Vijana wanaotaka kujiunga na Islamic State kukimbia umaskini

Kijana

Ahmed bado ni kijana mdogo lakini badala ya kusoma, kila siku anaenda kazini.

Anaishi katika mji wa Lebanon wa Tripoli, kaskazini mwa nchi, mojawapo ya maeneo maskini zaidi katika Mediterania.

Licha ya masaa anayoweka, anapata dola chache tu kwa wiki.Anahitaji kumsaidia mama yake mgonjwa, lakini kazi yake ngumu haimruhusu kupata pesa za kutosha kuwalisha wote wawili.

Hisia hiyo ya kukosa tumaini ilimfanya atafute njia ya kutoka. Akiwa kwenye mgahawa wa Intaneti mjini Tripoli, alianza kuzungumza na mtu ambaye alimwambia kuwa alikuwa mwajiri wa Islamic State, wanamgambo wenye itikadi kali wa Kiislamu wa Sunni ambao wakati fulani walidhibiti maeneo makubwa ya Syria na Iraq, na wamefanya ukatili na vitendo vya ugaidi. katika kanda na duniani kote.

"Nilikuwa nasoma sharia (sheria za Kiislamu), na siku baada ya siku walituambia kuhusu jihad," Ahmed anasema.

"Walituambia kuhusu Iraq na kundi la Islamic State (IS). Tuliipenda IS, kwa sababu ilikuwa maarufu.

Mwanamume mmoja gerezani aliwasiliana nami na kusema: 'Nitakupeleka huko.'

Mamake Bakr Seif, mmoja wa Walebanon ambaye amejiunga na Islamic State, anashikilia picha yake.
Maelezo ya picha, Mamake Bakr Seif, ambaye amejiunga na Islamic State, anashikilia picha yake.

Ahmed alikuwa amefanya uamuzi. Alimwambia mwajiri huyo kwamba alitaka kujiandikisha, kuondoka Lebanon na kusafiri kupigana na kundi hilo nchini Iraq na Syria. Lakini, ndani ya saa chache, polisi walimkamata.

Maafisa wa kijasusi wa jeshi la Lebanon walimhoji kwa siku tano kabla ya kumwachilia. Hili lilimfanya ajutie uamuzi huo, lakini bado hajapata suluhisho la matatizo yake mengi.

"Inanifanya nitamani kujiua. Nina deni la pesa nilizokopa kununua samani za chumba changu, lakini sina uwezo wa kurudisha. Hatujui kitakachotokea siku za usoni," anasema.

Katika mitaa ya viungani mwa mji wa Tripoli, hali ni ngumu. Hakuna umeme, maji, mafuta, dawa na ajira.

Inaaminika kuwa takriban vijana mia moja wa Lebanon wamejiunga na Islamic State mwaka uliopita.

Lakini sio tu kuambatana na itikadi kali inayowakisha kundi hilo. Pia wanajaribu kutoroka umaskini uliokithiri nchi yao inayokumbwa mgogoro.

Wengi, kwa sababu ya ushirika wao wa kidini au malezi ya familia, wana fursa chache za kufanikiwa.

Vita hivyo vya kujinusuru vimewafanya baadhi ya vijana kuchukua hatua za kukata tamaa.

hakuna fursa

Nabil Sari ni jaji maarufu wa Tripoli. Amewahi kushughulikia kesi za aina hii hapo awali. "Hawana nafasi za kazi, hawana nafasi za masomo. Na baadhi ya waliojiunga na IS ndiyo maana walitubu na kujaribu kuwasiliana na familia zao ili warudi, lakini sasa hawawezi."

Islamic State kwasasa haina nguvu iliyokuwa nayo Mashariki ya Kati. Kwa muda kundi hilo lilidhibiti maeneo nchini Syria na Iraq. Lakini lilishindwa katika vita vikali vya umwagaji damu huko Baghouz nchini Syria mnamo 2019.

Lakini wachache ambao hawakuuawa au kufungwa wanaendelea kushambulia maeneo waliyowahi kudhibiti. Na, mapema mwaka huu, taarifa zilianza kuibuka kuhusu washiriki wa Lebanon katika mashambulizi hayo.

Wadi Khaled, ambapo baadhi ya watu waliotoweka walikuwa wakiishi, ni kitongoji kinachokabiliwa na umaskini. Watoto hutumia siku nzima kucheza kwenye vichochoro vyenye vumbi. Kutokana na mgogoro huo, wengi hawana fursa ya kwenda shule.

Tripoli ni mojawapo ya maeneo maskini zaidi katika Bahari ya Mediterania.
Maelezo ya picha, Tripoli ni mojawapo ya maeneo maskini zaidi katika Bahari ya Mediterania.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Serikali haifiki hapa," anaelezea Mohammed Sablouh, wakili anayewakilisha familia za vijana kadhaa."

Angalia maeneo haya ya umaskini. Hakuna anayejali. Nchi haifanyi wajibu wake kwa raia wake. Na tabaka hili la watu masikini litatumika na kuajiriwa kwa IS."

Bakr Seif alitoweka mwaka mmoja uliopita. Alikuwa amebakiza wiki kadhaa kabla ya kufunga ndoa.

Ingawa alikuwa amekamatwa na kukaa gerezani kwa muda, alikuwa akijenga mustakabali na mchumba wake. Hakumwambia mama yake Umm Seif kwamba alipanga kuondoka.

“Alituambia kuwa anakwenda kumuona mchumba wake na atarudi saa sita mchana,” anasema huku macho yake yakibubujikwa na machozi. "Aliondoka na hakurudi tena."

"Tulipata taarifa kwenye mitandao ya kijamii," anaendelea babake, Mahdi. "Ilikuwa kwenye simu zetu zote. Hatukuamini. Na kisha kila mtu akaanza kupiga mayowe na kulia." Umm Seif ananyamaza na kufuta macho yake.

“Alikuwa na furaha, anajiandaa kwa harusi yake na alikuwa na furaha, alikuwa ametoka gerezani, alikuwa ni kijana mzuri sana, mwenye heshima, adabu, unaweza kufikiri nasema hivyo kwa sababu mimi ni mama yake, lakini huu ndio ukweli."

Wazazi

Haukupita mwezi mmoja, Umm Seif akapokea ujumbe wa sauti. Sauti mbaya iliyobadilishwa na kompyuta ilimwambia kwamba mtoto wake alikufa akiwapigania IS nchini Iraq.

Ajabu, alimtaja kama "aliyeuawa" badala ya "kuuawa kishahidi", neno ambalo ujumbe wa kweli wa IS ungetumia kawaida.

Wazazi wa Bakr hawaamini ujumbe huo wa sauti, wala kile ambacho mamlaka ya Lebanon imewaambia kuhusu hatima yake. Wanaamini kwamba hakuwahi kuondoka Lebanon na bado amefichwa na kuwekwa kizuizini mahali fulani nchini.

Baba yake Bakr, Mehdi, anaonyesha nyumba ya mwanawe. Ni safi na nadhifu, lakini tupu, na inaonekana kutelekezwa. Chokoleti zilizofunikwa kwa dhahabu ambazo Bakr alinunua kwa ajili ya harusi yake zimesalia kwenye onyesho, bila kuliwa

Jeshi la Iraq linadai kuwa Bakr aliondoka Lebanon na kusafiri kwenda huko kujiunga na Islamic State.

Wanadai kwamba alishiriki katika shambulio kwenye kambi ya jeshi huko Diyala ambalo liliua wanajeshi 10.

Siku kadhaa baadaye, wanamgambo tisa wa IS waliuawa katika shambulio la anga la vikosi vya Iraq. Nusu yao walikuwa Walebanon.

Jenerali wa Jeshi la Iraq Yahya Rasoul Abdulla anazungumzia watu hawa wanaoondoka Lebanon na kujiunga na Islamic State kwa kutumia maneno makali.

JeneralI wa Iraq Yahya Rasoul Abdulla.
Maelezo ya picha, JeneralI wa Iraq Yahya Rasoul Abdulla.

"Ujumbe wangu kwa ulimwengu wa Kiarabu, na haswa kwa vijana wa Lebanon, ni kwamba shirika hili la kigaidi linawatumia kama lishe ya mizinga. Unaweza kuwauliza Wairaqi waliokuwa wakiishi chini ya utawala wa Dola ya Kiislamu: waliua watu, waliwabaka wanawake, Waliwafanya watumwa, waliharibu urithi, waliharibu miundombinu yote, hata waliharibu makaburi ya nabii. Msiwe chachu ya vita vyao, msitumike nao", anathibitisha jenerali huyo.

Na anaongeza: "Jeshi la Iraq liko kila mahali. Popote ambapo shirika hili linakwenda, katika jangwa, milima, mabonde, tutawawinda na kuwaua."

Tangu kilele kilichorekodiwa mapema mwaka huu, idadi ya wanaojiunga na Islamic State imeanza kupungua. Hadithi za wale walioondoka sasa zinajulikana sana mjini Tripoli, na hilo linafanya matarajio ya kuwafuata yasiwe ya kuvutia.

Lakini wakati Lebanon inaendelea kupambana na mzozo wake wa kifedha na wanasiasa wake kukwama kuunda serikali mpya miezi kadhaa baada ya uchaguzi wa nchi hiyo, maisha hayawi rahisi.

Na kwa hivyo, waajiri wa Islamic State wanaendelea kukusanyika kwa matumaini ya kuvutia kizazi kipya cha vijana wa Lebanon walionyimwa haki.