Ni nini kilisababisha jeshi la Syria kushindwa kwa urahisi?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wapiganaji wakishangilia ndani ya Msikiti wa kihistoria wa Umayyad baada ya upinzani wenye silaha kuchukua udhibiti wa mji mkuu wa Syria, Damascus.
Muda wa kusoma: Dakika 6

Si wengi waliotarajia matukio ya haraka na mfululizo ambayo Syria imeshuhudia katika siku chache zilizopita, tangu upinzani wenye silaha unaoongozwa na waasi wa "Hay'at Tahrir al-Sham", wenye makao yao makuu katika Mkoa wa Idlib, kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo, kutangaza kuanza vita vyake kwake dhidi ya vikosi vya serikali.

Habari za kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad, ambaye alitishia takriban wiki moja iliyopita "kuwaangamiza magaidi," zilikuja kama mshangao kwa wachunguzi wengi wa masuala ya Syria.

Matukio haya yaliibua mshangao na maswali mengi, hasa kuhusu sababu za kusindwa kwa majeshi ya Syria kwa kasi ya ajabu, na kujiondoa kwao katika vita eneo moja baada ya jingine. Ni mambo gani yalichangia jambo hili?

Syria inashika nafasi ya sita katika ulimwengu wa Kiarabu na sitini kimataifa katika suala la nguvu za kijeshi, kulingana na Kiashiria cha Global Firepower cha 2024, ambacho kilijumuisha nchi 145. Uainishaji huu unazingatia mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na idadi ya wanajeshi, vifaa, rasilimali watu, na mambo ya kimkakati.

Jeshi la Syria linaundwa na idadi kubwa ya wanajeshi wanaoungwa mkono na vikosi vya kijeshi na wanamgambo, na linategemea mchanganyiko wa vifaa vilivyochakaa vya enzi ya Usovieti na zana za kisasa zaidi kutoka kwa washirika kama vile Urusi. Jeshi hilo lina zaidi ya vifaru 1,500 na magari 3,000 ya kivita, kulingana na Global Firepower, pamoja na mifumo ya mizinga na makombora.

Kwa upande wa uwezo wa anga, jeshi la Syria lina mchanganyiko wa wapiganaji, helikopta na ndege za mafunzo, na lina meli za kawaida za wanamaji, pamoja na viwanja vya ndege na bandari muhimu kama vile Latakia na Tartus.

Msimamo wa jeshi la Syria unaweza kuonekana kuwa mzuri kwa nadharia, lakini kuna mambo mengi ambayo yamelidhoofisha.

Iilipoteza sehemu kubwa ya wanajeshi wake, wanaokadiriwa kufikia askari 300,000 katika miaka ya kwanza ya vita, nusu kwa mujibu wa baadhi ya makadirio, ama kutokana na mapigano au kwa sababu baadhi ya askari walitoroka au kujiunga na makundi ya upinzani. Jeshi la anga pia lilipata hasara kubwa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe na mashambulizi ya anga ya Marekani

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sanamu ya aliyekuwa Rais Hafez al-Assad ikiburutwa na basi katika mitaa ya Hama.

Mshahara wa wanajeshi "hautoshi kwa siku tatu"

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Licha ya hifadhi kubwa ya mafuta na gesi ya Syria, uwezo wake wa kutumia mali hiyo umepunguzwa sana na vita.

Hali ya uchumi pia imezorota zaidi, hasa katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali ya Assad, kutokana na "Sheria ya Marekani iliyopitishwa Desemba 2019 na kuanza kutumika Juni 2020.

Sheria hiyo iliweka vikwazo vya kiuchumi kwa mashirika yoyote ya serikali au watu binafsi ambao wako katika serikali ya Syria.

Ripoti nyingi zimeeleza kuwa mishahara ya wanajeshi katika jeshi la serikali ya Assad ni midogo, na kwamba ni sawa na takriban dola 15 hadi 17 kwa mwezi, kiasi ambacho ni kidogo sana na ambacho "hakitoshi hata kwa siku tatu," kulingana na raia mmoja wa Syria.

Fawaz Gerges, profesa wa uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha London, anasema kwamba hali ya Syria imebadilika sana katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, na kwamba moja ya sababu za hili ni "vikwazo vya Marekani ambavyo vimewafanya watu wa Syria kuwa maskini na maafisa wa jeshi kuwa maskini zaidi. Kuna baadhi ya taarifa zinaonyesha kuwa askari hawapati chakula cha kutosha, hii ina maana kuwa wako katika hali ngumu ya kisaikolojia na wanakaribia njaa"

Jumatano iliyopita, Assad alitoa amri ya kuongeza mishahara ya wanajeshi kwa asilimia 50, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali ya Syria, katika hatua ambayo inaonekana ilinuiwa kuongeza ari huku vikosi vya upinzani vikiendelea kusonga mbele. Lakini hatua hiyo inaonekana kuchelewa sana.

Hali tete iliyochochewa na kuondolewa kwa msaada wa kijeshi kwa washirika wa Assad

Ilishangaza kwamba wanajeshi na maafisa wengi walijiondoa ghafla wakati wa vita na upinzani wenye silaha, ambao uliendelea kusonga mbele kwa kasi kutoka Aleppo hadi Damascus, wakipitia Hama na Homs, wakiwacha zana za kijeshi na silaha barabarani. Mwandishi wa BBC mjini Damascus, Barbara Belt Usher, pia alizungumzia kuhusu baadhi ya wanajeshi huko Damascus kuacha sare zao za kijeshi na kuvaa nguo za kiraia.

"Kuanguka kwa jeshi la Syria kumechangiwa kabisa na sera na mazoea ya Assad tangu apate ukuu dhidi ya upinzani mwaka 2016, hatua ambayo imedhoofisha nguzo kuu zilizomuweka madarakani," anasema Dk. Yezid Sayigh, "Matokeo yake yamekuwa kudhoofisha mihimili ya msingi iliyomuweka madarakani. Sera hizi zimeathiri jeshi ambalo makumi ya maelfu ya wanajeshi wake wamefukuzwa kazi, pamoja na kuzorota kwa hali ya maisha, kukithiri kwa rushwa, na uhaba wa chakula hata ndani ya jeshi lenyewe, jambo ambalo limeitenga jamii ya Alawite ambayo inatawala katika jeshi hilo.

"Motisha ya jeshi pia imepunguwa sana tangu kupoteza msaada wa moja kwa moja wa kijeshi kutoka Iran, Hezbollah na Urusi, ambao hawawezi tena kuingilia kati vya kutosha, au hata kuingilia kati kwa njia yoyote. Bila ahadi za kweli za usaidizi wa haraka, jeshi halina tena nia ya kupigana.

Mtaalamu wa kijeshi wa Uingereza Profesa Michael Clarke, katika Idara ya Mafunzo ya Vita katika Chuo cha King's College London, aliambia BBC kwamba msaada mkubwa wa kijeshi wa kigeni ambao serikali ya Assad ilikuwa ikipokea ulimfanya kuutegemea na kupuuza umuhimu wa jeshi lake.

"Viwango vya mafunzo yake vilishuka sana, na utendaji wa uongozi wa maafisa wake ukawa wa wastani. Wakati vitengo vyake vilipokabiliwa na mashambulizi ya Hay'at Tahrir al-Sham, maafisa wengi walijiondoa na wengine walikimbia''.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Abu Mohammed al-Julani, kiongozi wa Hay'at Tahrir al-Sham, akihutubia umati wa watu katika Msikiti wa Umayyad huko Damascus.

Jeshi la upinzani

Mbali na hali tete ya jeshi la Syria, waangalizi wengi wa matukio ya Syria tangu kuanza kwa Operesheni ya kuzuia Uchokozi mwezi Novemba 27 wamezungumza juu ya ukweli kwamba Umoja wa upinzani wenye silaha, maandalizi yao mazuri kwa vita hivi, na uwezo wao wa kijeshi yote yamechangia kuimarisha msimamo wao dhidi ya jeshi la Syria.

Mazungumzo ya wapinzani, haswa ujumbe wa kutia moyo uliotumwa kwa raia na sehemu mbali mbali za watu wa Syria na mazungumzo yake juu ya kuheshimu imani na uhuru wa kidini, uliwezesha kazi ya vikundi hivyo, kwa maoni ya wataalamu, kuvisaidia kupata mafanikio ya haraka katika gharama za vikosi vinavyoshirikiana na serikali ya Assad.

Takwimu zote zinaonekana kuchangia kuanguka kwa haraka kwa jeshi la Syria, na kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad, kwa njia ambayo Dk. Fawaz Gerges anaona "ni sawa na kuanguka kwa utawala wa Shah nchini Iran katika 1979."

Gerges anaongeza: "Upinzani wa Syria, ukiwa na mirengo yake ya Kiislamu na utaifa, uliweza kuharibu utawala wa Syria katika muda usiozidi wiki mbili... jeshi lilianguka na serikali ikaanguka kana kwamba ni nyumba ya vioo.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla