Mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza yako katika 'hatua za mwisho' - Qatar
Mkataba kati ya Israel na Hamas kuhusu usitishaji mapigano Gaza na kuachiwa kwa mateka "unakaribia sana kufikiwa," Qatar anasema.
Muhtasari
- Lema amuunga mkono Lissu na amshauri Mbowe akae pembeni
- Waokoaji watoa miili sita zaidi kutoka kwa mgodi wa Afrika Kusini
- Jeshi la Sudan na washirika wake watuhumiwa kuwaua raia Gezira
- India: Wanaume wa Kihindu waliopakwa majivu waongoza ibada ya kuoga
- Korea Kaskazini yarusha makombora ya masafa mafupi
- Trump angehukumiwa kwa kuingilia uchaguzi, ripoti ya DoJ inasema
- Kesi ya kumuondoa madarakani rais aliyesimamishwa kazi yaanza kusikilizwa
- Miili ya waliofariki katika mgodi wa Afrika Kusini yaonekana kwenye video
- Nyota adimu inaweza kuonekana kwa mara ya kwanza katika miaka 160,000
- TikTok inasema ripoti ya uwezekano wa kuuzwa kwa Musk ni 'uongo mtupu'
- Makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza yanakamilika, afisa wa Palestina aiambia BBC
Moja kwa moja
Na Asha Juma & Ambia Hirsi
Song ateuliwa kuwa kocha wa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rigobert Song aliichezea Cameroon zaidi ya mara 130 Beki wa zamani wa Liverpool na West Ham Rigobert Song ameteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).
Song mwenye umri wa miaka 48 anachukua nafasi ya Mswizi Raoul Savoy, ambaye alitimuliwa Oktoba kuelekea mwisho wa kampeni ya CAR ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2025 (Afcon) 2025.
Song, ambaye aliichezea Cameroon mara 137 katika kipindi cha miaka 17 ya soka lake la kimataifa aliwahi kuongoza timu ya soka ya nchi yake kwa miaka miwili.
Nyota huyo wa soka wa zamani aliiongoza Indomitable Lions kwenye michuano ya Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar na Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka jana, ambapo timu hiyo ilitolewa katika hatua ya 16 bora.
Lema amuunga mkono Lissu na amshauri Mbowe akae pembeni

Chanzo cha picha, MITANDAO
Maelezo ya picha, Godbless Lema Aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Godbless Lema, ametangaza rasmi kumuunga mkono Tundu Lissu anayegombea nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho na John Heche anayegombea makamu mwenyekiti.
Akizungumza na wanahabari leo Januari 15, 2025, jijini Dar es Salaam, Lema amesema licha ya kuwa mwenyekiti aliyepo madarakani, Freeman Mbowe ni kaka yake lakini anamuomba apumzike na amuachie Lissu nafasi hiyo.
“Nimeona hoja nyingi wanasema Lissu hana pesa, sio tajiri kwa hiyo hawezi kuendesha chama, sasa kama kuna kitu kinatakiwa kuwafanya wanachama wamchague Lissu basi ni kutokuwa kwake na pesa, kwa sababu chama hakipaswi kujengwa na fedha za mtu mmoja,” amesema.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, akizungumzia tuhuma alizopewa Lissu kuwa ni mropokaji amehoji, “hivi Lissu anaropoka nini? Kazi kubwa ya upinzani ni kupiga kelele.”
Lema amesema Mbowe alimwambia wajipange kwani anataka kuachia chama amechoka na anahitaji wamsaidie, sasa ameshangaa kuona anagombea tena badala ya kumuunga mkono Lissu.
“Mwenyekiti amefanya kazi kubwa sana, hakuna anayebisha, maisha yake yote ameishi ndani ya chama, amekaa kwenye chama akiwa mdogo, yeye ndiye muasisi wa chama hiki, anaweza kuwa hataki kugombea tena lakini ameshashambuliwa sana, kwa hiyo anataka kujisafisha, nimshauri tu zipo njia nyingi za kujisafisha na akamuunge mkono Lissu, ili yeye aendelee kukisaidia chama kwa heshima,” amesema Lema.
Uchaguzi wa Chadema unatarajiwa kufanyika Januari 21, 2025.
Pia unaweza kusoma:
Waokoaji watoa miili sita zaidi kutoka kwa mgodi wa Afrika Kusini

Chanzo cha picha, EPA
Miili sita zaidi imetolewa kutoka kwenye mgodi wa Afrika Kusini shughuli ya kuwasaidia wachimbaji madini wanaosadikiwa kukwama chini ya ardhi ikiendelea kwa siku ya pili,shirika la Sanco, limeiambia BBC.
Watu wanane walitolewa wakiwa hai siku ya Jumanne na kufikisha 26 idadi ya watu waliookolewa kutoka kwenye mgodi huo tangu Jumatatu.
Wanaume hao wamekuwa wa chini ya ardhi tangu polisi wa Afrika Kusini walipoanzisha msako dhidi ya wachimbaji madini haramu mwaka jana kote nchini.
Wiki iliyopita mahakama iliamuru serikali kuanzisha mpango wa uokoaji ambao ilikuwa imechelewa kwa muda mrefu.
Huku hayo yakijiri mamlaka nchini Afrika Kusini zimetetea ukandamizaji wake dhidi ya uchimbaji madini haramu, huku mamia ya wanaume wakiokolewa baada ya kunaswa kwenye mgodi ambao haukuwa unatumika kwa miezi kadhaa.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekosoa hatua kali iliyochukuliwa na serikali dhidi yauchimbaji madini haramu. Wachimbaji hawa walinyima chakula na maji ili kuwalazimisha kutoka kwenye mgodi huo.
Waziri wa Madini wa Afrika Kusini Gwede Mantashe amesema kuwa uchimbaji madini haramu ni vita dhidi ya uchumi.
Ameongeza kuwa kuna haja ya kuimarisha mapambano dhidi ya uchimbaji madini haramu.
Maelezo zaidi:
Jeshi la Sudan, washirika wake watuhumiwa kuwaua raia Gezira
Ripoti kutoka Sudan zinasema zaidi ya watu 100 waliuawa siku ya Jumatatu katika shambulio la makombora huko Omdurman, mji ulio karibu na mji mkuu, Khartoum.
Mtandao wa kujitolea, Chumba cha Kukabiliana na Dharura cha Ombada, haujabaini ni nani aliyehusika na shambulio hilo.
Jeshi la Sudan hivi karibuni limefanikiwa kurudisha nyuma waasi wa RSF.
Waokoaji wanasema wahudumu wa afya wanajitahidi kuhudumia idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa.
Mtandao wa kujitolea unasema idadi ya waliofariki ni ya awali kwa sababu ni vigumu kufikia baadhi ya maeneo kutokana na mapigano yanayoendelea.
Jeshi linasema kuwa limeteka maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa na RSF huko Omdurman, mji pacha wa mji mkuu Khartoum, katika mto Nile.
Wakaazi wameripoti kushambulia kwa makombora katika mto huo, huku mabomu na makombora yakishambulia nyumba mara kwa mara
Pande zote mbili zimeshutumiwa kwa kuwalenga raia wakiwemo wahudumu wa afya na kushambulia kwa makombora maeneo ya makazi.
India: Wanaume wa Kihindu waliopakwa majivu waongoza ibada ya kuoga

Chanzo cha picha, Ankit Srinivas
Wanaume watakatifu wa Kihindu waliopakwa majivu waliingia kwenye mto mtakatifu zaidi wa India wa Ganges alfajiri ya siku ya kwanza ambayo ni muhimu katika ibada ya kuoga ya sikukuu ya Kumbh Mela kwenye jiji la kaskazini la Prayagraj.
Waumi hao waliimba nyimbo zao za kidini, wakiita miungu ya Kihindu walipokuwa wakitumbukia ndani ya maji yenye barafu.
Baada ya kutoka majini, wengine waliokota mchanga wa rangi ya fedha mkononi na kuupaka mwilini mwao.
Pia kuna waliobeba panga na mkuki wenye ncha tatu huku mkono mwingine ukishikilia juu fimbo ya fedha yenye kichwa cha nyoka.
Kando ya watu hawa watakatifu - wanaojulikana kama Naga sadhus - mamilioni ya mahujaji wa Kihindu kutoka kote ulimwenguni wako Prayagraj kushiriki katika tamasha ambalo linaweza kuonekana kutoka angani na linadaiwa kuwa mkusanyiko mkubwa zaidi wa wanadamu.
Wahindu wanaamini kwamba tambiko la kuoga mtoni litawatakasa dhambi, nafsi zao na kuwasaidia kupata uwokovu kwa kuwakomboa kutoka katika mzunguko wa kuzaliwa na kifo.
Soma zaidi:
Korea Kaskazini yarusha makombora ya masafa mafupi

Chanzo cha picha, Reuters
Korea Kaskazini imerusha makombora mengi ya masafa mafupi kwenye pwani yake ya mashariki siku ya Jumanne, jeshi la Korea Kusini lilisema.
Makombora hayo yalisafiri takriban kilomita 250 (maili 155) baada ya kuruka mwendo wa saa 09:30 asubuhi (0030 GMT) kutoka Kanggye, Mkoa wa Jagang, karibu na mpaka wa nchi hiyo na China, Wakuu wa Pamoja wa Wafanyakazi wa Seoul (JCS) walisema.
"Tunalaani vikali uzinduzi huo kama uchochezi wa wazi ambao unatishia pakubwa amani na utulivu wa rasi ya Korea," JCS ilisema.
Kaimu Rais wa Korea Kusini Choi Sang-mok pia alilaani uzinduzi huo akisema ni ukiukaji wa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema Seoul itajibu vikali chokochoko za Korea Kaskazini.
Pia unaweza kusoma:
Trump angehukumiwa kwa kuingilia uchaguzi, ripoti ya DoJ inasema

Chanzo cha picha, Reuters
Rais mteule Donald Trump angehukumiwa kwa kujaribu kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2020 - ambayo alishindwa - ikiwa hangefanikiwa kuchaguliwa tena mwaka wa 2024, kulingana na ripoti ya Idara ya Sheria iliyotolewa kwa Bunge.
"Ushahidi unaokubalika ulitosha kumfungulia mashtaka," ripoti ya Wakili Maalum Jack Smith ilisema.
Smith "amechanganyikiwa" na matokeo yake ni "feki", Trump amejibu baada ya ripoti hiyo kutolewa.
Nyaraka hiyo ya kurasa 137 ilitumwa kwa Bunge baada ya Jaji Aileen Cannon kuruhusu kutolewa kwa sehemu ya kwanza kati ya mbili za ripoti ya Smith - kuhusu kesi ya kuingiliwa kwa uchaguzi.
Aliamuru kusikilizwa kwa kesi nyingine baadaye wiki hii kuhusu kutolewa kwa sehemu ya ripoti juu ya madai kwamba Trump alihifadhi hati za serikali kinyume cha sheria.
Rais mteule atachukua madaraka tarehe 20 Januari.
Wakili maalum, Jack Smith, alijiuzulu kutoka wadhifa wake wiki iliyopita.
Smith aliteuliwa mnamo 2022 kusimamia uchunguzi wa Idara ya Sheria ya Marekani juu ya Trump.
Mawakili maalum huchaguliwa na idara katika kesi ambapo kuna uwezekano wa mgongano wa maslahi.
Trump alishtakiwa kwa kuhifadhi hati kinyume cha sheria na, katika baadhi ya kesi, kuzihifadhi katika vyumba vya mapumziko ya Mar-a-Lago huko Florida, makazi yake ambayo anamiliki.
Katika kesi ya uingiliaji kati uchaguzi, alishtakiwa kwa kula njama ya kutengua matokeo ya uchaguzi wa 2020.
Kesi zote mbili zilisababisha mashtaka ya jinai dhidi ya Trump, ambaye alikanusha kuwa na hatia na kudai kuwa yaliyochochewa kisiasa.
Lakini Smith alifunga kesi hizo baada ya Trump kushinda uchaguzi mnamo mwezi Novemba, kwa mujibu wa kanuni za Idara ya Sheria zinazokataza kufunguliwa mashitaka kwa rais aliye madarakani.
Soma zaidi:
Kesi ya kumuondoa madarakani rais aliyesimamishwa kazi yaanza kusikilizwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Mahakama ya kikatiba ya Korea Kusini imefanya kikao chake cha kwanza kuamua iwapo Rais aliyesimamishwa kazi Yoon Suk Yeol aondolewe madarakani baada ya jaribio lake la kushtukiza la kutekeleza sheria ya kijeshi mwezi uliopita.
Hata hivyo kikao hicho kiliisha ndani ya dakika nne kwa sababu ya kutokuwepo kwa Yoon - mawakili wake walikuwa wamesema awali hatahudhuria kwa usalama wake, kwani kuna kibali cha kukamatwa kwake kwa mashtaka tofauti ya uasi.
Mnamo mwezi Desemba, Yoon alisimamishwa kazi baada ya wanachama wa chama chake pamoja na upinzani kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.
Hata hivyo ataondolewa rasmi afisini ikiwa tu angalau majaji sita kati ya wanane wa mahakama ya kikatiba watapiga kura kuunga mkono mashtaka hayo.
Kulingana na sheria za Korea Kusini, mahakama lazima ipange tarehe mpya ya kusikilizwa kwake kabla ya kuendelea bila ushiriki wake.
Kesi inayofuata imepangwa kufanyika Alhamisi.
Mawakili wa Yoon wameeleza kuwa atajitokeza kusikilizwa kwa "wakati mwafaka", lakini wamepinga "uamuzi wa upande mmoja" wa mahakama katika tarehe za kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Yoon hajatoa maoni yake hadharani tangu bunge lilipopiga kura ya kumshtaki tarehe 14 Desemba na amekuwa akizungumza hasa kupitia mawakili wake.
Yoon ni rais wa kwanza wa Korea Kusini kukabiliana na mashtaka ya kukamatwa.
Jitihada za pili za kumweka kizuizini zinaweza kufanyika mapema wiki hii, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.
Soma zaidi:
Miili ya waliofariki katika mgodi wa Afrika Kusini yaonekana kwenye video

Chanzo cha picha, Getty Images
Video za kuhuzunisha zimeibuka zikionyesha hali mbaya katika mgodi wa dhahabu uliotelekezwa nchini Afrika Kusini ambapo wachimbaji haramu wengi wameripotiwa kuishi chini ya ardhi kwa miezi kadhaa.
Wamekuwepo tangu operesheni za polisi kulenga uchimbaji haramu wa madini kuanza mwaka jana kote nchini humo.
Katika mojawapo ya video hizo, ambazo BBC haijathibitisha kwa kujitegemea, maiti zikiwa zimefungwa kwenye mifuko ya miili zinaonekana.
Ya pili inaonyesha wachimbaji madini ambao bado wako hai.
Shughuli ya uokoaji iliyocheleweshwa kwa muda mrefu, ambayo wiki iliyopita mahakama iliamuru serikali kuwezesha utekelezaji wake, ilianza Jumatatu.
Makala hii ina video ambayo baadhi ya watu wanaweza kuiona yenye kuhuzunisha
Mwaka jana, wakisema kwamba wachimbaji waliingia mgodini huko Stilfontein kwa makusudi bila ruhusa, mamlaka ilichukua msimamo mkali, kuzuia wasipewe chakula wala maji.
Mnamo mwezi Novemba, waziri mmoja wa serikali alisema: "Tutawalazimisha kutoka hadharani."
Zaidi ya wachimba migodi 100 haramu, wanaojulikana na wenyeji kama "zama zamas", wameripotiwa kufa chini ya ardhi tangu kuanza kwa msako mkali kwenye mgodi huo ulioko kilomita 145 (maili 90) kusini-magharibi mwa Johannesburg.
Mamlaka hata hivyo, hazijathibitisha takwimu hii kwa kuwa bado "haijathibitishwa na chanzo rasmi", msemaji aliiambia BBC.
Mamia wanakisiwa kuwa bado wako mgodini huku zaidi ya 1,000 wakijitokeza katika miezi michache iliyopita.
Katika moja ya video iliyotolewa na chama cha wafanyakazi, General Industries Workers of South Africa (Giwusa), makumi ya wanaume wasio na shati wanaweza kuonekana wakiwa wameketi kwenye sakafu chafu.
Nyuso zao zimezibwa. Sauti ya kiume nje ya kamera inaweza kusikika ikisema kuwa wanaume hao wana njaa na wanahitaji msaada.
Maelezo ya video, Video zinaonyesha miili na watu waliodhoofika za wachimba migodi "Tunaanza kukuonyesha miili ya waliokufa chini ya ardhi," anasema.
"Na hawa sio wote... Unaona jinsi watu wanavyohangaika? Tafadhali tunahitaji msaada."
Katika video nyingine, mwanamume mmoja anasema: "Hii ni njaa; watu wanakufa kwa sababu ya njaa." Kisha anaweka idadi ya vifo kuwa 96 na anaomba msaada, chakula na vifaa.
Insemekana video hiyo ilirekodiwa siku ya Jumamosi.

Chanzo cha picha, Giwusa
Maelezo ya picha, Mashine inayoshushwa chini kutoka juu ya mgodi isiyotumika ili kuwarudisha wachimbaji juu Katika kikao kilichofanyika Jumatatu karibu na eneo la operesheni ya uokoaji, uongozi wa Giwusa, pamoja na jamii, walisema video hizo "zilitoa picha mbaya sana" ya hali ilivyo chini ya mgodi.
"Kilichotokea hapa lazima kiitwe jinsi kilivyo; haya ni mauaji ya Stilfontein. Kwa sababu kile ambacho picha hii inafanya ni kuonyesha rundo la miili ya watu, ya wachimba migodi waliokufa bila sababu," rais wa Giwusa Mametlwe Sebei alisema.
Alizilaumu mamlaka kwa kile alichoeleza kuwa ni “sera za hiana” ambazo zilifuatwa kimakusudi.
Soma zaidi:
Nyota adimu inaweza kuonekana kwa mara ya kwanza katika miaka 160,000

Chanzo cha picha, Don Pettit/NASA
Maelezo ya picha, Nyota hiyo ilionekana kutoka Kituo cha Kimataifa cha Anga cha Juu mwishoni mwa juma Nyota angavu ya Comet C/2024 G3 inaweza kuonekana angani kote ulimwenguni katika siku zijazo kwa mara ya kwanza katika miaka 160,000.
Nasa ilisema mng'ao wa siku zijazo wa nyota hiyo "ni vigumu sana kutabiri," lakini inaweza kuendelea kung'aa vya kutosha kuonekana kwa macho.
Siku ya Jumatatu, nyota hiyo ilikuwa kwenye ‘Periheli’ mahali katika obiti ya sayari ambako ni karibu zaidi na jua, kunakochangia jinsi inavyoonekana yaani yenye kung’aa sana.
Wataalam wanasema inaweza kuonekana kuanzia Jumatatu usiku.
Ingawa maeneo kamili ya uwezekano wa kuonekana hayajulikani, wataalam wanaamini kwamba nyota Comet, ambayo inaweza kung'aa kama sayari ya Zuhura, itakuwa vizuri zaidi kuitazama kutoka upande wa Kizio cha Kusini.
Dk Shyam Balaji, mtafiti wa fizikia ya astroparticle na cosmology katika Chuo cha King's College London, alisema "hesabu za sasa za obiti zinaonyesha kuwa itapita takriban maili milioni 8.3 kutoka kwenye Jua".
Bw Balaji aliwashauri watu wanaotaka kuona nyota hiyo kutafuta eneo lililo mbali na uchafuzi wa mwanga na kutumia jozi ya darubini au darubini ndogo.
Aliwaonya waangalizi kuwa waangalifu wakati jua linachomoza na machweo, na kuongeza kuwa wafuatilie ili wajue mahali ambapo inaweza kuonekana angani.
Pia unaweza kusoma:
TikTok inasema ripoti ya uwezekano wa kuuzwa kwa Musk ni 'uongo mtupu'

Chanzo cha picha, Getty Images
TikTok imeita ripoti kwamba China inazingatia kuruhusu uuzaji wa shughuli za mtandao huo wa kijamii nchini Marekani kwa Elon Musk ni " uongo mtupu."
Maoni ya kampuni hiyo yanatolewa kujibu ripoti ya Bloomberg kwamba maafisa wa China wanazingatia chaguo ambalo linaweza kuhusisha biashara yake inayoendeshwa nchini Marekani kuuzwa kwa mtu tajiri zaidi duniani ikiwa Mahakama ya Juu Zaidi ya Marekani itadumisha marufuku dhidi ya mtandao huo.
Majaji wa Mahakama ya Juu Zaidi wanatakiwa kutoa uamuzi kuhusu sheria iliyoweka tarehe ya mwisho ya kuendesha mtandao huo wa TikTok kuwa Januari 19 ama kuuza uendeshaji wa shughuli zake nchini Marekani au ipigwe marufuku nchini humo.
TikTok imesema mara kwa mara kwamba haitauza uendeshaji wa shughuli zake nchini Marekani.
"Hatuwezi kutarajiwa kutoa maoni kuhusu kitu cha uwongo," msemaji wa TikTok aliambia BBC News.
Bloomberg iliripoti, ikitoa mfano wa watu wanaofahamu suala hilo, kwamba hatua moja inayowezekana kufikiriwa kuchukuliwa na maafisa wa China ni jukwaa hilo la mtandao wa kijamii wa TikTok kuanza kuendeshwa na Musk ambaye anaendesha mtandao wa X.
Musk ni mshirika wa karibu wa rais mteule wa Marekani Donald Trump, ambaye anatazamiwa kurejea Ikulu ya White House tarehe 20 Januari.
Mwezi uliopita, Trump aliitaka Mahakama ya Juu kuchelewesha uamuzi wake hadi atakapoingia madarakani ili kumwezesha kutafuta "azimio la kisiasa".
Soma zaidi:
Makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza yanakamilika, afisa wa Palestina aiambia BBC

Chanzo cha picha, Getty Images
Masharti ya makubaliano kati ya Israel na Hamas kwa ajili ya kusitisha mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka yanakamilika, afisa wa Palestina anayefahamu mazungumzo hayo ameiambia BBC.
Hilo linawadia wakati Rais wa Marekani Joe Biden alisema makubaliano "yapo karibu kufikiwa", na kwamba utawala wake unashughulikia suala hilo haraka.
Afisa wa Israel pia aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba mazungumzo yalikuwa katika "hatua za mwisho mwisho", na makubaliano yanawezekana kufikiwa ndani ya "saa, siku au zaidi".
Rais wa Marekani Joe Biden alizungumza na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Jumapili, na Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani wa Qatar - ambaye ni mpatanishi wa mazungumzo hayo – siku ya Jumatatu.
Afisa huyo wa Palestina aliambia BBC kuwa viongozi wa Hamas na Israel walikuwa wakifanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja katika jengo moja siku ya Jumatatu.
Akifichua maelezo ya uwezekano wa makubaliano hayo, afisa huyo alisema kuwa "majadiliano ya kina ya masuala yenye utata yalichukua muda mrefu".
Pande zote mbili zilikubaliana kuwa Hamas itawaachilia mateka watatu katika siku ya kwanza ya makubaliano hayo, na baada ya hapo Israel itaanza kuwaondoa wanajeshi katika maeneo yanayokaliwa na watu wengi.
Siku saba baadaye, Hamas itawaachilia mateka wanne zaidi, na Israel itaruhusu watu waliokimbia makazi yao kusini mwa nchi kurejea kaskazini, lakini kwa miguu tu kupitia barabara ya pwani.
Magari, mikokoteni ya kuendeshwa na wanyama na malori yataruhusiwa kupita kwenye njia iliyo karibu na Barabara ya Salah al-Din, ikifuatiliwa na mashine ya X-ray inayoendeshwa na timu ya usalama ya Qatar na Misri.
Makubaliano hayo yanajumuisha masharti ya vikosi vya Israel kubaki katika ukanda wa Philadelphi na kudumisha eneo salama la mita 800 kwenye mpaka wa mashariki na kaskazini wakati wa awamu ya kwanza, ambayo itadumu kwa siku 42.
Israel pia imekubali kuwaachilia wafungwa 1,000 wa Kipalestina, wakiwemo takriban 190 ambao wamekuwa wakitumikia kifungo cha miaka 15 au zaidi. Katika mpango wa mabadilishano, Hamas itawaachilia mateka 34.
Mazungumzo ya awamu ya pili na ya tatu ya makubaliano hayo yataanza siku ya 16 ya kusitisha mapigano.
Baba wa mateka Mwisraeli mwenye asili ya Marekani aliiambia BBC Newshour kwamba "anataka kuamini" kuwa Israel "imekubali" makubaliano hayo.
Pia unaweza kusoma:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 14/01/2025

