Kwa nini TikTok inaonekana kuwa ni hatari kwa nchi za Magharibi

Chanzo cha picha, AFP
China imeukosoa mswada uliopitishwa na Bunge la Marekani ambao unaweza kusababisha TikTok ipigwe marufuku nchini humo, ikiutaja kuwa mswada usio wa haki.
Ni hatua ya hivi punde katika mvutano wa miaka mingi kutokana na hofu ya usalama kuhusu programu hiyo ambayo inamilikiwa na kampuni ya Uchina.
Maafisa, wanasiasa na wafanyikazi wa masuala ya usalama katika nchi nyingi za Magharibi wamepigwa marufuku kutumia TikTok kwenye simu za kazi.
Kwa hivyo ni maswala gani matatu makubwa kuhusu TikTok, na kampuni imeyajibu kwa njia gani?
1. TikTok hukusanya kiwango kikubwa cha data
Wakosoaji mara nyingi hushtumu TikTok kwa kukusanya idadi kubwa ya data. Ripoti ya usalama wa mtandao iliyochapishwa Julai 2022 na watafiti katika Internet 2.0, kampuni ya mtandao ya Australia, mara nyingi hutajwa kama ushahidi.
Watafiti walichunguza app hiyo na wakaripoti kuwa inatekeleza "ukusanyaji wa data kupita kiasi". Wachambuzi walisema TikTok hukusanya maelezo kama vile eneo, ni kifaa gani kinatumika na ni app gani zingine ziko humo.
Hata hivyo, jaribio kama hilo lililofanywa na Citizen Lab lilibaini kuwa kwa kulinganisha na programu zingine maarufu za mitandao ya kijamii, TikTok hukusanya aina kama hizo za data ili kufuatilia mienendo ya mtumiaji"
Vile vile, ripoti ya Taasisi ya Teknolojia ya Georgia mwaka jana ilisema: "Ukweli ni kwamba mitandao mingine ya kijamii na programu za simu hufanya kama wao."
Vile vile, ripoti ya Taasisi ya Teknolojia ya Georgia mwaka jana ilisema: "Ukweli ni kwamba mitandao mingine ya kijamii na programu za simu hufanya mambo sawa."
2. TikTok inaweza kutumiwa na serikali ya China kupeleleza watumiaji
Ingawa inakera wataalam, wengi wetu tunakubali kwamba kukabidhi data nyingi za kibinafsi ndio makubaliano tunaofanya na mitandao ya kijamii.
Tukibadilishana kwa kutupa huduma zao bila malipo, wao hukusanya taarifa kutuhusu na kuyatumia kuuza matangazo kwenye mitandao yao, au kuuza data yetu kwa makampuni mengine yanayojaribu kututangazia mahali pengine kwenye mtandao.
Suala ambalo wakosoaji wanalo na TikTok ni kwamba inamilikiwa na kampuni kubwa ya teknolojia ya ByteDance ya Beijing, na kuifanya kuwa ya kipekee kama app kuu isiyo ya Kimarekani. Facebook, Instagram, Snapchat na YouTube, kwa mfano, zote hukusanya kiasi sawa cha data lakini zote ni kampuni zilizoanzishwa nchini Marekani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa miaka mingi, wabunge wa Marekani, pamoja na sehemu kubwa ya dunia, wamechukua kiwango cha uaminifu: kwamba data iliyokusanywa na mifumo hii haitatumika kwa sababu chafu ambazo zinaweza kuweka usalama wa taifa katika hatari.
Agizo la Donald Trump la 2020 lilidai kwamba ukusanyaji wa data wa TikTok unaweza kuruhusu Uchina "kufuatilia maeneo ya wafanyikazi wa serikali na wakandarasi, kuunda hati za habari za kibinafsi kwa ulaghai, na kufanya ujasusi".
Kufikia sasa, ushahidi unaonyesha kuwa hii ni hatari ya kinadharia tu - lakini hofu inachochewa na sheria isiyo wazi ya Uchina iliyopitishwa mnamo 2017.
Kifungu cha saba cha Sheria ya Kitaifa ya Ujasusi ya China kinasema kwamba mashirika na raia wote wa China wanapaswa "kuunga mkono, kusaidia na kushirikiana" na juhudi za kijasusi za nchi hiyo.
Sentensi hii mara nyingi hutajwa na watu wanaoshuku sio TikTok tu, bali kampuni zote za Wachina.
Tangu 2020, maafisa wa TikTok wamejaribu kuwahakikishia watu kwamba wafanyikazi wa China hawawezi kupata data ya watumiaji wasio Wachina.
Lakini mnamo 2022, ByteDance ilikiri kwamba wafanyikazi wake kadhaa wa Beijing walipata data ya angalau waandishi wawili wa habari nchini Marekani na Uingereza kufuatilia maeneo yao na kuangalia ikiwa walikuwa wakikutana na wafanyikazi wa TikTok wanaoshukiwa kuvujisha habari kwa vyombo vya habari.
Msemaji wa TikTok anasema wafanyikazi waliopata data hiyo walifutwa kazi.
Kampuni hiyo inasisitiza kwamba data ya mtumiaji haijawahi kuhifadhiwa nchini Uchina na inajenga vituo vya data huko Texas kwa data ya watumiaji wa Marekani, na katika tovuti za Ulaya kwa data kutoka kwa raia wake.
3.TikTok inaweza kutumika kama kifaa cha kushawishi
Mnamo Novemba 2022, Christopher Wray, mkurugenzi wa Ofisi ya Shirika ya Upelelezi FBI, aliwaambia wabunge wa Marekani kuwa "Serikali ya China inaweza kudhibiti teknolojia, ambayo inaweza kutumika kushawishi huduma." Dai hili limerudiwa mara nyingi.
Wasiwasi huo unachochewa zaidi na ukweli kwamba app dada ya TikTok, Douyin - ambayo inapatikana nchini Uchina pekee - imekaguliwa sana na inaripotiwa kuwa imeundwa ili kuhimiza nyenzo za kielimu na zinazofaa kuenea kwa watumiaji wake wachanga.
Mitandao yote ya kijamii imedhibitiwa sana nchini Uchina, huku jeshi la polisi wa mtandao likifuta maudhui ambayo yanaikosoa serikali au kuchochea machafuko ya kisiasa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanzoni mwa kuibuka kwa TikTok, kulikuwa na visa vya hali ya juu vya udhibiti kwenye app. Kwa mfano akaunti ya mtumiaji mmoja nchini Marekani ilifutwa kwa kujadili jinsi Beijing inavyowatendea Waislamu huko Xinjiang. Baada ya ukosoaji mkali wa umma, TikTok iliomba msamaha na kurejesha akaunti.
Tangu wakati huo kumekuwa na visa vichache vya udhibiti, zaidi ya aina ya maamuzi yenye utata ya udhibiti ambayo majukwaa yote yanapaswa kushughulikia.
Watafiti katika Citizen Lab walifanya ulinganisho wa TikTok na Douyin. Walihitimisha kuwa TikTok haitumii udhibiti sawa wa kisiasa.
Hatari ya kinadharia
Picha ya jumla ni hofu ya kinadharia - na hatari ya kinadharia.
Wakosoaji wanasema ingawa inaonekana haina madhara, inaweza kuwa silaha yenye nguvu, kwa mfano wakati wa migogoro.
App hiyo tayari imepigwa marufuku nchini India, ambayo ilichukua hatua mwaka wa 2020 na mitandao mingine kadhaa ya Kichina.
Lakini marufuku ya Marekani kwa TikTok inaweza kuwa na athari kubwa kwenye app, kwani kawaida washirika wa Marekani mara nyingi hufuatana na maamuzi kama haya.
Hilo lilionekana wazi wakati Marekani ilipofaulu kuzuia kampuni kubwa ya mawasiliano ya China Huawei kupelekwa katika miundombinu ya 5G.
China haina haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu app za Marekani kwa sababu ufikiaji wa raia wa China umezuiwa kwa miaka mingi.















