Trump alivyogundua Putin hana 'uswahiba' inapofika maslahi ya Urusi

s

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Na Sammy Awami
    • Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Rais wa Marekani Donald Trump ameamua kuiuzia Ukraine silaha za kukabiliana na makombora ya Urusi pamoja na kushambulia pia vikosi vya Urusi. Vifaa hivi vitalipiwa na nchi za Ulaya.

Haya ni mabadiliko makubwa katika msimamo wa Trump dhidi ya ushiriki wa Marekani katika vita vya Urusi na Ukraine.

"Nimefedheheshwa sana na Rais Putin, kwa sababu nilidhani kwamba tungekuwa tumefikia makubaliano miezi miwili iliyopita" alisema Trump wiki iliyopita.

Kwa muda mrefu, Trump amekuwa akiulaumu utawala wa mtangulizi wake Joe Biden kwamba ulichochea zaidi vita hiyo, uliidekeza Ukraine kwa kuipa silaha nyingi hata kufilisi akiba ya Marekani.

Trump ameelekeza lawama zake pia kwa Rais Volodymyr Zelenskyy na nchi za Ulaya kwamba hawakulichukulia kwa dhati suala la kusitisha vita, kuokoa maelfu ya wanajeshi wanaouwawa kila siku na hatari ya kuipoteza nchi ya Ukraine kwa Urusi.

"Unacheza na Vita ya Tatu ya Dunia" Trump alimwambia Zelensky mwezi Februari alipokwenda kumtembelea Ikulu ya White House, akiongeza kwamba Zelensky ameshindwa kuiheshimu Marekani kwa msaada mkubwa ambao hakustahili.

a

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mwanzoni mwa vita ya Ukraine, wakati wa utawala wa Rias Joe Biden, Marekani ilikuwa msaada mkubwa wa silaha kwa Ukraine, lakini tangu kuingia kwa Trump, uswahiba wake na Putin ulipunguza kasi ya misaada.

Wakati Trump akiwalaumu wote hawa, alikuwa na matumaini makubwa na Rais Vladimir Putin wa Urusi. Wachambuzi na vyombo vya habari kadhaa vya Marekani vilienda mbali hata kudai kwamba Trump alikuwa anampenda Putin, na kwamba alikuwa shabiki yake.

Tofauti na desturi ya viongozi wengi wa Marekani, huko nyuma Trump amewahi kumsifu Putin kama mtu mwenye akili sana na mjanja. Mara kadhaa pia ameelezea uwezekano wa kuwa rafiki yake wa karibu.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Nadhani naweza kuelewana vizuri sana na Vladimir Putin. Nahisi hivyo tu" alisema Trump mwezi Julai 2015 muda mfupi kabla hajaanza kampeni zake za Urais.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka jana, mara kadhaa Trump alijigamba kwamba akiingia madarakani hayatapita masaa 24 atakuwa ameutatua mgogoro wa Urusi na Ukraine. Mwezi Januari, Trump alisema kama angekuwa madarakani wakati wa Biden, hiyo vita hata isingeanza kabisa.

Hii imekuwa kinyume na misimamo ya viongozi wengi wa Marekani. Nchi hiyo na Urusi imekuwa na uhusiano wa kuviziana, na hasa dhidi ya kiongozi wake Vladimir Putin. Wamekuwa wakimuona kama dikteta anayetesa na kuwadhuru wapinzani wake na asiyependa demokrasia kwa wananchi wake kwa ujumla.

Marekani - na hata Ulaya pia – imekuwa inaamini kwamba anachokitaka Putin kwa nchi ya Ukraine ni kuiweka chini ya himaya ya Urusi, na hata kuufufua umoja wan chi za Kisovieti.

Lakini Trump amekuwa akimuona Putin kama mtu asiyeeleweka tu na kwamba yeye anajua namna ya kuhusiana nae kupata matokeo yatakayonufaisha maslahi ya Marekani.

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Trump (kulia) akiwa na Putin

Kwa ujumla, Trump anasifiwa angalau kwa kuanzisha mazungumzo ya kutafuta amani katika mgogoro huo kati ya Urusi na Ukraine. Hata hivyo Putin ameonekana kupiga chenga kufikia makubaliano ili kusitisha mapigano.

Kwa mfano, Urusi ilikubali mapendekezo ya awali ya kusitisha mapigano yaliyotolewa na Trump mwezi Machi mwaka huu, lakini ikaweka masharti kwamba nchi za Magharibi zisitishe msaada wa vifaa na intelijensia kwa Ukraine

Mara nyingine, Urusi ilikubali kufikia suluhisho la mgogoro huo, lakini ikatoa masharti kwamba mzizi wa vita hiyo ushughulikiwe. Changamoto ni kwamba mtazamo wa nchi za Magharibi na Urusi juu ya mzizi wa mgogoro huo unatofautiana kabisa.

Wakosoaji wa Urusi walikuwa wakisema kwamba chenga hizi ambazo Putin alikuwa anapiga, alikuwa anacheza na muda kujiimarisha kijeshi na kuishambulia Ukraine. Hata hivyo, Trump alikuwa ana matumaini kwamba angepata namna ya kumshawishi Putin kusitisha vita – hasa kupitia makubaliano ya kibiashara.

Baada ya danadana zote hizi, inaonekana Trump amegundua kwamba Putin si mtu aliyekuwa anamdhani

"Nimefadhaishwa sana na Rais Putin, nilidhani alikuwa mtu anayemaanisha anachosema. (Mchana) atazungumza kwa maneno mazuri sana, halafu usiku atawapiga mabomu watu. Hatupendi vitu vya hivyo" amesema Trump

Trump sasa ameipa Urusi siku 50 kuhakikisha kwamba inafikia makubaliano ya kusitisha mapigano au lah, itaiongezea ushuru wa biashara mara mia. Si watu wengi wana matumaini kwamba Urusi itafikia makubaliano kufikia hiyo mwishoni mwa Agosti. Badala yake, wengi wanaamini kwamba Putin atatumia muda huu kujijenga kijeshi na kuidhoofisha Ukraine.