‘Ilikuwa kama siku ya maangamizi, ningemuokoaje mwanangu?’

Chanzo cha picha, Ismael Alrej
Ni ndoto mbaya zaidi ya kila mzazi. Mtoto wako ni mgonjwa, unamleta hospitali na kulazwa.
Unapumua kidogo na unatoka nje kwa dakika moja.
Wakati huo huo, maisha ya Ismael mwandishi wa habari anayeishi katika mkoa wa Idlib kaskazini mwa Syria yalikuwa hatarini.
Saa 04:18 (01:18 GMT), tetemeko kubwa la ardhi la kipimo cha 7.8 lilitokea. Kila kitu kilichomzunguka kilitetemeka kwa nguvu kwa dakika mbili.
"Kisha tetemeko la ardhi likazidi kuwa na nguvu," ananiambia kupitia simu ambayo mawasiliano yalikuwa hafifu.
"Umeme ulikatika na mlango wa kuingilia hospitalini uliotengenezwa kwa kioo ukaanza kukatika."
Aliona majengo mawili ya makazi yakiporomoka umbali wa mita 150 na alichanganyikiwa kabisa na giza la ghafla.
"Ilikuwa kama hali ya siku ya mwisho," anasema. "Nilianza kufikiria jinsi ningelazimika kumwokoa mwanangu kutoka kwenye vifusi."
Dakika moja baadaye, alimuona mtoto wake Mustafa akimkimbilia huku akipiga kelele na kulia. Alikuwa ametoa dripu yake ya IV, na damu ilikuwa ikitoka mkononi mwake.
Kwa hadi saa moja, hakuna mtu aliyeweza kufikia majengo yaliyoporomoka. Hawakuweza kuita vitengo vya ulinzi wa raia ama kwa sababu ya nguvu na kupunguzwa kwa mtandao.

Chanzo cha picha, Syrian American Medical Society
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Al-Dana ni mji unaoshikiliwa na upinzani karibu na mpaka na Uturuki.
Vitengo vya ulinzi wa raia ndio watoa huduma wa kwanza wa dharura kwa kukosekana kwa huduma zozote za serikali, lakini ukubwa wa uharibifu ulifanya iwe vigumu kwao kufikia kila mtu aliyeathiriwa.
Saa chache baadaye, Ismael alikwenda kutathmini hali katika jimbo lote la Idlib.
"Uharibifu huo hauelezeki," anasema "Maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni yale ambayo hapo awali yalishambuliwa na serikali ya Syria au vikosi vya Urusi."
Machafuko ya Syria mwaka 2011 yaliingia katika vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe ambapo utawala wa Syria, ukiungwa mkono na Urusi, ulishambulia maeneo yanayodhibitiwa na waasi.
Sasa kaskazini-magharibi mwa Syria imegawanyika katika sehemu ndogo za kanda zinazodhibitiwa ama na vikosi vya upinzani vya Syria au serikali yenye makao yake mjini Damascus.
Ismael aliona makumi ya majengo ya makazi yameharibiwa katika mji wa Atareb, kaskazini mwa Aleppo.
"Kuna majengo mengi na vitongoji ambavyo timu za uokoaji haziwezi kufika kwa sababu ya uhaba wa vifaa," anasema.
"Kwa kweli tunahitaji msaada kutoka kwa mashirika ya kimataifa."
Rasilimali
Daktari Osama Salloum anafanya kazi katika Shirika la Madaktari la Syrian American Medical Society (SAMS) ambalo linasaidia idadi ya hospitali katika maeneo yanayoshikiliwa na upinzani kaskazini-magharibi.
"Nilikuwa katika hospitali ya SAMS huko Atareb saa chache baada ya tetemeko hilo," anasema.
"Nilipotoka hospitali kulikuwa na vifo karibu 53. Sikuweza kuhesabu idadi ya waliojeruhiwa."
Anasema zaidi ya watu 120 sasa wamefariki katika hospitali hiyo pekee.

Chanzo cha picha, Syrian American Medical Society
Dk Salloum anasema hospitali hizo zina rasilimali ndogo za kukabiliana na janga kama hilo.
"Wengi wa watu waliookolewa kutoka kwenye kifusi wana majeraha makubwa ambayo yanahitaji matibabu maalum na vifaa vya hali ya juu," anasema, akiongeza kuwa hospitali ya Atareb ina mashine moja ya zamani ya CT scanner.
Misaada mingi huja kupitia Uturuki na inakabiliwa na ukaguzi mkali wa mpakani.
Huku Uturuki ikikabiliwa na mzozo mkubwa wa kibinadamu yenyewe, haijafahamika ni vifaa gani vitafika katika maeneo yanayoshikiliwa na upinzani nchini Syria.
"Tukikosa vifaa vya matibabu vya sasa, tutateseka," anasema Dk Salloum.
Tetemeko hilo la ardhi pia lilikumba maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa serikali kaskazini.
Aya, ambaye alipenda kutaja jina lake la kwanza, alikuwa kwenye safari ya kutembelea familia yake katika jiji la Latakia ilipotokea.
Mpishi huyo mwenye umri wa miaka 26 alikuwa amelala na Mama yake na ndugu zake watatu wakati umeme ulipokatika.

Chanzo cha picha, Reuters via SANA
"Nilitoka kitandani lakini sikuwa na uhakika ni nini kiliniamsha," ananiambia.
"Sikuelewa kilichokuwa kikiendelea hadi nilipowakuta wengine wa familia yangu pia wakiwa wameamka."
Nyumba ya familia yake iko kwenye barabara kuu na ina madirisha ya kioo kote.
"Hatukuweza kusogea kwa sababu ya jinsi tetemeko hilo lilivyokuwa na nguvu," anasema. "Tulibaki tumeganda papo hapo."
Mama wa Aya ana ugonjwa wa Parkinson. Alikuwa amejawa na hofu.
"Nilikuwa na mshtuko na sikuweza kusonga," anasema Aya. "Niliendelea kuangalia jinsi kuta zilivyokuwa zikitikisika na kusonga mbele na nyuma."
"Siwezi kukuelezea jinsi hali ilivyokuwa ya kichaa."
Haneen, mbunifu mwenye umri wa miaka 26, pia anaishi Latakia. Ananiambia vijana wa mtaani kwake waliweka mahema ili watu wajikinge na mvua.
Kwa kawaida hema hizo hutumiwa kuwakaribisha waombolezaji wakati wa mazishi. Ni wazo gumu kwa Haneen.
Mama yake alikuwa kijijini kwao na yuko salama, lakini Haneen ana kiwewe.
"Sina hakika kama nilimsaidia dada yangu au mimi mwenyewe kuondoka nyumbani kwanza na siwezi kukabiliana na kumuuliza," anasema.
Walijihifadhi mbele ya duka lao la kuoka mikate kabla ya kurudi nyumbani.

Chanzo cha picha, BBC News
Mambo yalikuwa magumu zaidi kwa Aya kwani usiku wa manane hakuweza kupata teksi wala makazi wakati wa dhoruba kwa dada na mama yake.
Aya na familia yake hatimaye walifanikiwa kufika Damascus lakini hana uhakika kwamba anaweza kurejea kwenye nyumba huko Latakia.
"Tulishuhudia vita na tukalazimika kutoka nje ya nyumba yetu mnamo 2012," anasema.
"Hisia niliyokuwa nayo katikati ya tetemeko la ardhi ilikuwa tofauti sana na nilivyohisi wakati wa vita.
"Nilihisi kwamba wakati huo, kila kitu karibu nami kinaweza kuanguka," anasema.
"Ningeweza kumpoteza mama yangu au dada yangu. Ilikuwa ni hisia nzito sana na ngumu."
Hata kufikia usalama wa Damasko hakungeweza kusaidia kikamilifu.
Aya alihisi kizunguzungu kwa saa nyingi, kana kwamba tetemeko la ardhi bado lilikuwa likiendelea.
"Ilikuwa kama jeraha linalofunguka tena. Jeraha kubwa ambalo lilikuwa likipona polepole lakini limefunguka tena," anasema, akitafakari zaidi ya muongo mmoja wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
"Jeraha lilifunguliwa tena kwa kila mtu nchini Syria."














