Je, waasi waliompindua Assad waliidhibiti vipi Syria?

k

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Syria waliacha vifaa vya kijeshi, vikiwemo vifaru, na kutupa sare zao katika baadhi ya matukio
Muda wa kusoma: Dakika 4

Katika muda wa wiki mbili tu, waasi wa Syria kutoka katika eneo lao la kaskazini-magharibi wameteka msururu wa miji mikubwa, kabla ya kufika mji mkuu Damascus na kumuangusha Rais Bashar al-Assad, miaka 13 baada ya kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Katika misafara ya magari madogo na pikipiki, wapiganaji wakiongozwa na kundi la waasi la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) walisonga kwa kasi kwenye barabara kuu ya kaskazini-kusini ambayo ni uti wa mgongo wa nchi na kuuteka mji wa Damascus bila upinzani.

Lakini wakati watu wengi nchini humo wakisherehekea kuanguka kwa familia iliyotawala Syria kwa mkono wa chuma, mustakabali haujulikani na hali ya mambo bado haijabadilika. Makundi mbalimbali ya waasi yanadhibiti maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Baada ya kuuteka mji wa pili wa Syria wa Aleppo mwishoni mwa Novemba, waasi waliendelea na mashambulizi yao, wakielekea kusini kuchukua udhibiti wa mji wa Hama Alhamisi iliyopita.

Hatua hiyo iliendelea kwa kasi, huku mji wa tatu wa Syria, Homs, ukianguka siku ya Jumamosi muda mfupi kabla ya vikosi vya serikali pia kupoteza udhibiti wa mji mkuu.

Pia unaweza kusoma

Nani anadhibiti eneo gani Syria?

k

Chanzo cha picha, ge

Maelezo ya picha, Wasyria wanasherehekea kuanguka kwa Assad, lakini mustakabali wa nchi hiyo haujulikani

Kuanguka kwa utawala wa Assad kulitokana na mashambulizi ya ghafla na yasiyotarajiwa ya waasi wa HTS, ingawa kundi hilo linadhibiti miji mikuu ya Syria, halitawali nchi nzima.

Syria kwa miaka mingi imekuwa ikidhibitiwa na makundi ya waasi likiwemo kundi la HTS huko Idlib na makundi yanayoongozwa na Wakurdi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, ambayo baadhi yao yamechukua maeneo katika wiki za hivi karibuni.

Hakuna kundi lolote kati ya waasi litakaloomboleza kuanguka kwa utawala wa Assad, lakini kupata mwafaka kuhusu jinsi ya kuendesha nchi bado kunaweza kuwa vigumu na kaskazini mwa nchi hiyo kumekuwa na mapigano kati ya makundi hasimu.

Katika mji wa kaskazini wa Manbij kumekuwa na mapigano kati ya wanajeshi wanaoungwa mkono na Uturuki na waasi wanaoongozwa na wakurdi.

Pande zote mbili zinadai kuchukua sehemu za jiji na mapigano yanaripotiwa kuendelea katika baadhi ya vitongoji.

Wachambuzi katika Taasisi ya Utafiti wa Vita wanasema bado hawafahamu ni nani anayeudhibiti mji wa Manbij.

Majirani wa Syria wanahusika vipi?

KM
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Syria, yenye wakazi wapatao milioni 22, iko kwenye pwani ya mashariki ya bahari ya Mediterania. Inapakana na Uturuki upande wa kaskazini, Lebanoni na Israel upande wa magharibi na kusini-magharibi, Iraq upande wa mashariki na Jordan upande wa kusini.

Uturuki, mataifa yenye nguvu ya Magharibi na mataifa kadhaa ya Ghuba ya Kiarabu yanaunga mkono makundi tofauti ya waasi ya Syria kwa viwango tofauti wakati wa mzozo huo.

Harakati ya Hezbollah yenye makao yake nchini Lebanon, inayoungwa mkono na Iran, imepigana pamoja na jeshi la utawala wa Syria lakini imedhoofishwa sana na mzozo wake na Israel. Hii imeonekana kuwa sababu kuu iliyofanya harakati za waasi kufanikiwa.

Israel, ikiwa na wasiwasi wa kile inachokiita "maeneo ya kijeshi" ya Iran nchini Syria, imeanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya jeshi la Syria.

Siku ya Jumatatu Israel ilisema imefanya mashambulizi ya anga dhidi ya Syria ili kulenga maeneo yanayoshukiwa kuwa ya silaha za kemikali na makombora.

Israel pia imesema imetwaa udhibiti wa eneo lisilo na wanajeshi katika eneo la minuuko ya Golan, ikisema makubaliano ya mwaka 1974 ya kujiondoa na Syria "yameporomoka" baada waasi kuchukua nchi hiyo.

Milima ya Golan ni milima ya miamba kama kilomita 60 (maili 40) kusini-magharibi mwa Damascus.

Israel iliteka eneo hilo kutoka Syria katika hatua za mwisho za Vita vya Siku Sita vya 1967 na kulitwaa mwaka 1981. Hatua hiyo haikutambuliwa kimataifa, ingawa Marekani ilifanya hivyo mwaka 2019.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Seif Abdalla