 56 mwaka uliopita, huku Umoja huo ukiuza bidhaa zenye thamani ya euro bilioni 55.2 kwa nchi hizo.
Hata hivyo, Brussels ilisitisha mchakato wa makubaliano hayo mwezi uliopita kufuatia upinzani mkali kutoka kwa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, ambapo gazeti linaeleza kuwa wakulima wa Ufaransa wana wasiwasi na ushindani unaoongezeka kutoka kwa bidhaa za kilimo kutoka Amerika ya Kusini.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ginah Gahamanyi












