Putin: 'Tulitaka kuisaidia Iran katika ulinzi wa anga yao lakini ikapuuza'

Chanzo cha picha, Getty Images
Vladimir Putin amesema kuwa Iran haijaonyesha nia ya kushirikiana na Urusi katika mifumo ya ulinzi wa anga.
Siku ya Jumatano tarehe 18 mwezi Juni 2025 , Rais wa Urusi aliandaa kikao na wahariri wakuu wa mashirika ya habari, ambapo suala la vita vya Israel na Iran lilijadiliwa.
Kuhusu usaidizi kwa ulinzi wa anga wa Iran amesema: "Tuliwahi kutoa pendekezo kwa marafiki zetu wa Iran kwamba tushirikiane katika uga wa mifumo ya ulinzi wa anga, lakini washirika wetu hawakuonyesha nia kubwa wakati huo, na ndivyo ilivyokuwa."
Bw. Putin pia alisema: "Pendekezo letu lilikuwa kuunda mfumo kamili, sio uwasilishaji tofauti wa vifaa; mfumo mmoja.
Mwishowe, tulizingatia suala hili mara moja tu, lakini upande wa Iran haukuonyesha nia kubwa na suala hilo lilisitishwa.
Lakini kuhusu utoaji wa mifumo binafsi, ndio, bila shaka, tumewahi kufanya uwasilishaji huu katika siku za nyuma. Hii haina uhusiano wowote na tatizo la leo.
Hili ndilo jambo linaloitwa ushirikiano wa kijeshi na wa kimataifa katika nyanja ya kawaida ya ushirikiano wa sheria ya kimataifa .
Kuhusiana na mkataba wa kimkakati na Iran, Rais wa Russia alisema kwamba makubaliano hayo "hayana makubalinao yoyote yanayohusiana na nyanja ya ulinzi" na kwamba "marafiki zetu wa Iran hawajatuomba jambo kama hilo. Kwa hivyo hakuna chochote cha kujadili.
Nakala ya mkataba wa kimkakati kati ya Iran na Russia, ambayo ilianza kutekelezwa katika nchi zote mbili mwaka huu, imechapishwa.
Mkataba huo unajumuisha ushirikiano katika nyanja za kijeshi na usalama, lakini hauna vifungu vya ulinzi, na maafisa wa pande zote mbili wamesisitiza suala hili.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Andrei Rudenko alisema kuwa Moscow haitatoa msaada wa kijeshi kwa Iran iwapo vita vitazuka kati ya Iran na Marekani.
"Katika hali kama hiyo, Urusi hailazimiki kutoa msaada wa kijeshi," Bw. Rudenko aliwaambia manaibu mnamo Aprili 8 mwaka huu, wakati mkataba huo ulipoidhinishwa katika bunge la chini la Urusi (Duma), kulingana na shirika la habari la TASS.
Mfumo wa ulinzi wa anga wa S-300

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mnamo Septemba 2011, Brigedia Jenerali Farzad Esmaili, ambaye wakati huo alikuwa kamanda wa Kituo cha Ulinzi cha Anga cha Khatam Al-Anbiya, alitangaza muundo na ujenzi wa mfumo wa ndani unaofanana na mfumo wa anga wa S-300, badala ya toleo la Kirusi.
Mnamo 2007, Iran ilisaini mkataba na serikali ya Urusi kununua mfumo huu na kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Irani kutumia makombora ya mfumo wa nga wa S-300.
Ingawa idadi ya wanajeshi wa Iran walitumwa Urusi kwa mafunzo, hakukuwa na habari yoyote ya kuhamishiwa kwa vifaa vya mfumo wa makombora kwenda Iran.
Brigedia Jenerali Esmaili alisema wakati huo Iran ilitekeleza masharti yote ya mkataba na kwamba mfumo huo ulipaswa kukabidhiwa, lakini "kutokana na uovu wa serikali za Magharibi, hili halikufanyika."
Takriban mwaka mmoja kabla ya matamshi hayo, Bw. Putin alikuwa ametia saini sheria inayotekeleza azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu vikwazo vya silaha kwa Iran, kupiga marufuku utekelezaji wa mkataba huu na kuwasilisha vifaa vya mfumo wa makombora wa anga wa S-300 kwa Jamhuri ya Kiislamu.
Israel na Marekani walikuwa miongoni mwa wapinzani kuhusu kuwasilishwa kwa mfumo huo wa ulinzi wa anga wa S-300 kwa Iran, kwani waliamini kuwa Iran ingetumia mfumo huu wa ulinzi wa anga kulinda vifaa vya nyuklia na kuendeleza mpango wake wa kurutubisha madini ya uranium.
Wakati Urusi ilipokataa kuwasilisha mfumo wa ulinzi wa anga wa S-300 kwa Iran, Aprili 2012, Ahmad Vahidi, Waziri wa Ulinzi wa wakati huo, alitangaza kwamba mpango wa kujenga mfumo wa ulinzi kuchukua nafasi ya S-300 ulikuwa kwenye ajenda, na hatimaye mwaka wa 2020, mfumo wa "Bavar-373" wa Iran ulitambulishwa kama "Iranian S-300".
Mnamo Agosti 2015, shirika la habari la Interfax la Urusi liliripoti mkataba mpya wa kuwasilisha mifumo ya ulinzi ya S-300 kwa Iran, lakini maelezo ya mkataba huo hayakuchapishwa, na katika mwaka huo huo, Vladimir Putin, wakati akiondoa marufuku ya kuuza S-300 kwa Iran, alisema kuwa "Urusi haiwezi kuwasilisha mfumo huu wa ulinzi kwa Iran kwa kasi ambayo Iran inatazamia."
Mfumo wa S-300 hatimaye ulifika Iran bila tangazo rasmi na ulizinduliwa kwa mara ya kwanza mnamo Aprili 2016 kwenye gwaride la jeshi karibu na kaburi la Ayatollah Khomeini.
Mfumo wa S-300 ulipowasili Iran baada ya miaka 10, wengi walihoji kwa nini Iran haikununua mfumo wa kisasa zaidi wa S-400.
Abbasali Mansouri Arani, mshirika wa zamani wa kijeshi wa Iran nchini Saudi Arabia na mjumbe wa zamani wa Kamisheni ya Usalama ya Kitaifa na Sera ya Kigeni, alisema: "Sio lazima kwamba S-400 ina uwezo mkubwa zaidi kwa nchi yetu kuliko S-300," na Esmail Kowsari, mkuu wa Kamati ya Ulinzi ya Bunge la Tisa, pia alisema: "S-400s ni bora zaidi ya mfumo wa ulinzi wa S-300, lakini tofauti kati ya mifumo hii miwili ni ndogo sana na hatuhitaji sana mfumo wa S-400 leo."
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












