Mapungufu na mbinu za uchaguzi wa Serikali za Mitaa vinavyoakisi Uchaguzi Mkuu Tanzania

- Author, Sammy Awami
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Tanzania
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Siku moja kabla Watanzania hawajaenda kupiga kura kuchagua viongozi wa serikali za mitaa, wadadisi wa uchaguzi huo wanasema utamaduni wa kuwapuuza wananachi katika mambo ya maendeleo yao umepumbaza hamasa ya wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi huu.
Kasumba ya viongozi wa kitaifa pia kuonekana kufanya majukumu ya viongozi wa serikali za mitaa kumewaondolea uhalali na umuhimu viongozi wa eneo husika na kufanya wananchi wasione thamani ya uwepo wa viongozi wa maeneo yao.
“Maendeleo yanatakiwa yapangwe na wananchi. Sasa serikali imekuwa ikileta miradi mbalimbali ya maendeleo katika yale maeneo, na ile miradi inapokuja, kumekuwa hakuna muonekano wa wale viongozi wa eneo lile wamefanya nini, badala yake inakuwa ni “serikali ya Mama Samia ndio imeleta hayo maendeleo,” anasema Richard Temu, Afisa Uraghbishi Twaweza.
Wengine wamenyooshea kidole sheria na kanuni zinazoongoza uchaguzi huu, pamoja na kupokonywa kwa aina ya viongozi wananchi wanaowataka, kama chanzo cha wananchi kutokuwa na shauku ya kushiriki uchaguzi.
“Hebu fikiria, (ili ugombee) uenyekiti wa kitongoji au ujumbe wa kitongoji, lazima uwakilishwe na chama cha siasa. Kuna hizi mamlaka ambazo zimejikabidhi jukumu la kuendesha nchi na wanatunga haya ma kanuni, masheria ambayo yanazuia ushiriki halisi au ushiriki kamilifu wa wananchi katika kutoa ushawishi wa namna gani mambo katika maeneo yao yaendeshwe” anasema Khalifa Said, Mwanahabari na Mchambuzi wa Siasa.
Uchaguzi wa mwaka huu ulisubiriwa kwa hamu – hasa na wapinzani na wadau wengine wa demokrasia – ili kuona ikiwa utakuwa bora si tu tofauti na ule uliofanyika mwaka 2019 lakini pia ikiwa ungeakisi ahadi nyingi zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake mwanzo wa muhula wao wa uongozi.

Chanzo cha picha, Tamisemi/Instagram
Hata hivyo, baada ya malalamiko dhidi ya sheria, kanunu na usimamizi wa Wizara ya TAMISEMI katika uchaguzi huu, vilivyofuatana na visa vya wagombea wa upinzani kuenguliwa kwa mamia, tayari viongozi wa upinzani, wafuasi wao na wadau wengine wa demokrasia wamekata tamaa kwamba uchaguzi huu utakuwa tofauti na ule wa mwaka 2019 uliogubikwa na ukosoaji mkubwa.
“Ukiniuliza mimi nikwambie ukweli wa Mungu, nisizungumze mambo ya kisiasa siasa tu, kama uchaguzi huu kuna namna yoyote ile ya kuuokoa, nitakwambia haipo. Labda tuanze upya” alisema Tundu Lissu mwanzoni mwa mwezi huu.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hata hivyo serikali imekuwa ikiwaasa wapinzani kutumia njia za kisheria zilizopo kushughulikia malalamiko yako na kutoa msamaha kwa wagombea wa upinzani walioenguliwa kwa makosa yasiyo na msingi wa kisheria.
Wiki mbili zilizopita, Waziri wa Tamisemi Mohammed Mchengerwa alikwenda mbali na hata kuagiza kurejeshwa kwa wagombea wote wa upinzani waliokuwa wameenguliwa kwasababu ya kutodhaminiwa na vyama vyao katika ngazi ya Kijiji/Mtaa pamoja kuwa vyama vyao viliainisha kuwa ngazi ya chini ya udhamini kuwa ni Kata.
Lakini tofauti na miaka mitano iliyopita, katika uchaguzi huu, mabadiliko ya sheria yanayoruhusu kura ya NDIO au HAPANA yamewapa wapinzani na wafuasi wao silaha ya kukomesha mwanya uliowaruhusu wagombea wa chama tawala kuchaguliwa pasipo upinzani wa aina yoyote ile.
Pamoja na kutokususia uchaguzi huu, wapinzani pia wamefanikiwa kushirikiana katika baadhi ya maeneo, aidha kwa kufanya kampeni katika jukwaa moja, kuombeana kura na hata kugawana majimbo katika baadhi ya maeneo.
Mpango huu umeibuka dakika za mwisho na haujafanyika katika namna ya kama ile ya ushirikiano wa chini ya muamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na kuleta mshindo kwa chama tawala katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Hata hivyo, mafanikio ama kushindwa kwa ushirikiano huu na mbinu zingine ambazo upinzani na chama tawala vinatumia katika uchaguzi huu, kutatoa picha ya namna kambi zote mbili zitajiandaa katika kuukabili uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.














