Risasi na hofu – tamasha la Moscow lililogeuka eneo la mauaji makubwa

.
Maelezo ya picha, Shambulio la tamasha la Crocus

Ilikuwa kabla ya saa mbili kamili usiku wakati watu walipokuwa wakiminika katika ukumbi wa Crocus city kwa ajili ya tamasha la muziki la bendi ya Veteran band picnic.

“Baadhi ya watu waliovalia nguo za brauna, sijui ni kina nani- magaidi, wanajeshi, yoyote aliyevamia katika ukumbi huu na kuanza kushambulia watu kwa risasi.” Anasema mpiga picha Dave Primov, ambaye alishuhudia tukio hilo kutoka katika ubaraza wa ghorofani.

Onyo: Taarifa hii inaweza kuwa ni ya kuogofya

Watu hao wenye silaha waliwafuata watu waliokuwa nje ya ukumbi huo, na kuanza kuwashambulia, wakisababisha mauaji na majeruhi kwa raia.

Katika tamasha hilo, baadhi ya tikiti 6,200 zilikuwa zimeuzwa, lakini usalama nje ya mlango haukuweza kuhimili shambulio hilo. Mmoja kati ya walinzi wanne alisema wenzake walijificha nyuma ya bango la matangazo: "Washambuliaji hao walipita mita 10 (futi 30) kutoka kwetu na kuanza kuwafyatulia risasi watu bila mpangilio kwenye ghorofa ya chini."

Hakuna aliyejua kulikuwa na washambuliaji wangapi. Lakini video iliyorekodiwa kutoka ghorofa ya juu inaonyesha wanaume wanne wakitembea kando, wakiwa na umbali wa mita chache kati yao kwenye sakafu yenye vigae vya marumaru.

Maelezo ya video, Raia wanajificha huku watu wenye silaha wakiingia kwenye jumba la tamasha la Moscow

Kiongozi wa washambulizi hao alilenga watu waliokuwa wamejikusanya kwenye madirisha. Hawa ndio waathiriwa wa kwanza wa shambulio baya zaidi la Urusi dhidi ya raia kwa miaka mingi.

Wengi waliouawa na kujeruhiwa walitokea katika miji ya Krasnogorsk, Khimki na miji mingine ya karibu kwenye ukingo wa kaskazini-magharibi mwa Moscow.

Kisha mshambulizi wa pili akajiunga, huku wa tatu akifuata nyuma, akiwa amebeba begi la mgongoni. Mshambulizi wa nne akamkabidhi silaha yake na wakapita kwenye milango ya vigunduzi vya chuma isiyolindwa, na kuelekea ukumbini.

Mwanamke mmoja alikuwa na binti yake mwenye umri wa miaka 11, akinunua lambalamba katika mgahawa wa karibu na mlango wa kuingilia, pale waliposikia makelele na mtu akiwaambia walale chini.

“Tuliwakimbilia watoto, tukawalaza chini na kuanza kutengeneza uzio kwa kutumia meza na viti, na watu kadhaa waliojeruhiwa walitukimbilia.” Aliiambia BBC Urusi.

Ndani ya ukumbi, tamasha lilikuwa linatarajia kuanza ndani ya dakika chache tu na baadhi walidhani kelele zilizokuwa zikisikika zilikuwa sehemu ya tamasha hiyo.

Maelezo ya video, Video inaonyesha watu wenye silaha wakiwa kwenye ukumbi wa tamasha
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Sofiko Kvirikashvili alisikia kile alichofikiria hapo awali kuwa "aina fulani ya milipuko endelevu ya fataki - nilizunguka kwenye ukumbi mara moja, kisha tena. Mara ya tatu, niligundua kuwa kila mtu kwenye ukumbi ameanza kukimbia kutoka pande zote."

Mpiga picha Dave Primov, anasema kulikuwa na msongamano na watu walikuwa na hofu sana. Baadhi ya watu waliokuwa ndani ya ukumbi walijaribu kulala chini, lakini huku kukiwa na watu kadhaa wenye silaha wakishambulia, kufanya hivyo kuliwapa ulinzi kidogo sana.

Watazamaji walioweza, walikimbilia jukwaani. Wengine walijaribu kutafuta milango ya kutokea kwa juu, lakini walikuta milango imefungwa. Mashahidi wanasema kulikuwa na wazee pia Pamoja na Watoto, wote walijikuta katikati ya shambulizi hilo.

Mwanamke mmoja alikuwa kwenye viti vya juu zaidi na akakimbia kuelekea jukwaani, ambapo aliona mtu akifyatua risasi: "Tulikimbia nyuma ya pazia na mmoja wa wafanyakazi wa Crocus aliyevaa sare alituambia tukimbie na tukakimbia nje kwenye eneo la maegesho ya magari tukiwa bila nguo zozote za kuvaa majira ya baridi.”

.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Walionusurika walieleza juu ya hofu ndani ya jengo hilo huku watu wakijaribu kutoroka

Margarita Bunova alikuwa ametoka tu kuchukua miwani yake ya opera kwa ajili ya tamasha hilo pale aliposikia kile alichofikiri kuwa ni milipuko ya fataki, ambayo iligeuka kuwa milipuko mikubwa, ambayo yeye na mume wake walitambua kuwa ni milio ya risasi.

"Kuna mtu fulani alisema kimbia chini na kulikuwa na giza sana... bado tulikuwa tunasikia milio ya risasi nyuma yetu wakati tulipofanikiwa kutoka nje.”

Mwanaume mmoja katika eneo wanalokaa watu mashuhuri ama VIP alisimulia jinsi yeye na wengine walivyojaribu kujilinda, lakini waliona moshi ukienea katika ukumbi huo.

Mwanaume mwingine, Vitaly, alishuhudia shambulio hilo kutoka ubaraza wa ghorofani. “Walirusha mabomu ya petroli kisha kila kitu kikaanza kuungua.”

Iwe ni bomu la petroli au kifaa kingine cha kuwasha moto, moto ulienea kwa kasi sana.

.

Chanzo cha picha, Ostorozhno Novosti via Reuters

Maelezo ya picha, Mamlaka ya Urusi ilisema washambuliaji walitumia gari hili kutoroka shambulio la Krasnogorsk

Wazima moto hawakuweza kukaribia jengo hilo kwa sababu ya shambulio hilo. Moto ulienea hadi kwenye paa na ulionekana katika anga ya Krasnogorsk. Sehemu ya paa iliporomoka na moto ukaenea mbele ya jengo, na kuteketeza ghorofa mbili za juu.

Wengi wa waliokuwa katika ukumbi huo walikimbia kupitia maeneo mengine ya wazi ya ukumbi. Video moja ya picha inaonyesha watu wakiteremka kwa kasi kwenye eskaleta za umeme na kupita miili miwili iliyowekwa kwenye sofa.

Video nyingine inaonyesha watu wakikimbia huku milio ya risasi ikiendelea kusikika pande zao zote. Wanafanikiwa kufika sehemu ya nyuma ya jengo, ambapo wengine wanakaa wakiwa wamejikunyata na wengine wakishikiliana huku wakipita kwenye korido.

Kwa muda, televisheni inaonyesha hali ilivyo mbele ya jukwaa. Hakuna dalili yoyote ya polisi wa Urusi au vikosi maalum mahali popote kwenye jengo hilo.

Manusra walipanda ngazi hadi kwenye lango la biashara la Ukumbi wa Jiji la Crocus. Mwanamume mmoja alionekana akirudi nyuma, huku wengine wakiwapigia simu wapendwa wao na kuondoka.

Eva, msaidizi wa kikundi cha dansi, alikuwa nyuma ya jukwaa wakati washambuliaji walipoingia kwenye ukumbi. "Tulikuwa kwenye chumba cha kubadilishia nguo, umati wa watu ulitukimbilia. Tulisikia kelele na watu wakikimbia kwenye korido; tulishika makoti yetu na kukimbia na umati."

Wanachama wote wa kundi hilo la Picnic walitangazwa kuwa salama lakini baadaye taarifa ambazo hazijathibitishwa zilieleza kuwa mmoja wa wanamuziki hao hajulikani alipo.

Kadiri idadi ya waliouawa ikiongezeka zaidi ya 100 na idadi ya waliojeruhiwa zaidi ya 200, ukubwa na hali ya mauaji hayo ilizidi kuwa wazi, ndani na nje ya ukumbi huo. Orodha rasmi ya kwanza ya majeruhi ilionyesha kuwa mwathiriwa mkubwa zaidi alikuwa katika miaka yake ya 70, huku watoto pia wakiwa miongoni mwa waliokufa na kujeruhiwa.

Picha ya gari jeupe aina ya Renault likiwa na watu wawili lilionekana kwenye mitandao ya kijamii likihusishwa na vyombo vya usalama vya Urusi.

Kundi la kijihadi la Islamic State lilisema katika taarifa fupi kwamba ndilo lililohusika na shambulio hilo, bila kutaja ni tawi lipi linalohusishwa. Hiyo iliendana na kile kilichoonekana katika akaunti ya kijasusi ya Marekani inayoonyesha kuwa IS ilitaka kushambulia Urusi. Wiki mbili kabla ya hapo, Marekani ilikuwa imeonya kuhusu shambulio linaloweza kulenga "mikusanyiko mikubwa" huko Moscow, ingawa maafisa wa Urusi wamelalamika kwamba taarifa za kijasusi hazikuwa na maelezo maalum.

Ukraine ilikanusha haraka kuhusika, ikisisitiza kuwa mashambulio yake ni kwenye uwanja wa vita tu.

Lakini idara ya usalama ya FSB ya Urusi ilidai kuwa wahalifu walikuwa wamejaribu kuvuka Urusi na kuelekea Ukraine na walikuwa na "mawasiliano na watu muhimu" huko. Idadi ya watu wanashikiliwa, wakiwemo wale wanaodaiwa kuwa washambuliaji wanne, inasema FSB.

Wakirejea katika eneo la tukio Jumamosi, Margarita Bunova na mume wake Pavel walisema jambo la kwanza walilofanya walipofika nyumbani ni kuwakumbatia watoto wao.

Haikuwa hadi Jumamosi mchana huko Moscow ambapo rais alihutubia raia wa Urusi, akizungumzia jinsi taifa zima lilivyogubikwa na huzuni.

Alilinganisha wauaji na wapiganaji wa Nazi katika Vita vya Pili vya Dunia na akasema hakuna mtu anayeweza kudhoofisha umoja wa Urusi na kuongeza kuwa Siku ya maombolezo kitaifa ingefanyika siku ya Jumapili.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla