Jinsi mitandao ya simu inavyokumbatia akili mnemba (AI)

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
- Author, Matthew Wall
- Nafasi, BBC
Simu zetu janja zinazidi kuwa na akili zaidi. Wiki iliyopita, Apple imekuwa kampuni ya hivi karibuni ya simu za mkononi kutangaza itaongeza akili mnemba (AI) kwenye mfumo wa uendeshaji wa simu zake.
Ni baada ya Samsung Galaxy AI, na Gemini AI ya Google kupitia simu zake za Pixel, kuwekwa akili mnemba.
Ongezeko hili la matumizi ya akili mnemba lina maanisha simu zitafanya kazi kubwa zaidi, na zitazalisha na kutumia data ama taarifa nyingi zaidi.
Kampuni za Mawasiliano

Chanzo cha picha, getty images
Akili mnemba haitumiki katika mifumo ya simu janja pekee. Pia kampuni zinazotoa huduma za mawasiliano nazo hazijaachwa nyuma katika kutoa huduma kwa kutumia akili mnemba.
“Nchini Korea Kusini, mtandao wa mawasiliano ya simu za mkononi wa Korea Telecom sasa una uwezo wa kufahamu na kurekebisha hitilafu ndani ya dakika moja, kutokana na ufuatiliaji unaofanywa na akili mnemba,” anasema Alex Sinclair, afisa wa teknolojia wa GSMA, chombo kinachowakilisha mitandao ya simu duniani.
Mtandao wa mawasiliano wa AT&T nchini Marekani unatumia kanuni za ubashiri za akili mnemba zinazotokana na matrilioni ya taarifa za nyuma ili kutoa onyo kuhusu hatari.
Makampuni mengi ya mawasiliano ya simu kama vile Vodafone, wanatumia akili mnemba, kufuatilia jinsi mitandao yao inavyofanya kazi.
Na akili mnemba pia inatumiwa na vituo vikubwa vya kuhifadhi data vinavyotumia seva, kuongeza uwezo wa kuhifadhi taarifa.
Wingi wa taarifa unaotokana na kuongezeka kwa matumizi ya akili mnemba ni sababu nyingine ya makampuni ya mawasiliano kuwekeza katika mtandao wa mawasiliano wa kasi ya 5G.
5G hutumia miundombinu mipya, badala ya kutegemea au kuboresha mfumo wa 4G wa zamani, usio na ufanisi. 5G inatoa kasi na uwezo wa hali ya juu zaidi.
Lakini baadhi ya wataalamu wanaamini, teknolojia hii ya hali ya juu ya 5G, haitatosha kukabiliana na mahitaji ya enzi ya akili mnemba.
Akili mnemba na G5

Chanzo cha picha, VODAFONE
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika Kongamano la Dunia la Simu la mwaka huu huko Barcelona, Spain, baadhi ya wataalamu walisema, akili mnemba haitaweza kufikia uwezo wake kamili hadi itolewe kasi ya 6G mwaka 2028.
Lakini kwa sasa mitandao ya mawasiliano ya simu inatumai akili mnemba ili kuboresha kwa kiasi kikubwa jinsi wanavyoingiliana na kuwahudumia wateja.
Kwa mfano, Global Telco AI Alliance - kampuni ya ubia inayoundwa na Deutsche Telekom, e&, Singtel, Softbank na SK Telecom yenye wateja bilioni 1.3 katika nchi 50 – itaunda chatbot ya akili mnemba mahsusi kwa sekta ya mawasiliano, ili kujibu maswali ambayo wateja huuliza mara kwa mara.
Chatbot hii itashughulikia maswali mengi kutoka kwa wateja, na kuwaacha wafanyikazi wa kituo cha simu wakiwa huru kuangazia kesi ngumu zaidi, waanzilishi wa Alliance wanasema.
Wakati huo huo, Vodafone imeungana na Huduma ya Azure OpenAI ya Microsoft ili kuboresha huduma yake kwa wateja, kwa kutumia msaidizi wa kidijitali Tobi, ambaye huwasiliana na wateja zaidi ya milioni 40 kwa mwezi katika nchi 13 na katika lugha 15.
Kadiri Tobi anavyoweza kujibu maswali ya wateja bila kuhitaji uingiliaji kati wa binadamu, ndivyo huwa na malalamiko machache kutoka kwa wateja, na hilo huleta faida na sifa kwa shirika.
“Azure OpenAI inawasaidia wateja kupata kwa urahisi kile wanachotafuta kwenye tovuti zake,” anasema afisa wa teknolojia wa Vodafone, Scott Petty.
Ushahidi wa mapema unaonyesha kuna kuongezeka maradufu kwa idadi ya matatizo yanayopatiwa ufumbuzi kutoka kwa wateja, na kupungua kwa 10% simu za malalamiko za wateja.
Majibu juu ya wasiwasi wa AI

Chanzo cha picha, IAN FOGG
Ingawa baadhi ya watu wana wasiwasi kuwa AI inaweza kusababisha upotezaji mkubwa wa kazi katika sekta ya mawasiliano, kwani kazi zinazidi kuendeshwa programu moja kwa moja.
Lakini Sinclair wa GSMA ana maoni tofuati, anaamini huenda akili mnemba ikatoa fursa zaidi hasa kwa nchi za kipato cha chini.
"Akili mnemba itatoa uwezo kwa masoko yanayoibuka, kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia," anasema. "Tunajaribu kuiweka akili mnemba iwe kwa wote, isiwe matajiri tu ndio wanaoweza kuitumia."
Anaamini baadhi ya ukosoaji wa akili mnemba hutiwa chumvi kupita kiasi, lakini yeye analeta sauti ya matumaini.
Hata Ian Fogg wa CCS Insight ana maoni kama hayo: “Akili mnemba imekuwapo kwa miaka kadhaa, ikitumika kwa matukio mahususi [ya simu]. Lakini sasa inatumika katika maeneo mengi zaidi - mtandao, vifaa, programu - kila zana tunayotumia sasa ina uwezo wa kuwa bora zaidi.
"Akili mnemba ina uwezo wa kufanya mitandao ya mawasiliano ya simu kuwa rafiki na mazingira, na ulimwengu kuwa mahali pazuri zaidi," anahitimisha Fogg.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Lizzy Masinga












