Mjane wa kiongozi wa IS afichua maisha aliyoishi na mumewe

Katika mahojiano nadra kutoka gerezani, mjane wa kiongozi wa kundi la Islamic State ameelezea maisha yao.
Umm Hudaifa alikuwa mke wa kwanza wa Abu Bakr al-Baghdadi na aliolewa naye huku akisimamia utawala wa kikatili wa IS kwenye sehemu kubwa za Syria na Iraq.
Sasa anazuiliwa katika jela ya Iraq huku akichunguzwa kwa uhalifu unaohusiana na ugaidi.
Katika majira ya joto ya 2014, Umm Hudaifa alikuwa akiishi Raqqa, ngome ya IS nchini Syria wakati huo, pamoja na mumewe.
Akiwa kiongozi anayetafutwa wa kundi la wanajihadi wenye msimamo mkali, Abu Bakr al-Baghdadi mara nyingi alitumia muda katika maeneo mengine, na katika moja ya matukio hayo alimtuma mlinzi kwenye nyumba hiyo kuwachukua watoto wao wawili wa kiume.
"Aliniambia walikuwa wakisafiri kwenda kuwafundisha wavulana jinsi ya kuogelea," anasema Umm Hudaifa.
Kulikuwa na televisheni ndani ya nyumba ambayo alikuwa akiitazama kwa siri. "Nilikuwa nikiiwasha wakati hayupo nyumbani," anasema, akielezea kuwa alifikiri haikufanya kazi.
Anasema alitengwa na ulimwengu na hakumruhusu kutazama televisheni au kutumia teknolojia nyingine yoyote, kama vile simu za mkononi, tangu mwaka 2007.
Siku chache baada ya mlinzi kuwachukua watoto, anasema aliwasha televisheni na kupigwa na "mshangao mkubwa". Alimuona mumewe akihutubia Msikiti Mkuu wa al-Nuri katika mji wa Mosul kaskazini mwa Iraq, akijionesha kwa mara ya kwanza kama mkuu wa ukhalifa wa Kiislamu uliojitangaza wenyewe. Ilikuwa ni wiki chache tu baada ya wapiganaji wake kuchukua udhibiti wa eneo hilo.

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Picha za video za al-Baghdadi akionekana hadharani kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, akiwa na ndevu zake ndefu, akiwa amevalia kanzu nyeusi na kutaka utiifu kutoka kwa Waislamu, ilionekana duniani kote na kuashiria wakati muhimu kwa IS ilipoenea Iraq na Syria.
Umm Hudaifa anasema alishtuka kujua wanawe walikuwa Mosul pamoja naye badala ya kwenda kujifunza kuogelea.
Anaelezea tukio la gereza lenye watu wengi katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, ambako anazuiliwa huku mamlaka ya Iraq ikichunguza jukumu lake katika IS na uhalifu wa kundi hilo.
Huwa ni kelele wakati wafungwa wanaotuhumiwa kwa uhalifu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utumiaji wa dawa za kulevya na biashara ya ngono, wanaposogezwa karibu na gereza hilo na chakula kikifika kutoka nje.
Huwa tunapata sehemu tulivu katika maktaba na kuzungumza kwa karibu saa mbili.
Wakati wa mazungumzo yetu anajiweka kama mwathiriwa ambaye alijaribu kutoroka kutoka kwa mumewe na anakanusha kuwa alihusika katika shughuli zozote za kikatili za IS.
Hii ni tofauti kabisa na jinsi anavyoelezewa katika kesi iliyowasilishwa mahakamani na Wayazidi waliotekwa nyara na kubakwa na wanachama wa IS, wanamtuhumu kwa kushirikiana katika utumwa wa kingono wa wasichana na wanawake waliotekwa nyara.
Wakati wa mahojiano, yeye hainuI kichwa chake, hata mara moja. Amevaa nguo nyeusi na anaonesha tu sehemu ya uso wake, hadi chini ya pua yake.
Umm Hudaifa alizaliwa mwaka wa 1976 katika familia ya kihafidhina ya Iraq na aliolewa na Ibrahim Awad al-Badri, ambaye baadaye alijulikana kwa jina la bandia Abu Bakr al-Baghdadi, mwaka wa 1999.

Chanzo cha picha, Iraqi Intelligence Service
Alikuwa amemaliza masomo ya Sharia, au sheria ya Kiislamu, katika Chuo Kikuu cha Baghdad na anasema wakati huo alikuwa "mtu aliyeshika dini lakini si mwenye msimamo mkali''.
Kisha mwaka wa 2004, mwaka mmoja baada ya uvamizi ulioongozwa na Marekani nchini Iraq, majeshi ya Marekani yalimtia kizuizini al-Baghdadi na kumweka katika kituo cha Camp Bucca kusini kwa takribani mwaka mmoja, pamoja na wanaume wengine wengi ambao walikuwa viongozi wakuu nchini wa IS na makundi mengine ya kijihadi.
Katika miaka iliyofuata baada ya kuachiliwa kwake, anadai alibadilika: “Akawa mwenye hasira za karibu.”
Wengine waliomfahamu al-Baghdadi wanasema alijihusisha na al-Qaeda kabla ya wakati wake huko Bucca, lakini kwake, hiyo ilikuwa hatua ya mabadiliko ambayo baadaye ilizidi kukithiri.
"Alianza kusumbuliwa na matatizo ya kisaikolojia," anasema. Alipouliza kwa nini, alimwambia kwamba "alikuwa akikabiliwa na kitu ambacho 'huwezi kuelewa'".
Anaamini kwamba ingawa hakusema hivyo kwa uwazi, "wakati wa kuzuiliwa kwake aliteswa kingono". Picha kutoka kwenye gereza lingine linalosimamiwa na Marekani nchini Iraq, Abu Ghraib, ambazo zilikuja kujulikana mwaka huo zilionesha wafungwa wakilazimishwa kuiga vitendo vya ngono na kutembea miondoko ya kufedhehesha.
Tulipeleka madai yake kwa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, lakini hatujapata jibu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Anasema alianza kujiuliza ikiwa alikuwa wa kundi la wanamgambo. “Nilikuwa napekua nguo zake akirudi nyumbani, anaoga au anapokwenda kulala.
"Hata niliukagua mwili wake ili kuona michubuko au majeraha... nilichanganyikiwa," anasema, lakini hakupata chochote.
"Nilimwambia wakati huo, 'Umepotoka' ...alipandwa na hasira kali."
Anaeleza jinsi mara nyingi walivyohama nyumba, walikuwa na vitambulisho bandia na mumewe alioa mke wa pili. Umm Hudaifa anasema aliomba talaka lakini hakukubaliana na sharti lake kwamba awaache watoto wao, hivyo akabaki naye.
Wakati Iraq ilipoanguka katika vita vya umwagaji damu vya kidini vilivyodumu kutoka 2006 hadi 2008, hakuwa na shaka tena kwamba alihusika katika vikundi vya kijihadi vya Sunni.
Mnamo 2010 alikua kiongozi wa Jimbo la Kiislam la Iraqi, lililoundwa mnamo 2006 hili lilikuwa kundi mwavuli la mashirika ya jihadi ya Iraqi.
"Tulihamia mashambani mwa mji wa Idlib nchini Syria mnamo Januari 2012, na hapo ikawa wazi kwangu kwamba alikuwa amiri (kiongozi)," Umm Hudaifa anasema.
Islamic State ya Iraq ilikuwa ni moja ya makundi ambayo baadaye yaliungana na kuunda kundi pana la Islamic State ambalo lilitangaza ukhalifa, IS inayotawaliwa kwa mujibu wa Sharia na mtu anayechukuliwa kuwa naibu wa Mungu Duniani, miaka miwili baadaye.
Wakati huo, anasema alianza kuvaa mavazi ya Kiafghani, akafuga ndevu, na kubeba bastola.
Wakati hali ya usalama ilipozidi kuzorota kaskazini-magharibi mwa Syria wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, walihamia mashariki hadi mji wa Raqqa, ambao baadaye ulikuja kuchukuliwa kuwa mji mkuu wa "ukhalifa" wa IS. Hapa ndipo alipokuwa akiishi alipomwona mumewe kwenye televisheni.
Ukatili wa makundi yaliyoungana kuunda IS ulikuwa tayari unajulikana lakini katika mwaka 2014 na 2015, ukatili huo ulienea zaidi na wa kutisha zaidi.
Timu ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa iliripoti kwamba imepata ushahidi kwamba IS ilifanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wayazidi walio wachache nchini Iraq na kwamba kundi hilo lilitekeleza uhalifu dhidi ya binadamu ikiwa ni pamoja na mauaji, mateso, utekaji nyara na utumwa.
IS ilitangaza ukatili wake kwenye mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na kukatwa vichwa kwa mateka na kuchomwa moto kwa rubani wa Jordan.
Katika tukio jingine la kusikitisha, liliwaua takribani wanajeshi 1,700 ambao wengi wao ni Shia wa Iraq walipokuwa wakirejea kutoka kituo cha jeshi cha Speicher kaskazini mwa Baghdad kwenye miji yao ya asili.
Baadhi ya wanawake ambao walikwenda kuishi na IS sasa wanasema hawakuelewa wanachokipata hivyo nikamshinikiza Umm Hudaifa kuhusu maoni yake wakati huo, anasema hata wakati huo hakuweza kutazama picha hizo, akielezea ukatili huo kuwa mbaya. "mshtuko mkubwa, usio wa kibinadamu" na "kumwaga damu bila haki ni jambo la kutisha na katika suala hilo walivuka mstari wa ubinadamu".
Umm Hudaifa anasema alimueleza mumewe kuhusu kuwa na "damu ya watu hao wasio na hatia" mikononi mwake na akamwambia kwamba "kulingana na sheria ya Kiislamu kuna mambo mengine ambayo yangeweza kufanywa, kama kuwaongoza kwenye toba".
Anaeleza jinsi mumewe alivyokuwa akiwasiliana na viongozi wa IS kwenye kompyuta yake ya mkononi.
Akaifungia kompyuta kwenye mkoba. "Nilijaribu kuingia ndani ili kujua kinachoendelea," asema, "lakini sikujua kusoma na kuandika kiteknolojia na kila mara ilinitaka nitoe nambari ya siri."

Chanzo cha picha, Reuters
Anasema alijaribu kutoroka, lakini watu waliokuwa na silaha kwenye kizuizi walikataa kumruhusu kupita na kumrudisha nyumbani.
Kuhusu kupigana, anasema kuhusu mume wake kwamba kwa kadiri alivyojua "hakushiriki katika mapigano yoyote au vita", akiongeza kuwa alikuwa Raqqa wakati IS ilipochukua udhibiti wa Mosul,alisafiri hadi Mosul baadaye kutoa hotuba.
Muda mfupi baada ya mahubiri hayo, al-Baghdadi alimuoza binti yao Umaima mwenye umri wa miaka 12 kwa rafiki, Mansour, ambaye alikabidhiwa kusimamia mambo ya familia hiyo. Umm Hudaifa anasema alijaribu kuzuia, lakini alipuuzwa.
Chanzo cha usalama cha Iraq kilituambia kuwa Umaima alikuwa tayari ameolewa mara moja hapo awali, akiwa na umri wa miaka minane, na msemaji wa IS wa Syria. Hata hivyo, alisema ndoa ya kwanza ilipangwa ili mwanaume huyo aingie nyumbani wakati al-Baghdadi hayupo, na uhusiano huo haukuwa wa ngono.
Kisha mnamo Agosti 2014, Umm Hudaifa alijifungua binti mwingine, Nasiba, ambaye alikuwa na shida ya moyo. Hii iliambatana na Mansour kuleta wasichana na wanawake tisa wa Yazidi nyumbani. Umri wao ulikuwa kati ya tisa hadi takribani 30.
Walikuwa ni maelfu ya wanawake na watoto wa Yazidi waliokuwa watumwa wa IS, maelfu zaidi waliuawa.
Umm Hudaifa anasema alishtuka na "aliona aibu".

Kulikuwa na wasichana wawili wadogo katika kundi, Samar na Zena, si majina yao halisi. Umm Hudaifa anadai walikaa tu nyumbani kwake huko Raqqa kwa siku chache kabla ya kuhamishwa.
Lakini baadaye familia ilihamia Mosul na Samar akatokea tena, akakaa nao kwa takribani miezi miwili.
Nilimtafuta baba yake Samar, Hamid, ambaye alikumbuka kwa machozi wakati alipochukuliwa.
Alisema alikuwa na wake wawili na kwamba wao, pamoja na watoto wake 26, kaka wawili na familia zao wote walitekwa nyara kutoka mji wa Khansour huko Sinjar. Alitorokea kwenye milima ya karibu.
Watoto wake sita, akiwemo Samar bado hawajulikani walipo. Wengine walirudi baada ya kulipwa fidia na wengine walirudi nyumbani baada ya maeneo waliyokuwa wanashikiliwa kukombolewa.
Msichana mwingine, Zena, ni mpwa wake na anadhaniwa kuwa amekwama kaskazini mwa Syria. Dada yake Zena, Soad, hakukutana na Umm Hudaifa mwenyewe, lakini alifanywa mtumwa, kubakwa na kuuzwa mara saba.
Hamid na Soad wamefungua kesi ya madai dhidi ya Umm Hudaifa kwa kushirikiana katika utekaji nyara na utumwa wa wasichana wa Yazidi. Hawaamini kwamba alikuwa mwathirika asiye na msaada na wanatoa wito wa hukumu ya kifo.
"Aliwajibika kwa kila kitu. Alifanya uchaguzi, huyu wa kumhudumia, yule wa kumtumikia mumewe... na dada yangu alikuwa mmoja wa wasichana hao,” anasema Soad. Amezingatia haya juu ya shuhuda za waathiriwa wengine ambao wamerejea nyumbani.
"Yeye ni mke wa mhalifu Abu Bakr al-Baghdadi, na ni mhalifu kama yeye."

Tunamuwekea Umm Hudaifa rekodi ya mahojiano yetu na Soad na anasema: "Sikatai kuwa mume wangu alikuwa mhalifu," lakini anaongeza "nawapa pole sana kwa yaliyowapata", na anakanusha tuhuma zinazoelekezwa kwake. .
Umm Hudaifa anasema kwamba baadaye kidogo, Januari 2015, alikutana kwa muda mfupi na mfanyakazi wa misaada wa Marekani aliyetekwa nyara, Kayla Mueller, ambaye alishikiliwa mateka kwa miezi 18 na kufariki akiwa kifungoni.
Mazingira ya kifo cha Kayla bado hayajajulikana, wakati IS ilidai aliuawa kwa shambulio la anga la Jordan, lakini Marekani kila wakati ilipinga hili na chanzo cha usalama cha Iraq sasa kimetuambia kuwa aliuawa na IS.
Mnamo mwaka wa 2019, vikosi vya Marekani vilivamia mahali ambapo al-Baghdadi alikuwa amejificha kaskazini-magharibi mwa Syria na baadhi ya familia yake. Baghdadi ialipojikita kwenye mtaro na kujiua kwa vilipuzi yeye na watoto wawili, huku wake zake wawili kati ya wanne wakiuawa katika majibizano ya risasi.
Umm Hudaifa hakuwepo hata hivyo, alikuwa akiishi Uturuki kwa jina la uongo ambapo alikamatwa mwaka wa 2018. Alirejeshwa Iraq mwezi Februari mwaka huu, ambako amehifadhiwa gerezani huku mamlaka ikichunguza jukumu lake katika IS. .
Binti yake mkubwa Umaima yuko gerezani naye, wakati Fatima ambaye ana umri wa miaka 12 yuko katika kituo cha mahabusu cha vijana. Mmoja wa wanawe aliuawa katika shambulio la anga la Urusi huko Syria karibu na Homs, mwingine alikufa na baba yake kwenye handaki na mvulana mdogo yuko katika kituo cha watoto yatima.
Tunapomaliza kuongea, anainua kichwa chake na kwa muda mfupi nikamwona uso mzima. Afisa wa ujasusi anapompeleka gerezani, anasihi apate habari zaidi kuhusu watoto wake wachanga zaidi. Na sasa, akiwa ndani ya gereza lake, lazima asubiri kujua kama atakabiliwa na mashtaka ya uhalifu.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga












