Walikwenda Syria kuishi na IS, sasa wamerudi nyumbani

- Author, Na Eleanora Kulenbekova na Daniel Wittenberg
- Nafasi, BBC World Service, Kyrgyzstan
"Karibu tena Kyrgyzstan," anasema Shukur Shermatov, akihutubia darasa la wanawake 20. Amevaa kofia ya kitamaduni, lakini hakuna kitu cha kitamaduni kuhusu kituo hiki. Kiko ndani ya uzio wa kijeshi na wanafunzi ni wanawake waliorejeshwa nyumbani kutoka Syria, ambako waliishi na kundi la Islamic State.
Kituo hicho cha kurekebisha tabia kiko kwenye milima ya kaskazini mwa Kyrgyzstan, na ndipo wanawake na watoto wa wanaume wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa IS hutumia wiki zao sita za kwanza baada ya kurejeshwa makwao.
Timu yetu ya BBC ni miongoni mwa wageni wa mwanzo mwanzo kufika hapa – na kila tunachosema na kufanya kinafuatiliwa kwa karibu na shirika la kijasusi la serikali.
Wanawake wanamsikiliza Shukur kwa makini anapowapa somo lao la kwanza linalohusu uraia, maadili ya kidini na udhibiti wa hasira. Mabango ukutani yanatoa vidokezo kuhusu jinsi ya kudhibiti hisia zako.
Pamoja na mpango huu wa elimu, familia hupokea matibabu, usaidizi wa kisaikolojia, na vilevile kuna chakula cha kutosha, maji na makazi.
Tunaongozwa kwenye bweni lenye vitanda vinne ambapo tunakutana na mwanamke aliyevalia hijabu ya zambarau. Tunamwita Fatima, sio jina lake halisi. Kupitia dirisha dogo, mandhari ya nje ni ziwa la theluji.
"Jambo kubwa hapa ni utulivu. Kila mtu anashukuru sana kwa hilo. Watoto wanapapenda."
Fatima alimfuata mumewe hadi Uturuki mwaka 2013 aliposema anakwenda kufanya kazi huko. Familia nzima ilikwenda, wakiwemo watoto wawili wa kiume wa Fatima, binti yake na mjukuu. Anasema aligundua wako Syria aliposikia sauti ya ndege zikiwa juu na wapiganaji wa IS.
Tulimuuliza ikiwa hakujua wanakwenda wapi (kama wanawake wengi tuliokutana nao) alisisitiza hakujua na ilikuwa kawaida kwa mwanamke kumfuata mume wake.
Siku chache baada ya kufika Syria, aliungua moto karibu kufa baada ya bomu kugonga gari lake na mtoto mmoja wa Fatima aliuwawa na mdunguaji. Mwanawe mwingine aliugua na kufariki muda mfupi baadaye.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hawakuweza kuondoka, wanawake hao walitumia karibu miaka sita chini ya utawala wa IS nchini Iraq na Syria. Binti wa Fatima alipata watoto zaidi.
Wakati wapiganaji wa IS walipofukuzwa, Fatima, binti yake na wajukuu wanne waliishia katika kambi ya al-Hol - ni kubwa zaidi nchini Syria, inahifadhi washukiwa wa IS na familia zao. Walikaa miaka minne huko, wakitamani sana kurudi nyumbani.
"Wanawake walikuwa wagonjwa na watoto walikuwa wakilia kila wakati. Tulikuwa tukiwaomba watuache tuondoke," anasema. "Tulipona kwa shida. Watu kutoka Kyrgyzstan walipokuja kuchukua kundi la kwanza, kila mtu alishtuka."
Oktoba, binti yake na wajukuu waliambiwa wanarejeshwa nyumbani, lakini sio Fatima, ambaye alilazimika kusubiri kwa muda mrefu zaidi.
"Nililia waliponiambia sikuwepo kwenye orodha hiyo. Vipi sikuwa kwenye orodha? Mimi ni mama yao. Lakini kwa kuwa sasa nipo hapa na hivi karibuni nitaungana na familia yangu, nina furaha sana. Nina furaha wajukuu wangu wanaweza kupata elimu. Nataka wasome sayansi, waielewe dunia vizuri zaidi."
Ana umri wa miaka 57, Fatima ndiye mwanamke mkubwa zaidi kwa umri katika kituo hiki na alikuwa mmoja wa akina mama 110 na watoto 229 wa ki-Kyrgyzstan waliorudishwa kutoka Syria mwaka 2023. Kyrgyzstan ilirudisha watu wengi zaidi mwaka jana kuliko nchi yoyote isipokuwa Iraq.
Inapanga kuwarejesha wanawake wengine 260 na watoto, baada ya miaka mingi ya kampeni za jamaa wa watu waliokwama nchini Syria. Lengo ni kuwapa fursa ya pili watu ambao serikali inaamini ni waathiriwa.
Wanaorudishwa wote wanahojiwa na wanapomaliza kozi na kurudi nyumbani, wanabaki chini ya uangalizi.
Mkuu wa baraza la usalama la taifa la Kyrgyzstan alituambia wanawake tisa wanakabiliwa na uchunguzi kuhusu uhalifu huku timu yake ikijaribu kujua ni lini hasa waliondoka Kyrgyzstan.
Pia kujua, walikuwa na nani na kama wana hatia ya kusaidia ugaidi au kusafirisha watoto kwenye eneo la vita. Bado hakuna aliyeshtakiwa au kuhukumiwa, lakini adhabu ya juu zaidi ni kifungo cha miaka 11 jela.
Tunakutana na mwanamke mwingine, Elmira, amepitia kozi hiyo na sasa anajenga upya maisha yake katika mji ulio nje ya mji mkuu, Bishkek. Anatembelewa mara kwa mara na kupata usaidizi wa kifedha kutoka Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu.
Muda mfupi baada ya kupanga kuonana naye, tulipigiwa simu na mfanyakazi wake wa kijamii, akitujulisha naye atakuwepo pia kwenye mahojiano. Tulipofika, polisi wawili wa kukabiliana na ugaidi, vilevile walikuwepo. Baada ya mazungumzo, walikubli kusubiri nje.

Elmira anadai alilaghaiwa kwenda Syria na mwanaume aliyekutana naye mtandaoni. Alimshawishi ajiunge naye Uturuki. Siku nne baada ya kutimiza miak 18 alisafiri kwenda kukutana naye.
Lakini alipofika huko, alilakiwa na mwanaume tofauti aliyesema ni rafiki yake na kusafiri naye kwa saa 17 kuvuka mpaka wa Siria. Anadai baada ya kujua kilichokuwa kikiendelea, alishachelewa kurudi nyuma.
Aliolewa mara mbili. Mume wake wa kwanza alifariki baada ya miezi michache, kisha akaolewa na mwanaume kutoka Dagestan na kupata mtoto. Hakusema alichokuwa akikifanya nchini Syria lakini anaeleza walikuwa wakitafuta njia ya kutoroka kabla ya mume kuuwawa katika shambulio la roketi.
Elmira anasema wakati mgumu zaidi ni pale alipofikiri binti yake ameuwawa. Alikuwa ametoka nje, akamwacha mtoto wake mdogo ndani, wakati makombora yalipopiga eneo la jirani. Akiwa na hofu, Elmira alirudi nyumbani huku akilia lakini alimkuta akiwa hai.
Kama Fatima, Elmira na binti yake waliishia katika kambi ya al-Hol.
"Bado siamini. Wakati mwingine huamka usiku na sijui kama ninaota," anatuambia. "Ninashukuru sana kwa kila mtu ambaye alisaidia kututoa huko na hawakutuacha. Tunajua sio kila nchi hufanya hivyo."
Elmira, ambaye sasa anajifunza ushonaji, alituomba tusifichue jina lake halisi. Baada ya kuona namna watu wanavyozungumza juu ya kurejeshwa kwao kwenye mitandao ya kijamii, ameamua kutomwambia mtu yeyote kuhusu maisha yake ya nyuma.
"Watu wanafikiri tumerudi hapa na bunduki na mikanda ya kujilipua, sio hivyo. Sisi ni watu kama wao. Pia tuna familia, tuna watoto pia tunataka kuishi maisha ya amani na furaha.
"Na kwa nini niwaambie watu, wakati mimi mwenyewe nataka kusahau?" Elmira anaongeza. "Nilikuwa na umri wa miaka 18 wakati huo. Nina miaka 27 sasa. Nimejifunza kutokuwa mjinga."
Binti wa Elmira mwenye umri wa miaka tisa - ametumia muda mwingi wa maisha yake katika kambi ya al-Hol. Anatuonyesha michoro yake ikisomeka, "Tunataka kurudi Kyrgyzstan" na "Turudisheni kwenye usalama."

Chanzo cha picha, Getty Images
Mama yake Elmira, Hamida Yusupova, alitumia muongo mmoja uliopita kuomba mamlaka kumrudisha bintiye na mjukuu wake, na alianzisha kikundi cha kampeni kwa ajili ya wazazi wa wasichana waliokwenda Syria.
"Namshukuru Mungu, amerejea nyumbani na hatimaye nimekutana na mjukuu wangu. Lakini Elmira amepoteza miaka tisa ya ujana wake. Ni muda mrefu."
Hamida alipokuja kumchukua Elmira katika kituo hiki, alijaa machozi zaidi ya maneno. "Elmira alikuwa akisema tu: 'Mama, nisamehe, nisamehe.' Hakuna kingine. Mbali na hilo, aliniambia jinsi nilivyo zeeka!"
Asilimia 90% ya raia wa Kyrgyzstan wanajitambulisha kuwa Waislamu – watu wengi walijiunga na IS, kundi la kigaidi kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Hamida anaamini binti yake alikuwa mwathirika wa wanaume wadanganyifu.
Tulizungumza na wanawake wa Kyrgyz wenye umri sawa na Elmira ambao wana wasiwasi kwamba wanaorejea wanaweza kuwabadili watu wengine.
“Kama mama nimesikia matusi na kejeli nyingi, sitaki mtoto wangu asikie, sitaki watu wamnyooshee mtoto wangu vidole na kumwita gaidi,” Hamida anasema.

Naibu Waziri Mkuu, Edil Baisalov, ana shauku ya kuonyesha dunia kuwa sera ya kuwarejesha makwao ni uthibitisho kwamba Kyrgyzstan ina demokrasia ya uvumilivu ya kuwajali raia wake wote.
"Jambo bora zaidi ni kwamba wasahau jinamizi ambalo wamepitia," ametuambia.
Baisalov anajua hili ni jambo lenye utata, hasa katika baadhi ya nchi za Magharibi. Baisalov alikuwa balozi nchini Uingereza muda mfupi baada ya Shamima Begum, mmoja wa wasichana watatu wa shule kutoka London walioondoka na kujiunga na IS na kunyang'anywa uraia wake wa Uingereza.
"Kwa Kyrgyzstan, huu haukuwa uamuzi rahisi," anasema. "Bila shaka aina yetu ya Uislamu haina misimamo mikali. Ni Uislamu wa uvumilivu sana, unaoheshimu dini nyingine. Sisi ni taifa dogo linalohitaji kujaliana. Hata wale wanaofanya makosa."
Mpango huo unaungwa mkono na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto Unicef na Sylvi Hill, ambao wanaongoza juhudi za kuwarejesha makwao nchini Kyrgyzstan.
Wanawake tuliozungumza nao wanasema wanashukuru kupewa nafasi hii ya pili, na wanafahamu vyema kuna karibu wengine 50,000 kutoka kote ulimwenguni bado wamekwama kwenye kambi kaskazini mwa Syria.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












