Mkutano wa Alaska : Ni kipi Putin na Trump wanatarajiwa kuafikiana?

Chanzo cha picha, Mikhail Svetlov/Getty Images
- Author, Newsroom
- Nafasi, Idhaa ya Urusi ya BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Ijumaa hii, tarehe 15 Agosti, macho ya dunia yataelekezwa Alaska ambako marais wa Marekani na Urusi, Donald Trump na Vladimir Putin, wanakutana ana kwa ana kujadili vita vya Ukraine na pia makubaliano ya amani.
Huu ni mkutano ambao wengi wanasema unaweza kuwa mwanzo wa mwisho wa vita hiyo ya muda mrefu.
Lakini bado kuna maswali mazito yanayoendelea kuulizwa.
Je, Putin atapendekeza nini?
Trump atakubali masharti gani?
Na muhimu zaidi, Ukraine na mataifa ya Ulaya watalikubali hilo?
Kulingana na muangalizi wa BBC , kile kinachojitokeza wazi ni kuwa, ni vigumu kutafakari kuna mtu atafaidika zaidi kutokana na mkutano huu wa Alaska zaidi ya Vladimir Putin.
Kile Kinachosemwa Washington
Wiki iliyopita, Makataa yaliyotolewa na Rais Trump dhidi ya Urusi yalitamatika.
Alikuwa ameapa kuiwekea Urusi vikwazo vikubwa kabisa iwapo hakutakuwa na hatua kuelekea makubaliano ya amani na Ukraine.
Hili lilitokea baada ya miezi ya kauli kali kutoka kwa Trump mwenyewe.
Mwishoni mwa mwezi Julai, alipozungumza na waandishi wa habari akiwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, alikatisha matumaini ya mazungumzo yoyote akisema, "Sina nia ya kuzungumza tena."
Lakini mambo yalibadilika ghafla.
Trump alimtuma mjumbe wake maalum, Steve Witkoff, kwenda Moscow.
Baada ya mazungumzo kati ya Witkoff na Putin, kukawa na mabadiliko ya haraka na sasa, mkutano wa Alaska umewekwa mezani rasmi.
Mpango wa Kubadilishana Maeneo?

Chanzo cha picha, Oleksandr GIMANOV/AFP
Baada ya ziara ya Witkoff nchini Urusi, Trump alianza kuzungumza kwa matumaini.
Alisema kuna nafasi ya kusitisha vita.
Kwa mujibu wa Bloomberg, Trumo aliwafahamisha Ukraine na viongozi wa Ulaya kuhusianana uamuzi huu wa hivi punde.

Chanzo cha picha, Gavriil Grigorov/TASS
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Trump akiweka wazi kuwa Urusi iko tayari kuzungumza ikiwa "suala la kubadilishana maeneo" litazingatiwa, hii ni kwa mujibu wa Bloomberg.
Maudhui ya mazungumzo yalianza kujitokeza.
Kulingana na Bloomberg Interlocutors, ambao ni wajuzi wa masuala haya ya vita vya Ukraine wanaeleza kuwa huenda kulikuwa na makubaliano ya awali kwamba Urusi inataka kuhakikishiwa udhibiti wa maeneo ya Donbas na Crimea maeneo ambayo tayari imeyateka.
Kwa upande mwingine, Urusi italazimika kusitisha mashambulizi yake kwenye mikoa ya Kherson na Zaporizhia, angalau kwa sasa, vyanzo vinasema.
Vyanzo vya habari vinadai kuwa mpango huu utasitisha hali ya vita kwa muda, wakati pande zote zikiendelea na mazungumzo ya kina juu ya amani ya kudumu.
Lakini kuna tatizo kubwa: hadi sasa, haijafahamika ni maeneo gani Ukraine itarudishiwa au kulipwa kwa "kubadilishana."
Ulaya imetaka maelezo zaidi kutoka Marekani kuhusu mpango huu. Wanahoji — je, Urusi inataka tu kusimamisha mapigano? Au inalenga kuchukua kabisa maeneo hayo?
Katika mazungumzo ya baadaye, Witkoff aliwaambia viongozi wa Ulaya kwamba kuna hatua mbili:
Ukraine iondoke kwenye baadhi ya maeneo ya Donetsk, kisha mstari wa mbele usimamishwe.
Kisha Trump na Putin wakubaliane kuhusu mpango wa mwisho wa amani, ambao baadaye utawasilishwa kwa Ukraine kwa mashauriano.
Lakini hadi sasa, hakuna upande uliotoa maelezo kamili kuhusu yaliyomo kwenye makubaliano hayo ya awali. Wote – White House na Kremlin – wamesalia kimya.
Wakati huo huo, gazeti la Wall Street limeripoti kuwa mapendekezo haya yanaibua maswali mengi chungu nzima.
Viongozi wa Ulaya wamepiga simu Washington mara tatu kupata uelewa ni kipi kitafanyika katika maeneo ya Zaporizhia na Kherson .
Wanahoji je, Urusi inataka tu kusimamisha mapigano?
Au inalenga kuchukua kabisa maeneo hayo?
Kulingana na afisa wa Marekani ambaye alizungumza na gazeti hilo, Putin alitaka kusitishwa kwa mapiganikatika maeneo hayo. Baadaye Urusi wataafikiana na Ukraine ni maeneo gani Ukraine itaachiwa.
Katika mazungumzo ya baadaye, Witkoff aliwaambia viongozi wa Ulaya kwamba kuna hatua mbili:
Ukraine iondoke kwenye baadhi ya maeneo ya Donetsk, kisha mstari wa mbele usimamishwe.
Kisha Trump na Putin wakubaliane kuhusu mpango wa mwisho wa amani, ambao baadaye utawasilishwa kwa Ukraine kwa mashauriano.
Ikulu ya White House ingeweza kufafanua hali hiyo, lakini walisema kwamba "kutokana na kuheshimu mazungumzo yetu nyeti ya kidiplomasia na Urusi, Ukraine na washirika wetu wa Ulaya, Ikulu ya White House haitazungumzia maelezo ambayo yanadaiwa kuonekana kwenye vyombo vya habari."
Lakini hadi sasa, hakuna upande uliotoa maelezo kamili kuhusu yaliyomo kwenye makubaliano hayo ya awali. Wote White House na Kremlin wamesalia kimya.
Masharti ya Ukraine na Ulaya

Chanzo cha picha, Lina Selg - Pool/Getty Images
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, hakusubiri muda mrefu kujibu. Kauli yake ilikuwa kuhusu kubadilishana maeneo ilikuwa inatarajiwa kwani amekuwa akisema hayuko tayari kupatiana ardhi yao.
"Majibu kuhusu ardhi ya Ukraine tayari yapo kwenye Katiba yetu. Hakuna mtu atakayeruhusiwa kutupoka ardhi yetu. Waukraine hawatakubali kamwe kumpa wavamizi hata kipande cha nchi yao."
Aliongeza kuwa:
"Tuko tayari kwa suluhisho la kweli linaloweza kuleta amani. Lakini lolote linalofanyika bila sisi ni kinyume na amani."
Na Ulaya pia imemuunga mkono kutokana na uamuzi wake.
Katika tamko la pamoja lililotiwa saini na viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Italia, Finland, Poland na Tume ya Ulaya, walisema wazi kwamba:
"Amani ya Ukraine haiwezi kupangwa bila Ukraine yenyewe."na kubadilisha mipaka inayojulikana kimataifa haiwezekani.''

Chanzo cha picha, WPA Pool/Getty Images
Makamu wa Rais wa Marekani J.D. Vance alihudhuria mkutano huo na alikabidhiwa msimamo wa Ulaya na Ukraine kwamba hawapingi kabisa mazungumzo ya kubadilishana maeneo, lakini ni lazima yafanyike kwa masharti makubwa.
Kwa mujibu wa Wall Street Journal, Ulaya na Ukraine waliwasilisha pendekezo mbadala kwa Marekani:
Kwanza, sitisho la mapigano liwe rasmi.
Kisha, mazungumzo ya "kubadilishana maeneo" yafanyike kwa masharti ya pande zote.
Kwa mfano, ikiwa Ukraine itaondoka kwenye baadhi ya maeneo ya Donetsk, basi Urusi nayo iondoke kwenye Kherson na Zaporizhia.
Lakini pia kuna masharti mengine magumu kama vile Ukraine kupewa dhamana za usalama za moja kwa moja, ikiwa ni pamoja na uanachama wa NATO.
Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, akihojiwa na ABC News alieleza kuwa inawezekana kutambua hali halisi ya udhibiti wa maeneo, lakini si kwa njia ya kisheria.
"Ukraine inapaswa kuwa huru kuchagua mustakabali wake, bila vizuizi vyovyote kutoka kwa Urusi au yeyote yule," alisema Rutte.
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, alisisitiza kuwa sheria za kimataifa haziwezi kuhalalisha uvamizi wowote.
"Makubaliano haya yasije yakawa kichocheo cha uvamizi mpya wa Urusi dhidi ya Ukraine, Ulaya, au ushirikiano wa Magharibi," alisema.
"Tunazungumzia juu ya eneo [la Ukraine]. Tunazungumza, kwa kweli, juu ya dhamana ya usalama, lakini pia juu ya hitaji kamili la kutambua kwamba Ukraine yenyewe inaamua mustakabali wake mwenyewe, kwamba Ukraine lazima iwe nchi huru ambayo huamua kwa uhuru mustakabali wake wa kijiografia bila shaka, bila vikwazo vyovyote juu ya ukubwa wa vikosi vyake vya silaha. Na kwa NATO bila vikwazo vyovyote juu ya uwepo wetu mashariki," Rutte alisema.
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, alisisitiza kuwa sheria za kimataifa haziwezi kuhalalisha uvamizi wowote.
Kulingana naye maeneo ya Ukraine ambayo yamedhibitiwa kwa muda na Urusi yanamilikiwa na Ukraine.
"Makubaliano haya yasije yakawa kichocheo cha uvamizi mpya wa Urusi dhidi ya Ukraine, Ulaya, au ushirikiano wa Magharibi," alisema haya siku ya Jumapili.
Kulingana na Bloomberg, viongozi wa Ulaya wanataka kuzungumza na Trump ana kwa ana kabla ya kukutana na Putin ili wajadiliane changamoto zilizopo.
Je, mkutano wa Alaska utakuwa ni ushindi wa Putin?
Ni vigumu kutafakari kuwa kuna mtu atafaidika zaidi kutokana na mkutano wa Alaska kama vile Vladimir Putin.
Kwa miaka mitatu na nusu, nchi za Magharibi, zikiongozwa na Marekani (angalau hadi Donald Trump aliporudi White House), zilifanya kila kitu kumtenga kiongozi huyo wa Urusi.
Kwa hivyo, bila kujali jinsi mkutano huo utamalizika Ijumaa, ukweli wa kusafiri kwenda Marekani kwa mwaliko wa Rais wa Marekani ni mafanikio makubwa kwa Kremlin.
Hasa kwa kuzingatia ishara inayohusishwa na eneo la mkutano huo: Alaska iliwahi kuwa eneo la Urusi.
Muktadha ambao mkutano huo unafanyika pia unaonekana mzuri kwa Moscow.
Wiki moja tu iliyopita, vyombo vya habari na wataalam walikuwa wakishangaa jinsi Trump angekuwa mgumu wakati alitoa uamuzi kwa Vladimir Putin.
Sasa hakuna anayekumbuka kauli hiyo ya mwisho.
Swali kuu ni iwapo Putin alikubali maafikiano yoyote kabla ya mkutano huo na iwapo Trump atazingatia msimamo wa Ukraine na washirika wake wa Ulaya.
Mkutano usio na ahadi na matokeo maalum ungefaa tu Putin katika hali hii.
Ni mapema mno kutoa hitimisho la mapema kuhusu ushindi wa mwisho wa Moscow.
Tumeona hali ya Donald Trump ikibadilika na kuwa kinyume mara kadhaa katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
Baada ya kumkemea Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika Ofisi ya Oval mwezi Machi, ilikuwa vigumu kufikiria kwamba majira ya joto hii Rais wa Marekani angekuwa akizungumza kuhusu jinsi alivyokatishwa tamaa na Vladimir Putin na kuahidi msaada wa kijeshi kwa Ukraine (ingawa kwa gharama ya Ulaya).
Na kinyume chake: ilionekana kutoridhika kwa Trump, ambayo iligeuka kuwa vitisho dhidi ya Kremlin, haikuweza kutulizwa.
Lakini baada ya ziara ya Steve Witkoff huko Moscow (wanasiasa na vyombo vya habari vya dunia bado vinaonekana kutoelewa alichokubaliana na Putin), hali ilibadilika tena.
Kwa hivyo mengi yatategemea hali ya Trump baada ya kuzungumza na Putin ana kwa ana huko Alaska.
*Mamlaka za Urusi zimejumuisha Elizaveta Foght katika rejista ya "mawakala wa kigeni". BBC inapinga vikali uamuzi huu na inaupinga mahakamani.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












