Kwa nini Urusi haiisaidii Iran dhidi ya Israel? Je, haitaki au haiwezi?

a

Chanzo cha picha, AFP

    • Author, Ksenia Gogitidze
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Vita vipya huko Mashariki ya kati vinaweza kubadili ramani ya eneo lisilo tulivu zaidi duniani, ambapo Urusi imekuwa mhusika mkuu kwa muda mrefu. Msimamo wa Urusi ulikuwa tayari umedhoofishwa na kuanguka kwa Bashar al-Assad nchini Syria na vita nchini Ukraine. Sasa, ikiwa vita vya Israel na Iran vitasababisha kuyumba au kuanguka kwa nchi ambayo Vladimir Putin aliiita "mshirika mkakati" wa Urusi miezi sita tu iliyopita, Moscow inahatarisha pigo jingine kwa uaminifu wake.

Hivi sasa hakuna dalili za kumalizika kwa vita hivi, na kuna hatari kwamba Marekani pia itaingia, jambo ambalo lingebadili mzozo huu wa kikanda kuwa vita vya kimataifa na uwepo wa jeshi lenye nguvu zaidi duniani. Wakati huo huo, Urusi kwa sasa inaridhika na hatua za kidiplomasia na haina haraka kutoa msaada wa kijeshi kwa mshirika wake na jirani yake ng'ambo ya Bahari ya Caspian. Kwa nini?

Wataalamu wanasema, kwanza, kwa sababu hataki, na pili, kwa sababu hawezi.

Urusi imeingilia moja kwa moja katika mzozo wa Mashariki ya kati mara moja tu, nchini Syria. Katika hatua nyingine, imetegemea diplomasia na kutoegemea upande wowote, na kuna uwezekano mkubwa itafanya hivyo tena wakati huu. Kremlin imekuwa ikidai kucheza katika nafasi ya upatanishi, ikisisitiza kuwa Urusi ndio nchi pekee yenye nguvu ambayo pande zote zinazopigana katika eneo hilo ziko tayari kuzungumza nayo.

Lakini uaminifu wa Urusi kama mshirika anayetegemewa sasa unahojiwa. Fabrice Balanche, mtaalamu wa Mashariki ya kati katika Taasisi ya Washington, aliiambia BBC: "Miezi sita iliyopita, Urusi haikuja kusaidia utawala uliodhoofika nchini Syria, wa Bashar al-Assad. Vivyo hivyo, haioni sababu ya kuisaidia Iran iliyodhoofika sasa."

"Zaidi ya hayo, Urusi haitaki kuibuka kwa nguvu mpya ya nyuklia," anasema.

urusi

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Urusi na Iran zimetia saini "mkataba wa kina wa kimkakati," lakini tofauti kati ya nchi hizo mbili bado zinaendelea.

Kremlin haina haraka ya kudhoofisha uhusiano wake na watawala wa Ghuba au kukata uhusiano wake na Israel. Maafisa wa Urusi tayari wanatathmini hatari ya kuanguka kwa utawala wa Iran na wanazingatia jinsi ya kushirikiana na serikali mpya ikiwa Maayatullah wataangushwa.

Jukumu la mwangalizi au mpatanishi kwa sasa linafaa sana kwa Putin. Vita vimeongeza bei ya mafuta, ambayo ni bidhaa kuu ya Urusi inayouzwa nje. Kwa kuongeza, kulingana na Hannah Note, mtaalamu katika Kituo cha James Martin cha Mafunzo ya kutokukua kwa silaha za nyuklia (James Martin Center for Nonproliferation Studies), mzozo katika eneo muhimu lenye mitambo ya nyuklia unatoa tahadhari ya jumuiya ya kimataifa na vyombo vya habari kutoka kwa uchokozi wa Urusi nchini Ukraine.

"Putin anataka kujionyesha kwa Wamarekani kama mpatanishi na mzungumzaji juu ya masuala ya kimataifa na kuzungumza juu ya chochote isipokuwa Ukraine," aliiambia BBC. Hata hivyo, Donald Trump hadi sasa amekataa mapendekezo ya Putin. "Alijitolea kupatanisha," Trump alisema Jumatano. "Nilimwambia, 'Tafadhali, kwanza tatua matatizo yako mwenyewe. Anza Urusi (na Ukraine) iwe sawa, ndipo labda unaweza kuwa na wasiwasi juu ya hili (vita vya Iran-Israel.'"

Urusi ina njia chache za kuleta athiri

a

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Iran iliisaidia Urusi kwa kuipa ndege zisizo na rubani (drones) mwanzoni mwa vita yake na Ukraine.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati huo huo, Urusi ina mengi ya kupoteza: kuipoteza Iran kutakuwa pigo kubwa kwa Moscow katika eneo hilo na kudhoofisha zaidi msimamo wake katika Mashariki ya Kati. Lakini kadiri vita vinavyoendelea, bado kuna nafasi ya kufanya jambo: Ikiwa ofa ya upatanishi ya Kremlin itakubaliwa, Putin ataweza kujionyesha kama mpenda amani, hata kama anajishughulisha na vita nchini Ukraine.

"Ikiwa Urusi itapewa jukumu la upatanishi, haitaongeza tu msimamo wake kama nchi yenye nguvu duniani inayohusika katika kutatua migogoro, bali pia itaondoa tahadhari kuhusu vita nchini Ukraine," alisema Anna Borshevskaya, mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya Washington kwa Sera ya Mashariki (Washington Institute for Near East Policy).

Lakini si Israel wala Iran hawajazungumza juu ya amani, na kwa pande zote mbili, duru mpya ya makabiliano ni vita vitakavyoishi. Jinsi hali ya upatanishi ya Putin ilivyo halisi bado haijabainika, kutokana na kwamba nchi za Ulaya zimeweka wazi kwamba hawataki kumwalika rais mchokozi kwenye meza ya mazungumzo.

Hanna pia anathibitisha kwamba Urusi haina njia zozote za karibu za kuathiri mwenendo wa vita. Moscow itaendelea kutoa wito mkubwa wa mazungumzo na suluhisho la kidiplomasia la mivutano, lakini mwisho wa mzozo hautategemea maamuzi ya Urusi.

"Kwa kweli, Urusi haitakuwa sababu kuu kuhusu lini, vipi, na chini ya masharti gani makabiliano kati ya Iran na Israel yataisha," mtaalamu anasema.

Sasa kadi zote za turufu ziko mikononi mwa Donald Trump. Wakati Urusi ikijitolea kupatanisha, Israel inamwomba rais wa Marekani asaidie kuikabili Iran moja kwa moja.