Mambo muhimu katika mazungumzo ya Trump na Zelensky huko Washington

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Bernd Debusmann Jr & Laura Gozzi
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Rais Volodymyr Zelensky amerejea White House siku ya Jumatatu kukutana na Rais wa Marekani Donald Trump kwa mazungumzo mapya yenye lengo la kumaliza vita nchini Ukraine.
Viongozi kadhaa wa Ulaya pia walisafiri kwa ndege hadi Washington kuhudhuria mkutano huo, siku chache baada ya Trump kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin huko Alaska kwa mkutano ambao haukufanikiwa kuleta usitishaji vita.
Licha ya maneno ya matumaini ya Trump na tathmini isiyo na matumaini kutoka kwa washirika wake wa Ulaya, kufikia Jumatatu jioni hakukuwa na ahadi madhubuti ya usalama au hatua za kufikia makubaliano ya amani.
Putin na Zelensky kukutana?
Kufuatia mkutano huo, Trump alichapisha taarifa kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social kwamba amempigia simu Putin ili kuanza kupanga mazungumzo kati ya kiongozi huyo wa Urusi na Zelensky.
Trump amesema mkutano wa wawili hao utafanyika katika eneo litakaloamuliwa, utakuwa mkutano wa pande tatu, ambapo rais wa Marekani ataungana nao.
Mshauri wa Putin amesema Trump na Putin walizungumza kwa dakika 40 kwa simu siku ya Jumatatu.
Kabla ya viongozi wa Ulaya kuketi na Trump katika chumba cha Ikulu ya White House, kulikuwa na mazungumzo kati ya kiongozi huyo wa Marekani na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
"Naamini anataka kufanya makubaliano. Naamini anataka kufanya makubaliano kwa ajili yangu. Unaelewa?" Trump alimwambia Macron, akimzungumzia rais Putin.
Ni jambo la kusubiri kuona maadui wawili wakikutana uso kwa uso kwenye meza ya mazungumzo kwa mara ya kwanza tangu uvamizi wa Urusi uanze Februari 2022.
Kwa miezi kadhaa, Zelensky amekuwa akishinikiza kukutana na Putin, ingawa hii inawezekana ilikuwa njia ya kuthibitisha hoja yake kwamba Urusi haiko tayari katika kutafuta amani, kwani aliamini Kremlin haikuwa na nia ya mkutano kama huo.
Moscow imekataa mara kwa mara wazo la Putin na Zelensky kukaa chini katika meza ya mazungumzo.
Lakini taarifa ya mshauri wa Putin wa masuala ya nje, Yuri Ushakov siku ya Jumatatu usiku ilisema, "inafaa kutazama uwezekano wa kuongeza idadi ya wawakilishi katika ujumbe wa Urusi na Ukraine katika mazungumzo.”
Msimamo wa Ulaya

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Trump alionekana kutupilia mbali hitaji la kusitisha mapigano kabla ya mazungumzo ya kumaliza vita kufanyika.
Hapo awali, hilo lilikuwa takwa kuu la Ukraine, ambayo iliweka wazi kwamba inaona kumalizika kwa mapigano kama sharti la mazungumzo zaidi na Urusi na, hatimaye, kupatikana suluhu ya muda mrefu.
Usitishaji mapigano unaweza pia kuwa rahisi zaidi kuafikiwa kuliko makubaliano kamili ya kupata amani ya kudumu, ambayo yatachukua miezi mingi ya mazungumzo, katika kipindi ambacho mashambulizi ya Urusi kwa Ukraine huenda yakaendelea.
"Sijui kama hilo ni muhimu," Trump alisema kuhusu usitishaji mapigano.
Lakini viongozi hao wa Ulaya walionekana kupinga hilo, huku upinzani mkali ukitoka kwa Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz.
"Siwezi kufikiria ni kwa namna gani mkutano unaofuata utafanyika bila kusitishwa kwa mapigano," Merz alisema. "Kwa hiyo, hebu tulifanyie kazi hilo na tujaribu kuweka shinikizo kwa Urusi."
Alipotakiwa kuzungumza, Zelensky hakusisitiza wito wake wa awali wa kusitishwa kwa mapigano kwanza.
Usalama wa Ukraine
Trump amemwambia Zelensky kwamba Marekani itasaidia kudhamini usalama wa Ukraine baada ya makubaliano yoyote ya kumaliza vita, bila kutaja kiwango cha dhamana hiyo.
Rais wa Marekani hakutoa uhakikisho kuwa atapeleka wana jeshi wa ardhini. Lakini alipoulizwa na waandishi wa habari iwapo dhamana ya usalama ya Marekani kwa Ukraine inaweza kujumuisha jeshi la Marekani nchini humo, Trump hakukataa hilo.
Alisema Ulaya ndio "safu ya kwanza ya ulinzi," lakini "tutahusika. Tutawapa ulinzi mzuri," alisema.
Kauli ya Trump ndio uamuzi mkubwa zaidi kuwahi kuutoa kuhusu suala la dhamana ya usalama kwa Ukraine, ambayo kwa ujumla inaonekana ni muhimu kwa aina yoyote ya makubaliano na Urusi.
Pia alisema wakati wa mkutano wa kilele wa Alaska wiki iliyopita kuwa Putin alikubali kutakuwa na hakikisho la usalama kwa Ukraine kama sehemu ya makubaliano yoyote ya amani.
Katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mikutano ya Jumatatu, Zelensky alisema sehemu ya dhamana ya usalama itahusisha mkataba wa silaha wa dola bilioni 90 (£67bn) kati ya Marekani na Ukraine.
Alisema hii itajumuisha silaha za Marekani ambazo Ukraine haina, ikiwa ni pamoja na mifumo ya silaha za anga, makombora ya ulinzi wa anga "na mambo mengine ambayo sitafichua."
Zelensky pia alisema Marekani itanunua ndege zisizo na rubani za Ukraine, pesa ambazo zitasaidia kufadhili uzalishaji wa ndani wa ndege hizo.
Rais wa Ukraine aliwaambia waandishi wa habari, dhamana ya usalama kwa Kyiv labda itaelezwa ndani ya siku 10.
Hakukuwa na mabishano

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa kuzingatia ziara yake ya mwisho katika Ofisi ya Ikulu ya Marekani mwezi Februari, rais wa Ukraine amejitahidi sana kuwaridhisha wenyeji wake wa Marekani - ikiwa ni pamoja na msururu wa "asante" sita ndani ya dakika chache za kwanza za mkutano.
Mara ya mwisho alipokuwa katika Ikulu ya White House, Zelensky alikaripiwa na Makamu wa Rais JD Vance kwa kukosa shukrani kwa msaada wa Marekani kwa Ukraine.
Pia wakati huu, Zelensy alivaa suti nyeusi badala ya vazi lake la kijeshi la kaki, suti ambayo imevutia hisia kutoka kwa Trump na kusema mgeni wake "amevaa vizuri leo."
Zelensky pia alitaka kuunda uhusiano wa kifamilia wakati wa mkutano huo, akimkabidhi mwenyeji wake barua kutoka kwa mke wake Olena Zelenska ili ipelekwe kwa Mke wa Rais wa Marekani Melania Trump.
"Si yako - [ni] ya mke wako," alimwambia Trump.
Viongozi wa Ulaya walizungumza na Trump kabla ya mkutano wao wa kimataifa, wakimsifu kwa kazi yake ya kuwaleta pamoja.
"Kwa kweli nataka kukushukuru kwa uongozi wako," mkuu wa Nato Mark Rutte alisema.
Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni alisema ingawa hapo awali hakukuwa na dalili kwamba Urusi inataka kuelekea kwenye amani "kuna kitu kimebadilika" shukrani kwa Trump.
Licha ya kauli hizo, viongozi wa Ulaya pia walijaribu kueleza wao pia, wana hofu na uvamizi wa Urusi katika siku za baadaye.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliwaambia viongozi wenzake: "Tunapozungumza juu ya dhamana ya usalama, tunazungumza pia juu ya suala la usalama wa bara la Ulaya."















