Je, Marekani imeipa Ukraine msaada wa kijeshi kiasi gani?

Wanajeshi wa Ukraine watumia silaha ya milimita 105 ya kivita ya Marekani M101 Howitzer kwenye mstari wa mbele wa Ukraine wa kaskazini mashariki na Urusi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Ukraine watumia silaha ya milimita 105 ya kivita ya Marekani M101 Howitzer kwenye mstari wa mbele wa Ukraine wa kaskazini mashariki na Urusi.
    • Author, Tom Edgington Na Nick Eardley
    • Nafasi, BBC Verify
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Ziara ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya White House kwa mazungumzo yenye lengo la kumaliza vita imeweka kiwango cha uungaji mkono wa Marekani (Marekani) kwa Ukraine chini ya uangalizi tena.

Rais Donald Trump amekosoa kiwango cha misaada inayotolewa na Marekani ikilinganishwa na mchango wa Ulaya.

Lakini takwimu alizozitaja haziungwi mkono na ushahidi.

BBC Verify imekuwa ikichunguza kwa makini ni kiasi gani Marekani imetumia tangu Urusi ilipovamia Ukraine kikamilifu Februari 2022 na jinsi inavyolinganishwa na mchango wa Ulaya.

Pia unaweza kusoma:

Je, Marekani imetumia kiasi gani kwa jumla?

Marekani imetumia jumla ya dola 130.6bn (£98.9bn) kati ya tarehe 24 Januari 2022 na 30 Juni 2025, kulingana na Taasisi ya Kiel, taasisi yenye makao yake makuu Ujerumani inayofuatilia uungwaji mkono wa kimataifa kwa Ukraine.

Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, Marekani imekuwa ikiongoza kwa kutoa msaada wa kijeshi na kifedha kwa Ukraine.

Sasa, Wizara ya Ulinzi ya Marekani imetoa takwimu mpya zinazoonyesha kuwa tayari imetenga zaidi ya dola bilioni 184 kusaidia juhudi hizi hasa kwa mafunzo ya kijeshi barani Ulaya na kujaza tena akiba ya vifaa vya kijeshi vilivyotumika.

Lakini kiasi hicho kinahesabiwa hadi Machi 2025 tu si takwimu za sasa kabisa na ni juu zaidi kuliko makadirio ya Taasisi ya Kiel, taasisi huru inayofuatilia misaada ya kimataifa kwa Ukraine.

BBC Verify timu maalum ya uchunguzi wa habari imeomba wizara za Marekani kutoa takwimu mpya zaidi.

Trump alidai nini hapo awali?

Mwezi Februari, Donald Trump, alipokutana na Rais Macron wa Ufaransa, alidai kuwa:

"Marekani imetumia zaidi ya dola bilioni 300, lakini Ulaya imetoa karibu bilioni 100 tu hiyo ni tofauti kubwa sana."


Rais Macron alikaa karibu na Rais Trump katika Ofisi ya Oval

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais Macron alikaa karibu na Rais Trump katika Ofisi ya Oval

Lakini kwa mujibu wa takwimu rasmi, dai hilo halilingani na ukweli.

BBC Verify imegundua Marekani bado haijafikia matumizi ya dola bilioni 300.

Kwa hivyo, kauli ya Trump haikuwiana na hali halisi na hiyo bado haijabadilika baada ya miezi sita.

Je, matumizi ya Marekani yanalinganishwa vipi na yale ya Ulaya?

Hili ni swali muhimu.

Ukweli ni kwamba Marekani, kama nchi moja, ndiyo inayotoa msaada mkubwa zaidi kwa Ukraine.

Lakini kama ukiangalia Ulaya kwa pamoja ikijumuisha nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya na baadhi ya nchi zingine basi Ulaya ndiyo inayoongoza.

Haya ni kwa mujibu wa Taasisi ya Kiel.

Kwa mfano, kutoka Januari 2022 hadi Juni 2025, Ulaya imetoa zaidi ya dola bilioni 165 kwa Ukraine, wakati Marekani imetoa karibu dola bilioni 130 katika kipindi hicho hicho.

Idadi hiyo inajumuisha misaada ya moja kwa moja kutoka Umoja wa Ulaya (EU), lakini pia kutoka kwa mikataba baina ya nchi za Ulaya, ndani na nje ya EU.

Msaada huu unahusisha silaha, fedha taslimu na misaada ya kibinadamu kama chakula, makazi na dawa.

Je, Ulaya itarejeshewa fedha zake ilhali Marekani hairejeshewi?

Trump amedai kuwa Ulaya itarejeshewa fedha zake kwa sababu misaada yao ni ya mkopo, tofauti na Marekani inayotoa msaada kama ruzuku (yaani, hauna ulazima wa kurejeshwa).

Katika mkutano huo wa Februari, Rais Macron alimwambia Trump kuwa pande zote mbili Ulaya na Marekani zimechanganya misaada ya ruzuku na mikopo.

Taasisi ya Kiel inakubaliana na hili: Marekani imekuwa ikitoa zaidi kwa njia ya ruzuku, huku Ulaya ikitoa kiasi kikubwa kupitia mikopo.

Hata hivyo, mikopo hiyo ya EU imekuwa na masharti nafuu sana na wakati mwingine, Ukraine haitarajiwi kulipa chochote.

Kufikia Julai 18, EU inasema wanachama wake wametoa takriban dola bilioni 180 hadi sasa, huku mikopo ikiwa ni asilimia 35% ya jumla.

Baadhi ya marejesho yanatarajiwa kutoka kwenye mali za Urusi zilizogandishwa na mataifa ya Magharibi.

Kwa hivyo, tunaweza kusema wazi kuwa msaada kwa Ukraine ni mchanganyiko wa mikopo na ruzuku kutoka pande zote mbili.

Uingereza imetoa kiasi gani kwa Ukraine?

Mnamo tarehe 1 Machi, wakati wa ziara ya Rais Zelensky jijini London, Uingereza ilisaini makubaliano ya mkopo wa dola bilioni 2.8.

Hadi mwishoni mwa Julai, Uingereza ilikuwa imetoa jumla ya dola bilioni 29.5 kwa Ukraine karibu dola bilioni 17 kati ya hizo zikiwa ni msaada wa kijeshi.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Kiel, nchi pekee zilizotoa zaidi ni Marekani na Ujerumani.

Hata hivyo, mchango wa Uingereza bado ni mdogo ukilinganisha na wa Marekani.

Inaibua swali kubwa.

Ikiwa Marekani itaamua kupunguza misaada yake au kujiondoa kabisa je, mataifa ya Ulaya yanaweza kuziba pengo hilo?

Jibu, kwa sasa, linaonekana kuwa hapana isipokuwa Ulaya itoe msaada mkubwa zaidi kuliko inavyofanya sasa.

BBC Verify banner
Mada zinazohusiana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid