Jeshi la Urusi latangaza msaada kwa jeshi la serikali ya Syria dhidi ya vikundi pinzani

..

Chanzo cha picha, Reuters

Muda wa kusoma: Dakika 6

Jeshi la Urusi lilitangaza kuwa linalisaidia jeshi la Syria "kuondoa" makundi ya upinzani katika majimbo matatu kaskazini mwa nchi hiyo.

Jeshi la Urusi limesema katika taarifa fupi kwenye tovuti yake kwamba "Jeshi la Waarabu wa Syria, likisaidiwa na Jeshi la anga la Urusi, linaendelea na operesheni yake yenye lengo la kuzima hujuma za kigaidi katika majimbo ya Idlib, Hama na Aleppo."

Aliongeza, "Siku iliyopita, mashambulizi ya makombora yalitekelezwa katika maeneo ambayo wanaharakati walikuwa wamekusanyika au ambapo vifaa vilihifadhiwa," akibainisha kuwa "wanaharakati 320 waliuawa."

Urusi ilitangaza wiki hii kuwa imeshambulia kwa mabomu ngome za upinzani nchini Syria, na Shirika la Haki za Binadamu la Syria liliripoti kuwa limetumia ndege za kivita kushambulia sehemu za Aleppo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2016.

Kwa upande wa shirika la kiraia nchini humo Syrian Civil Defense, ambalo linafanya kazi katika maeneo yanayodhibitiwa na wapinzani wa Syria na linajulikana kwa kifupi " White Helmets " katika mtandao wa X, lilisema kuwa watu wasiopungua 25 waliuawa kaskazini magharibi mwa Syria katika mashambulizi ya anga yaliyotekelezwa na serikali ya Syria na Urusi siku ya Jumapili.

Wakati wa mazungumzo na Fidan, Blinken alisisitiza "haja ya kudhibiti uhasama zaidi na kulinda maisha ya raia na miundombinu," Ikulu ya Marekani ilisema katika taarifa yake.

Marekani na washirika wake Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zimetoa wito siku ya Jumapili "kudhibiti mzozo" nchini Syria, zikitaka katika taarifa ya pamoja kulinda raia na miundombinu.

Shirika hilo liliongeza kuwa "watoto kumi ni miongoni mwa waliouawa katika mashambulizi ya anga ndani na karibu na Idlib na katika maeneo mengine yanayodhibitiwa na upinzani karibu na Aleppo."

"jumla ya watu waliouawa katika mashambulizi ya anga ya Syria na Urusi tangu Novemba 27 imeongezeka hadi 56, ikiwa ni pamoja na watoto 20."

Katika tukio linalohusiana na hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alimpigia simu mwenzake wa Uturuki, Hakan Fidan, Jumapili kujadili "haja ya kutuliza hali ya mambo nchini Syria, baada ya mirengo ya upinzani kuchukua udhibiti wa maeneo kadhaa katika siku za hivi karibuni.

"Kuongezeka kwa sasa kunasisitiza hitaji la dharura la suluhisho la kisiasa linaloongozwa na Syria katika mzozo huo, kulingana na azimio nambari 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa," ilisema taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, ikirejelea azimio la Umoja wa Mataifa la 2015 lililoidhinisha mchakato wa amani nchini humo Syria.

..

Chanzo cha picha, Reuters

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wizara ya Ulinzi ya Syria ilitangaza Jumapili kwamba makumi ya wanamgambo waliuawa na kujeruhiwa katika shambulio la pamoja la Syria na Urusi kwenye viunga vya mji wa Al-Safira katika mashamba ya Aleppo, wakati ambapo jeshi la Syria lilituma nguvu kubwa ya kijeshi katika mji wa Hama na kuimarisha nafasi zake zinazozunguka mji huo na Jabal Zain Al-Abidin unaopakana na mji huo kwa kaskazini.

Wakati mirengo pinzani inayoongozwa na "Hay'at Tahrir al-Sham" ikiendelea kudhibiti miji mingi ya kaskazini mwa Hama, mirengo hiyo ilitangaza amri ya kutotoka nje katika mji wa Aleppo kuanzia saa 7 mchana Jumapili saa za Syria hadi saa 7 asubuhi siku ya Jumatatu.

Alisema kuwa uamuzi huo unakuja "kulinda usalama wa watu wetu katika jiji na kulinda mali binafsi na ya umma dhidi ya kuharibiwa."

Jeshi lilisema kuwa vikosi vyake vinakabiliana na mashambulizi ya makundi yenye silaha katika maeneo kadhaa ya kaskazini-magharibi mwa nchi, na limethibitisha kwamba litasonga mbele "hivi karibuni" kwenye makabiliano ya kutwaa tena maeneo yote na kuyakomboa kutoka kwa makundi hayo.

Wizara ya Ulinzi ya Syria pia ilithibitisha kuwasili kwa wanajeshi, ndege za kivita na magari ya kijeshi kaskazini mwa Hama kukutana na "wapiganaji wa upinzani."

Vikosi vya serikali ya Syria viliondoka Aleppo, mji wa pili kwa ukubwa nchini humo, baada ya shambulio la kushtukiza la Hay'at Tahrir al-Sham, ambalo lilianzishwa na kundi la Islamic State, kisha kujiunga na al-Qaeda na kujitenga miaka iliyopita na kuungana na makundi mengine yenye silaha na kuunda kundi la upinzani linalomiliki silaha nchini Syria.

Iran: Syria itashinda kama awali

..

Chanzo cha picha, EPA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi aliwasili Damascus Jumapili jioni kujadili hali ya kijeshi na maafisa wa Syria, kufuatia shambulio la kushtukiza la vikosi pinzani vyenye silaha Jumatano iliyopita.

Wakati wa mkutano wake na Rais wa Syria Bashar al-Assad, Araqchi alisema kuwa hali nchini Syria ni "ngumu" lakini ana imani kwamba serikali itashinda kama ilivyofanya awali,limeeleza Shirika la Habari la Iran.

Kwa upande wake, Assad alisisitiza kwa waziri wa mambo ya nje wa Iran "umuhimu wa kuunga mkono washirika na marafiki katika kukabiliana na mashambulizi ya kigaidi yanayoungwa mkono kutoka nje,"ilieleza taarifa ya ikulu

Araghchi anatarajiwa kuondoka Damascus hadi Ankara ili kujadili hali hiyo na maafisa wa Uturuki pia, haswa kwa vile Uturuki ‘’ina jukumu kubwa" katika kuunga mkono upinzani wa Syria.

Hapo awali, Araghchi alizitaja harakati za hivi karibuni za makundi yenye silaha nchini Syria kuwa ni sehemu ya mpango wa "Wamarekani wenye asili ya kiyahudi wenye lengo la kuyumbisha usalama katika eneo la Asia Magharibi, katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov.

Kwa upande wa Marekani ilikanusha uhusiano wowote na shambulio hilo, ambalo liliongozwa na "shirika linalotajwa kuwa la kigaidi," kulingana na msemaji wa Baraza la Usalama la Marekani Sean Savitt.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema, wakati wa ziara yake ya kuwatembelea wanajeshi wapya katika kambi moja katikati mwa Israel siku ya Jumapili, kwamba Israel inafuatilia kwa karibu matukio nchini Syria,kwa mujibu wa Reuters.

Uingereza ilimlaumu Rais Bashar al-Assad kwa "kuongezeka" kwa vita vya Syria vilivyoshuhudia "mji wa Aleppo ukianguka mikononi mwa vikosi vya waasi," kulingana na taarifa kutoka Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza iliyonukuliwa na Agence France-Presse.

"Utawala wa Assad ulitengeneza mazingira yaliyochangia hali inayoshuhudiwa kwa sasa kwa kuendelea kukataa kushiriki katika mchakato wa kisiasa na kuitegemea Urusi na Iran," wizara hiyo ilisema katika taarifa yake, ikitoa wito kwa pande zote mbili "kulinda maisha ya raia na miundombinu."

Hisia mseto, matumaini na wasiwasi

Raia wakimbia Aleppo baada ya Hayat Tahrir al-Sham kudhibiti jiji hilo

Chanzo cha picha, Getty Images

Waandishi wa BBC kitengo maalum cha ufuatiliaji kimeelezea hali ya Aleppo kuwa yenye hisia mseto matumaini na wasiwasi huku matarajio ya wengi wakishindwa kuelewa mustakabli wao kutokana na hali inavyoendelea.

Baada ya miaka kadhaa ya kukimbia makazi waandishi hao wanasema wakiwanukuu baadhi ya mashuhuda ambao ni baadhi ya wakazi wa jiji hilo wameanza kurejea makwao kama fursa ya kujenga upya maisha yao lakini wengine bado wanachukua tahadhari kubwa kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya utawala na udhibiti wa jiji hilo.''anaeleza

Alisema makundi yenye silaha yanatafuta "kuwatuliza raia" na kuwahakikishia kuwa hali itaimarika.

Katika tukio linalohusiana na hilo, Shirika la kutetea Haki za Binadamu la Syria limesema kuwa watu 12 waliuawa katika shambulizi lililotekelezwa katika hospitali moja mjini Aleppo, huku uvamizi ndani ya mji wa Idlib kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ukisababisha vifo vya raia 8 na kujeruhi wengine zaidi ya 50.

Shirika la Observatory lenye makao yake mjini London limesema takriban watu 372 wameuawa tangu mashambulizi makubwa kaskazini magharibi mwa Syria yaanze siku ya Jumatano.

Wakati huo huo, televisheni ya taifa ya Syria ilisema kuwa jeshi "liliwaua takriban wanamgambo 1,000 katika muda wa siku tatu zilizopita."

Mamia ya wakazi wa Aleppo walikimbia kwa kuhofia kisasi kutoka kwa makundi yenye silaha, na picha zilionyesha barabara zinazotoka Aleppo zikiwa na magari mengi siku ya Jumamosi wakati watu wakijaribu kuondoka, na moshi ukitanda kwenye anga ya jiji hilo.

Syria imekuwa shwari tangu kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano mwaka 2020, lakini vikosi vya upinzani vimeimarisha udhibiti wa mji wa kaskazini-magharibi wa Idlib na maeneo mengi ya jirani.

Idlib iko kilomita 55 tu kutoka Aleppo, ambayo ilikuwa ngome ya makundi yenye silaha hadi serikali ya Syria ilipoiteka tena kwa msaada wa Urusi mwaka 2016.

Unaweza pia kusoma

Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Seif Abdalla