Nani anamiliki mwezi?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Rebecca Morrell
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Idadi ya nchi na makampuni ambayo yako katika mbio za kupata nafasi katika mwezi inaongezeka siku baada ya siku.
Miezi michache iliyopita, picha za bendera ya China ikipepea juu ya mwezi zilionekana duniani. Hii ilikuwa ni mara ya nne kwa nchi hiyo kutua katika uso wa mwezi na ikawa ndio misheni ya kwanza ambayo ilirudisha sampuli za udongo kutoka mwezini.
Takribani mwaka mmoja uliopita, India na Japan pia zimepeleka vyombo vya anga za juu kwenye uso wa mwezi. Februari, kampuni ya Marekani ikawa kampuni ya kwanza binafsi kutua mwezini, na zingine nyingi ziko kwenye mipango.
Na NASA inataka kuwarudisha wanadamu kwenye uso wa mwezi mwaka 2026. China pia imetangaza kwamba itatuma chombo cha anga za juu mwezini mwaka 2030. Na malengo ni kujenga kambi ya kudumu.
Sheria kuhusu mwezi

Chanzo cha picha, Getty Images
Moja ya makubaliano ya Umoja wa Mataifa ya 1967 yanasema kuwa hakuna nchi inayoweza kumiliki mwezi. Mkataba huo unaoitwa "Mkataba wa Anga za Juu" unasema mwezi ni wa kila mtu na uchunguzi wowote unapaswa kuwa kwa manufaa ya wanadamu wote na kwa manufaa ya nchi zote.
Wakati wa siasa za enzi ya Vita Baridi na mvutano ulipoongezeka kati ya Marekani na Umoja wa Kisovieti baada ya Vita vya Pili ya Dunia, kulikuwa na wasiwasi, huenda anga ya juu inaweza kugeuka kuwa uwanja wa vita vya kijeshi, sehemu muhimu ya mkataba huo inasema - hakuna silaha za nyuklia zitatumwa angani. Zaidi ya nchi 100 zilitia saini mkataba huu.
“Ingawa makampuni ya binafsi yanataka kushiriki katika safari za mwezini, serikali zinasalia kuwa wahusika wakuu,” anasema Saeed Mansher, mkurugenzi wa Taasisi ya Sera na Sheria ya Anga ya London. Anasema kila kampuni inahitaji leseni kutoka nchi ambayo serikali yake inafuata mikataba ya kimataifa.
Ingawa mwezini kunaonekana kutupu, lakini kuna madini adimu, kama vile iron (chuma) na titanium, ambayo hutumiwa katika mambo mengi kama kutengeneza vifaa vya kusafirisha umeme na vifaa vya matibabu.
Makadirio ya thamani ya rasilimali hizi yanaweza kufika mabilioni hadi quadrillion ya dola. Kwa hiyo ni rahisi kuona kwa nini baadhi ya watu huona mwezi ni mahali pa kupata pesa nyingi.
Hata hivyo, ni lazima ieleweke kwamba huo ni uwekezaji utakao chukua muda mrefu sana na bado hatuna teknolojia inayoweza kuchimba na kurejesha rasilimali hizi duniani.
Mwaka 1979, mkataba wa kimataifa ulitangaza, hakuna serikali au shirika linaloweza kudai umiliki wa rasilimali zilizopo mwezini. Ingawa ni nchi 17 pekee zilizojiunga na makubaliano hayo, na hayajumuishi nchi yoyote iliyokwenda mwezini, ikiwemo Marekani.
Marekani ilipitisha sheria mwaka 2015 ambayo inaruhusu wananchi wake na viwanda kuchimba, kutumia, na kuuza nyenzo zozote za angani.
Sheria hii ilisababisha wasiwasi mkubwa katika jumuiya ya kimataifa. Na hatua kwa hatua, nchi nyingine pia zilitunga sheria kama hizo. Zikiwemo, Luxembourg, Falme za Kiarabu, Japan na India.
Rasilimali za mwezini

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
“Baada ya kuchunguza jiwe la kwanza lililoletwa duniani kutoka mwezini na wanaanga wa Apollo, ilidhaniwa kuwa mwezi ni mkavu," asema Sarah Russell, profesa wa sayari katika Jumba la Makumbusho la Natural History huko Uingereza.
"Lakini karibu miaka 10 iliyopita, tuligundua kwamba miamba hii ina athari ya maji. Wale watakao tembelea huko siku zijazo wataweza kutumia maji hayo kwa kunywa, pia kuzalisha oksijeni, na kuyafanya kuwa hidrojeni na oksijeni wanaanga wanaweza kuyatumia kutengeneza mafuta ya roketi ambayo yataweza kuziruhusu kutoka mwezini hadi sayari ya Mars na kwenda mbele zaidi.”
Marekani sasa inafanya kazi kutengeneza miongozo ya uchunguzi wa mwezi na kupata rasilimali za mwezi. Mkataba huo unaojulikana kwa jina la Artemis, unasema uchimbaji na utumiaji wa rasilimali za mwezi lazima ufanywe kwa njia ambayo inaendana na Mkataba wa Kimataifa wa Anga, ingawa mkataba huo unasema sheria mpya zitahitajika kutungwa.
Saeed Manshar anasema: "Kwa kweli, kazi hii inapaswa kufanywa kupitia Umoja wa Mataifa kwa sababu ni suala ambalo linahusu nchi zote."
Kuna uwezekano mkubwa kwamba Walowezi wa kwanza katika mwezi watatoka Marekani au China, na hilo litaongeza ushindani kwenye uhusiano wao wa mvutano wao.
Baadhi ya wataalamu wa anga ambao nimezungumza nao wanaamini kutakuwa na mkataba mwingine mkubwa wa kimataifa wa anga. Mambo ya unayoweza kufanya na yale usiyoweza kufanya katika uchunguzi wa mwezi na yataamuliwa na hati mpya au maazimio mapya.
Wakati mbio hizi mpya za anga za juu zinapoanza, tunahitaji kufikiria tunataka mwezi wetu uwe ni eneo la aina gani, na iwapo kuna hatari ya kuwa uwanja wa mashindano ya viumbe kutoka duniani.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












