Tajiri mpya wa China: Je, muanzilishi wa TikTok ni nani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuongezeka kwa umaarufu wa TikTok kimataifa kumemuwezesha mwanzilishi mwenza wa kampuni yake mama, ByteDance, kuwa mtu tajiri zaidi wa Uchina.
Zhang Yiming sasa ana utajiri wa thamani ya dola bilioni 49.3, ikiwa ni ongezeko la asilimia 43 kutoka mwaka 2023, kwa mujibu wa orodha ya taasisi ya utafiti ya Hurun.
Zhang, mwenye umri wa miaka 41, alijiuzulu kama afisa mkuu mtendaji wa ByteDance mnamo 2021, lakini inaaminika kuwa bado anamiliki karibu 20% ya kampuni.
TikTok imekuwa moja ya programu maarufu zaidi za mitandao ya kijamii ulimwenguni, licha ya wasiwasi katika nchi nyingine kuhusu uhusiano wake na serikali ya China.
Wakati TikTok na ByteDance wanadai kuwa huru na serikali ya China, Marekani inapanga kuipiga marufuku TikTok mnamo Januari 2025 isipokuwa ByteDance ikiuza shughuli zake nchini.
Licha ya shinikizo kutoka Marekani, faida ya kimataifa ya ByteDance iliongezeka kwa 60% mwaka jana, na kuongeza utajiri wa kibinafsi wa Zhang Yiming.
"Zhang Yiming ni mtu wa 18 kuongoza kwenye orodha ya matajiri Wachina katika miaka 26 tu," alisema Rupert Hoogewerf, mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Hurun.
"Marekani, kwa kulinganisha, orodha yake ya matajiri imekuwa na idadi ya watu wanne tu: Bill Gates, Warren Buffett, Jeff Bezos na Elon Musk. Hii inatoa ishara ya kuyumba kwa uchumi wa China."
Kabla ya Zhang, mtu tajiri zaidi nchini China alikuwa Zhong Shanshan, mwenyekiti wa kampuni kubwa ya vinywaji nchini China, Nongfu Spring, kwa mujibu wa Reuters.
Zhang Yiming ni nani?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Zhang Yiming alizaliwa Longyan, kusini mashariki mwa China, mwaka 1983.
Kabla ya kuanza kampuni yake mwenyewe, ByteDance, mwaka 2012, alifanya kazi katika makampuni ya Microsoft na Kuxun, moja ya tovuti za uchukuzi na usafirishaji zinazosakwa zaidi mtandaoni nchini China, ambayo baadaye ilinunuliwa na TripAdvisor.
Mhandisi huyo wa programu alianza safari ya kampuni yake kwa programu ya akili mnemba (AI) inayokusanya habari kuhusiana na mambo mbali mbali, ambayo ilifanikiwa sana nchini China.
Yeye mwenyewe aliielezea kama "biashara ya utafutaji" au "mtandao wa kijamii", zaidi ya kampuni ya habari tu, katika mahojiano na Bloomberg mnamo 2017.
Baada ya kuwekeza katika programu kadhaa, ByteDance ilitengeneza mtandao uliotangulia TikTok, unaoitwa Douyin, ambao ulizinduliwa ndani ya nchi mnamo 2016. Wazo lilikuwa kuunda video za muziki za sekunde 15 ambazo zitashirikiwa mtandaoni.
Mnamo 2017, Douyin iliingia kwenye soko la kimataifa chini ya jina TikTok. Huu ulikuwa mwaka huo huo ambapo ByteDance ilipata programu ya Musical.ly, ikirithi zaidi ya watumiaji milioni 20, ambao uliisaidia TikTok kupanuka.
Katika wasifu wake uliochapishwa katika jarida la Marekani la Time, Zhang anaelezewa kama "Mtu myenyekevu lakini mwenye ushawishi" na "kijana lakini wenye busara".
Zhang alijiuzulu kama mwenyekiti wa ByteDance mnamo 2021 baada ya kujiuzulu kama kkurugenzi ttendaji mapema mwaka huo, ikiripotiwa kuwa alifanya hivyo kutokana na shinikizo kutoka serikali ya China.

Chanzo cha picha, Reuters
Mabilionea wa Teknolojia
Zhang Yiming sio mwakilishi pekee wa sekta kubwa ya teknolojia ya China kwenye orodha.
Pony Ma, mkuu wa michezo ya bahati nasibu wa kampuni ya teknolojia, burudani na Akili mnemba (AI), ni wa tatu kwenye orodha.
Hata hivyo, utajiri wao hauelezewi tu na kuwa umetokana na mafanikio ya makampuni yao, kwani washindani wao wamepata pesa kidogo katika mwaka ambao uchumi wa China unakiwa katika hali ya msukosuko.
Ni asilimia 30 tu ya watu walio kwenye orodha hiyo walio na ongezeko la thamani ya utajiri wao katika mwaka uliopita; Wengine walishuhudia kushuka kwa utajiri wao.
"Orodha ya matajiri wa China ilipungua kwa mwaka wa tatu mfululizo wakati uchumi wa China na masoko ya hisa yalikuwa na mwaka mgumu," alisema Rupert Hoogewerf, mkuu wa taasisi ya Hurun.
"Idadi ya watu kwenye orodha hiyo imeshuka kwa asilimia 12 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita hadi chini ya 1,100, ikiwa ni punguzo la asilimia 25 kutoka mwaka 2021."
Hoogewerf alielezea kuwa ulikuwa mwaka mzuri kwa watengenezaji wa smartphone kama Xiaomi, wakati soko la nishati ya kijani lilijitahidi kuongezeka.
"Watengenezaji wa paneli za jua, na magari ya umeme wamekuwa na mwaka mgumu, huku wakikabiliwa na ushindani unaoongezeka unaosababisha kuongezeka kwa usambazaji, na kuongezeka kwa tisho la ushuru," alisema.
"Watengenezaji wa paneli za jua wameshuhudia kushuka kwa kiwango cha utajiri wao ukwa kiasi cha 80% kutoka mwaka 2021, wakati thamani ya kampuni za betri na magari ya umeme zimeanguka kwa nusu na robo mtawaliwa.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Ambia Hirsi












