Je, huu ni mfano wa makazi yetu ya mwezini yatakavyokuwa?

Chanzo cha picha, AAKA Space Studio
- Author, Geeta Pandey
- Nafasi, BBC News, Delhi
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Je, kasha hili lenye muundo wa yai ndio utakuwa makazi ya muda kwa wanaanga wa India watakoenda mwezini siku za usoni?
Hab-1, kifupi cha Habitat-1, ni mradi wa kwanza wa "misheni ya kizamani'' wa shirika la anga la India, Isro, unaolenga kufanana na hali halisi ya anga ili kuwaandaa wanaanga kwa safari za anga za kweli.
Mradi huu ulijaribiwa kwa wiki tatu katika milima ya juu ya Himalaya, huko Ladakh.
Msanifu wa kibumba cha anga, Aastha Kacha-Jhala kutoka kampuni ya Aaka, aliiambia BBC kuwa majaribio haya husaidia kugundua na kushughulikia changamoto ambazo wanaanga na vifaa vyao wanaweza kukutana nazo kabla ya safari za anga.
Hab-1 imetengenezwa kwa rasilimali ya Teflon ya kiwango cha anga na imetiwa kihami kwa povu la matumizi ya viwandani.
Pia ina kitanda, trei ambayo ni mahali unaweza kujificha na kutumika kama meza ya kazi, nafasi ya kuhifadhi vifaa na vifaa vya dharura, chumba cha kupikia au kupasha chakula moto, na choo. Mwanaanga mmoja alikaa katika kasha hili kwa wiki tatu.
Kacha-Jhala anasema, "Hab-1 imeundwa kwa kuzingatia kuwa nafasi itakuwa ndogo sana kwenye Mwezi au Mars." Aliongeza kuwa, "Wanaanga watakuwa na upungufu wa maji , hivyo tulibuni choo kavu na mfumo wa kutupa taka vizuri ili kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa safi."
Kacha-Jhala sasa yuko kwa mazungumzo na shirika la Isro kujenga kituo cha majaribio cha kudumu kwa ajili ya India huko Ladakh.

Chanzo cha picha, AAKA Space Studio
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Huu mradi unakuja wakati India inajiandaa kutuma wanaanga wake wa kwanza angani.
Mradi wa Gaganyaan wa Isro unapanga kuwatuma wanaanga watatu katika mzunguko wa chini wa dunia kwa urefu wa kilomita 400 kwa siku tatu.
Ikiwa kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa, uzinduzi unatarajiwa kufanyika mwakani.
India pia inapanga kujenga kituo chake cha anga cha kwanza ifikapo 2035 na kutuma mtu Mwezini ifikapo 2040.
Nasa, Shirika la Anga la Ulaya, Urusi, China na nchi nyingine pamoja na kampuni binafsi zinazohusika na anga, zinafanya majaribio mengi, na wanaanga wawili kati ya wanne walioteuliwa kwa mradi wa Gaganyaan wanapata mafunzo kwa sasa katika shirika la Nasa.
Prof. Subrat Sharma, mkuu wa masomo ya utafiti katika Chuo Kikuu cha Ladakh, anasema: "Pindi tutakapokuwa na mradi wetu wa majaribio, hatutalazimika kutegemea mashirika ya anga ya kigeni kuwafundisha wanaanga wetu."
Ladakh ilichaguliwa kwa majaribio haya kwa sababu "kwa mtazamo wa kijiografia, mandhari yake ya miamba na udongo ina ufanano na nyenzo na mawe yaliyopo Mars na baadhi ya maeneo ya Mwezi, hivyo ni mahali bora kwa utafiti wa anga."
Maji ya udongo yaliyokusanywa wakati wa mradi huu yanachunguzwa na chuo kikuu ili kuona kama wanaanga wataweza kutumia nyenzo zinazopatikana kwa eneo hili kujenga makazi angani.

Chanzo cha picha, AAKA Space Studio
Ladakh ambayo iko mpakani wa India na China na iko kwenye kimo cha mita 3,500 na ina hali ya hewa kali na hewa nyembamba.
Hali ya hewa hapa inaweza kubadilika kutoka joto la 20°C hadi -18°C kwa siku moja. Ingawa si sawa na Mars au Mwezi, ambapo joto linaweza kushuka hadi -153°C na -250°C katika mashimo ya kina, bado ni majaribio ya uvumilivu wa binadamu.
Prof. Sharma anasema: "Kwa kuwa huwezi kwenda angani kila mara kwa majaribio, unahitaji vituo kama hivi ambapo hali za angani zinaweza kutengenezwa."
Ladakh pia ni mojawapo ya maeneo ya India ambapo ardhi ya kavu inaenea kwa maili nyingi, "inakupa hisia ya kuwa peke yako kwenye sayari."
Na ndivyo ilivyokuwa kwa mwanaanga wa majaribio ambaye alikaa wiki tatu kwenye kapsuli ya baridi katika jangwa hili la barafu.
"Nilitengwa kutoka kwa mazingira ya binadamu. Kila harakati niliyofanya ilikuwa imepangwa, nilijua ni lini niamke, nifanye nini na lini nikalale," alisema mwanaanga huyo wa miaka 24, ambaye hakutaka kutajwa jina lake. "Siku chache za mwanzo zilikuwa nzuri, lakini kisha ilianza kuwa ya kurudia na ilinianza kunisumbua. Iliathiri utendaji wangu wa kila siku. Ratiba yangu ya kulala ilikosewa kidogo na umakini wangu ulipungua." anaendelea kuelezea alichokipitia.
Mwanaanga wa majaribio alivaa vifaa vya kibaometri kufuatilia mzunguko wake wa usingizi, mapigo ya moyo na viwango vya mafadhaiko.
Damu na mate yake yalichunguzwa kila siku ili kuona jinsi alivyokuwa akimudu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanasayansi wanasema kuwa kuiga mambo ya kisaikolojia ili kuona jinsi yanavyoathiri wanadamu angani ni sehemu muhimu ya mradi huu.
Kwa kuwa mashirika ya anga duniani yanajiandaa kutuma wanaanga kwenye Mwezi na kuanzisha vituo vya kudumu huko, majaribio ya aina hii yatakuwa na umuhimu mkubwa katika utafiti na mafunzo.
Mwezi Aprili ,kikosi cha wanasanyansi na wahandisi kilianza majaribio regon ili kuandaa Mbwa wa roboti - Lassie - kutembea juu y amwezi, huku China na Urusi wanashirikiana kwa mikakati yao.
India haikutaka kubaki nyuma.
Prof. Sharma anasema, "Pindi data itakapochanganuliwa, itatusaidia kubuni teknolojia za matibabu ili kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo wanaanga wetu wanapokutana na matatizo angani."
''Tunataka kujua iwapo mwili wetu utamudu hali mwezini ambapo mchana na usiku ni mrefu ukilinganisha na ardhini tulikokuzoea. Au angani ambapo hakuna oksijeni ya kutosha,'' anasema Prof.Sharma
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












