Makumi ya wa wauawa katika shambulio la Israel kabla ya mkataba wa kusitisha mapigano Gaza kuanza kutekelezwa
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema mkutano wa Baraza la Mawaziri la Israel uliopangwa kuidhidnisha makubaliano hayo kuanza kutekelezwa Jumapili umeahirishwa.
Muhtasari
- Afrika CDC iko tayari kuisaidia Tanzania kufuatilia visa vinvyoshukiwa kuwa vya Marburg
- Tunachojua kufikia sasa kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza
- India yafanikiwa kutua chombo chake anga za juu
- CHAN 2024: Wasemavyo wadau wa soka kuhusu droo, kuahirishwa kwa michuano
- Rwanda yakana taarifa kuwa imegundua hifadhi ya mafuta
- Baraza la mawaziri la Israel kuidhinisha makubaliano ya kusitisha mapigano
- Mwanamke alaghaiwa $850,000 na waliojifanya mwigizaji Brad Pitt iliyoundwa na akili mnemba
- Nyota wa Bollywood Saif Ali Khan adungwa visu nyumbani kwake
- Australia: Mshawishi wa mtandaoni ashtakiwa kwa kumtilia mtoto wake sumu
- Biden aonya juu ya utawala wa "wachache" katika hotuba yake ya kuaga
- Wakazi wa Gaza wapata hisia mseto kwa habari za makubaliano ya kusitisha mapigano
- Tanzania yasema sampuli zilizopimwa hazijathibitisha uwepo wa virusi vya Marburg
- Makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza yaliokubaliwa na Israel na Hamas, Qatar na Marekani zinasema
Moja kwa moja
Na Ambia Hirsi & Asha Juma
Afrika CDC iko tayari kuisaidia Tanzania kufuatilia visa vinavyoshukiwa kuwa vya Marburg

Chanzo cha picha, Getty Images
Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC) kimesema kiko tayari kutoa msaada kwa Tanzania kuendelea kufuatilia visa vinavyoshukiwa vya ugonjwa wa Marburg katika eneo la Kagera,kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Haya yanajiri baada ya shirika la Afya Duniani (WHO) kuripoti mlipuko wa Marburg likitangaza kuwa watu wanane wamefariki kutokana na ugonjwa huo katika siku tano zilizopita nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Afrika CDC, sampuli zilizochunguzwa ni za watu watano pekee.
Takriban watu 300 wanasadikiwa kutangamana na waathiriwa wa ugonjwa huo, 56 kati yao wakiwa ni wahudumu wa afya.16 wanadaiwa kuwa walikuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na wagonjwa wa Marburg.
Afrika CDC inasema kuwa kisa cha kwanza kinachoshukiwa kilikuwa cha mwanamke mwenye umri wa miaka 27 ambaye alikuwa na ujauzito wa miezi miwili.
Ugonjwa ulipoendelea, alianza kutokwa na damu kutoka kwenye matundu ya sehemu za mwili. Alifariki tarehe 16 Desemba mwaka jana.
Mmoja wa wahudumu wa afya aliyehumdumia alikufa baada ya siku kumi na moja.
Hata hivyo serikali ya Tanzania siku ya Jumatano ilikanusha kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa Maburg baada ya sampuli zilizopimwa kwenye maabara kutothibitisha hilo.
Kanuni za Afya za Kimataifa (IHR) za mwaka 2005 zinahitaji nchi kuripoti matukio ya afya ya umma na dharura zinazoweza kuvuka mipaka.
Mkoa wa Kagera, unaokumbwa na mlipuko unaoshukiwa kuwa wa ugonjwa huo, unapakana na Rwanda, Burundi, na Uganda.
CDC Afrika inasema kuwa itatoa tamko kuhusu mlipuko huu baada ya tamko rasmi kutoka kwa serikali ya Tanzania au endapo ugonjwa utasambaa kwenda nchi nyingine za Afrika.
Maelezo zaidi:
Ujumbe wa Israel bado uko Doha - Msemaji wa serikali
Msemaji wa serikali ya Israel, David Mencer anasema ujumbe wa Israel bado uko Doha na kwamba Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisisitiza usiku wa jana kuwa Hamas watimize ombi lao la dakika za mwisho la kubadilisha uwekaji wa Vikosi vya Ulinzi vya Israel katika ukanda wa Philadelphi kwenye mpaka wa Misri, ambao anautaja kuwa hatua muhimu itakayokomesha usafirishaji wa silaha wa Hamas".
Mencer hakujibu swali kuhusu ni sehemu gani za makubaliano ambayo Hamas imekataa kutekeleza.
Akijibu swali la iwapo Israel inatafuta kura ya turufu kuhusu kuachiwa kwa wafungwa wa Hamas, Mencer anasema kuwa maelezo kuhusina na suala hilo yatajumuishwa makubaliano hayo yatakapokamilika
Tunachojua kufikia sasa kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza

Chanzo cha picha, Getty Images
- Shirika la ulinzi wa raia linaloendeshwa na Hamas limesema takriban watu 71 wameuawa katika mashambulizi ya anga huko Gaza kabla ya makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza kutekelezwa. Shirika hilo linasema takwimu hii inajumuisha zaidi ya watoto 19 na wanawake 24.
- Jeshi la Israel bado halijatoa tamko lolote.
- Mkutano wa baraza la mawaziri la Israel uliokuwa umepangwa ili kuidhinisha makubaliano hayo umecheleweshwa baada ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kulishutumu kundi la Hamas kwa kutoa masharti ya dakika za mwisho.
- Msemaji wa Hamas amesema kundi hilo bado linajitolea kwa makubaliano hayo, na kupingamadai ya Netanyahu.
- Maelezo kamili kuhusu yaliomo kwenye makubaliano hayo hazijatolewa - lakini zinajumuisha kusitishwa kwa mapigano katika eleo la Gaza, kuondolewa kwa awamu kwa vikosi vya Israel na kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa huko Gaza.
India yafanikiwa kutua chombo chake anga za juu

Chanzo cha picha, Isro
Shirika la India la anga za juu, Isro kwa mara ya kwanza limefanikisha jaribio kutua angani chombo chake katika hatua hiyo ya kihistori.
Nchi hiyo ya Asia ilifanya hivyo kwa kuunganisha pamoja vyombo viwili vidogo angani.
Teknolojia hiyo ni muhimu kwa misheni za siku zijazo za kujenga kituo cha anga za juu cha India na kuwasafirisha watu mwezini.
Vyombo viwili vya anga za juu, vilivyorushwa kwa roketi moja, vilivyotenganishwa angani.
Jaribio hilo lilikuwa limepangwa kufanyika Januari tarehe 7, lakini likabadilishwa.
Hatimaye asubuhi ya leo Alhamisi, shirika la anga za juu likatangaza kuwa limeandikisha historia kwa kuwa nchi ya nne duniani kutumia teknolojia hiyo baada ya Marekani, Urusi na China.
Waziri Mkuu Narendra Modi alikuwa katika ofisi ya Isro mjini Bangalore wakati wanasayansi walipofanya jaribio hilo.
"Ni hatua muhimu kwa misheni ya India katika anga za juu miaka ijayo," alichapisha baadaye kwenye X.
Soma pia:
CHAN 2024: Wasemavyo wadau wa soka kuhusu droo, kuahirishwa kwa michuano

Chanzo cha picha, CAF
Shirikisho la soka barani Afrika CAF limetangaza droo ya michuano ya CHAN inayoandaliwa mwaka huu kwa ushirikiano wa nchi ya Kenya,Tanzania na Uganda.
Droo hiI ilitangazwa siku moja tu baada ya michuano hiyo kuahirishwa kutoka mwezi Februari hadi Agosti mwaka huu kwa ajili ya kutoa fursa kwa nchi wenyeji kukamilisha maandalizi .
Viongozi wa soka,wadau,wachezaji na mashabiki wametoa kauli zao kuhusu droo hiyo pamoja na kuzungumzia hatua ya kuahirishwa kwa mashindnao hayo.
Rais wa shirikisho la soka nchini Tanzania Wallace Karia ameunga mkono hatua ya kuahirishwa kwa michuano akisema itatoa fursa kwa ligi kuu ya Tanzania iliyosimamishwa awali ili kuipisha CHAN kufikia Agosti.
Kuhusu droo ya michuano hiyo,Wallace amesema Taifa stars ya Tanzania haiogopi timu yoyote kutoka Afrika akipuuza madai kuwa Tanzania imepewa kundi rahisi.
Rais huyo wa TFF amesema Tanzania ina uwezo wa kuwabwaga timu vigogo na kufika hatua za nusu fainali ama hata kunyakua ubingwa wa mashindano hayo kwa mara ya kwanza katika historia.
Rais wa klabu ya Yanga nchini Tanzania aliyehudhuria droo hiyo Said Hersi amesema umewadia wakati wa timu za Afrika mashariki kumaliza utawala wa timu za Afrika Magharibi katika soka la Afrika.
Amesema ana Imani Tanzania itatoboa hatua ya makundi kwa urahisi.
Rais wa Soka nchini Kenya Hussein Mohamed ametofautiana na mashabiki wa Kenya waliosisitiza kuwa Kenya imejikuta katika kundi gumu dhidi ya Morocco,Jamhuri ya demokrasi ya Congo,Zambia na Angola akiahidi kuwa Kenya itafaulu hatua ya makundi kwa maandalizi bora.
Mchezaji wa Harambee stars ya Kenya Keneth Muguna amefurahishwa na kuahirishwa kwa michuano hiyo akisema itawapa fursa kujenga kikosi thabiti pamoja na kumpa kocha mpya Francis Kimanzi aliyejiunga nao hivi karibuni muda wa kupanga kikosi bora.
Mfungaji wa pili bora katika timu ya taifa stars Mrisho Ngassa, amesema michuano hii itatoa jukwaa kwa wachezaji chipukizi wanaofanya vyema katika timu ya Tanzania kuonekana na mawakala wa kimataifa wa soka hivyo kuwafungulia soka katika vilabu vya ulaya.
Waziri wa michezo nchini Kenya Salim Mvurya upande wake amekanusha uvumi wa kuwa Kenya ndio sababu ya CHAN Kuahirishwa akisisitiza kuwa ilikamilisha ukarabati na mikakati yote iliyotakiwa na CAF kwa michuano hiyo.
Rwanda yakana taarifa kuwa imegundua hifadhi ya mafuta, yasema uchunguzi unaendelea

Chanzo cha picha, Getty Images
Rwanda imekanusha madai ya awali kwamba imegundua hifadhi yake ya kwanza ya mafuta katika eneo la Ziwa Kivu, ikisema watafiti wake wangali katika hatua ya mwanzo ya uchunguzi na kuwa ni mapema sana kubainisha ikiwa kuna mafuta katika eneo hilo.
Francis Kamanzi, mtendaji mkuu wa Bodi ya Migodi, Petroli na Gesi ya Rwanda awali aliliambia kikao cha bunge kuwa watafiti wake wamegundua mafuta baada ya utafiti wa kina uliofanyika katika eneo la kaskazini magharibi mwa nchi hiyo karibu na Ziwa Kivu.
Lakini muda mfupi baada ya tangalo hilo bodi ya shirika hilo la linalothibiti shughuli za madina, mafuta na gesi ilitoa taarifa inayoonesha kuwa ilikuwa mapema sana.
Ilisema uchunguzi wa mitetemo ya pande mbili katika Ziwa Kivu, ambalo inapakana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, umebainisha maeneo 13 yanayoweza kuchimbwa ili kuthibitisha uwepo na asilia ya kemikali za haidrokaboni ili kuthibitisha ikiwa kweli kuna mafuta katika eneo hilo.
Shirika hilo la RMB aidha limesema kuwa Rwanda inapanga kuwaalika wawekezaji ili kushiriki katika hatua zaidi za utafutaji, maendeleo na uzalishaji wa mafuta na gesi katika bonde la Ziwa Kivu," iliongeza.
Kwa kuzingatia hifadhi kubwa ya mafuta iliyopatikana katika eneo la Maziwa Makuu na nchi Jirani za Uganda na DR Congo, kuna uwezekano mkubwa wa kupata hifadhi ya mafuta katika ardhi ya Rwanda.
Rwanda tayari inachimba gesi ya methane kutoka Ziwa Kivu na imekuwa ikifanya majaribio na uchunguzi kwa zaidi ya muongo mmoja.
Rwanda Imeendeleza majadiliano na serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuhusu mpango wa pamoja wa kutafuta na kuchimba mafuta katika bonde la Mto Kivu licha ya mzozo unaoendelea mashariki mwa Congo.
Wanajeshi wa waasi wanaosadikiwa kuungwa mkono na Rwanda wanaojulikana kama M23 wameteka maeneo mengi na shughuli za uchimbaji madini katika eneo hilo la Mashariki mwa DRC na kusababisha mgogoro wa kibinadamu.
Hata hivyo Serikali ya Rwanda imekanusha madai ya kuunga kundi lolote la waasi nchini DRC, ikisema kuwa mzozo unaoendelea mashariki mwa DRC ni suala la ndani la nchi hiyo na wala Rwanda haihusiki kwa vyovyote vile.
Mkuu wa jeshi la Sudan aagiza uchunguzi kufanywa kufuatia madai ya mauaji ya raia
Mkuu wa jeshi la Sudan ameagiza kufanywa kwa uchunguzi kuhusiana na madai kwamba wanajeshi wake walifanya ukatili mkubwa walipoukomboa mji mkuu wa jimbo la Gezira kutoka kwa waasi wa RSF.
Hatua ya Jenerali Abdel Fattah al-Burhan inajiri baada ya ripoti kuibuka kwamba raia - wakiwemo raia wa kigeni - waliuawa wakati jeshi lilipochukua udhibiti wa mji wa Wad Madani kutoka mikononi mwa wanamgambo wa RSF.
Nchi jirani ya Sudan Kusini siku ya Jumatano ilikutana na balozi Sudan nchini humo kulalamikia "kuuawa kwa raia wao amabo hawakuwa na hatia".
Sudan imekumbwa na vita tangu Aprili 2023, wakati mapigano yalipozuka kati ya jeshi na Kikosi cha waasi wa RSF.
Mkuu wa jeshi la Sudan ameunda kamati ya kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa wakati jeshi lake lililpoukomboa mji wa Wad Madani kutoka kwa waasi wa RSF.
RSF inadai kuwa wanajeshi wa serikali na washirika wao waliwashambulia raia, kwa tuhuma za kushirikiana na wanamgambo.
Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Clementine Nkweta-Salami, ameelezea wasiwasi wake kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mali ambao umesababisha watu wengi zaidi kukimbia makazi yao.
Mji wa Wad Madani ulio na miundombinu ya barabara zinazounganisha majimbo kadhaa, ulikuwa chini ya udhibiti wa RSF wakati wa mzozo wa miezi ishirini.
Pande zote mbili zinakabiliwa na tuhuma za uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na kushambulia kwa makombora maeneo ya makazi.
Baraza la mawaziri la Israel kuidhinisha makubaliano ya kusitisha mapigano

Chanzo cha picha, Getty Images
Taarifa tunazoendelea kuzipa kipaumbele ni za Hamas na Israeli kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka baada ya miezi 15 ya vita.
Rais wa Marekani Joe Biden alipongeza hatua hiyo, akisema "utasitisha mapigano huko Gaza, na kuongeza msaada wa kibinadamu unaohitajika kwa raia wa Palestina, na kuwaunganisha mateka na familia zao".
Baraza la Mawaziri la Israel linatazamiwa kukutana baadaye leo ili kuidhinisha makubaliano hayo, huku makubaliano ya awali ya wiki sita yakitarajiwa kuanza Jumapili hii.
Wapalestina wengi na familia za mateka wa Israel zimesherehekea habari hizo.
Shirika la ulinzi wa kiraia la Gaza linasema kuwa takriban Wapalestina 20 wameuawa tangu makubaliano hayo yalipotangazwa jana jioni.
Soma zaidi:
Mwanamke alaghaiwa $850,000 na waliojifanya mwigizaji Brad Pitt iliyoundwa na akili mnemba

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanamke mmoja Mfaransa alilaghaiwa $850,000 na wanaojifanya mwigizaji Brad Pitt kwa usaidizi wa akili mnemba.
Kisa hicho kilitangazwa na kituo cha televisheni cha Ufaransa cha TF1, ambacho kiliamua kuondoa kipindi kumhusu mwanake huyo kutokana na wimbi la kejeli zilizotolewa dhidi ya yake.
Kipindi hicho kinachopeperushwa wakati wasikilizaji wengi wanasikiliza siku ya Jumapili, kilifanya wengi wao kuvutiwa na mwanamke huyo ambaye ni mbunifu na mpambaji wa majumba Anne, 53, ambaye alidhani alikuwa kwenye uhusiano na Pitt kwa mwaka mmoja na nusu.
Katika kipindi maarufu cha YouTube cha Ufaransa, Anne baadaye alisema yeye "sio kichaa wala mjinga": "Nilidanganywa tu, nakubali na ndiyo maana nimejitokeza, kwa sababu sio mimi peke yangu."
Mwakilishi wa Pitt aliiambia Entertainment Weekly kwamba "ilikuwa kitu kibaya kwamba matapeli huchukua fursa ya uhusiano mzuri wa mashabiki na watu mashuhuri" na kwamba watu hawapaswi kujibu mawasiliano ya mtu usiyemfahamu, "haswa kutoka kwa waigizaji ambao hawapo kwenye mitandao ya kijamii.
Mamia ya watumiaji mitandao walimdhihaki Anne, ambaye alikuwa amepoteza akiba yake na alijaribu kujitoa uhai mara tatu tangu ulaghai huo ulipotokea, kipindi cha televisheni kilisema.
Pia unaweza kusoma:
Nyota wa Bollywood Saif Ali Khan adungwa visu nyumbani kwake

Chanzo cha picha, Getty Images
Muigizaji maarufu wa Bollywood Saif Ali Khan amelazwa hospitalini akiwa na majeraha mengi ya kuchomwa visu baada ya mvamizi kuripotiwa kuvamia nyumba yake na kumshambulia.
Shambulio hilo lilitokea mapema Alhamisi asubuhi katika kitongoji cha juu cha jiji la Mumbai, ambapo Khan anaishi na familia yake.
Polisi wa jiji hilo waliambia BBC Marathi kwamba mwigizaji huyo alijeruhiwa baada ya kutokea ugomvi kati yake na mtu asiyejulikana ambaye aliingia nyumbani kwake muda wa saa sita usiku.
Familia ya Khan haijatoa taarifa yoyote kwa umma lakini timu yake ya utangazaji ilisema ni kesi ya "jaribio la kuiba" bila kutoa maelezo zaidi.
Australia: Mshawishi wa mtandaoni ashtakiwa kwa kumtilia mtoto wake sumu

Chanzo cha picha, Queensland Police
Mwanamke mwenye ushawishi mkubwa nchini Australia ameshtakiwa kwa kumtilia sumu mtoto wake wa kike ili kuchangisha pesa na kuongeza wafuasi mtandaoni.
Mwanamke huyo wa Queensland alidai kwamba alikuwa na wakati mgumu kukabiliana na ugonjwa mbaya wa mtoto wake kwenye mitandao ya kijamii, lakini wapelelezi wanadai kuwa alikuwa akimpa dawa za kulevya mtoto huyo wa mwaka mmoja na kisha kumrekodi akiwa katika hali ya "dhiki na maumivu makali".
Madaktari walipaza sauti mnamo mwezi Oktoba, wakati mtoto alilazwa hospitalini akiwa mgonjwa sana.
Baada ya uchunguzi wa miezi kadhaa, mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 34 alishtakiwa kwa kumtesa mtoto, kumpa sumu, kumtumia mtoto vibaya nak wa ulaghai.
Pia unaweza kusoma:
Biden aonya juu ya utawala wa "wachache" katika hotuba yake ya kuaga

Chanzo cha picha, Reuters
Rais anayemaliza muda wake wa Marekani Joe Biden ameonya juu ya utawala wa "wachache" unaojitokeza Marekani, alipokuwa akitoa hotuba yake ya kuaga na kumaliza taaluma yake ya miongo mingi katika siasa.
"Leo, utawala wa wachache umeanza kujitokeza katika Marekani ya utajiri mkubwa, nguvu na ushawishi ambao unatishia demokrasia yetu yote, haki zetu za msingi na uhuru," alisema Jumatano.
Biden, mwenye umri wa miaka 82, alilenga wenye utajiri mkubwa "kijamii na kiuchumi" na kusema kunaweza kuwa na nguvu ya ajabu isiyodhibitiwa yenye kuwashinda Wamarekani.
Pia alitumia hotuba yake ya mwisho iliyopeperushwa moja kwa moja kutoka Ikulu ya White House kutoa maonyo kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na upotoshaji wa mitandao ya kijamii.
Akizungumza kutoka Ikulu ambapo familia yake ilikuwa imekusanyika kutazama, aliangazia rekodi yake ya utawala wa muhula mmoja, akirejelea utengenezaji wa fursa za ajira, matumizi ya miundombinu, huduma ya afya, kuongoza nchi kutoka katika janga la corona, na kuifanya Marekani kuwa nchi salama.
Aliongeza, hata hivyo, kwamba "itachukua muda kuona matokeo kamili ya yote ambayo tumefanya pamoja, lakini mbegu zimepandwa, zitakua, zitachipuza na kuchanua kwa miongo kadhaa ijayo".
Biden alitakia mafanikio utawala unaokuja wa Donald Trump, lakini akatoa maonyo kadhaa, huku rais akisema "mengi yako hatarini hivi sasa".
Soma zaidi:
Wakazi wa Gaza wapata hisia mseto kwa habari za makubaliano ya kusitisha mapigano

Chanzo cha picha, Reuters
Wapalestina huko Gaza walizungumza na BBC Arabic kuhusu hisia zao juu ya makubaliano ya kusitisha mapigano.
Mwanamke ambaye mwanawe, Nabil Mohammed Zidan Nasser, aliuawa wakati wa vita, alisema alihisi mchanganyiko wa furaha na huzuni aliposikia habari hizo.
Aliongeza: "Asante Mungu, ninawapongeza watu wetu kwa mapatano haya, watu wa Gaza waliozingirwa na wanaohangaika, na Mungu akipenda utatekelezwa kikamilifu"
Mwanaume mmoja, akizungumza na BBC Arabic, alitoa shukrani zake kwa nchi za Kiarabu kwa juhudi zao zilizosaidia kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.
Alisema: “Tuliogopa kwamba zamu yetu ingefika na tukafa katika vita hivi, bila kutaja mateso tuliopitia kutokana na ukosefu wa chakula na vinywaji, na kutopatikana kwa maji.”
Ameongeza kuwa: "Tunazishukuru nchi za Kiarabu kwa kufanya juhudi hizo kubwa na kuishinikiza Israel kusitisha vita dhidi yetu
Soma zaidi:
Tanzania yasema sampuli zilizopimwa hazijathibitisha uwepo wa virusi vya Marburg

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Tanzania imesema kuwa sampuli zilizochukuliwa hazijathibitisha uwepo wa virusi vya Marburg, hayo ni kulingana na taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya.
"Mpaka leo tarehe 15 Januari 2025, majibu ya uchunguzi wa kimaabara…hayajathibitisha uwepo wa virusi vya Marburg".
Hayo yanawadia baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kusema kuwa mlipuko unaoshukiwa kuwa wa virusi vya ugonjwa wa Marburg umewaua watu wanane katika mkoa wa Kagera Kaskazini magharibi mwa Tanzania.
Wizara hiyo ilithibitisha kupokea tetesi za uwepo wa ugonjwa huo na kusema kuwa imechukua hatua za haraka.
"Tumetuma timu ya wataalamu; kufanya uchunguzi wa suala hili; kuchukua sampuli na kufanya vipimo vya maabara", taarifa ya Waziri wa Afya Jenista Mhagama imesema.
Wizara hiyo imehakikishia wananchi pamoja na jumuiya ya kimataifa kuwa imeimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa na kwamba itaendelea kutoa taarifa.
Soma zaidi:
Makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza yaliokubaliwa na Israel na Hamas, Qatar na Marekani zinasema

Chanzo cha picha, Reuters
Israel na Hamas wamekubaliana kusitisha mapigano Gaza na kuwaachilia mateka baada ya miezi 15 ya vita, wapatanishi wa Qatar na Marekani wanasema.
Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdul Rahman Al Thani alisema makubaliano hayo yataanza kutekelezwa siku ya Jumapili mradi tu yaidhinishwe na baraza la mawaziri la Israel.
Rais wa Marekani Joe Biden alisema "itasitisha mapigano huko Gaza, kuongeza msaada wa kibinadamu unaohitajika kwa raia wa Palestina, na kuwaunganisha mateka na familia zao".
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema maelezo ya mwisho ya mkataba huo bado yanashughulikiwa, lakini alimshukuru Biden kwa "kuuendeleza". Kiongozi wa Hamas Khalil al-Hayya alisema ni matokeo ya "ustahimilivu" wa Wapalestina.
Wapalestina wengi na familia za mateka wa Israel zilisherehekea habari hizo, lakini hali ilikuwa tofauti katika uwanja wa vita vya ardhini huko Gaza.
Shirika la Ulinzi la Raia linaloendeshwa na Hamas liliripoti kuwa mashambulizi ya anga ya Israel yameua zaidi ya watu 20 kufuatia tangazo hilo la Qatar.
Walijumuisha watu 12 ambao walikuwa wakiishi katika kizuizi cha makazi katika kitongoji cha Sheikh Radwan cha Jiji la Gaza, ilisema. Hakukuwa na maoni ya mara moja kutoka kwa jeshi la Israeli.
Israel ilianzisha kampeni ya kuiangamiza Hamas - ambayo imechukuliwa kama shirika la kigaidi na Israel, Marekani na wengine - kujibu shambulio la kuvuka mpaka la tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka. .
Zaidi ya watu 46,700 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas. Wengi wa watu milioni 2.3 pia wamekimbia makazi yao, kuna uharibifu mkubwa, na kuna uhaba mkubwa wa chakula, mafuta, dawa na makazi kutokana na ugumu wa kupata misaada kwa wale wanaohitaji.
Israel inasema mateka 94 bado wanazuiliwa na Hamas, ambapo 34 kati yao wanakisiwa kufariki. Aidha, kuna Waisraeli wanne waliotekwa nyara kabla ya vita, wawili kati yao wamefariki dunia.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ya tarehe 16/01/2025
