Nini cha kufanya linapotokea tetemeko la ardhi?

Chanzo cha picha, Reuters
Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.8 katika kipimo cha Richter lililozikumba nchi za Uturuki na Syria siku ya Jumatatu huenda likawa mojawapo ya matetemeko yaliyosababsha vifo vya watu wengi zaidi muongo huu, huku zaidi ya vifo 2,600 vimeripotiwa katika nchi zote mbili.
Uturuki ni nchi inayokabiliwa na matetemeko ya ardhi yenye uharibifu mkubwa. Kati ya mwaka 1939 na 1999, ilishuhudia matetemeko makubwa matano.
Tangu 1900, zaidi ya watu 90,000 wamepoteza maisha katika matetemeko karibu 76. Nusu ya vifo hivyo vilitokea kati ya mwaka 1939 na 1999.
Matetemeko mengine makubwa ya ardhi katika miongo miwili iliyopita yalitokea Haiti mnamo mwaka 2021 - na kusababisha vifo vya zaidi ya 2,200 - na Indonesia mnamo 2018, na kuua zaidi ya watu 4,300. Nchini Iran mnamo mwaka 2017, zaidi ya watu 400 walikufa katika tetemeko la ardhi.

Chanzo cha picha, Reuters
Utabiri wa matetemeko
Wanasayansi wanasema, hata ikiwezekana kujua ni wapi kuna uwezekano wa kutokea matetemeko ya ardhi, bado tuko nyuma sana kukadiria ni lini yatatokea. Kwa hivyo yanaweza kutabirik?
"Kwa kusikitisha hapana," anasema mtaalam, Dk Stephen Hicks kutoka Imperial College London.
"Lakini tunachoweza kufanya ni kutabiri matetemeko ya ardhi. Tunaweza kutoa uwezekano. Katika [maeneo] kama vile California, Marekani, na Japan, utabiri wa tetemeko la ardhi unaanza kufanya kazi zaidi."
Kwa hivyo unaweza kufanya nini ili ubaki salama na nini usifanye?

Chanzo cha picha, Reuters
Jiandae
Ingawa si rahisi kutabiri ni lini tetemeko la ardhi litatokea, kulingana na wataalamu unapaswa kuwa tayari kila wakati, kumaanisha kuwa unapaswa kuwa na mpango dhidi ya tetemeko la ardhi.
"Ikiwa unaishi katika eneo [ambalo yanakumbata na matetemeko mengi ya ardhi], ni vizuri kuwa na boksi, mfuko au pakiti ya dharura nyumbani kwako," anasema Dk Hicks. Anasema inapaswa kuwa na maji ya akiba, tochi, kifaa cha huduma ya kwanza na baadhi ya vyakula.
Kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu, seti hiyo inapaswa pia kuwa na pesa taslimu za ziada na nakala za hati muhimu binafsi, kama vile orodha ya dawa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Salia ulipo, ikiwa jengo ulilomo ni salama
Kulingana na Utafiti wa Jiolojia wa Marekani, taasisi ya kisayansi ya serikali ya Marekani, kuna uwezekano mdogo wa kujeruhiwa ukikaa mahali ulipo. Kwa hivyo usijaribu kukimbia nje au kwenye vyumba vingine wakati wa tetemeko la ardhi, wakala anashauri.
"Lala chini, jibanze na ujishikilie" ndio kauli mbiu ya kukaa salama, wataalam wanasema. Kutambaa chini kwa mikono na magoti yako kungekulinda kutokana na vitu vinavyoanguka na bado kuruhusu nafasi kusonga kidogo, ikiwa ni lazima. Unapokuwa umejibanza chini ya meza au dawati, ikiwa hakuna sehemu nyingine karibu, ushauri ni kusalia hapo mpaka tetemeko lipite.
Mojawapo ya kimbilio la kwanza la kukinga ni kusimama kwenye mlango. Lakini wataalam wanasema utakuwa salama chini ya meza ikiwa unaishi katika nyumba ya zamani.
Madirisha na mbele mara nyingi ni sehemu za kwanza za jengo kuanguka. Kwa hivyo, ushauri ni kukaa mbali na maeneo haya hatari.

Chanzo cha picha, Reuters
Nenda nje ikiwa salama kufanya hivyo
Mara tu mtikisiko unapokoma, kwa ujumla ni salama zaidi kutoka nje ikiwa jengo ulilomo litaanguka.
Yote hii ni kama limekukuta ukiwa ndani. Lakini vipi ikiwa tetemeko litapiga ukiwa nje?
“Kaa hapo ulipo,” wanasema wataalamu hao. Kuondoka kutoka kwenye majengo, nyaya za umeme, shimo, njia za mafuta na gesi kunaweza kupunguza hatari ya kuumia. Pia, ni bora kwenda kwenye eneo la wazi, mbali na miti, nguzo za simu na majengo.

Chanzo cha picha, Reuters
Kaa mbali na hatari
Kwa mujibu wa Mamlaka za kushughulikia majanga, majeraha na vifo vingi husababishwa na kuanguka au kuruka vitu kama vile televisheni, taa, vioo na makabati ya vitabu. Njia moja ya kuepuka kuumia ni kuweka samani zenye uzito wa juu kwenye kuta.
Hatari nyingine inayoweza kutokea ni gesi inayotoka kwenye mabomba yaliyopasuka baada ya tetemeko la ardhi.
Dk Hicks anatoa mfano wa tetemeko la ardhi la San Francisco mwaka 1906, ambapo zaidi ya watu 3,000 waliuawa.
"Vifo vingi vilitokea kwa sababu ya kulipuka kwa mabomba ya gesi, badala ya kutikisika [au] majengo kuporomoka," anasema, akishauri kujiepusha na vitu vyote vinavyoweza kusababisha moto katika eneo hilo.

Chanzo cha picha, Reuters
Mazoezi
Dk Hicks pia anasisitiza umuhimu wa mazoezi ya tetemeko la ardhi.
"Katika baadhi ya nchi, wana mazoezi yanayohusu tetemeko la ardhi ambapo kila mtu anatakiwa kwenda kwenye zoezi hili kuhusu nini cha kufanya. Lakini hii pengine haikutokea katika eneo hili la Uturuki kwa vile hakujawa na tetemeko la ardhi kwa muda mrefu hivyo."

Chanzo cha picha, Reuters














