Moja kwa moja, Trump asisitiza msimamo wake kuhusu Greenland, akisema kuwa “hakuna kurudi nyuma”

Rais wa Marekani Donald Trump amesisitiza tena vitisho vyake vya kuchukua udhibiti wa Greenland, akisema kwenye mitandao ya kijamii kwamba “hakuna kurudi nyuma” na kwamba “Greenland ni muhimu sana”.

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Rais wa zamani atuhumiwa kwa njama ya mauaji afukuzwa Togo, arejeshwa Burkina Faso

    Paul-Henri Sandaogo Damiba

    Chanzo cha picha, Reuters

    Togo imemkamata na kumrudisha nchini Burkina Faso aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo, baada ya mamlaka mjini Ouagadougou kumtuhumu kupanga njama ya kumuua mrithi wake.

    Paul-Henri Sandaogo Damiba, aliyepata madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 2022 kabla ya kuondolewa madarakani na Ibrahim Traoré miezi minane baadaye, anatuhumiwa na utawala wa sasa kuwa ndiye aliyepanga jaribio la kumuua Traoré.

    Kwa mujibu wa wizara ya sheria ya Togo, Damiba alikabidhiwa kwa mamlaka ya Burkina Faso siku ya Jumamosi.

    Wizara hiyo ilisema kuwa kama sehemu ya makubaliano hayo, Burkina Faso iliahidi kuhakikisha “usalama, heshima na kesi ya haki kwa Bw. Paul-Henri Sandaogo Damiba, pamoja na kutotumika kwa adhabu ya kifo.”

    Kati ya mashtaka yaliyowekwa dhidi ya Damiba na serikali ya kijeshi ya Burkina Faso ni pamoja na “kuiba fedha za umma, kupata utajiri kinyemela, ufisadi, kupokea mali zilizoporwa kwa hali ya hatari na utakatishaji wa fedha,” kulingana na taarifa ya wizara ya sheria ya Togo.

    Hakuna maoni yoyote kutoka kwa Damiba kuhusu mashtaka hayo yaliyoripotiwa, na wala simu za BBC hazijapokelewa.

    Yaliyozidi kuwa makubwa ni mashtaka ya njama za mauaji.

    Mapema mwezi huu, Waziri wa Usalama wa Burkina Faso, Mahamadou Sana, alitangaza kwenye televisheni ya serikali kwamba vikosi vya usalama vilizuia mpango wa mfululizo wa mauaji yaliyozingatia kulenga watu binafsi kwa lengo la kutuliza serikali.

    Maafisa mjini Ouagadougou mara kwa mara wamemshutumu Damiba kwa kupanga njama kutoka uhamishoni. Mwishoni mwa mwaka 2024, alitajwa tena hadharani kama kiongozi wa kile mamlaka yalichokiita “tawi la kijeshi” la njama kubwa zaidi.

    Damiba aliibuka madarakani kwa mara ya kwanza Januari 2022, baada ya kuangusha serikali iliyochaguliwa ya Roch Marc Christian Kaboré kutokana na kutoaminika kwa serikali kushughulikia vurugu za kiislamu.

    Lakini baada ya miezi minane tu, yeye mwenyewe aliondolewa madarakani na Traoré, afisa wa makombora wa umri wa miaka 34 ambaye alimdai kushindwa kuboresha usalama.

    Tangu wakati huo, junta inayosimamiwa na Traoré imeimarisha udhibiti wake nchini, ikituma walowezi wa Kifaransa, ikichukua msimamo mkali wa kitaifa na hivi karibuni kurejesha adhabu ya kifo, ikiwemo kwa makosa ya uhaini ya hali ya juu.

    Licha ya ahadi za kurejesha utulivu, Burkina Faso bado inakabiliwa na moja ya migogoro mikali ya usalama duniani, huku mashambulizi ya kigaidi ya kiislamu yakiendelea katika sehemu kubwa za nchi.

    Unaweza kusoma;

  2. Aliyekiri kumuua aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, anatarajiwa kuhukumiwa leo

    Tetsuya Yamagami alikamatwa mwaka 2022 muda mfupi baada ya tukio la mauaji hayo.

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Tetsuya Yamagami alikamatwa mwaka 2022 muda mfupi baada ya tukio la mauaji hayo.

    Hakuna shaka kwamba mwanaume aliyemuua aliyekuwa waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe, mwaka 2022 atapatikana na hatia wakati mahakama itakapotoa uamuzi wake, kwani Tetsuya Yamagami mwenyewe alikiri kosa hilo mwanzoni mwa kesi mwaka jana.

    Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 45 anatarajiwa kuhukumiwa siku ya leo, lakini adhabu anayostahili imezua maoni tofauti ya umma nchini Japan.

    Wakati wengi wanamwona Yamagami kama muuaji katili, wengine wanaonesha huruma wakitaja maisha yake ya utotoni yaliyojaa matatizo.

    Waendesha mashtaka wameomba ahukumiwe kifungo cha maisha gerezani kwa kile walichokiita “kitendo kizito” cha kumpiga risasi na kumuua Abe.

    Waziri mkuu huyo wa zamani alikuwa mtu mashuhuri sana katika maisha ya umma nchini Japan, ambako uhalifu wa kutumia bunduki ni nadra sana, na taifa lilishtushwa na mauaji yake.

    Wakiiomba mahakama imuonee huruma, mawakili wa utetezi wa Yamagami wanasema alikuwa muathirika wa “unyanyasaji wa kidini.”

    Wanadai kuwa kujitolea kwa mama yake kwa Kanisa la Unification kulifilisi familia, na Yamagami alimchukia Abe baada ya kugundua uhusiano wa kiongozi huyo wa zamani na kanisa hilo lenye utata.

    Kifo cha kushtua cha Abe alipokuwa akitoa hotuba mchana kweupe kilisababisha uchunguzi kuhusu Kanisa la Unification na mienendo yake yenye utata, ikiwemo kukusanya michango mikubwa ya fedha kutoka kwa waumini wake kiasi cha kuwaangamiza kifedha.

    Kesi hiyo pia ilifichua uhusiano kati ya kanisa hilo na wanasiasa wa Chama cha Liberal Democratic Party kinachotawala Japan, na ilisababisha kujiuzulu kwa mawaziri kadhaa wa baraza la mawaziri.

    Mauaji ya mtu mashuhuri zaidi nchini Japan wakati huo ,Abe, ambaye bado anabaki kuwa waziri mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Japan,yalitikisa dunia nzima.

    Wakiiomba mahakama imhukumu kifungo kisichozidi miaka 20 gerezani, mawakili wa Yamagami walisema alikuwa mhanga wa “unyanyasaji wa kidini.”

    Mahakama iliambiwa kuwa alilichukia kanisa hilo kwa sababu mama yake alitoa kwa kanisa bima ya maisha ya marehemu baba yake pamoja na mali nyingine, jumla ya yen milioni 100.

    Unaweza kusoma;

  3. Trump asisitiza msimamo wake kuhusu Greenland, akisema kuwa “hakuna kurudi nyuma”

    Trump

    Chanzo cha picha, EPA

    Rais wa Marekani Donald Trump amesisitiza tena vitisho vyake vya udhibiti wa Greenland, akisema kwenye mitandao ya kijamii kwamba “hakuna kurudi nyuma” na kwamba “Greenland ni muhimu sana”.

    Wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House, Trump aliulizwa ni kwa kiwango gani yuko tayari kwenda ili kupata Greenland, naye akajibu, “Mtajua”.

    Wakati huo huo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alionya katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) nchini Uswisi kuhusu “mabadiliko kuelekea dunia isiyo na sheria”, huku Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney akisema kwamba “utaratibu wa zamani hautarudi”.

    Trump anatarajiwa kuwasili Davos siku ya Jumatano, ambapo amesema kuna “mikutano mingi iliyopangwa kuhusu Greenland”.

    Wakati wa mkutano mrefu na waandishi wa habari, Trump pia aliwaambia waandishi wa habari kwamba “mambo yataenda vizuri sana” huko Greenland.

    Alipoulizwa na BBC kama kuvunjika kwa muungano wa NATO kungekuwa gharama ambayo rais yuko tayari kulipa ili kupata Greenland, alijibu: “Hakuna mtu aliyefanya zaidi kwa ajili ya NATO kuliko mimi, kwa kila njia,” na akaongeza kuwa “NATO itakuwa na furaha na sisi pia tutakuwa na furaha,” akisema pia, “Tunaihitaji kwa usalama wa dunia.”

    Hata hivyo, awali alihoji kama NATO ingekuja kusaidia Marekani endapo ingehitajika.

    “Najua sisi tutakuja kuwaokoa (NATO), lakini nina mashaka makubwa kama wao watakuja kutuokoa,” aliwaambia waandishi wa habari.

    NATO, yaani Shirika la Mkataba wa Atlantiki ya Kaskazini , kwa sasa lina nchi wanachama 32, huku Marekani ikiwa miongoni mwa nchi 12 zilizoanzisha muungano huo.

    Unaweza kusoma;

  4. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu hii leo