Je, Marekani inajiandaa kuishambulia Iran?

S

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Katikati ya mvutano unaoendelea kati ya Israel na Iran, shughuli zisizo za kawaida za kijeshi za Marekani zimezua maswali mengi kuhusu uwezekano wa Washington kujiandaa kwa mashambulizi makubwa dhidi ya Tehran.

Takwimu za ufuatiliaji wa ndege zilizochambuliwa na BBC zimeonesha kuwa angalau ndege 30 za kijeshi za Marekani zimetoka kambi zao nchini Marekani kuelekea Ulaya ndani ya siku tatu zilizopita.

Ndege hizi ni ndege za kijeshi za Marekani zinazotumika kujaza mafuta ndege za kivita na mabomu. Kwa mujibu wa Flightradar24, angalau saba kati ya ndege hizi zote zikiwa aina ya KC-135 zilisimama katika kambi za anga za Marekani nchini Hispania, Scotland, na Uingereza.

Safari hizi za ndege zinakuja wakati Israel na Iran zikiendelea kurushiana mashambulizi, baada ya Israel kuanzisha operesheni Ijumaa ambayo ilisema ililenga kuharibu mpango wa nyuklia wa Tehran.

Ingawa haijabainika wazi kama harakati hizi za Marekani zimeunganishwa moja kwa moja na mzozo huo, mtaalam mmoja aliiambia BBC Verify kuwa safari hizo za ndege za kujaza mafuta zilikuwa "zisizo za kawaida."

Justin Bronk, mchambuzi mkuu katika taasisi ya Royal United Services Institute (Rusi), alisema kuwa kupelekwa kwa ndege hizo kuna "ashiria wazi" kuwa Marekani inaweka mipango ya dharura ya "kusaidia operesheni kali za kijeshi" katika eneo hilo katika wiki zijazo.

d

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ndege aina ya KC-135

Ndege saba zilizofuatiliwa na BBC zimeendelea na safari zao, na kwa mujibu wa takwimu za ufuatiliaji wa ndege, zilionekana zikiruka mashariki mwa Sicily kufikia Jumanne mchana. Sita hazikuwa na eneo maalum la kuelekea moja ilitua kwenye kisiwa cha Ugiriki cha Crete.

Hata hivyo, aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Ulinzi cha Ireland, Makamu Admeli Mark Mellett, alisema kuwa harakati hizo zinaweza kuwa sehemu ya sera pana ya "kutokuwa wazi kimkakati" ambayo inaweza kuwa inajaribu kuishawishi Iran kutoa masharti katika mazungumzo juu ya mpango wake wa nyuklia.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Harakati za ndege hizi zinakuja huku kukiwa na ripoti kwamba Marekani pia imehamisha meli kubwa ya kubebea ndege za kivita, USS Nimitz, kutoka Bahari ya Kusini ya China kuelekea Mashariki ya Kati. Shirika la habari la Reuters liliripoti kuwa tukio lililopangwa lililohusisha meli hiyo nchini Vietnam lilihairishwa baada ya kile ubalozi wa Marekani huko Hanoi ulichokiita "hitaji la kiutendaji la dharura."

MarineTraffic, tovuti ya kufuatilia meli, ilionesha kuwa eneo la mwisho la USS Nimitz lilikuwa katika Mlango wa Malacca ikielekea Singapore mapema Jumanne. Meli ya Nimitz hubeba ndege za kivita na husindikizwa na meli kadhaa za kuharibu makombora.

Marekani pia imehamisha ndege za kivita aina ya F-16, F-22, na F-35 kwenda kambi za Mashariki ya Kati, maafisa watatu wa ulinzi waliiambia Reuters Jumanne. Ndege za kujaza mafuta zilizohamishwa kwenda Ulaya siku chache zilizopita zinaweza kutumika kujaza mafuta ndege hizi.

Mapema Jumanne, Makamu wa Rais JD Vance alidokeza kuwa Marekani inaweza kuingilia kati kusaidia kampeni ya Israel, akiandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba Trump "anaweza kuamua anahitaji kuchukua hatua zaidi" kumaliza mpango wa nyuklia wa Iran.

Inaaminika kuwa Tehran ina vituo viwili vikuu vya kurutubisha urani chini ya ardhi. Natanz tayari imeshambuliwa na Israel, na Fordo imezikwa ndani kabisa ya mlima karibu na mji wa Qom. Ili kupenya kituo hicho, Marekani ingeweza kutumia makombora ya GBU-57A/B Massive Ordnance Penetrator (MOP), maafisa wawili wakuu wa kijeshi wa Magharibi waliiambia BBC Verify.

MOPs ni mabomu makubwa, yenye uzito wa pauni 30,000 (kilo 13,600) pia yanayojulikana kama "bunker busters." Bomu hili ni silaha pekee ya kawaida ya aina yake ambayo inaaminika kuwa na uwezo wa kupenya hadi futi 200 (mita 60) za saruji. Ni ndege ya kivita ya siri aina ya B-2 pekee ndiyo inayoweza kubeba silaha hizo.

a

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ripoti zinasema Trump ameidhinisha mpango wa kushambulia Iran lakini hajafanya uamuzi wa mwisho.

Hivi karibuni, Marekani imekuwa na kikosi cha ndege za B-2 katika kambi yake kwenye kisiwa cha Diego Garcia. Ingawa kisiwa hicho kiko umbali wa maili 2,400 kutoka pwani ya kusini ya Iran, eneo lao huko Diego Garcia lingewaweka vizuri ndani ya eneo la mashambulizi ya Iran.

"Ungeweza kudumisha operesheni endelevu kutoka Diego Garcia kwa ufanisi zaidi," Luteni Jenerali wa Anga Greg Bagwell, aliyekuwa naibu mkuu wa operesheni wa RAF – aliiambia BBC Verify. "Zinaweza kufanya kazi saa nzima."

Picha za satelaiti zilionyesha kwa mara ya kwanza ndege za B-2 zikiwa zimepangwa Diego Garcia mwishoni mwa Machi, lakini picha za hivi karibuni zaidi kutoka kisiwa hicho hazioneshi tena ndege hizo.

Makamu Admeli Mellett alisema angetarajia kuona ndege hizo kwenye kisiwa hicho kabla ya operesheni yoyote inayolenga Iran na alitaja kutokuwepo kwa ndege hizo ni kama "kipande kilichokosekana cha fumbo." Luteni Jenerali wa Anga Bagwell alikubali. Lakini alibainisha kuwa ndege za B-2 zimejulikana kufanya kazi kwa masaa 24 kwa wakati mmoja na zinaweza kuruka kutoka bara la Marekani ikiwa Ikulu ya White House itaamua kuanzisha shambulizi.

"Wameondoa njia yoyote kwa Iran kujilinda, jambo ambalo bila shaka linaacha malengo yoyote ya kijeshi au hata ya nyuklia kwenye huruma ya kile Israel inataka kuifanyia Iran."

Ripoti zinasema Trump ameidhinisha mpango wa kushambulia Iran lakini hajafanya uamuzi wa mwisho.