Je, mpango wa Israel wa "Y1" nini na kwanini unatishia wazo la taifa huru la Palestina?

Waziri wa Fedha wa Israel Bezalel Smotrich akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu "upanuzi wa makazi" na mradi wa "Yi1" katika Ukingo wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu, ambao umekwama kwa miaka mingi.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Waziri wa Fedha wa Israel Bezalel Smotrich akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu "upanuzi wa makazi" na mradi wa "Yi1" katika Ukingo wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu, ambao umekwama kwa miaka mingi.
Muda wa kusoma: Dakika 9

Mipango ya miradi ya makazi yenye utata katika Ukingo wa mto Jordan ama Westbank unaokaliwa na walowezi umezua ukosoaji mkubwa.

Waziri wa Fedha wa mrengo wa kulia wa Israel Bezalel Smotrich alisema mradi huo "utazika wazo la taifa la Palestina."

Mpango huo unaojulikana kama "E1," ambao unahusisha ujenzi wa nyumba 3,401 katika Ukingo wa mto Jordan ama West bank kati ya Jerusalem Mashariki na makazi ya Ma'ale Adumim, umekwama kwa miongo kadhaa kutokana na upinzani mkali.

Wengi wa jumuiya ya kimataifa wanaona kuwa ujenzi wa makaazi haya ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa, lakini Israel inakanusha hilo.

Waziri wa Fedha wa Israel Smotrich aliunga mkono mpango huo siku ya Jumatano, akiuita uamuzi huo "mafanikio ya kihistoria."

Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeutaja mpango huo kuwa ni muendelezo wa jinai 'zinazohusiana' za mauaji ya halaiki, kuhama na kunyakua makazi yao."

Israel imekanusha mara kwa mara mashtaka hayo.

Pia unaweza kusoma:

Nchi mbalimbali duniani zikiwemo Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Uingereza na Uturuki zimeshutumu mpango wa suluhu wa "E1" na kutaka ufungwe.

Je, ni mpango gani wa makazi ya "Yi1"

Israel imejenga makazi mengi, kama vile Ma'ale Adumim, katika Ukingo wa Mto Jordan unaokaliwa.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Israel imejenga makazi mengi, kama vile Ma'ale Adumim, katika Ukingo wa Mto Jordan unaokaliwa.

Ujenzi wa makazi ni mojawapo ya masuala yenye utata kati ya Waisraeli na Wapalestina.

Mradi wa makazi wa "Yi1", uliopendekezwa kwanza katika miaka ya 1990 wakati wa utawala wa waziri mkuu wa Yitzhak Rabin, ulianza na mpango wa awali wa nyumba 2,500.

Mnamo 2004, mpango huo ulipanuliwa na kujumuisha nyumba 4,000, pamoja na vitengo vya biashara na vivutio vya utalii.

Kwa nini mradi huu una utata sana?

Ramani ya Ukingo wa Magharibi, Israel na Gaza
Maelezo ya picha, Ramani ya Ukingo wa Magharibi, Israel na Gaza

Maendeleo ya mradi wa "Yi1" yameonekana kwa muda mrefu kuwa kikwazo kikubwa kwa kuundwa kwa taifa huru la Palestina.

Sababu ni eneo la kimkakati la eneo la "Y1": mradi huu unatenganisha sehemu ya kusini ya Yerusalemu kutoka sehemu ya kaskazini na kuzuia kuundwa kwa eneo la miji la Palestina kati ya Ramallah, Jerusalem Mashariki na Bethlehem.

Kundi la Israel la Peace Now, ambalo linafuatilia shughuli za makazi katika Ukingo wa Mto Jordan, linasema nyumba hizo mpya zitakuwa kubwa kwa asilimia 33 kuliko makazi ya Ma'ale Adumim, ambayo kwa sasa yana takriban wakazi 38,000.

Kulingana na Peace Now, mradi wa "Yi1" utafungua njia kwa Israel kuunganisha makazi na maeneo ya viwanda na kupanua udhibiti wake katika sehemu kubwa za Ukingo wa Magharibi.

Kundi hilo linasema mkutano wa mwisho wa kuidhinisha mpango wa suluhu wa "Yi1" utafanywa na kamati ya kiufundi ambayo hapo awali ilikataa ukosoaji wowote wa mpango huo.

Maeneo yanayokaliwa ya Ukingo wa Mto Jordan yako wapi?

Wakaazi wa makazi ya Israel karibu na Ramallah wakitazama kwa mbali wanajeshi wa Israel wakiwazuia wakimbizi wa Kipalestina kuvuna zeituni.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wakaazi wa makazi ya Israel karibu na Ramallah wakitazama kwa mbali wanajeshi wa Israel wakiwazuia wakimbizi wa Kipalestina kuvuna zeituni.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ukingo wa Magharibi ni eneo lililoko kati ya Israel na Mto Jordan, ambako takriban Wapalestina milioni tatu wanaishi.

Eneo hili, pamoja na Jerusalem ya Mashariki na Ukanda wa Gaza, linajulikana kimataifa kama Maeneo ya Palestina Yanayokaliwa kimabavu.

Katika Ukingo wa Mto Jordan ama Westbank na Jerusalem ya Mashariki, kuna zaidi ya makazi 160 ya Waisraeli, yenye jumla ya takriban wakazi Wayahudi 700,000.

Uwepo wa makazi haya umeendelea kuwa kiini cha mzozo wa muda mrefu kati ya Wapalestina na Israel, huku Wapalestina wakiupinga vikali na kuuona kama kikwazo kwa ndoto yao ya kujenga taifa huru.

Ingawa Israel bado inadhibiti Ukingo wa Mto Jordan, tangu miaka ya 1990, baadhi ya miji na vijiji katika eneo hilo vimekuwa vikisimamiwa na Mamlaka ya Palestina, chombo cha utawala kinachotambuliwa kwa kiasi katika jamii ya kimataifa.

Hata hivyo, hali ya usalama na haki katika eneo hilo imezidi kuzorota, hasa baada ya shambulio la Hamas dhidi ya Israel la tarehe 7 Oktoba 2023.

Tangu wakati huo, shinikizo la Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Mto Jordan limeongezeka kwa kasi.

Serikali ya Israel inatetea hatua hizo kuwa ni za kiusalama, lakini kwa Wapalestina na mashirika ya haki za binadamu, hali hiyo inaelezwa kuwa ni dhuluma inayokithiri.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa mwezi Juni 2025 pekee, watu 100 walijeruhiwa katika mashambulio yaliyofanywa na wakazi wa makazi ya Waisraeli dhidi ya Wapalestina idadi kubwa zaidi kwa mwezi mmoja katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita.

Kwa jumla, katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025, mashambulio 757 yameripotiwa kufanywa na wakazi wa makazi yaliyoko ukingo wa mto Jordan, yakisababisha majeruhi kwa Wapalestina au uharibifu wa mali.

Hii ni ongezeko la karibu asilimia 13 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu pamoja na Wapalestina wameilaumu Israel kwa kutotimiza wajibu wake wa kisheria kama taifa linalokalia kwa mabavu.

Wanaituhumu si tu kwa kushindwa kuwalinda Wapalestina, bali pia kwa kuruhusu na hata kushiriki katika mashambulio ya wakazi wa makazi dhidi ya raia wa Palestina.

Kwa mujibu wa ripoti ya Human Rights Watch ya mwaka 2024, majeshi ya Israel mara kadhaa yamehusishwa moja kwa moja na mashambulio hayo, au yameshutumiwa kwa kufumbia macho vitendo vya dhuluma dhidi ya Wapalestina.

Msimamo wa Israel na jamii ya kimataifa

Israel inadai kuwa Mikataba ya Geneva, inayopiga marufuku ujenzi wa makazi ya raia katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu, haitumiki katika muktadha wa Ukingo wa Mto Jordan.

Hata hivyo, madai haya yanakataliwa na mataifa mengi washirika wa Israel pamoja na wataalamu wa sheria wa kimataifa.

Kwa upande wao, Wapalestina wanasisitiza kuwa Ukingo wa Mto Jordan ni sehemu ya ardhi ya taifa lao la baadaye, na kwamba makazi yote ya Waisraeli yanapaswa kuondolewa.

Lakini serikali ya Israel haikubali madai ya Wapalestina ya kuanzisha taifa huru, na inadai kuwa Ukingo wa Mto Jordan ni sehemu ya kihistoria ya ardhi ya Israeli.

Uamuzi wa mahakama ya kimataifa ya haki

Mnamo Julai 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), chombo cha juu kabisa cha kisheria cha Umoja wa Mataifa, ilitoa uamuzi mzito:

Uwepo unaoendelea wa Israel katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu ni kinyume cha sheria za kimataifa, na kwamba Israel inapaswa kuwaondoa wakazi wote wa makazi hayo.

Mahakama hiyo pia ilisema kuwa vizuizi vinavyowekwa na Israel dhidi ya Wapalestina katika maeneo hayo vinawakilisha aina ya ubaguzi wa kimfumo unaotokana na rangi, dini au asili ya kikabila.

Majibu ya Israel

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alikataa uamuzi huo na kuukosoa vikali.

Katika taarifa yake alisema:

"Wayahudi si wavamizi wa ardhi yao si katika mji mkuu wetu wa milele, Jerusalem, wala katika nchi ya mababu zetu, Yudea na Samaria {Ukingo wa Mto Jordan}."

Kauli hiyo inadhihirisha msimamo wa muda mrefu wa serikali ya Israel kwamba ardhi hiyo ni ya kihistoria kwa taifa la Kiyahudi.

Msimamo ambao unakinzana moja kwa moja na maazimio na misimamo ya kimataifa kuhusu haki na uhuru wa Wapalestina.

Wanajeshi wa Israel wakiwazuia wakulima wawili wazee wa Kipalestina kuvuna mizeituni yao katika Ukingo wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Israel wakiwazuia wakulima wawili wazee wa Kipalestina kuvuna mizeituni yao katika Ukingo wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu.

Maoni ya kimataifa kuhusu ujenzi mpya wa makazi katika Ukingo wa Mto Jordan

Tangazo la utekelezaji wa mpango mpya wa Israel ujulikanao kama "Y1", unaolenga kujenga makazi mapya ya Waisraeli katika Ukingo wa Mto Jordan, limezua maoni na ukosoaji kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, huku athari zake zikihofiwa kuhujumu kabisa juhudi za kufikia suluhisho la mataifa mawili.

Mara baada ya kutangazwa kwa mpango huo, Bezalel Smotrich, waziri wa Israel mwenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia, alitoa shukrani kwa Rais wa Marekani Donald Trump na Balozi wa Marekani nchini Israel Mike Huckabee, kwa kile alichokiita "msaada wao wa wazi."

Alisisitiza kwamba anaamini Ukingo wa mto Jordan ni sehemu isiyotenganishwa ya ardhi ya Israeli aliyoahidi Mungu kwa watu wa Kiyahudi.

Smotrich aliongeza kuwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu pia ameunga mkono mpango huo, ambao unalenga kuwahamisha hadi watu milioni moja kuishi katika makazi mapya katika Ukingo wa Mto Jordan hatua inayotazamwa kama ishara ya kuendelea kwa sera za ujenzi wa makazi ambazo zimekuwa chanzo cha mvutano wa muda mrefu katika eneo hilo.

Msimamo wa Palestina na jumuiya ya kimataifa

Wizara ya Mambo ya Nje ya Mamlaka ya Palestina ililaani vikali mpango huo, ikiutaja kuwa shambulio la moja kwa moja dhidi ya uadilifu wa ardhi ya Palestina, na pigo la wazi kwa matarajio ya kuundwa kwa taifa huru la Wapalestina.

Ilieleza kuwa mpango huo unadhoofisha uhusiano wa kijiografia na kidemografia kati ya maeneo ya Palestina, huku ukigawanya Ukingo wa Mto Jordan katika vipande visivyohusiana, hivyo kuweka msingi wa kuunganishwa kwa mabavu ya maeneo hayo na Israel.

Katika kauli yake kuhusu mpango huo, Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani ilieleza wasiwasi wake kwa kusema:

"Ukingo wa Mto jordan wenye utulivu ni kichocheo cha usalama wa Israel, na unaendana na lengo la serikali ya Israeli la kufanikisha amani katika eneo hili."

Hata hivyo, kauli hiyo haikufikia kiwango cha kulaani au kuzuia moja kwa moja utekelezaji wa mpango huo tofauti na misimamo ya mashirika mengine ya kimataifa.

Umoja wa Mataifa ulionya kuwa utekelezaji wa mpango wa "Y1" utasababisha mgawanyiko mkubwa kati ya kaskazini na kusini mwa Ukingo wa Mto Jordan, na hivyo "kuhujumu kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kuanzishwa kwa taifa la Palestina lenye mshikamano na utulivu."

Kwa upande wake, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaia Kalas, alisema:

"Mpango wa makazi mapya katika eneo la E1 unahujumu zaidi suluhisho la mataifa mawili, na unakiuka sheria za kimataifa."

Msimamo huo uliungwa mkono na mataifa mbalimbali.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uingereza, David Lammy, alisema mpango huo "utagawanya taifa la Palestina la baadaye katika sehemu mbili na ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa."

Misri iliutaja mradi huo kuwa "uvunjaji wa wazi wa sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama."

Uturuki nayo ilieleza kuwa mpango huo "unapuuzia sheria za kimataifa na unatishia ukamilifu wa ardhi ya taifa la Palestina."

Jordan, ambayo ina uhusiano wa kidiplomasia na Israel, ilitoa msimamo mkali, ikisema kuwa mpango huo ni "shambulio dhidi ya haki isiyonyang'anywa ya watu wa Palestina ya kuunda taifa huru kulingana na mipaka ya Juni 4, 1967, na Jerusalem ya Mashariki kuwa mji wake mkuu.

Utambuzi wa Palestina kama nchi Huru

Tangazo la mpango wa "Y1" linakuja katika kipindi ambacho baadhi ya mataifa, ikiwemo Ufaransa na Kanada, yameashiria nia ya kutambua taifa la Palestina rasmi ndani ya mwaka huu.

Hadi sasa, nchi 147 kati ya wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa zimeitambua taifa la Palestina.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, ametangaza kuwa endapo Israel haitatimiza masharti fulani ikiwemo kusitisha mapigano huko Gaza na kufufua mchakato wa suluhisho la mataifa mawili basi serikali yake itatambua rasmi Palestina ifikapo mwezi Septemba.

Katika kujibu vuguvugu hilo, Smotrich alisema:

"Hakutakuwa tena na nchi zaidi za kutambua Palestina."

Akaongeza:

"Sasa kwa kuwa kila mtu duniani anajaribu kutambua taifa la Palestina, jibu letu halitakuwa kwenye nyaraka, wala katika maazimio au matamko, bali katika hali halisi hali ya nyumba, na hali ya majirani."

Mada zinazohusiana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid