Je, mchuano wa Lissu na Mbowe kuijenga ama kuibomoa Chadema?

Viongozi wakuu wa Chadema Freeman Mbowe (kushoto) na Tundu Lissu

Chanzo cha picha, EAGAN SALLA/BBC

Maelezo ya picha, Viongozi wakuu wa Chadema Freeman Mbowe (kushoto) na Tundu Lissu
    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mwandishi
    • Akiripoti kutoka, Tanzania
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Ndani ya ndege kwenda Mwanza takribani miaka kumi nyuma, mmoja wa watu wa karibu na Makamu Mwenyekitiwa CHADEMA, Tundu Lissu, alimuuliza rafikiye kama ana mpango wowote wa kuwania nafasi ya juu ya uongozi wachama hicho au urais; jibu la Lissu lilikuwa rahisi, namnukuu rafikiye huyo; "Hawawezi kunipa nafasi. I am too radical for them (Mimi nina msimamo mkali sana kwao)". Wakati huo, Lissu, alikuwa mbunge kupitia chama hicho.

Leo hii, Lissu ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA – nafasi ya pili kwa mamlaka ndani ya chama hicho na hivi majuzi ametangaza nia ya kuwania nafasi ya juu kabisa ya uongozi ndani ya chama hicho. Ni wazi atashindana na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, ambaye ameshikilia wadhifa huo kwa takribani miaka 20 sasa.

Miaka kumi - au hata mitano tu nyuma, hili ni jambo ambalo halingeweza kufikirika. Lakini nini hasa kimesababisha Lissu afikie hatua ya kuona anaweza kutoshana nguvu na Mbowe ambaye kwa muda mrefu amekuwa mwanasiasa asiye na mshindani ndani ya CHADEMA?

Kinachoweza kumpa msuli Lissu

Tundu Lissu

Chanzo cha picha, CHADEMA

Maelezo ya picha, Tundu Lissu

Mambo makubwa matatu yamempa Lissu msuli na imani yakuweza kutwaa nafasi hiyo. Kwanza ni tukio la Septemba, 2017 ambako alinusurika kuuawa baada ya kufyatuliwa risasi na watu wasiojulikana.

Tukio lile lilimfanya Lissu atoke kuwa kiongozi wa kawaida wa CHADEMA na kuwa kiongozi wa kitaifa. Wale waliokuwa wakikubaliana naye, walizidi kumpenda na wale ambao hawakuwahi kuwa upande wake, walau walikuwa na huruma naye.

Jambo la pili ni hatua ya CHADEMA kumtangaza kuwamgombea urais mwaka 2020. Katika siasa za Tanzania kwa vyama vikubwa, kwa kawaida nafasi ya urais hugombewa na kiongozi wa juu zaidi wa chama. Ni CHADEMA pekee ambako mtu ambaye hakuwa kiongozi wa juu wa chama amepata nafasi ya kuwania urais mara tatu – mwaka 2010 kwa Dk. Wilbrod Slaa, Edward Lowassa mwaka 2015 na Lissu mwaka 2020.

Kwa nini hili limetokea CHADEMA pekee tena mara tatu? Sababu kubwa ni Mbowe. Yeye ni aina ya wanasiasa ambao hawaogopi kufanya maamuzi magumu na pili ni bahati yakembaya kisiasa kwamba ingawa anapendwa, hajawahi kuwa kipenzi cha watu kama alioamua kuwapa nafasi. Kwenye lugha ya Kiingereza ningesema respected but not popular. (anaheshimika lakini si maarufu).

Jambo la tatu ni uamuzi wa CHADEMA mwaka 2010 na mabadiliko katika siasa za Tanzania na duniani kuanzia mwaka 2012 yaliyoletwa na kuongezeka kwa ushawishi wa mitandao ya kijamii.

xx

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwaka 2010, waanzilishi wa CHADEMA walipatwa na mshtuko baada ya chama hicho kuamua kufuata mrengo wa kushoto kwenye kampeni zake za uchaguzi mkuu wakati huo.

Wapanga mikakati wa CHADEMA akina Profesa Kitila Mkumbo, Profesa Mwesiga Baregu, Zitto Kabwe na wengine waliamua chama kitangaze sera za elimu na afya bure ambazo ni kinyume cha siasa za kibepari za waanzilishi wa CHADEMA.

Zitto aliwahi kunieleza namna Mwenyekiti mwanzilishi wa CHADEMA, Edwin Mtei, alivyowahoji kuhusu ni vipi wanauza sera ambazo ni kinyume cha kuanzishwa kwa CHADEMA na misingi yake. Lakini akina Baregu na Kitila waliona hiyo ndiyo namna pekee ya kufanya chama chao kipendwe badala ya kuheshimika tu kama ilivyokuwa kabla ya mwaka 2005.

Athari ya uamuzi ule wa mwaka 2010 ni kwamba CHADEMA kikabadilika kuwa chama kinachoangalia matokeo ya kisiasa zaidi ya misingi yake. Ndiyo sababu mwaka 2015 hakikupata taabu kumsimamisha Lowassa kuwa mgombea wake wa urais ingawa chenyewe kilikuwa kinara wa kumhusisha na ufisadi wakati akiwa CCM. Lengo likawa kushinda uchaguzi.

Kwa hiyo Lissu anataka kuwania Uenyekiti wa CHADEMA na baadaye Urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa sababu kwa sasa yeye ndiye mwanasiasa mashuhuri zaidi ndani ya chama hicho na kama lengo la chama ni kushinda uchaguzi ujao – na kwa kuzingatia mwenendo wa chama kuanzia mwaka 2010, kampeni ya #NIYEYE, ina mantiki.

Utajuaje kama Lissu ni maarufu kuliko Mbowe? Namna rahisi kuliko zote ni kupitia kwenye mtandao wa X (zamani twitter) ambao ni uga maarufu wa propaganda wa CHADEMA. Lissu ana wafuasi takribani 695,000 ilhali Mbowe akiwa na wafuasi 660,000.

Kona ya Mbowe

Mbowe

Chanzo cha picha, CHADEMA/X

Kufikiri kisiasa, CHADEMA ina nafasi zaidi ya kupiga hatua mbele ikiwa na Mwenyekiti Mbowe kuliko Lissu. Mbowe anasifa zinazofanya vyama vya siasa vya Tanzania vikue kuliko Lissu.

Mbowe ni mwanasiasa mfanyabiashara mwenye uwezo mkubwa wa kusoma upepo na kujua cha kufanya kwenye wakati sahihi. Uongozi wake na tabia yake ya kutoogopa kufanya maamuzi magumu kama ilivyokuwa mwaka 2010 waliapoamua kuachana na CHADEMA ya zamani, ni silaha kubwa.

Kwa upande mwingine, Lissu ni mhafidhina na mtu ambayeni mgumu kubadilika akishaamua kufuata mwelekeo fulani. Wakati Mbowe anaweza kuficha hisia zake mpaka mwishoni, Lissu atasema kama nyeupe ni nyeupe tangu awali.

Kwa chama ambacho sasa kina makundi ndani yake kama vilivyo vyama vingi vikubwa, ni muhimu kuwa na kiongozi ambaye anaweza kusikiliza na kuamua. Kiongozi tofauti, anaweza kukipasua chama badala ya kujenga.

Lakini historia ya vyama Tanzania ni historia pia ya rasilimali fedha kwenye vyama. Vyama vyote vya upinzani vimepata umaarufu na kukua ni vyama vilivyokuwa na ama viongozi wenye ukwasi au waliokuwa na uwezo wa kukusanya fedha.

Maalim Seif Shariff Hamad hakuwa tajiri lakini alikuwa na uwezo wa kupata fedha kufanya siasa. John Cheyo wa UDP alikuwa na ukwasi. Augustine Mrema hakuwa na ukwasi lakini aliweza kuvutia matajiri kumchangia.

Kupanda kwa chama cha ACT Wazalendo kwa sehemu kubwa kumetokana na uwezo wa Zitto Kabwe ambaye ingawa si tajiri, lakini anajua namna ya kutafuta fedha za kufanya siasa.

Mbowe ni tajiri lakini mwenye uwezo pia wa kutafuta fedha. Lissu si tajiri lakini hadi sasa hakuna ushahidi kuwa anauwezo wa kutafuta fedha za kuendesha shughuli za kisiasa za CHADEMA ambacho sasa kimekua sana.

Katika historia ya Tanzania, hakuna chama cha kisiasa kilichowahi kukua na kutishia CCM wakati kinaongozwa na mtu wa aina ya Lissu kwenye suala la rasilimali fedha.

Kimahesabu, hakuna uwezekano wa Lissu kumzidi Mbowekwenye sanduku la kura ndani ya CHADEMA. Katika uchaguzi uliofanyika katika kanda tofauti za chama hicho nchini, wengi wa walioshinda ni wafuasi wa Mbowe. Kwa hiyo, kwa sasa, Mbowe ana namba za kutosha kushinda uchaguzi.

Anachoweza kufanya Lissu ni kutoa shinikizo kuwa endapo atakosa nafasi hiyo, anaweza kuchukua uamuzi mgumu wa kuhama chama na kwenda kufanya siasa kwenye chama kingine. Kuna hisia kwamba tofauti kati ya wafuasi wa wawili hao – Mbowe na Lissu, kwa sasa ni kubwa kiasi kwamba hawawezi tena kukaa kwenye zizi moja.

Lissu tayari ametoa madai ya rushwa dhidi ya viongozi wenzake na kuna hatari kwamba katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwakani, huenda tuhuma hizo zikapazwa zaidi kiasi kwamba upande utakaoshinda utakuwa umepakwa matope ya kutosha.

Jambo lingine muhimu la kufahamu kuhusu Tanzania ni kwamba jambo la kushindana na Mwenyekiti wa chama – na tena mwanzilishi, si jambo linaloweza kuvumiliwa au lililozoeleka. Ni jambo ambalo limewahi kuvunja vyama huko nyuma.

Uamuzi wa Lissu kumvaa Mbowe kwenye uchaguzi ni uamuzi unaoiingiza CHADEMA katika maji ambayo haijawahi kuyaogelea na ni uamuzi wenye hatari katika mustakabali wa chama hicho endapo nyufa zilizojitokeza hazitazibwa.

Lissu na Mbowe sasa ni mafahali wawili. Wahenga walikuwana msemo mmoja maarufu kuhusu mafahari wawili wanapokuwa katika nyumba moja.

Ezekiel Kamwaga ni mchambuzi wa siasa za Tanzania na Afrika.