Rais aliyepigana na Israel hadi dakika ya mwisho ya uhai wake

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hafez al- Assad
Muda wa kusoma: Dakika 8

Wakati Rais wa Marekani Richard Nixon alipokutana na Rais wa Syria Hafez al-Assad mjini Damascus mwaka 1974, Nixon alimuona Assad kuwa "mtu wa ajabu" ambaye alikuwa na "nguvu zisizo na mipaka na haiba kubwa". .

"Nixon alivutiwa sana na rais wa Syria," Moshe Maoz, profesa katika Chuo Kikuu cha Jerusalem, aliandika katika kitabu chake "Assad: The Sphinx of Damascus."

Alisema, "Kwa ujumla yeye ni mtu mwenye nguvu sana. Kwa wakati huu, akiwa na umri wa miaka 44, ikiwa maisha yake yataendelea kuwa salama na kujiokoa na kuondolewa madarakani, basi atathibitika kuwa kiongozi mkuu katika sehemu hii ya dunia."

Baada ya kuwa madarakani kwa takriban miongo mitatu, Hafez Assad alithibitisha utabiri wa Richard Nixon.

'Hafidh Asad alifanya kazi saa 14 kwa siku'

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hafez al-Adas na Kanali wa Libya Muammar Gaddafi

Assad daima alichukia umati. Kulikuwa na matukio machache sana ambapo angetokea mbele ya watu wake.

Lakini watu wa Syria walikumbushwa kila mara kwamba Hafez Assad alikuwa kiongozi wao.

Assad alikuwa amezoea kuishi maisha ya siri. Alioa Anisa Makhlouf mnamo 1958, lakini mkewe alionekana mara chache nje ya nyumba.

Charles Patterson anaandika katika kitabu chake 'Hafiz al-Assad wa Syria', "Assad siku zote alikuwa mchapakazi.

Alikuwa akifanya kazi kwa saa 14 kwa siku na alilala kidogo sana. Hakuwahi kuonekana akienda likizo.

Hakuwa na hata wakati wa kula na watoto wake. Wakati wa siku za shida, hakukutana na watoto wake kwa siku nyingi."

Salah Jadid aondolewa madarakani

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hafez al-Assad alitembelea Moscow kama Waziri wa Ulinzi wa Syria mnamo 1971
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Assad alianza kazi yake ya kijeshi mwaka wa 1951. Alikuwa miongoni mwa watu kumi na watano kutoka Syria ambao walichaguliwa kwa mafunzo ya urubani katika shule ya urubani.

Inasemekana kuwa wakati wa mafunzo yake ya miezi sita huko Cairo, Misri, alishawishiwa sana na Rais wa Misri Jamal Abdul Nasser na utaifa wake wa Kiarabu.

Mwaka 1964, Assad alifanywa kamanda wa Jeshi la Wanahewa la Syria. Mnamo 1966, Wana-Baath waliingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi na Assad akafanywa kuwa Waziri wa Ulinzi katika serikali mpya.

Changamoto kubwa ya Hafez Assad kama Waziri wa Ulinzi ilikuwa Vita vya Siku Sita na Israeli mnamo 1967.

Katika vita hivi, Israel sio tu iliteka Milima ya Golan bali pia mji wa Quneitra. Mnamo Novemba 16, 1970, wakati mkutano wa dharura wa Chama cha Baathist ukiendelea, Hafez Assad aliamuru askari wake kuzingira mahali pa mkutano.

Aliamuru kukamatwa kwa kiongozi wa chama hicho, Salah Jadid. Kwa vile serikali ya Jadid ilikuwa imepoteza umaarufu wake nchini Syria, Wasyria walikaribisha ujio wa Hafez Assad madarakani.

Alikua Rais wa Syria mnamo 1971

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hafez al-Assad, aliyekuwa Rais wa Syria wakati huo, akiwa na familia yake, picha hii ni ya mwaka 1974.

Tofauti na watawala wengine waliotangulia, Hafidh alianza kwenda katika vijiji vya Syria na kusikiliza matatizo ya raia wake.

Charles Patterson anaandika, "Hapo awali, Assad alipendelea kutawala akiwa nyuma ya pazia, bila kuchukua nafasi ya juu katika serikali.

Baada ya uasi wa kijeshi, alimfanya mwalimu wa Sunni asiyejulikana kuwa mkuu wa serikali.

Yeye mwenyewe alichukua wadhifa usio na umuhimu wa Waziri Mkuu, lakini mamlaka yote ya utawala yalibakia kwake."

"Hata hivyo, haikuwa asili ya Assad kubaki nyuma ya pazia. Alikua Rais wa Syria tarehe 22 Februari 1971. Alifanya kura ya maoni tarehe 22 Machi 1971 ambapo asilimia 99.2 ya watu waliunga mkono kuwa kwake Rais."

Kwa mujibu wa Charles Patterson, "Vile vile, katika kura za maoni zilizofanyika mwaka 1978, 1985 na 1992, watu wa Syria waliunga mkono urais wa Hafez Assad.

Kura hizi hazikuwa uchaguzi za kweli kwa sababu hakuna mgombea mwingine aliyependekezwa kushika wadhifa wa rais."

70% ya bajeti ya nchi ilitumika kwa ulinzi

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hafez Assad akiwa na kiongozi wa Palestina Yasser Arafat (picha ya faili)

Hatua zilizochukuliwa na Assad baada ya kuingia madarakani zilionyesha kwamba hawezi kamwe kusahau kushindwa kwake dhidi ya Israel mwaka 1967.

Alikuwa Waziri wa Ulinzi wa Syria wakati huo. Baada ya kuingia madarakani mwaka 1970, alianza kupanga kulipiza kisasi kwa kushindwa huku.

Majid Khadduri anaandika katika kitabu chake 'Arab Personalities in Politics', "Mwaka 1971, Assad alitenga asilimia 70 ya bajeti ya Syria kwa vikosi vya kijeshi.

Pesa ambazo zilipaswa kutumika katika shule, barabara na hospitali zilitumika kwa kazi za kijeshi."

"Mwaka 1972 alikwenda Moscow kutia saini makubaliano ya kijeshi na Umoja wa Kisovieti. Alitumia dola milioni 700 kununua ndege za MiG-21 na makombora ya kuzuia ndege ya SAM."

Umoja wa Kisovieti ulituma washauri wa kijeshi nchini Syria pamoja na silaha. Hivi karibuni idadi ya washauri wa kijeshi wa Soviet huko Syria iliongezeka kutoka mia saba hadi elfu tatu.

Lakini Syria ilipodai ndege ya kisasa zaidi ya MiG-23 kutoka kwa Umoja wa Kisovieti, Umoja wa Kisovieti haukukubali ombi lao.

Alipanga mashambulizi dhidi ya Israeli kwa ushirikiano na Misri

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hafez Assad akiwa na Rais wa Marekani Jimmy Carter mwaka 1977

Mnamo Februari 1973, Waziri wa Vita wa Misri alipowasilisha mpango wa vita vya Misri na Syria dhidi ya Israeli, Assad alikubali mara moja.

Charles Patterson anaandika, "Kwa kweli Rais wa Misri wa wakati huo Anwar Sadat alitaka kushambulia Israeli mwezi Mei, lakini Assad hakuwa tayari kwa hilo. Kwa hiyo, kwa ushauri wa Assad, Sadat alikubali kuahirisha mashambulizi hadi Oktoba."

"Assad alikwenda Moscow ili kuimarisha uhusiano kati ya Misri na Umoja wa Kisovieti. Mapema mwaka 1972, Sadat alikuwa amewafukuza washauri wa kijeshi wa Soviet kutoka nchi yake.

Lakini alihitaji Umoja wa Kisovieti kwa mara nyingine tena katika vita dhidi ya Israel. Sadat alichukua msaada wa Assad kwa hili."

Kwa mujibu wa Charles Patterson, "Kwa kuwa Jordan ilikuwa na mpaka mrefu na Israel, Assad alitaka kushambulia Israel kupitia Milima ya Golan pamoja na Jordan, lakini Jordan haikuwa tayari kufanya hivyo.

Hata hivyo, ili kusaidia juhudi za vita vya Syria, Jordan ilituma brigedi zake mbili kupigana na Israel katika Milima ya Golan."

Walishambulia Israeli kwa wanajeshi elfu thelathini na tano na vifaru mia nane

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mnamo 1973, shambulio kubwa lilizinduliwa dhidi ya Israeli chini ya uongozi wa Syria na Misri (picha ya faili)

Ili kuiweka Israel katika hali ya kuchanganyikiwa, Hafez al-Assad alimkaribisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kurt Waldheim mjini Damascus kama sehemu ya juhudi za kutatua mzozo wa Mashariki ya Kati kwa amani.

Ambapo asubuhi ya tarehe 6 Oktoba 1973, Misri ilishambulia Israeli ghafla. Assad aliingia kwenye chumba cha vita cha chini ya ardhi.

Moshe Maoz anaandika, "Assad alikuwa amezama sana katika shambulio hili hivi kwamba alisahau kwamba Oktoba 6 ilikuwa muhimu kwake kwa sababu nyingine.

Baadaye, mtu alipomkumbusha kwamba ilikuwa siku yake ya kuzaliwa ya 43, alisema, uko sahihi. Sikukumbuka hilo."

Katika wakati uliopangwa, Misri na Syria zilianzisha mashambulizi ya pande mbili dhidi ya Israeli. Syria ilishambulia Israel kwenye milima ya Golan ikiwa na wanajeshi 35,000 na vifaru 800.

Awali, Assad alifikiri kwamba alikuwa karibu sana kurejesha ardhi aliyoipoteza mwaka wa 1967.

Wakati Misri pia ilipoishambulia kwa ghafla Israel kwa bunduki 4,000 na ndege 250, vifaru 300 vya Israeli viliharibiwa katika vita vya kwanza.

Kukatishwa tamaa na mtazamo wa Misri

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Anwar Sadat na Hafez Assad (file photo)

Mafanikio ya mashambulizi haya ya awali yaliwafanya Sadat na Assad kuwa mashujaa wa ulimwengu wa Kiarabu mara moja. Lakini ushindi wa awali wa Waarabu ulidumu kwa siku chache tu.

Patrick Seale anaandika katika kitabu chake 'Assad: The Struggle for the Middle East', "Assad alishtuka kwamba Misri ilipunguza makali ya mashambulizi yake baada ya kuvuka Mfereji wa Suez.

Misri haikuwa na nia ya kusonga mbele katika jangwa kwa sababu haikutaka wanajeshi wake wakabiliwe na jeshi la anga la Israeli."

"Wakati Assad alitaka Misri kuzidisha mashambulizi yake dhidi ya Israel kati ya tarehe 7 na 14 Oktoba, Misri haikufanya hivyo. Kukatishwa tamaa kwa Assad na Misri kuligeuka kuwa uchungu, na Syria iliachwa kukabiliana na nguvu kamili ya mashambulizi ya Israel ikiwa peke yake."

Israel iliishambulia Syria kwa mashambulizi makali sana ya roketi, makombora, vifaru na ndege zake hadi ikabidi warudi nyuma. Baadaye, Assad, huku akikosoa tabia ya Misri, alisema kuwa kwake hii ilikuwa ni tamaa kubwa ya vita.

Assad ni mpatanishi mkali

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hafez al-Assad akiwa na Richard Nixon na Henry Kissinger (picha ya faili)

Misri iliongeza juhudi zake dhidi ya Israel tarehe 14 Oktoba, lakini kufikia wakati huo Israel ilikuwa si tu imetwaa tena Milima ya Golan iliyokuwa imepoteza hapo awali, lakini pia ilikuwa imekaribia sana mji mkuu wa Syria, Damascus.

Hivyo ndoto ya Assad ya kuikomboa Milima ya Golan na kubadilisha mizani ya madaraka katika Mashariki ya Kati ilivunjwa.

Wakati pendekezo la kusitisha mapigano lilipoletwa kwa mpango wa Marekani na Umoja wa Kisovieti, Israel na Misri zilikubali mara moja, lakini Assad hakuwa tayari kulikubali.

Wakati silaha za Israel zilipobakia maili 20 tu kutoka Damascus, Assad pia ilimbidi kukubali kusitishwa kwa mapigano.

Baada ya vita, Henry Kissinger alichukua nafasi ya mpatanishi mkuu wa makubaliano kati ya Israeli, Misri na Syria.

"Assad alichukua msimamo mkali, akitaka Israel irejeshe ardhi yote iliyokuwa imeteka mwaka 1973 na sehemu kubwa ya ardhi iliyoiteka mwaka wa 1967," aliandika katika kitabu chake Years of Renewal.

"Kwa sababu Anwar Sadat hakushirikiana na Assad, Assad ilibidi afanye mazungumzo ya makubaliano tofauti na Israel kupitia mimi.

Kwa maoni yangu, Assad alikuwa mpatanishi mwenye kiburi, mkali na mwerevu."

Henry Kissinger anaandika, "Ingawa Assad hakupata kila alichodai, alifanikiwa kurejesha karibu ardhi yote aliyopoteza mwaka wa 1973.

Assad pia alifanikiwa kurejesha jiji la Quneitra kutoka kwa Israeli, ambalo Syria ilipoteza katika vita vya 1967. Alisherehekea hili kwa kwenda Quneitra binafsi na kuinua bendera ya Syria huko."

Hivi ndivyo Assad alivyokufa

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mnamo Desemba 2024, waasi walichoma moto kaburi la Hafez Assad

Afya ya Assad ilianza kuzorota katika miaka ya 90. Wanadiplomasia wa Marekani walibainisha kuwa alianza kuwa na ugumu wa kufuatilia chochote.

Mnamo tarehe 10 Juni, 2000, alipokuwa akizungumza kwa simu na Waziri Mkuu wa Lebanon, Salim al-Hass, alipata mshtuko wa moyo na akafa.

Alikuwa na umri wa miaka 69 wakati huo. Siku tatu baadaye, alizikwa katika mji wa baba yake wa Kardha.

Mnamo Desemba 11, 2024, wakati mwanawe Bashar al-Assad alipoondolewa mamlakani, waasi walichoma moto kaburi la Hafez Assad.

Siku chache baadaye, watu wasiojulikana waliutoa mwili wake kwenye kaburi lake na kuuzika mahali pasipojulikana.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla