Uraibu wa simu: 'Binti yetu mdogo, 13, anatupangia njama ya kutuua'

.

Chanzo cha picha, Getty Images

''Binti yetu mwenye umri wa miaka 13 alianza kupanga njama ya kutuua.

''Alianza kuchanganya dawa kwenye mkebe wa sukari jikoni inayotumika wakati wa kutengeneza chai, na kila asubuhi wakati wa kwenda chooni, alianza kutupa vitu vya kuteleza bafuni kabla tuingie, kumbe alikuwa akitazama video za mauaji kwenye YouTube kila wakati.''

Maneno haya ni ya baba mwenye umri wa miaka 56 anayeishi katika eneo la mji wa Ahmedabad. Alipiga simu nambari 181 'Abhyam' inayoendeshwa na serikali ya Gujarat kwa ajili ya kutoa usaidizi kwa umma.

Mnamo Juni 7, 2022, simu ilipokelewa kwenye nambari ya 181 kutoka kwa baba akielezea wasiwasi wake. Alilalamika kuwa 'hali nyumbani kwangu si nzuri, hali ya kiakili ya binti yangu si nzuri, munapaswa kuja ili kumshauri.'

Mara tu simu ilipopokelewa, wale maofisa wa simu 181 walifika mahali alipoelekeza baba. Kwanza walipata taarifa kuwahusu kutoka kwa wazazi wao ambao walisema kuwa wameoana kwa miaka 26.

Mume alikuwa na umri wa miaka 56 huku mkewe akiwa na miaka 46. Wana watoto wawili. Umri wa binti ni miaka 13 wakati umri wa mtoto wa kiume ni miaka saba.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

'Alianza kututishia kutuua'

Baada ya muda mrefu wa maisha ya ndoa, binti yao wa kwanza alizaliwa na miaka mitano baadaye, mtoto wa kiume alizaliwa.

Baba alielezea masikitiko yake. Mshauri wa nambari ya usaidizi 181 Falguni Patel amezungumza na BBC kuhusu hili.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati wa ushauri nasaha, baba alisema, 'Tulifurahi sana mtoto wetu wa kwanza alipokuja duniani.

Lakini sasa tunahisi kwamba tulikuwa sawa bila watoto. Tuna binti mwenye umri wa miaka 13, ambaye hutufedhehesha kila siku. Hatuamini tunachokutana nacho. Hukesha usiku kucha, na kuamka saa sita mchana, hutazama TV siku nzima, hutoka nje bila kutuambia na zaidi ya yote hutishia kutuua.'

''Anasema hataki mtu yeyote ndani ya nyumba. Anataka kuwa peke yake. Hajaenda shule kwa muda wa miezi 4 iliyopita. Kwa sasa yuko darasa la saba. Alishikwa shuleni akishirikiana na makundi mabaya licha ya umri wake mdogo. Wakati kulipokuwa kumewekwa masharti ya kutotoka nje kwasababu ya janga la corona, elimu ya mtandaoni ilianza na kwa sababu hiyo, nilimpa binti yangu simu ya smart phone.''

Baba yake alisema, 'Katika enzi ya mitandao ya kijamii, binti yangu amejiunga na makundi mbaya. Anazungumza na wavulana tofauti kupitia mitandao ya kijamii. Yeye pia huenda kukutana na wavulana kisiri. Amejifunza mambo mengi ambayo si mazuri. Tulipojua kuhusu hili, mke wangu alichukua simu ya smart phone kutoka kwa binti yake. Hajakuwa na simu kwa miezi miwili sasa. Baada ya kunyang'anywa simu, alianza kututishia waziwazi ndani ya nyumba na kupanga njama ya kutuua.'

'Alipata mpenzi kupitia mtandao wa kijamii'

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Baba alimwambia mshauri, akirejelea Juni 7, 2022: 'Alichanganya dawa na sukari kwenye mkebe wa sukari jikoni, kila asubuhi nilipolazimika kwenda chooni alikuwa akitupa kioevu bafuni. Binti yetu, ambaye anatazama video za mauaji kwenye YouTube, anapata vifurushi vya noti 100 na 500 kutoka mahali fulani, hatujui ni nani anayemlipia.'

Aliongeza: 'Tukimzuia kuondoka nyumbani, anaanza kuvunja vitu vya nyumbani. Anampiga mtoto wangu wa miaka 7. Hatusemi chochote kuhusu hilo kwa kuogopa majirani na jamaa wa karibu. Tulimruhusu binti atoke. Binti yetu anasema anaenda kwa nyumba ya rafiki yake. Angerudi nyumbani baada ya saa tano au sita. Binti yetu anasema hii nyumba mutanirithisha mimi, muiandike jina langu. Nyote mutajiua na kufa. Nataka kuuza nyumba hii nihamie nje ya nchi.'

Falguni Patel anasema wakati akisimulia hayo yote, babake msichana huyo alianza kulia mbele ya timu 181.

Mama ya msichana huyo aliiambia timu ya 181: 'Lolote mtakalofanya, mshauri binti yangu na mtuambie anachofikiri na anachotaka kufanya.'

Wakati wakimshauri binti huyo mwenye umri wa miaka 13, timu hiyo iligundua kwamba alikuwa akipendana na mvulana kwa miaka miwili iliyopita, ambaye alikutana naye kupitia programu ya mtandao wa kijamii wa Instagram.

Ana akaunti 13 hadi 14 tofauti kwenye mtandao huo.

Anawasiliana na kijana huyo kupitia mitandao ya kijamii. Anaelewa mambo yote ya mapenzi na ngono.'

Alisema wakati wa ushauri kwamba, ‘nilikuwa nikimpigia simu mvulana huyu mimi mwenyewe. Nilikuwa namtembelea rafiki yangu kwa kisingizio cha kwenda nyumbani kwake. Sikujua kwamba sikupaswa kufanya haya yote.'

'Tangu nipate simu nilianza kujua kila kitu. Wasichana wa mtaani kwetu, shuleni na katika jamii yangu walinipa ushauri na kunieleza juu yake. Kutokana na hili, nikaanza kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mvulana huyo.'

Wahusika wote watatu walishauriwa

Timu ya usaidizi ilisema kwamba 'Wakati wa ushauri nasaha, msichana huyo mwenye umri wa miaka 13 alisimulia kuhusu rafiki yake. Kwa hivyo timu hiyo ilimpigia simu rafiki huyo kutoka eneo jirani.

Rafiki yake alisema msichana huyo alikuwa na uhusiano na mvulana.

Miaka miwili au mitatu iliyopita alikuwa na uhusiano wa kimapenzi naye kisha wakaachana na kijana huyo akaingia kwenye uhusiano na msichana huyu wa miaka 13.'

Wakati wa ushauri nasaha, ilibainika kuwa wasichana wote wawili wanawasiliana na mvulana wa umri wa miaka 19 ambaye anaishi katika eneo jirani.

Timu ya 181 ilipata utambulisho wa mvulana huyo na kumwita kwa ushauri.

Wakati wa ushauri nasaha na mvulana huyo, iligundulika kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na wasichana wote wawili.

Baada ya maelezo haya yote kufichuliwa, timu 181 ilifanya ushauri wa pamoja na wote watatu. Baada ya kuwashauri, walikiri kosa lao na kuomba msamaha kwa wazazi wao.

Ilisemekana kwamba wanaweza pia kuchukua simu za smart phone kutoka kwao. Rafiki wa binti huyo pia aliomba msamaha kwa wazazi wa binti huyo mwenye umri wa miaka 13.

Binti huyo mwenye umri wa miaka 13 aliomba msamaha na kuahidi kuzingatia masomo yake na kamwe hatakuwa mkaidi. Aliwahakikishia wazazi kwamba hatawadhuru kimwili.'

Uraibu wa simu na mitandao ya kijamii

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Tukio lingine kama hilo lilitokea hivi karibuni. Mnamo Juni 9, 2023, mlezi wa msichana wa miaka 20 kutoka eneo la Maninagar la Ahmedabad alipiga simu 181.

Tmu hiyo iliitwa ili kunusuru mustakabali wa binti mmoja na kumshawishi kuwa makini na masomo yake.

Timu ya 181 pia iliambia BBC kuhusu tukio hilo, 'Maya (jina limebadilishwa) ana umri wa miaka 20, mwaka wa tatu chuo kikuu.

Msichana anavutiwa sana na simu ya smart phone, haachi simu yake au laptop yake.

Haendi chuo kikuu lakini kwa jina la masomo na chuoni, anaondoka nyumbani na kuzurura na marafiki siku nzima.'

'Anazungumza na watu kwenye mitandao ya kijamii kwa kutengeneza utambulisho tofauti.

Msichana huyo anakasirika kwa mambo madogo. Hamsikilizi mtu yeyote. Amekuwa na uhusiano wa kimapenzi kwa muda wa miezi sita iliyopita. Alikuwa amejitengenezea video za ngono kwenye simu yake ya mkononi na kuzituma kwa mpenzi wake. Hazingatii masomo kazi yake ni kutengeneza na kutazama video za ngono tu.'

'Mama yake alichukua simu alipompata akiitumia vibaya. Baba yake alipojua kuhusu hilo, alitafuta usaidizi wa timu ya 181 na kuomba Maya apewe ushauri kuhusu wakati ujao wenye matumani, maisha mazuri na umuhimu wa familia.

Timu ya kutoa usaidizi ilisema: 'Ilimweleza Maya faida za elimu, kuzingatia hilo, kuishi maisha mazuri na kutumia mitandao ya kijamii vizuri, kuepuka marafiki wabaya na kuwaheshimu wazazi.'

Pia 'aliwashawishi wazazi washirikiane naye na wampe wakati binti yao muda wala sio shinikizo.'

Matibabu ya uraibu wa simu

Wakati huo huo, Dk Nimesh Parekh, mkuu wa idara ya magonjwa ya akili katika Hospitali ya SVP ya Ahmedabad Municipal Corporation-inayoendeshwa na Shirika la SVP, aliiambia BBC Gujarati: "Kwa wastani, idara yetu inapokea kisa kimoja cha uraibu wa simu kwa watoto kila siku.

Kuna sababu mbalimbali za uraibu wa simu. Wakati mwingine wazazi wote wawili hawawezi kumfuatilia mtoto kwa sababu ya kazi na katika baadhi ya matukio watoto ni wakaidi.

Wakati mwingine watoto hupata uraibu wa kutumia simu kwa sababu ya mzunguko wa marafiki wanaowazunguka.'

Dk Parekh anaongeza: 'Wazazi wanapaswa kuweka kikomo cha muda wa matumizi ya simu baada ya kuwapa watoto simu na kufuatilia kile ambacho watoto wanatafuta.

Pia wazazi wanapaswa kuchukua watoto kucheza michezo ya ndani na michezo ya nje.

Kuna matumizi mazuri ya simu kwa elimu ya watoto na mzazi anaweza kuweka ukomo wa matumizi ya simu ikihitajika.'

Dk. Parekh anasema kwamba katika kesi ya uraibu wa simu, watoto wengi wanavutiwa zaidi na michezo.

Anasema: ''Asilimia 60 hadi 70 ya kesi za uraibu wa simu zinahusisha watoto kupenda michezo sana, wakati asilimia 30 ya kesi ni kutumia mtandao. Katika asilimia 10 ya visa, vijana wanavutiwa na kutazama tovuti za ponografia. Katika 80 hadi 85% ya kesi, watoto wanaweza kuachishwa tabia hii kupitia ushauri nasaha. Wakati asilimia 10 hadi 15 ya kesi zinaweza kuhitaji matibabu. Dawa za kupunguza mfadhaiko pia zinaweza kutolewa.''