Safari ya mvulana wa miaka 11 kutoka Syria kwenda Ulaya

- Author, Stefan Veselinovic and Selin Girit
- Nafasi, BBC World Service
Khalil alikuwa na umri wa miaka sita wakati alipoondoka Syria, wakati huo mapigano ya kila siku ya vita vya wenyewe kwa wenyewe yakiendelea.
Alikuwa akiishi katika mkoa wa Homs, magharibi mwa Syria, na baba yake alikuwa dereva wa teksi, pia akiishi na mama yake na dada zake wadogo wawili.
Homs, mji wa tatu kwa ukubwa nchini Syria, wenye watu milioni 1.5 kabla ya mzozo huo, ulikuwa uwanja wa vita katika uasi dhidi ya Rais Bashar al-Assad mapema 2011.
"Kijiji changu kilikuwa kati ya milima miwili, na kulikuwa na mapigano kila usiku," anasema Khalil.

Chanzo cha picha, AFP
Mwishoni mwa 2015 vikosi vya waasi viliondoka Homs na ukawa mikononi mwa serikali.
Wakati wa ghasia maelfu ya watu walishikiliwa chini ya 'sheria ya kukabiliana na ugaidi' ambayo iliharamisha takribani shughuli zote za upinzani, hata za amani.
Baba yake Khalil Ibrahim alikuwa mmoja wa wale waliowekwa kizuizini.
“Serikali ilimtia jela. Alipotoka, sisi [kama familia] tulipitia mengi. Kwa hiyo, tuliamua kuondoka Syria,” anasema Khalil.
Hivyo ndivyo safari yake ndefu ya muongo mmoja akiwa mvulana mkimbizi ilipoanza.
Kituo cha kwanza: Lebanon
Tangu kuanza kwa mzozo wa Syria, watu milioni 12 wamelazimika kuyahama makazi yao. Zaidi ya milioni sita wameondoka nchi hiyo. Inakadiriwa kuwa Wasyria milioni 1.5 wanaishi katika nchi jirani ya Lebanon.

Kwa familia ya Khalil Lebanon ilikuwa kituo cha kwanza pia. Walikaa kwenye nyumba ya rafiki wa familia yao, naye kutoka Syria kwa karibu mwaka mmoja, lakini hatimaye waliamua kuondoka kwani waliona hakuna mustakabali wa maisha yao hapo.
Walisafiri hadi Uturuki, kisheria, kwa ndege.
Uturuki ilikuwa imepitisha sera ya kufungua milango kwa Wasyria tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe kuanza na inaendelea kuwahifadhi wakimbizi wa Syria waliosajiliwa zaidi ya milioni 3.6.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Khalil na familia yake waliishi Istanbul, jiji kubwa zaidi la Uturuki, lenye zaidi ya Wasyria 500,000, kati ya watu milioni 16.
Waliishi huko kwa miaka minne, lakini walipata ugumu kutamalakiana na jamii huku kukiwa na ongezeko la mivutano kati ya wenyeji na wakimbizi.
"Huko Istanbul, watoto [wa Kituruki] walikuja kwangu na kusema: 'Kwa nini usirudi Syria?' Nilikabiliana na matatizo mengi,” anasema.
Kufikia katikati ya mwaka 2019, ripoti zilianza kuibuka za Uturuki kuwafukuza mamia ya Wasyria warejee nchini mwao kinyume na matakwa yao. Serikali ya Uturuki ilikanusha jambo hilo.
Kwa kuogopa hali kama hiyo, familia ya Khalil iliamua kuendelea na safari. Walisafiri hadi mji wa pwani wa kusini-magharibi wa Bodrum ili kuanza safari ya kuvuka Bahari ya Aegean kuelekea Ugiriki.
Walijaribu mara tatu bila mafanikio. Katika jaribio lao la nne, kwenye mashua iliyobeba watu wapatao 50, Khalil na familia yake walifanikiwa kukanyaga kisiwa cha Ugiriki cha Kos.
"Tulifikiri tuko katika ndoto. Tulikuwa na furaha, tuko salama na tulimshukuru Mungu kwa hilo. Sasa tunaweza kujenga maisha yetu,'” anasema Khalil.
Kuiacha familia
Lakini mwaka 2020, visa vya wahamiaji na wakimbizi kufukuzwa Ugiriki na kurudishwa Uturuki viliripotiwa.
Mashirika ya haki za binadamu yaliikosoa serikali kwa kuwatendea vibaya wanaotafuta hifadhi. Mamlaka za Ugiriki wakati huo zilikanusha kuwatendea vibaya wahamiaji.
Ibrahim aliogopa zamu yao ingefika. Khalil alipendekeza aachane na familia yake na asafiri hadi Ulaya peke yake.
"Mwanzoni baba yangu alisema, hapana. Lakini baada ya kutafakari, aliniuliza: 'Mwanangu, una uhakika?' 'Ndiyo,' nikajibu. 'Sawa,' alisema. “Utakwenda hivi karibuni. Jitayarishe."
Aliiacha familia yake, Oktoba 2020, akiwa na umri wa miaka 13, Khalil alikwenda Albania pamoja na kikundi cha wakimbizi wengine.
Walitembea zaidi ya kilomita 165, kupanda milima na kuvuka mito, bila chakula, wakiwa na chokoleti tui ili kuupa mwili nguvu.
Kundi hilo lilikuwa na maji na mifuko ya kulalia. Walirekodi safari yao ya majaribio kwenye simu zao, na wakafanya mzaha ili wawe na matumaini.

Baada ya majuma mawili safarini, walifika Pristina, jiji kuu la Kosovo. Wakiwa wamedhamiria kwenda mbali zaidi, walianza kuelekea nchi jirani ya Serbia.
Novemba 2020, Khalil aliwasili katika mji mkuu wa Serbia, Belgrade. "Nimechoka sana," alisema wakati akijirekodi saa 5 asubuhi kwenye kamera ya simu yake.
Safari inaendelea
Khalil alitaka kusafiri zaidi magharibi mwa Serbia hadi Austria au Uholanzi.
Alifanya majaribio mengi ya kuvuka mipaka ya Umoja wa Ulata. Mara 11 Hungary, mara tatu Croatia na mara moja Romani. Yote yalishindwa.
Baada ya miezi minne ya kujaribu, alipata matatizo ya afya kutokana na kutembea kwa muda mrefu katika hali mbaya ya hewa. Hatimaye alilazimika kukata tamaa na kuishi Belgrade.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya wahamiaji milioni moja na wakimbizi kutoka kote ulimwenguni wametumia njia inayoitwa Balkan kujaribu kufikia nchi za Ulaya tangu 2015.
Baraza la Umoja wa Ulaya la Wakimbizi na Wahamiaji (ECRE) linasema, watu hao hukabiliwa na ghasia, unyanyasaji na kurudishwa na wasafirishaji haramu au vikosi vya usalama huku wakiishi katika mazingira magumu yenye hatari za kiafya.
"Sihisi kama Belgrade ni jiji langu, lakini nina furaha hapa," Khalil, ambaye sasa ni kijana mwenye umri wa miaka 17, aliiambia BBC.
Kwa miaka mitatu, mji mkuu wa Serbia ndio ukawa makao mapya ya Khalil, alianza kwenda shule, kujifunza Kiingereza na Kiserbia, na kupata marafiki wengi.

“Hiki ni chumba changu, na hii ni michoro yangu. Ninapenda kuchora,” alisema huku akionyesha chumba cha kawaida alichopewa na Jessuit Refugee Service (JRS), moja ya mashirika yasiyo ya kiserikali yanayosaidia watoto wakimbizi nchini Serbia.
Michoro hiyo ilibandikwa ukutani. Mmoja wao unaonyesha herufi ya kwanza ya jina la mama yake katika umbo la moyo, mwingine unaonyesha msichana, mwenye mbawa kama malaika, akiruka kutoka baharini kuelekea angani.
"Nilikuwa nimechoka sana baada ya kila kitu kilichotokea Ugiriki, Albania, Kosovo... nilikuja hapa na 'Asante Mungu, nitapumzika. Naweza kulala. Naweza kwenda shule.”

Familia yaungana tena
Khalil alipokuwa Serbia, na baba yake na dada zake walikuwa bado Ugiriki, mama yake alifanikiwa kufika Uholanzi na kufanikiwa kupata hadhi ya ukimbizi.
Septemba 2023, familia iliunganishwa tena, baada ya miezi michache, Khalil aliweza kujiunga nao huko Uholanzi. Hakuwa amewaona wapendwa wake kwa karibu miaka minne. Sasa wote wamepewa hifadhi.

Anatarajia kwenda chuo kikuu mwaka ujao na kusoma kompyuta.
"Nataka kupata marafiki wapya na kuishi maisha ya amani na familia yangu, na kuwa mbali na vita," anasema.
"Niliyopitia maishani mwangu yamenifundisha kujiamini, na kuwa hodari ili kufikia chochote ninachotaka."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla












