Jinsi tulivyompata msichana mdogo aliyenaswa kwenye picha ya wafungwa wa Gaza

A group of dozens of detained Gazan men pictured in their underwear, during what appears to be an Israeli check for weapons and signs of any links to Hamas. They are sitting or squatting, some young and some older. At the far left of the picture, in the middle of the group, a little girl with dark hair can be seen. The BBC has chosen to blur the faces of the men nearer the front of the picture. In the background is a destroyed building, collapsed into rubble.

Chanzo cha picha, supplied

Maelezo ya picha, Katika kundi la wanaume wa Gaza, wanaozuiliwa na majeshi ya Israeli, msichana mdogo anaweza kuonekana (amezungukwa). BBC imeamua kuficha nyuso za wale wanaoweza kutambulika zaidi.
    • Author, Fergal Keane
    • Nafasi, Mwandishi maalum
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Ni vigumu kumuona katika umati wa wanaume. Sura yake ni ndogo iliyojificha huko nyuma.

Askari hao wamewaamuru watu hao kuvua nguo zao za ndani. Hata baadhi ya wazee. Wanamtazama mtu anayepiga picha. Huenda ni mwanajeshi wa Israel.

Picha hiyo inaonekana kuchapishwa kwanza kwenye akaunti ya Telegram ya mwandishi wa habari mwenye vyanzo katika Jeshi la Ulinzi la Israel.

Wanaume wanaonekana wanyonge, wenye hofu na wamechoka. Msichana mdogo, ambaye alionekana kwenye picha na mtayarishaji wa vipindi wa BBC, anaangalia pembeni. Labda kitu kisichoonekana kwenye kamera kimevutia umakini wake. Au labda hataki tu kuangalia askari na bunduki zao.

Wanajeshi wamewaambia watu wakae hapa. Majengo yaliyolipuliwa na bomu yanaonekana hadi nyuma yao. Wawakagua watu hao kutafuta silaha, nyaraka, ishara yoyote ya uhusianowao na Hamas.

Kwa hivyo mara nyingi mateso ya vita hivi hupatikana katika undani wa maisha ya mtu binafsi. Uwepo wa mtoto, usemi wake anapotazama kando, ni maelezo ambayo huzua maswali mengi.

Kwanza, alikuwa nani? Nini kilimpata? Picha hiyo ilipigwa wiki moja iliyopita.

Wiki moja ya mamia waliouawa, wengi walijeruhiwa, na maelfu kuhamishwa kutoka kwa nyumba zao. Watoto walikufa kutokana na mashambulizi ya anga au kwa sababu hakukuwa na dawa au wahudumu wa matibabu wa kuwatibu.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tukifanya kazi na kipindi cha BBC Arabic 'Gaza Today' tulianza kumtafuta mtoto huyo. Israel hairuhusu BBC au vyombo vingine vya habari vya kimataifa kufikia Gaza kuripoti kwa njia uhuru, kwa hivyo BBC inategemea mtandao unaoaminika wa waandishi wa habari wa kujitegemea. Wenzetu walizungumza na washirika wao ndani ya mashirika ya misaada kaskazini mwa Gaza , wakionyesha picha hiyo katika maeneo ambayo waliokimbia makazi yao walikuwa wamekimbilia.

Ndani ya masaa 48 jibu likarudi. Ujumbe kwenye simu ulisema hivi: “Tumempata!”

Julia Abu Warda, mwenye umri wa miaka mitatu, alikuwa hai. Mwanahabari wetu alipofikia familia katika Jiji la Gaza - ambapo wengi kutoka Jabalia wamekimbia - Julia alikuwa na baba yake, babu na mama yake.

Alikuwa akitazama katuni ya kuku wakiimba, vigumu kusikia kwa sababu ya mlio wa kutisha wa ndege isiyo na rubani ya Israel.

Julia alishangaa ghafla kuwa lengo la tahadhari ya mgeni.

"Wewe ni nani?" baba yake aliuliza, kimzaha

"Jooliaa" alijibu huku akinyoosha neno kwa msisitizo.

Julia Abu Warda, aged three, sits on her father's knee, as he looks down. There is a wary expression in her brown eyes. She is dressed in a peach-coloured jumper, with her hair in two buns tied with blue bobbles.
Maelezo ya picha, BBC ilimpata Julia na babake, Mohammed, katika mji wa Gaza

Julia hakuwa amejeruhiwa kimwili. Akiwa amevalia fulana na suruali ya jeans, nywele zake zikiwa zimeshikiliwa na kipira cha maua ya buluu angavu. Lakini usemi wake ulikuwa wa kuhofia.

Kisha Muhammad akaanza kusimulia hadithi nyuma ya picha iliyosambaa.

Familia hiyo ilihamishwa mara tano katika siku 21 zilizopita. Kila wakati walikuwa wakikimbia kutokana na mashambulizi ya anga na milio ya risasi.

Siku ambayo picha hiyo ilipigwa walisikia ndege isiyo na rubani ya Israel ikitangaza onyo la kuhama.

Hii ilikuwa katika wilaya ya Al-Khalufa ambapo IDF ilikuwa ikisonga mbele dhidi ya Hamas.

"Kulikuwa na makombora yaliyolipuliwa hapa na pale. Tulikwenda katikati ya kambi ya wakimbizi ya Jabalia, kwenye barabara ya kituo cha ukaguzi.

Familia hiyo ilibeba nguo zao, makopo ya vyakula vilivyowekwa kwenye mikebe ya bati, na vitu vichache vya kibinafsi.

Mwanzoni kila mtu alikuwa pamoja. Baba ya Julia, mama yake Amal, kaka yake Hamza wa miezi 15, babu, wajomba wawili na binamu.

Lakini katika machafuko hayo, Mohammed na Julia walitenganishwa na wengine.

“Nilitengana na mama yake kutokana na wingi wa watu na vitu vyote tulivyokuwa tumebeba. Aliweza kuondoka, na mimi nilibaki mahali pamoja,” Mohammed alisema.

Baba na binti hatimaye waliendelea na mtiririko wa watu waliokuwa wakitoka nje. Mitaa ilijaa taswira ya kifo. "Tuliona uharibifu na miili imetawanyika ardhini," Mohammed alisema. Hakukuwa na jinsi ya kumzuia Julia kuona baadhi ya uharibifu na wafu. Baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa vita, watoto wamezoea kuona wale ambao wamekufa kikatili.

Kundi hilo lilifika kituo cha ukaguzi cha Israeli.

"Kulikuwa na askari kwenye vifaru na askari waliokuwa chini. Wakawasogelea watu na kuanza kufyatua risasi juu ya vichwa vyao. Watu walikuwa wakisukumana wakati wa ufyatuaji risasi.

Wanaume hao waliamriwa kuvua nguo zao za ndani. Huu ni utaratibu wa kawaida wakati IDF inapotafuta silaha zilizofichwa au walipuaji wa kujitoa mhanga. Mohammed anasema walizuiliwa katika kizuizi hicho kwa saa sita hadi saba. Katika picha Julia anaonekana mtulivu. Lakini baba yake alikumbuka huzuni yake baadaye.

"Alianza kupiga kelele na kuniambia kuwa anamtaka mama yake."

Familia iliunganishwa tena. Waliohamishwa wamejaa katika maeneo madogo. Mafungamano wa kifamilia umeboreshwa. Habari husafiri haraka katika Jiji la Gaza wakati jamaa anawasili kutoka Jabalia. Julia alifarijiwa na watu waliompenda. Kulikuwa na peremende na vibanzi, vitamutamu ambavyo vilikuwa vimehifadhiwa vizuri.

Kisha Mohammed akafichua kwa mwenzetu kiwewe kikubwa alichopata Julia, kabla ya siku hiyo ya kukimbia kutoka Jabalia hadi Gaza City. Alikuwa na binamu aliyempenda zaidi. Jina lake lilikuwa Yahya na alikuwa na umri wa miaka saba. Walikuwa wakicheza pamoja mitaani. Takriban wiki mbili zilizopita Yahya alikuwa mtaani wakati Waisraeli walipoanzisha shambulio la ndege zisizo na rubani. Mtoto huyo aliuawa.

"Maisha yalikuwa ya kawaida. Angekimbia na kucheza,” alisema. "Lakini sasa, wakati wowote kunapotokea makombora, yeye huelekeza na kusema, 'ndege!' Tukiwa tumenaswa anatazama juu na kuelekezea ndege isiyo na rubani inayoruka juu yetu."

Julia rubs one of her eyes with a hand as she leans against her father, who holds her on his lap. Mohammed is a young man with dark hair and a trimmed beard. They are sitting down in a plastic chair, outside.
Maelezo ya picha, Binamu kipenzi cha Julia, Yahya, aliuawa barabarani katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Israeli

Kulingana na Unicef ​​- shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto -watoto 14,000 wameripotiwa kuuawa katika vita hivyo.

"Kila siku watoto wanalipia gharama ya vita ambavyo hawakuvianzisha," alisema msemaji wa Unicef, Jonathan Crickx.

"Watoto wengi ambao nimekutana nao wamefiwa na mpendwa katika hali mbaya sana."

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa karibu watoto wote katika Ukanda wa Gaza - karibu milioni moja - wanahitaji msaada wa afya ya akili.

Ni vigumu kumwita mtoto kama Julia kuwa mwenye bahati. Unapofikiria kile ambacho amekiona na kupoteza na wapi amenaswa. Nani anajua nini kitarudi katika ndoto na kumbukumbu katika siku zijazo. Kufikia sasa anajua kuwa maisha yanaweza kuisha kwa ghafla na kwa njia mbaya sana.

Bahati yake nzuri iko katika familia ambayo itafanya chochote kinachowezekana kibinadamu - mbele ya mashambulio ya anga, mapigano ya bunduki, njaa na magonjwa - kumlinda.

Ripoti ya ziada kutoka kwa Haneen Abdeen, Alice Doyard, Moose Campbell na Rudaba Abbass. Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Ambia Hirsi