Tunachojua kuhusu mpango wa kusitisha mapigano Gaza

Chanzo cha picha, Reuters
Israel na Hamas wameingia kwenye mapatano ambayo yanaweza kusitisha vita huko Gaza na kushuhudia kuachiliwa kwa mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina, Marekani na wapatanishi Qatar wamesema.
Yatakuwa mafanikio makubwa zaidi katika miezi 15 ya vita, ambayo yalianza wakati kundi la wapalestina lenye silaha la Hamas liliposhambulia Israeli mnamo Oktoba 2023.
Je, ni nini kinaweza kuwa katika mpango wa kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas?
Taarifa za mpango huo unaoripotiwa kuidhinishwa na pande zote mbili bado hazijatangazwa.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema bado kuna vifungu kadhaa ambavyo havijatatuliwa, ambavyo alikuwa ana matumaini ya kukamilishwa Jumatano jioni.
Mkataba uliokamilika utafanya vita huko Gaza kusitishwa na kubadilishana mateka na wafungwa.
Hamas iliwakamata mateka 251 iliposhambulia Israel mnamo Oktoba 2023. Bado inawashikilia mateka 94, ingawa Israel inaamini kuwa ni 60 pekee ambao bado wako hai.
Israel inatarajiwa kuwaachilia wafungwa wapatao 1,000 wa Kipalestina, baadhi yao wamefungwa kwa miaka mingi, ili kuwalipa mateka hao.
Usitishaji mapigano unawezaje kufanya kazi?
Usitishaji huu wa mapigano unatarajiwa kutokea katika hatua tatu, mara tu mpango huo utakapotangazwa.
Na wakati pande zote mbili sasa zinasemekana kukubaliana nalo, baraza la mawaziri la usalama la Israel na serikali itahitaji kuidhinisha mpango huo kabla ya kutekelezwa.
Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdul Rahman Al Thani alisema makubaliano hayo yataanza kutekelezwa Jumapili iwapo yataidhinishwa.
Hatua hii ndio inaweza kuwa katika mpango huo.
Hatua ya kwanza
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hatua ya kwanza itadumu kwa wiki sita na kuona "kusitishwa kikamilifu kwa mapigano", Rais wa Marekani Joe Biden alisema alipokuwa akithibitisha makubaliano yamefikiwa siku ya Jumatano.
"Idadi ya mateka" wanaoshikiliwa na Hamas, wakiwemo wanawake, wazee na wagonjwa, wataachiliwa kwa kubadilishana na mamia ya wafungwa wa Kipalestina, Biden alisema.
Hakutaja ni mateka wangapi wataachiliwa katika hatua hii ya kwanza, lakini Al Thani wa Qatar aliuambia mkutano wa wanahabari mapema jioni kwamba watakuwa 33.
Msemaji wa serikali ya Israel David Mencer hapo awali alisema wengi lakini sio mateka wote 33 wanaotarajiwa kubadilishana, wakiwemo watoto, walidhaniwa kuwa bado wako hai.
Mateka watatu wataachiliwa mara moja, afisa mmoja wa Palestina aliiambia BBC hapo awali, huku mazungumzo mengine yakifanyika kwa muda wa wiki sita.
Katika hatua hii, wanajeshi wa Israel wataondoka katika maeneo "yote" yenye wakazi wa Gaza, Biden alisema, wakati "Wapalestina [wanaweza] pia kurejea katika vitongoji vyao katika maeneo yote ya Gaza".
Takribani watu wote milioni 2.3 wa Gaza wamelazimika kuyahama makazi yao kwa sababu ya amri za Waisraeli za kuhama, mashambulizi ya Israel na mapigano ya ardhini.
Pia kutakuwa na ongezeko la usambazaji wa misaada ya kibinadamu hadi Gaza, huku mamia ya malori yakiruhusiwa kila siku.
Afisa huyo wa Palestina hapo awali alisema mazungumzo ya kina kwa ajili ya hatua ya pili na ya tatu yataanza tarehe 16 ya usitishaji vita.
Biden alisema usitishaji mapigano utaendelea "wakati mazungumzo yakiendelea".
Hatua ya pili
Hatua ya pili itakuwa "mwisho wa kudumu kwa vita," kulingana na Biden.
Mateka waliobaki hai, wakiwemo wanaume, wataachiliwa kwa malipo ya wafungwa zaidi wa Kipalestina.
Kati ya wafungwa 1,000 wa Kipalestina Israel inadhaniwa kuwa imekubali kuachiliwa kwa jumla, takribani 190 wanaotumikia kifungo cha miaka 15 au zaidi.
Afisa mmoja wa Israel hapo awali aliiambia BBC kwamba wale waliopatikana na hatia ya mauaji hawataachiliwa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.
Pia kutakuwa na uondoaji wa wanajeshi wa Israel kutoka Gaza.
Hatua ya tatu
Hatua ya tatu na ya mwisho itahusisha ujenzi wa Gaza, jambo ambalo linaweza kuchukua miaka na kurejeshwa kwa miili ya mateka iliyobaki.
Je, ni maswali gani ambayo hayajajibiwa kuhusu mpango huo?
Kufikia hatua hii kumechukua miezi mingi ya mazungumzo ya moja kwa moja yenye uchungu, si haba kwa sababu Israel na Hamas haziaminiani kabisa.
Hamas ilitaka kukomeshwa kabisa kwa vita kabla ya kuwaachilia mateka, jambo ambalo halikukubalika kwa Israel.
Usitishaji wa mapigano utasitisha vita wakati masharti yake yanatekelezwa.
Hatahivyo, haijulikani ikiwa itamaanisha vita vimekwisha kabisa.
Moja ya malengo makuu ya vita vya Israel imekuwa kuharibu uwezo wa kijeshi wa Hamas na kiutawala. Ingawa Israel imeiharibu vibaya, Hamas bado ina uwezo wa kufanya kazi na kujipanga upya.
Haijulikani pia ni mateka gani walio hai au wamekufa au kama Hamas wanajua walipo wale wote ambao bado hawajulikani walipo.
Kwa upande wake, Hamas imetaka kuachiliwa kwa baadhi ya wafungwa ambao Israel inasema haitawaachia huru. Inaaminika kuwa ni pamoja na wale waliohusika katika mashambulizi ya Oktoba 7.
Haijulikani pia ikiwa Israeli itakubali kujiondoa kwenye eneo salama kufikia tarehe fulani, au ikiwa uwepo wake huko utakuwa wazi.
Usitishaji wowote wa mapigano unaweza kuwa dhaifu.
Mapigano kati ya Israel na Hamas ambayo yamesitisha vita vya hapo awali yametikiswa na mapigano na hatimaye kuvunjika.
Ratiba na utata wa usitishaji vita huu unamaanisha hata tukio dogo linaweza kugeuka kuwa tishio kubwa.
Ni nini kilichofanyika mnamo 7 Oktoba 2023 na nini kimetokea huko Gaza?
Mamia ya wapiganaji wanaoongozwa na Hamas walifanya shambulizi ambalo halijawahi kushuhudiwa kusini mwa Israel, na kuvunja uzio wa mpaka na kulenga jamii, vituo vya polisi na kambi za jeshi.
Takribani watu 1,200 waliuawa na mateka zaidi ya 250 walirejeshwa Gaza. Hamas pia ilirusha maelfu ya roketi nchini Israel.
Israel ilijibu kwa kampeni kubwa ya kijeshi, kwanza kwa ndege na kisha uvamizi wa ardhini. Tangu wakati huo, Israel imeshambulia maeneo yote ya Gaza kwa njia ya ardhini, baharini na angani, huku Hamas ikiishambulia Israel kwa roketi.
Mashambulizi ya Israel yameiharibu Gaza na kusababisha uhaba mkubwa wa chakula, huku msaada ukijitahidi kuwafikia wale wanaohitaji zaidi.
Zaidi ya watu 46,700, wengi wao raia, wameuawa na mashabulizi ya Israeli, kulingana na wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga.












