'Tumechoshwa na vita': Waisraeli na Wagaza wanahofu na kuvunjika mpango wa usitishaji mapigano

Chanzo cha picha, Imad Qudaih
- Author, Gabriela Pomeroy & Maia Davies
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Israel imeionya Hamas kuwa itaanzisha tena operesheni zake za kijeshi huko Gaza ikiwa kundi hilo la wapiganaji wa Palestina "halitawarudisha mateka ifikapo Jumamosi."
Hilo limezua wasiwasi mpya kwa watu wa pande zote mbili za mzozo.
Matamshi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu yamekuja baada ya Hamas kusema haitawaachilia huru mateka zaidi hadi itakapotoa taarifa zaidi, ikidai Israel imekiuka masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyodumu kwa muda wa wiki tatu sasa.
Katika mitaa ya Khan Younis, mji wa pili kwa ukubwa wa Gaza, Imad Qudaih mwenye umri wa miaka 21 anasema "fadhaa na hofu" vimetawala.
"Hakuna anayetaka vita kurejea tena," anasema akiwa katika mji wa kusini, ambako hali bado ni "ngumu sana."
Imad anasema kuna hasira kuhusu pendekezo la Trump la kutaka Wagaza waondoke kwenye ukanda huo, pamoja na hofu ya kufurushwa - lakini anaamini mpango wa Trump "hautowezekana" na "ni maneno tu."
Salman Mahmoud Abed alikimbia kutoka mashariki mwa Gaza, anasema" anatumai kwa Mungu" usitishaji mapigano utaendelea.
"Sisi ni watu ambao tumefurushwa na hatuna makazi," ameiambia BBC.
"Tumepoteza watoto wetu, na nyumba zetu, na tunakaribia kupoteza afya zetu za akili.
"Maisha hayajarudi kama kawaida, hakuna chakula kinachotosha au hakuna nafuu yoyote ya kisaikolojia.
"Tunawaomba Hamas na Israel kutoanzisha tena vita, kwa sababu tumechoshwa na vita."
'Vita havijamaliza Gaza'
Ali Ismail Royshid - Mpalestina mwingine ambaye amekimbia mara kadhaa, ameiambia BBC: "Msiba huu unatosha, maigizo yametosha."
"Tunawataka wajaribu kufuata masharti, wasitishe mapigano na kusimamisha vita."
Hata baada na kusimama kwa mapigano, bado vita havijamaliza, anasema, na kuongeza: "Vita bado vipo, bado hatuna makazi.
"Tunawezaje kusahau vita ilhali bado hatuna makazi na tunaishi katika mahema?"

Abu Ahmed, ambaye alikimbia kutoka kaskazini mwa Gaza, anasema hana hofu na vita wala matamshi ya Trump.
"Hatuna hofu na vita, kwa sababu tumeshuhudia mengi, na chochote kitakachotokea, wacha kitokee," amesema.
"Tuko hapa na chochote Mungu anachotaka kitokee, kitatokea."
Waisraeli wana hofu

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati huohuo nchini Israel, Liron Berman, ambaye kaka zake mapacha Gali na Ziv wenye umri wa miaka 27 wanashikiliwa mateka, wamepata ishara kuwa wawili hao wako hai.
"Kupata ishara kuwa ndugu zangu wako hai, ni jambo kubwa kwetu, inafurahisha," ameiambia BBC, sauti yake ikitetemeka kwa hisia.
"Inatupa ahueni kidogo na tunapambana ili warudi."
Lakini anasema nafasi pekee ya wao kurudi ni mpango kuendelea kutekelezwa.
"Dhamira ya familia yangu ni kuhakikisha mpango wa kuwaachilia mateka unasalia. Kuwaachilia mateka, ndipo usitishaji wa mapigano utaendelea kuwepo," anasema.
Vicki Cohen - ambaye mtoto wake Nimrod alichukuliwa mateka na Hamas tarehe 7 Oktoba 2023 - amezungumza kuhusu hali hiyo.
"Ni suala la maisha na kifo," anasema. "Wako hatarini muda wote."
Mateka wa mwisho kuachiliwa wamewafanya watu kuwa na hofu.
Wiki iliyopita, mateka watatu wanaume wakiwa mbele ya kamera na watu wenye silaha wa kundi la Hamas wakati wa makabidhiano - watatu hao walionekana wamedhoofu na macho yamezama.
"Ninaogopa sana na nina wasiwasi juu ya mwanangu," anasema.
Ombi lake kwa Netanyahu ni kuhakikisha mateka wanarudi, anasema: "Fanya jambo sahihi, fanya lililo jema kwa jamii nzima."
Wasiwasi wake ni kama ule alionao Dudi Zalmanovich, jamaa mwingine wa mmoja wa mateka ambaye bado anazuiliwa na Hamas.
Mpwa wake Omer Shem Tov mwenye umri wa miaka 22 alipaswa kuwa miongoni mwa wale walioachiliwa wakati wa awamu ya kwanza ya usitishaji mapigano kwa sababu za kiafya.
"Habari hizi kuhusu uwezekano wa mpango huo kukwama, zinatutisha sana," anasema bwana Zalmanovich.
Kama Vicki, anasema hali "mbaya sana" ya kimwili ya mateka walioachiliwa hivi karibuni imezidisha wasiwasi wake.
Zalmanovich anasema, anahofia kuwa "kisingizio chochote" kinaweza kutumiwa kuvunja mpango huo.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












