Trump: 'Mimi ni mkali zaidi kwa Urusi kuliko kwa Iran'

mm

Chanzo cha picha, AFP

Muda wa kusoma: Dakika 3

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa amefanya mazungumza na Rais Vladimir Putin kuhusu vikwazo anavyoweza kuwekewa katika mazungumzo yao ya simu.

Akiwa kwenye ndege ya Air Force One, aliwaambia waandishi wa habari, "Nimekuwa mkali zaidi kwa Urusi kuliko nilivyo kwa Iran. Na kuliko nilivyo kwa nchi nyingine yoyote. Mpaka sasa tumeelewana vizuri kuhusu vikwazo, na anaelewa kwa nini vinaweza kuwekwa. Yeye ni mtaalamu," Trump ameeleza

Hata hivyo Trump amekuwa akikosolewa kwa kulegeza msimamo kwa Moscow, ameongeza kusema kuwa uvumilivu wake unaweza kuisha.

Pia unaweza kusoma:
mm

Chanzo cha picha, Getty Images

Rais huyo wa Marekani alisema anafikiria kuweka vikwazo vipya dhidi ya Urusi baada ya kukatishwa tamaa na mazungumzo ya hivi karibuni na Putin kuhusu vita vya Ukraine.

"Nilivunjika moyo sana na mazungumzo yangu na Rais Putin. Anataka kwenda mbali mno, kuendelea tu kuua watu, hiyo haikubaliki," Trump aliwaambia waandishi wa habari akiwa safarini ndani ya Air Force One.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Mazungumzo kati ya Trump na Putin yalifanyika Julai 3.

Trump alisema alijadili vita vya Ukraine na Putin, pamoja na hali ya Iran.

Donald Trump alieleza kuwa hakuwa amepata mafanikio yoyote kuhusu kusitisha mapigano nchini Ukraine.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Trump alisema pia amezungumza na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz kuhusu ombi la Ukraine la makombora ya Patriot lakini hakuna uamuzi wowote uliotolewa wa kupeleka makombora hayo ya hali ya juu.

Baada ya kuzungumza na Putin, Trump alizungumza na Zelensky Julai 4, lakini kuna taarifa chache rasmi kuhusu mazungumzo hayo.

"Tulijadili njia za ulinzi wa anga na tukakubaliana kuwa tutafanya kazi ya kuimarisha ulinzi wa anga," Zelensky aliandika katika telegram baada ya mazungumzo hayo.

Chombo cha habari cha Marekani Axios kiliripoti, kikinukuu vyanzo ambavyo havikutajwa jina, kwamba Trump alizungumza kwa simu na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky iliyodumu kwa takriban dakika 40 na kwamba Trump alimwambia Zelenskiy ataangalia ni silaha gani za Marekani zinazopaswa kupelekwa Ukraine, ikiwa kuna zile zilizositishwa.

Zelensky, katika hotuba yake ya kila usiku ya video, alisema yeye na Trump walikubaliana "kupanga mkutano kati ya timu zetu ili kuimarisha ulinzi wa anga.

"Tulikuwa na mjadala wa kina sana juu ya uzalishaji wa pamoja. Tunauhitaji, Marekani inauhitaji."

Urusi imefanya mashambulizi makubwa zaidi ya ndege zisizo na rubani katika mji mkuu saa chache baada ya mazungumzo ya Trump na Putin siku ya Alhamisi.

Zelenskiy aliita shambulio hilo "lenye kukusudiwa na lisilo na maana."