Druze ni kina nani na kwa nini Israel inaishambulia Syria?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Wimbi jipya la ghasia za kidini zimeitikisa Syria, na kutilia mashaka hali ya usalama ya nchi hiyo wakati serikali mpya ikijaribu kudhibiti mamlaka yake katika eneo lake lililosambaratika.

Siku ya Jumapili Julai 13, tukio la kutekwa nyara kwa mfanyabiashara kutoka jamii ya wachache ya Druze lilisababisha mapigano makali kati ya wanamgambo wa Druze na Sunni Bedouin kusini mwa Syria.

Baadaye siku ya Jumanne Julai 15, Israel iliingilia kati mzozo huo, ikisema lengo la vikosi vyake ni kuwalinda Waduze na kuwaondoa wanajeshi wanaounga mkono serikali wanaotuhumiwa kuwashambulia huko Suweida. Takriban watu 300 wameripotiwa kuuawa huko Suweida tangu Jumapili, kulingana na Shirika la Kutetea Haki za kibinadamu la Syrian Observatory.

Ghasia hizo ni za kwanza katika jimbo la Suweida lenye wakazi wengi wa Druze tangu mapigano ya mwezi Aprili na Mei kati ya wapiganaji wa Druze na vikosi vipya vya usalama vya Syria vilivyowaua makumi ya watu. Kabla ya hili, mapigano katika majimbo ya pwani ya Syria mwezi Machi yalisemekana kuwa yalisababisha vifo vya mamia ya watu wa jamii ya Alawite walio wachache wa wachache wa Alawite, ambayo rais wa zamani Bashar al-Assad anatoka.

Machafuko hayo mabaya, pamoja na mashambulizi makali ya Israel, yamezua tena hofu ya kusambaratika kwa usalama nchini Syria, wakati nchi hiyo ikikabiliana na anguko la vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya muongo mmoja, na waasi wa hivi karibuni wanaoongozwa na waasi wa Kiislamu kuuteka mji wa Damascus mwezi Desemba 2024. Kiongozi wa sasa wa Syria, mpiganaji wa zamani wa kijihadi Ahmed al-Sharaa, ameapa kuilinda Syria.

Druze ni kina nani?

Druze ni kundi la kidini linaloishi kwenye maeneo ya kaskazini mwa Israel, Lebanon, Jordan na Syria. Nchini Israel wana haki ya uraia na wanakadiriwa kuwa1.5% ya raia wote wa nchi hiyo.

Wale wanaoishi katika eneo la Golan walipewa uraia wa Israel, wakati eneo hilo la Syria lilipokaliwa kimabavu na Israel mwaka 1981, lakini sio kila mtu alikubaliana na uraia wa aina hiyo.

Jamii ya Druze inayoishi katika eneo la milima ya Golan bado wanaweza kusoma na kufanya kazi, ingawa ni wale wenye uraia rasmi ndio wanaoweza kupiga kura.

Wanaume katika jamii ya Druze wanatakiwa kujiunga na jeshi. Hili ndio kundi kubwa zaidi ambalo lina asili ya uyahudi kwenye vikosi vya kijeshi vya Israel, IDF.

Nchi nyingi bado hazitambui umiliki wa Israel wa eneo la milima ya Golan.

Jamii ya Druze inayoishi katika milima ya Golan iliendelea kudumisha uhusiano wa karibu na Syria hata baada ya Israel kuliteka eneo hilo mwaka 1967 na kulichukuwa mwaka 1981, gazeti la Times of Israel linasema.

Tangu kuanguka kwa utawala wa Assad mwezi Desemba, Wadruze wamepinga majaribio la kudhibitiwa kwa mamlaka kusini mwa Syria. Wakati jamii ya Wadruze nchini Syria imegawanyika katika mtazamo wao kwa mamlaka mpya, baadhi ya wanapinga uwepo rasmi wa usalama wa Syria huko Suweida na wamekataa kujumuishwa katika jeshi la Syria - wakitegemea wanamgambo wa ndani.

Ramani
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Licha ya serikali ya Syria kulaani mashambulizi ya hivi majuzi dhidi ya watu wa jamii ya Druze na kuahidi kurejesha hali ya utulivu kusini mwa Syria, vikosi vyake pia vimeshutumiwa kwa kushambulia jamii hiyo ya walio wachache - huku shirika la la kutetea haki za binadamu la Syrian Observatory (SOHR) lenye makao yake makuu nchini Uingereza likiandika juu ya "mauaji ya kukusudia" yanayofanywa na vikosi vya serikali dhidi ya Wadruze. Ripoti kama hizo zimechochea hali ya kutoaminiana kati ya watu wa jamii hiyo na mamlaka huko Damascus.

Baada ya kuondolewa ghafla kwa Assad madarakani, Israel imekuwa ikifikia jamii ya Druze karibu na mpaka wake wa kaskazini kwa nia ya kuunda ushirikiano na nao nchini Syria. Imezidi kujinadi kama mlinzi wa kikanda kwa ya wachache, ikiwa ni pamoja na Wakurdi, Druze na Alawites nchini Syria, huku ikishambulia maeneo ya kijeshi nchini Syria na vikosi vya serikali.

Wakati wa mapigano ya kidini mwezi Mei, Israel ilifanya mashambulizi karibu na ikulu ya rais mjini Damascus, ikisema ilikuwa onyo la kupinga mashambulizi dhidi ya Wadruze. Hata hivyo, baadhi ya watu wa jamii hiyo nchini Syria na Lebanon wameishutumu Israel kwa kuchochea migawanyiko ya kidini ili kuendeleza nia yake ya kujitanua katika eneo hilo.

Kwa nini Israel inaishambulia Syria sasa?

Mashambulizi ya hivi punde kimsingi yametumika kama onyo kwa jeshi la Syria lililopelekwa kusini mwa Syria, huku Israel ikitaka kuunda eneo lisilo la kijeshi katika sehemu hiyo. Israel inahofia uwepo kwa wapiganaji wa Kiislamu karibu na mpaka wake wa kaskazini, kwenye Milima ya Golan inayokaliwa na Israel.

Wakati mashambulizi ya anga ya Israel tarehe 15 Julai yalikusudiwa kulenga vikosi vya usalama na magari huko Suweida, jeshi la Israel lilipanua wigo wa mashambulizi yake tarehe 16 Julai, na kushambulia Wizara ya Ulinzi na makao makuu ya jeshi la Syria huko Damascus. Syria imelaani mashambulizi hayo.

Mashambulizi hayo yaliashiria ongezeko la uhasama wa Israel nchini Syria tangu Desemba 2024, wakati ilipoharibu mamia ya maeneo ya kijeshi kote nchini humo na kuteka eneo salama linalodhibitiwa na Umoja wa Mataifa katika Milima ya Golan ya Syria. Israel imeishambulia Syria kadhaa, kwa lengo la kuzuia mamlaka mpya kujenga uwezo wake wa kijeshi - inayoonekana kama tishio kwa usalama wa Israel.

"Muda wa kuionya Damascus umeisha - sasa mapigo yanafuata," Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz aliandika kwenye mtandao wa kijamii Julai 16, muda mfupi baada ya mashambulizi ya Israel mjini Damascus kuanza.

Hatua ya Israel kushambulia makao makuu ya jeshi la Syria ilitangazwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni ya Syria, kutoka kwa studio zake zilizopo karibu na jengo hilo - huku mwandishi akionyeshwa hewani akikimbia shambilizi hilo.

Maelezo ya video, Tazama: Jinsi mabomu ya Israel yalivyoitikisa Damascus

Ulimwengu umepokea vipi ghasia hizo?

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema Marekani "ina wasiwasi sana" na ghasia hizo na akatangaza Julai 16 : "Tutakubaliana hatua ambazo zitakomesha hali hii ya kutatanisha na ya kutisha usiku wa kuamkia leo."

Mataifa kadhaa ya Kiarabu yakiwemo Lebanon, Iraq, Qatar, Jordan, Misri na Kuwait yamelaani mashambulizi ya Israel yaliyolenga serikali ya Syria na vikosi vya usalama. Wizara ya mambo ya nje ya Saudi Arabia ilishutumu kile ilichokitaja kuwa "mashambulizi ya wazi ya Israel" dhidi ya Syria, huku Iran ikitaja mashambulizi hayo kuwa "kitu kinachoweza kutabirika".

Uturuki, mshirika mkuu wa Syria baada ya utawala wa Assad, ilielezea shambulio hilo kama "kitendo cha hujuma dhidi ya juhudi za Syria za kupata amani, utulivu na usalama".

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia alilaani mashambulizi "yaliyokithiri" ya Israel huko Suweida na Damascus.

Nini kinaweza kutokea baadaye?

Ghasia hizo zimedhihirisha udhaifu wa hali ya usalama na kisiasa baada ya vita vya Syria, huku wimbi la hivi karibuni la ghasia likichochea hofu ya kutokea tena mashambulizi ya kidini nchini Syria.

Huku Sharaa akijaribu kudumisha udhibiti wa Syria na kuunganisha makundi yake mbalimbali, kitakachosali ni kuona kama serikali yake inayotawaliwa na Waislam itaweza kusuluhisha migawanyiko ya kidini iliyokita mizizi nchini Syria, iliyochochewa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mingi.

Mapigano hayo ya kidini, mashambulizi ya Israel, yanatishia kusambaratisha juhudi za serikali za kuleta mshikamano baada mgogoro wa muda mrefu.