Kwa nini Islamic State inaichukulia Urusi kama adui

xx

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Washukiwa wanne wa shambulio hilo wamefikishwa mahakamani.

Saa chache baada ya shambulio la silaha dhidi ya ukumbi wa tamasha kaskazini mwa Moscow Ijumaa iliyopita, kundi la Islamic State (IS) lilidai kuhusika na shambulio hilo kwenye akaunti yake ya Telegram.

Kundi hilo lenye itikadi kali lilichapisha video ya shambulio hilo kama uthibitisho wa ujumbe wake na Marekani ilikuwa imetoa tahadhari siku kadhaa kabla ya kuwaonya raia wake nchini Urusi kuepuka maeneo ya umma kutokana na tishio la shambulio la "kigaidi".

Marekani inasema iliitahadharisha Moscow, ambayo iko kimya kwa sasa, lakini maelezo ya onyo hayajulikani wakati wa mvutano mkubwa kati ya nchi zote mbili kutokana na vita vya Ukraine.

Mnamo Jumapili, Urusi iliwasilisha washukiwa wanne wa shambulio hilo, ambalo lilisababisha vifo vya watu 137 na zaidi ya mia moja kujeruhiwa, na kuwashutumu kwa ugaidi.

Shambulio hilo lilisababisha ukumbi kuteketea kwa moto. Sehemu ya paa ilianguka na moto ukahamia eneo la mbele la ukumbi, na kuharibu sakafu mbili za juu.

Serikali ya Urusi bado haijatoa taarifa rasmi ya ni nani anaweza kuwa amehusika kwenye shambulio hilo na propaganda za Urusi zilidai kuwa taarifa hiyo ya Islamic State ilikuwa ya uwongo.

Mamlaka bado haijabainisha iwapo washukiwa wanne waliofikishwa mbele ya mahakama ni wa IS au sababu za shambulio hilo.

Kwa kuzingatia hali ya kutokuwa na uhakika, wachambuzi kadhaa wanaelezea kwa nini Urusi inalengwa na ISIS na jinsi inavyowezekana kwamba kundi ndilo lilifanya shambulio kwenye ukumbi.

Wakazi wa Moscowa wafanya ibada maalum

Chanzo cha picha, Getty Images

Sababu ya Taliban

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Islamic State ina historia ya vurugu ya mashambulizi dhidi ya Urusi. Mnamo mwaka wa 2015, kundi hilo lilidai kuhusika na mlipuko wa ndege ya Urusi iliyokuwa ikitoka Misri ikiwa na watu 224. Mnamo 2022, shirika hilo lilishambulia ubalozi wa Urusi huko Kabul, na kuua wanadiplomasia wawili wa Urusi na Waafghanistan wanne.

Miongoni mwa malalamiko ya kihistoria ya Waislam dhidi ya Urusi ni vita vya Afghanistan na Chechnya. Kundi hilo kwa sasa linalaani mashambulizi ya Urusi dhidi ya vikosi vyake nchini Syria na Afrika Magharibi.

"Ushiriki wa Urusi katika operesheni dhidi ya IS na washirika wake, haswa nchini Syria, na majaribio ya kuanzisha uhusiano na Taliban, unaifanya Urusi kuwa adui mkuu," kulingana na Amira Jadoon, profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Clemson nchini Marekani na mwandishi mwenza wa kitabu "IS in Afghanistan and Pakistan."

Shambulio hilo kwenye ukumbi wa mikutano linahusishwa na ngome ya IS ya Afghanistan ambayo ilitokea katika mkoa wa Khorasan mashariki mwa Afghanistan. Kundi hili liliibuka mwaka wa 2015 katika eneo ambalo Osama bin Laden aliwahi kujificha.

Hapo awali shabaha zake zilikuwa sana sana za ndani zikemo Jamiii ya Shiite ya Afghanistan, ambayo IS inawachukulia kuwa wazushi, na vuguvugu la Taliban, ambalo lilikosolewa kwa ushiriki wake katika mazungumzo ya amani na Marekani.

Lakini sasa sababu kuu ya shambulio la IS katika jimbo la Khorasan la Afghanistan dhidi ya Urusi itakuwa sababu ya Taliban.

"Taliban ni adui mbaya zaidi wa IS na kundi hili linaiona Urusi kuwa rafiki wa Taliban," anasema Michael Kugelman, mkurugenzi wa Taasisi ya Asia Kusini katika Kituo cha Wilson, kilichopo Washington.

 Dalerdzhon Mirzoyev (kushoto) na Saidakrami Murodali Rachabalizoda (kulia) ni watuhumiwa wawili waliofikishwa mahakamani.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Dalerdzhon Mirzoyev (kushoto) na Saidakrami Murodali Rachabalizoda (kulia) ni watuhumiwa wawili waliofikishwa mahakamani.

Maadui wenye itikadi kali

Propaganda za IS katika miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikimuonyesha Rais wa Urusi Vladimir Putin kuwa ni adui wa Waislamu na chanzo cha mateso dhidi yao nchini Urusi na nje ya nchi.

"Mapambano ya Marekani na ulimwengu wa kidemokrasia dhdi ya mamlaka za kimabavu kama vile (Urusi, Iran na China) yameongezeka kati ya vita vya Ukraine na Gaza. Lakini kwa Dola ya Kiislamu, wote ni maadui wa imani ya Kiislamu na wote lazima waangamizwe,” wataalamu wawili wa Islamic State waliandika katika jarida la Wall Street .

"Mkakati wa IS ni kushambulia si mara nyingi sana lakini kwa usahihi," alielezea Riccardo Valle, mtaalamu wa Uislamu na mkurugenzi wa Jarida la Khorasan Diary huko Islamabad. "Lengo ni kutoa taswira ya ujasiri ili kuvutia wafuasi."

"Leo wako Moscow. Hivi karibuni walikuwa nchini Iran. Kutakuwa na mashambulizi zaidi, ikiwezekana katika miji mikuu mingine,” mchambuzi wa kijeshi na kanali wa zamani wa jeshi la Uturuki Murat Aslan aliambia Al Jazeera.

Kukataliwa kwa wahamiaji wa Asia ya Kati wanaokwenda Urusi kama vibarua na mamlaka ya Urusi inaweza kuwa sababu nyingine iliyochochea shambulio hilo.

Ingawa wahamiaji wanatafuta kutumia fursa za ajira zilizoachwa na ukusanyaji wa raia kwenye mstari wa mbele wa vita nchini Ukraine, mara nyingi wanazungumza Kirusi duni na wananyanyaswa au kushambuliwa na polisi.

Miongozo mipya

Siku moja baada ya shambulio hilo, IS ilitoa taarifa mpya ikidai kuhusika na kile kilichotokea kwenye ukumbi wa tamasha.

Shirika la habari la Amak, linalodaiwa kuwa na uhusiano na IS, lilichapisha picha inayoonyesha washiriki wanne katika shambulio hilo. Nyuso zao zinaonekana nusu zimefunikwa na kufichwa na kichujio cha picha.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Mina Al-Lami, mtaalamu wa BBC kuhusu makundi yenye itikadi kali, ujumbe huu hautaji ni ofisi gani ya kanda iliyotayarisha na kutekeleza shambulio hilo.

Al-Lami anaonya kwamba kukosekana kwa kutajwa kwa tawi la kikanda ni mbinu za kawaida za IS. Katika kesi hii, anaweza kuonyesha kuwa kundi linajaribu kulinda ngome yake nchini Urusi kutoka kwa hatua za vikosi vya usalama.

Au inaweza hata kumaanisha kwamba tawi la eneo hilo halikuhusika katika shambulio hilo.

Idhaa za Urusi zinazoiunga mkono serikali pia ziliangazia kutotajwa kwa tawi la kikanda la IS. Kwa hivyo, wanachukulia taarifa ya kundi hilo kuwa ya uwongo na kuilaumu Ukraine, jambo ambalo Kyiv anakanusha.

Mnamo Januari 2024, wakati IS ilidai kuhusika na mashambulio katika mji wa Kerman nchini Iran, pia haikutambua washirika wa kikanda waliofanya shambulio hilo.

 Vladimir Putin

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Urusi Vladimir Putin

Washukiwa

Washukiwa wanaotuhumiwa kutekeleza shambulizi hilo nje ya mji wa Moscow walitambuliwa na mamlaka ya Urusi kuwa ni Dalerdzhon Mirzoyev, Saidakrami Murodali Rachabalizoda, Shamsidin Fariduni na Muhammadsobir Fayzov.

Walipofika mahakamani Jumapili hii, Mirzoyev na Rachabalizoda walikuwa na michubuko machoni, na sikio la Rachabalizoda lilikuwa limefungwa bandeji. Mamlaka ilisema aliipata jeraha wakati wa kukamatwa.

Fayzov alifikishwa mahakamani akiwa kwenye kiti cha magurudumu na alionekana kukosa jicho, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters. Uso wa Fariduni ulikuwa umevimba sana.

Wataalamu wanakubaliana kwamba IS na wafuasi wake wataona mashambulizi ya mwaka huu nchini Urusi na Iran kama propaganda kubwa inayonuiwa kulisaidia kundi hilo kurejesha sura yake ya kuwa tishio la kimataifa na kuongeza juhudi za kusajili.

Pia uanaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Jason Nyakundi